Jumapili, Mei 26, 2013

SIMULIZI YA KOSA LANGU NI NINI.....SURA YA .....1..........



“ Mungu naomba unisaidie maisha yangu yamekuwa na matatizo mengi kila ninalofanya linashindikana, sijui nikimbilie wapi nashindwa kuelewa kosa langu ni nini? nimepitia tabu nyingi sana, lakini bado maisha yangu sina raha siku zote mimi nimekuwa ni mtu wa kulia nisaidie Mungu wangu ”.

“Nimechoka sana leo na bado kuna kazi zinanisubiri halafu sijisikii vizuri nahisi nataka kuugua” ni maneno aliyokuwa akiwaza moyoni Mama Joyce ambaye alikuwa alikuwa akiosha vyombo, “Hii hali yangu  nahisi kama kuna jambo ambalo haliko sawa embu niandae chakula cha mchana Joyce na James wakirudi wakute nimekwisha waandalia chakula” Alinyanyuka na kuelekea jikoni kuandaa chakula.

Ilikuwa ni siku ya jumanne mida ya saa kumi na mbili jioni Mzee Ndesanjo alikuwa akiendesha  gari aina ya Eskudo. Alifika nyumbani   na haraka alishuka ndani ya gari  kitendo cha kuingia ndani tu  alianza kuita kwa sauti "Mama Joyce Mama Joyce" huko chumbani Mama Joyce alimsikia na kuitika "Abeeee Mume wangu,vipi mbona mbiyo mbiyo hivyo "?  Alihoji  Mama Jocye huku akiwa anamuangalia mume wake kwa umakini.

 Mzee Ndesanjo ambaye ni mume wa Mama Joyce, alionekana kuwa na wasiwasi mwingi huku akimsisitiza mke wake ajiandae haraka "Hakuna muda wa kupoteza,  "Mimi ndani siingii nenda kajiandae tunasafari ya kwenda Morogoro, kuna matatizo yamejitokeza. Rafiki yangu Mzee Simba ambaye tunafanya kazi ofisi moja  amefiwa na mke wake wake inabidi tuwahi kwenda msibani”

Mama Joyce alinyamaza kimya kidogo kana kwamba kuna kitu anatafakari kwani ile habari ilimshtua "Mmmh jamani ni nini tena kilimfika kwani alikuwa anaumwa! masikini" Aliongea kwa masikitiko  "Alikuwa anaumwa na ameugua kwa muda mfupi sana,wewe nenda kajiandae tuondoke".  Mama Joyce akamjibu  "Lakini mume wangu watoto tutawaacha na nani"? Aliuliza Mama Joyce.


  Wakati huo Jocye na mdogo wake aliyeitwa James walikuwa wameenda shule , Joyce alikuwa darasa la tano na James akiwa darasa la kwanza. Na pale walipokuwa wakiishi ilikuwa ni nyumba ya kupanga Maeneo ya Kimara Stop Over jijini Dar es salaam. Baba Joyce alimgeukia tena mke wake  "Hawa watoto tutamkabidhi jirani yetu Mzee Ngonyani na mkewe,  kwani hatuendi kukaa zaidi ya siku mbili wewe jiandae tuondoke wakirudi kutoka shule watakuta maagizo kutoka kwa mke wa Ngonyani".Baba Joyce aliongea kwa msisitizo. 

Kwa haraka  Mama Joyce akaenda kwenye chumba cha Mke wa Ngonyani na kumwachia maagizo ya kuwaangalia watoto wake kwa muda wa  siku mbili. Baada ya hapo aliingia chumbani na kujiandaa tayari kwa safari, ambapo safari ilianza taratibu na baadaye Baba Joyce alionekana kuendesha gari kwa mwendo wa kasi “Mume wangu mbona unaendesha kwa kasi hivyo jamani punguza mwendo kidogo”  Aliongea kwa kuonyesha hali ya uoga.

 Baba Joyce alicheka kidogo na kusema “Acha kuogopa  Mke wangu mbona naendesha katika mwendo wa kawaida sana”. Safari iliendelea  wakiwa njiani maeneo ya  Kidatu, ghafla gari lilipata pancha tairi ya mbele na kupinduka.  Ilikuwa ni ajali mbaya sana kwani Baba Joyce alifariki palepale na Mama Jocye alikuwa ameumia sana sehemu za kichwani hivyo wasamaria wema walimchukua na kumkimbiza hospitalini.
Baada ya wasamaria kumkimbiza hospitalini Mama Joyce ambaye kwa wakati huo alikuwa hajitambui,  Askari  Polisi walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu wa Baba Joyce na kuupeleka chumba cha maiti hospitali ya Morogoro. Gari lilikuwa limeharibika sana kutokana na ajali ilivyokuwa mbaya hivyo ulifanyka utaratibu wa kulisogeza hadi kituo cha polisi, wakiwa hospitalini Mama Joyce alikuwa hajitambui kabisa.

Polisi waliamua kufanya utaratibu wa kufahamu ndugu ambao wangeweza kuwa naye karibu kwa wakati huo, mmoja wa wale Askari Polisi alimwambia mwenzake "Sasa tutafanyaje kuwapata ndugu zao kwani huyu mama hajitambui na mume wake amekwisha fariki inabidi tuwatafute ili waendelee na taratibu nyingine". Mwenzake ambaye alikuwa naye akamjibu na kusema  "Inabidi tuangalie namba zilizopo katika simu zao ili tuweze kuwasiliana na ndugu zao".
........nini kitaendelea usikose sura ya .....2........ NI SIMULIZI YA KUSISIMUA AMBAYO KITABU CHAKE KIPO JIKONI. Niliwahi kuiweka kidogo zamani sana lakini hii ya sasa imekamilika na marekebisho yamefanyika kwa umakini. Endelea kupata uhondo.

Maoni 5 :

Bila jina alisema ...

jmn uwiiiiiiiiii,kuanza na mikosi,ila c ungetumalizia ya mama bilionea na hkna siri mpz?au hutaweza kumudu kutuwekea zote?

ADELA KAVISHE alisema ...

asante rafiki nimeweka ratiba kila siku ya jumatatu na siku ya alhamisi ni simulizi ya Bado mimi na siku ya jumanne na siku ya ijumaa ni hakuna siri lakini siku ya jumatano na siku ya jumamosi itakuwa kosa langu ni nini...karibu sana tuendelee kuwa pamoja

Bila jina alisema ...

Kma ivyo hkn neno mpz,mdau no moja ktk blog yako,mana kile kitabu cha kwanza nilitumiwa kutoka bongo

ADELA KAVISHE alisema ...

asante sana mdau tuko pamoja

Bila jina alisema ...

Thanx

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom