Jumatatu, Juni 03, 2013

SIMULIZI .....BADO MIMI....SURA YA .....18


ILIPOISHIA
Baada ya kumaliza kuongea  ghafla  niliona giza kali sana bila ya kuona mwanga wowote niliogopa huku nikipapasa huku na kule bila ya kushika chochote "Bibi Bilionea usiniuwe jamani nakuomba usiniuwe"  Nilizungumza bila ya kujielewa nguvu zilikuwa zinaniishia taratibu baadaye sauti ilinikauka kabisa sikuweza tena kuzungumza. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA ....18........

INAPOENDELEA
Baadaye  nilizinduka, na kidogo nikaanza kuona mwanga kwa mbali nilikuwa  kama mtu mwenye matatizo ya macho, nilifikicha macho yangu huku nikitizama kwa umakini nishangaa kujikuta nipo nyumbani kwa Mama Bilionea tena chumbani kwangu ambapo huwa nalala "Mmmmh inamaana nilikuwa naota au? Haiwezekani jamani mbona....kama...."Nilikuwa naongea mwenyewe bila kujielewa nimefikaje pale kwa Mama Bilionea nilisikia sauti ikinisemesha "Haikuwa ndoto Kandida,kila kitu kilikuwa ni kweli.

 Naimani sasa umejua ni kwa kiasi gani nakupenda hadi nimekuchagua uwe mrithi wangu. Vinginevyo usingeweza kurudi hapa lazima ungekufa hakuna mtu anayekwenda kwenye hekalu la Bilionea nakurudi akiwa hai." Alikuwa akizungumza Mama Bilionea huku akinitizama, Mimi nilikuwa nimeketi kitandani huku nikionekana kuwa na wasiwasi sana kutokana na mambo yote yaliyonitokea. Nilikuwa nimechoka sana kwani kwa muda wote niliokuwa katika hekalu la Bilionea nilikuwa sijala kitu chochote.Niliongea kwa sauti ndogo na ya upole "Mama Bilionea, kwanini umenichagua mimi, naomba usiimalize familia yangu".

"Hahahahahahahahah" Alicheka Mama Bilionea huku akinisogelea taratibu pale kitandani   na kunishika usoni huku akiinua shingo yangu kwa kunishika kidevu  changu kwa mkono wake "Hivi wewe Kandida, unajua nini maana ya Maisha, Wewe ni Binti mrembo sana nashindwa kuelewa ni kwanini unakuwa mgumu kufahamu  mambo yote haya ni kwa faida yako.Halafu kuhusu familia Mama yako ni mgonjwa na amepelekwa Hospitali."Nilihisi kuishiwa nguvu baada ya Mama Bilionea kuniambia kuwa Mama yangu yupo Hospitalini "Mungu wangu Mama Bilionea umeamua kumtoa kafara Mama yangu, tafadhali nakuomba usimuuwe Mama yangu" Nilinyanuka na kupiga magoti chini huku nikimuomba Mama Bilionea.

 "Hivi Kandida unasahau kuwa Mama yako ana matatizo ya uvimbe tumboni? Sasa nashangaa unasema nimemtoa kafara. Hata na hivyo kutokana na tatizo alilonalo Mama yako hawezi kupona."Mwili ulikuwa ukinitetemeka kwa hasira huku nikilia kwa uchungu nikasema "Mama Bilionea kwanini unaitesa familia yangu, kwanini mimi jamani, hata kama Mama yangu ni mgonjwa ni bora nijue Mama yangu amefariki kwa kuugua kuliko kumtoa kafara, unaitesa familia yangu Mama Bilionea". 


Mama Bilionea alinitizama juu mpaka chini kisha akasema "Unaonekana hauna nguvu ni vyema ukaenda kula chakula kwanza kisha tuende Hospitali kumjulia hali Mama yako. Na pia kuwa makini sana mambo yote ya humu ndani si yakumueleza kila mtu kumbuka kauli ya mwisho uliyoambiwa na Bibi Bilionea. Unaweza kuangamia wewe pamoja na kizazi chako chote. Nakushauri mwanangu Kandida ni vyema ukanisikiliza kile ninachokuambia na hii ni kwa ajili yako na maisha yako." 

Nilikuwa nimeketi pale chini huku natokwa na machozi nilizungumza na nafsi yangu "Mungu naomba unisaidie. sijui nitafanya nini mimi, mbele yangu naona giza nene, sina wa kunitoa katika shimo hili nisaidie Mungu wangu" Nilikuwa katika wakati mgumu sana.Mwili ulikuwa hauna nguvu, kutokana  na njaa kali niliyokuwa naisikia, pamoja na kuchoka na misukosuko ya maisha niliyonayo. Nilichukua chakula pamoja na chai kisha nilikula harakaharaka ili niweze kupata nguvu ya kwenda Hospitali.

Nikiwa naendelea kula chakula Mama Bilionea alikuja akiwa anatokea chumbani kwake. Alikuja na kuketi pale mezani huku akinitizama kana kwamba kuna jambo anataka kuniambia lakini alisita kunieleza. Nilikula kile chakula na kukimaliza kisha nikachukua maji ya kunywa nikaweka kwenye kikombe  cha kunywea maji. Muda wote huo Mama Bilionea alikuwa amenyamaza kimya nilijua alikuwa ananisubiri ili tuanze safari ya kwenda kumtizama Mama yangu Hospitali. 

"Nipo tayari tunaweza kwenda Mama Bilionea" Niliamua kumsemesha huku nikiwa na haraka ya kwenda kumtizama Mama yangu, Mama Bilionea alinitizama nakusema "Embu keti kwanza kuna jambo nataka kukueleza " Nilivuta kiti na kuketi huku nikiwa na mashaka ni kitu gani anataka kunieleza Mama Bilionea. "Kandida Mwanangu, najua ni kwa kiasi gani unampenda Mama yako, lakini hapa Duniani kila mtu atakufa hakuna atakayebaki milele." Niliamua kumkatisha mazungumzo kabla hajamaliza kuongea "Mbona unazungusha sana maneno, Mama Bilionea Kuna nini kimetokea Mama yangu amefariki?" Niliuliza huku nikisimama na kuzunguka huku na kule kama nimechanganyikiwa.

 Mama Bilionea alisimama na kunishika mabegani "Pole sana Kandida ni kweli, nimepigiwa simu na Daktari aliyekuwa anamuhudumia Mama yako amesema kuwa amefariki muda mchache uliopita." Nilikuwa kama nimechomwa sindano ya ganzi huku nikimtizama Mama Bilionea bila ya kuzungumza chochote. Sikuamini kile nilichokuwa nakisikia na wala sikuweza kuzungumza zaidi ya kuketi chini huku machozi yakiwa yananitoka. Moyoni mwangu nilikuwa nasikia maumivu makali sana. "Mama na Baba yangu wote wamefariki  katika mazingira ya ajabu sana, Mungu nisaidie najiona kama mimi ndiye chanzo cha kila kitu. Yalaiti nisingekubali kusaidiwa na Mama Bilionea, najuta sana   nisaidie Mungu wangu kwani sijui nini hatima yangu na wadogo zangu Renata na Tumaini". ......JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA ....... 19......... SIKU YA ALHAMISI.  NA KESHO USIKOSE KUSIKILIZA SIMULIZI YA HAKUNA SIRI.

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Naomba htafute mchungaji fasta la sivyo htajuta,maskn kadinda

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom