Alhamisi, Aprili 18, 2013

SIMULIZI ...BADO MIMI..... SURA YA ....5.......



ILIPOISHIA:
Maisha yaliendela hali ya Mama ilikuwa ni njema aliweza kuandaa chakula na kumpelekea Baba gerezani mara kwa mara. Kwa upande wangu nilikuwa nimekaa nyumbani kwa kipindi kirefu bila kwenda shule.Kutokana na hali ya pale nyumbani Mama aliniambia  hawezi kunilipia ada ya shule kwahiyo ilinibidi nibaki nyumbani , ijapokuwa nilitamani sana kusoma lakini kutokana na hali halisi ya maisha ya pale nyumbani sikuwa na namna nyingine yoyote.Nini kitaendelea usikose sura ya ......5..........

INAPOENDELEA
Katika maisha yangu nilitamani sana na mimi ningeendelea  na Shule. Nilijaribu kuwasiliana na shangazi yangu ili aweze kunisaidia. Lakini ilishindikana kwani aliniiambia anayo majukumu ya kuwasomesha watoto wake. Ilinibidi nikubaliane na hali halisi ya maisha kwamba sintoendelea tena na masomo, na elimu yangu ya sekondari ndiyo imeishia kidato cha pili.Nikiwa nyumbani nilianza kumsaidia Mama katika biashara ya kuuza mbogamboga na matunda, nilikuwa nikiamka asubuhi na mapema na kwenda kufanya biashara.

Katika kufanya biashara hii ya kuuza matunda, nilijuana na watu mbalimbali kwasababu nilikuwa nikiwauzia matunda watu katika maeneo mbalimbali. Siku moja nikiwa njiani nauza matunda  ambapo kulikuwa na mvua  ikinyesha, huku maji yakiwa yamejaa kwenye madimbwi ya barabarani. Lilipita gari moja aina ya Vitara na dereva aliyekuwa anaendesha alikuwa akiendesha kwa kasi sana.Gari lilipita kwa mwendo kasi wa ajabu, karibu  na miguu yangu,  Kulikuwa na shimo dogo lililojaa maji yale maji yalinirukia na kunichafua nguo zangu zote.

 Kutokana mshtuko matunda yangu yote yalimwagika na kuingia katika dimbwi la maji, nilihuzunika sana. "Mama yangu! nini tena hiki, inamaana huyu dereva hanioni hadi kanimwagia maji kiasi hiki, nitafanya nini mimi matunda yote yamemwagika sijui nitamueleza nini Mama " Nilijikuta machozi yakinitoka huku nikiinama kuokota matunda niliyodondosha katika maji yale machafu.Lile gari liliondoka bila hata ya kusimama.


 Pembeni yangu kulikuwa na Mama mmoja amepaki gari la kifahari aina ya Range Rover alinisogelea "Pole binti hawa madereva wasikuhizi wengine unakuta ni walevi" Niliendelea kulia "Mimi nitafanyaje nyumbani Mama hana hela, na matunda yote yamedondoka nitapata wapi pesa na leo sijauza kabisa matunda" Yule Mama alijitahidi kunibembeleza na baadaye  aliniambia atanipa pesa ya matunda yote niliyodondosha. Nilifarijika sana "Asante sana Mama Mungu akuzidishie" niliongea huku nikijifuta machozi yaliyokuwa yakinibubujika "Usijali mwanangu embu tusogee hapa pembeni kidogo, ningependa kukufahamu zaidi.

Kulikuwa na mgahawa mdogo kwa pembeni ilikuwa ni maeneo ya Mwenge Kijitonyama, niliketi na kuagiza soda pamoja na chakula "Mimi naitwa Mama Bilionea sijui wewe unaitwa nani?" Alijitambulisha yule Mama nilimjibu kwa haraka bila kusita "Naitwa Kandida naishi maeneo ya Mbagala Mgeni nani"  Mama Bilionea akaniuliza "Kandida huko Mbagala Mgeni nani  si ni mbali sana? Unawezaje kuja kuuza matunda huku Mwenge kila siku" nilimuelezea hali halisi ya maisha niliyonayo, sikutaka kumficha jambo lolote kwani nilimuona ni mtu ambaye angeweza kunisaidia hata kazi yoyote ili niweze kuisaidia familia yangu. 

Baada ya kumuelezea yule Mama hali halisi ya Maisha yangu alisikitika sana na kuahidi kunisaidia, siku hiyo alinipa namba zake za simu pamoja na kiasi cha pesa shilingi elfu hamsini, nilimshukuru sana kwasababu sikuwahi kutegemea kama ningeweza kushika kiasi cha pesa nyingi kiasi kile kwa siku hiyo. Mama Bilionea  aliondoka na kunisisitiza nimtafute atanisaidia. Niliondoka na kuelekea kwenye kituo cha daladala za Mbagala ili kurudi nyumbani huku nikiwa nimeshika kwa umakini kiasi cha pesa alichonipa yule Mama.

Nilipofika nyumbani nilimkuta Mama akiwa amejilaza kwenye mkeka "Mbona leo mapema inaonekana biashara ilikuwa nzuri sana" Ilikuwa ni sauti ya Mama ikiniuliza "Ndiyo Mama leo nimepata bahati nzuri sana" Nikiwa naendelea kuongea " Ooooh Mungu wangu ni nini tena hiki, yaani najisikia vibaya sana leo" Mama alilalamika huku akiwa anajiinua taratibu kutoka pale kwenye mkeka " Mama vipi unaumwa?" Nilipatwa na wasiwasi kutokana na hali aliyokuwa nayo "Tokea asubuhi nilipotoka gerezani kumuangalia Baba yako hali yangu sijisikii vizuri nasikia maumivu tumboni yanakuja kidogo, halafu yanapoa lakini naona ni hali inayojirudia mara kwa mara". Nilijihisi kukosa amani "Lakini Mama dawa aluzokupa Daktari umezitumia zote kesho twende hospitalini ukapime".NINI KINAENDELEA USIKOSE SURA YA .....6......

Maoni 3 :

Bila jina alisema ...

HONGERA SANA ADELA KWA UTUNZI MZURI UNAFUNDISHA SANA

Bila jina alisema ...

Hongera, mbona ile simulizi nyingine haiendelei ya jamaa wa kgm

ADELA KAVISHE alisema ...

mdau simulizi ya JAMAA wa kigoma kesho usikose inaendelea sehemu ya mwisho

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom