Wakati huo Mama Joyce alikuwa hajitambui walimuhamishia Hospitali ya
Muhimbili Dar es salaam kuendelea na matibabu. Huko nyumbani mazishi yalifanyika, vilio na
simanzi vilitawala, watoto walilia sana kwa uchungu na hata kupoteza fahamu
huku wakiwa hawajui nini hatima ya Mama yao mzazi. Hapo ndipo maisha ya Joyce
na mdogo wake yalianza kubadilika. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA...3..
INAPOENDELEA
Baada ya kumuhifadhi Marehemu kwenye makazi yake ya milele.Watu
walitawanyika pale nyumbani na kuwaacha akina Joyce wakiwa na simanzi na wakati
huo waliishi kwa kumtegemea Mzee Ngonyani na mke wake. Maisha yaliendelea huku
baadhi ya watu ambao walikuwa ni majirani na marafiki wa karibu, walitoa michango yao kwa ajili ya matibabu ya
Mama Joyce ambaye alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Yule rafiki yake na marehemu Mzee Ndesanjo alirudi Dar es salaam baada ya
mazishi ya mke wake. Akiwa anatokea Morogoro alikuwa hajui hili wala lile, na nini kimempata rafiki yake kipenzi. Kwani hata
marafiki zake walimficha kwasababu naye pia alikuwa katika matatizo ya kufiwa
na mke wake. Aliporudi Dar es salaam alienda
nyumbani kwa marehemu ili kumjulia hali, alipofika alimkuta Mama
Ngonyani akiwa pamoja na Joyce wakiwa wanajiandaa kwenda Hospitali kumuona
mgonjwa.
Joyce alikuwa akimfahamu rafiki wa Baba yake ambaye alikuwa
akifahamika kwa jina la Mzee Simba. Alipomuona akaanza kumfuata huku akilia kwa
uchungu “Baba mdogo Baba mdogo, ulikuwa wapi Baba yangu amefariki na Mama
anaumwa sana” Mzee Simba alimuangalia Joyce kisha akasema kwa mshtuko "Eti nini! Mzee Ndesanjo amefariki
haiwezekani jamani nini kilitokea, siamini mimi haya maneno” alizungumza huku
akiwa amemshika mkono Joyce aliyekuwa analia kwa uchungu.
Mama Ngonyani akamsimulia kila kitu kuhusu ajali waliyoipata
marehemu Mzee Ndesanjo na mkewe wakati wakielekea msibani Morogoro, Mzee Simba
aliinama kwa uchungu na machozi yalimbubujika katika paji la uso wake. Alisikitika sana kumpoteza rafiki yake, "Siamini
kilichotokea sasa kwanini walinificha jambo hili jamani eeh Mungu ilaze
roho ya marehemu mahali pema peponi".
Alisema Mzee Simba.Baadaye waliondoka pamoja hadi hospitalini kwenda
kumjulia hali Mama Joyce.
Walipofika walimkuta amepata fahamu
lakini alikuwa haongei chochote muda wote alikuwa kimya na
alimshangaa kila aliyekuwa anamuona Joyce aliyekuwa karibu na Mama yake
alimuita “Mama, Mama mimi mwanao Joyce ongea basi Mama hata kidogo” alimuita
bila mafanikio Mama yake alibaki akimshangaa bila kusema chochote, hali ile
iliwatatiza sana Mzee Simba na Mama Ngonyani iliwabidi waende haraka kumuona Daktari ili waweze kufahamu Mama Joyce ana matatizo gani.
Daktari akawaeleza kuwa "Mgonjwa
amepoteza kumbukumbu zote kwani katika hali aliyonayo hawezi kumkumbuka hata
mtoto wake, na pia kuna uwezekano hata kama akirudi katika hali yake ya
kawaida basi atakuwa hana akili vizuri."
Mama Ngonyani kusikia hivyo alishtuka na kusema “Mungu wangu sasa itakuwaje
ndiyo tumekwisha mpoteza Mama Joyce, ina maana Daktari hakuna njia yoyote ya
kumrudisha katika hali yake ya kawaida, tusaidie jamani”. Aliongea mama
Ngonyani huku machozi yakiwa yanambubujika Daktari alimjibu akisema “Uwezekano
hakuna mama, kilichobaki ni Kumuomba Mungu amsaidie pia tunaweza kumruhusu
kesho ili muweze kumuangalia kwa ukaribu
akiwa nyumbani”.
Walibaki wanahuzunika na kutafakari, Joyce alilia sana huku akiwaza
nini hatima ya Mama yake. Baadaye ilibidi waondoke na kesho yake walirudi
kwaajili ya kumchukua Mama Joyce ambaye alikuwa haelewi chochote. Maisha
yalianza kubadilika kwa upande wa Joyce aliyekuwa na Malengo ya kusoma na
baadaye kuja kuwa Mwanasheria. Hali ya maisha
ilizidi kuwa ngumu. Kwani Mama Joyce alikuwa akihitaji huduma wakati wote
ilifikia kipindi familia ya Mzee Ngonyani ikaanza kuwatenga na hata
waliokuwa marafiki waliwaacha wakitaabika wenyewe. "Mwanzoni kabla Baba hajafariki majirani walikuwa wanatupenda lakini leo hii tunabaki tukitaabika peke yetu, tizama Mama yangu ni mgonjwa sana" Alikuwa akiwaza Joyce.
Kutokana na hali kuwa mbaya
Joyce aliamua kuacha masomo akiwa darasa la sita ili aweze kumsaidia mama
yake pale nyumbani. Mzee Ngonyani na Mkewe waliamua kuhama katika ile nyumba. Na
tokea walipohama hawakuwahi kurudi hata siku moja kwenda kumjulia hali Mama Joyce. Maisha yalizidi kuwa magumu, Joyce na
mdogo wake ilibidi wakati mwingine waende mitaani na kuomba msaada angalau
wapate pesa ya kununua chakula pale nyumbani.
Siku moja Mama Joyce aliamka asubuhi kichwa kilikuwa kinamuuma sana
hivyo alitakiwa apelekwe hospitalini. Joyce alikuwa hana chochote kwani
alikuwa akitegemea biashara ya kuuza maandazi na pesa ilikuwa ni ndogo
alihangaika sana bila kupata msaada wowote. Hatimaye kutokana na hali ya maisha na Joyce bado alikuwa ni msichana
mdogo alishindwa namna ya kumsaidia Mama yake. Masikini Mama Joyce alifariki Dunia kutokana na kuumwa
sana bila kupata matibabu.
Aliwaacha Joyce na James ambao sasa walikuwa
ni yatima. Maisha yalikuwa magumu hawakujua nini cha kufanya kwani hata
nyumba waliyokuwa wakiishi walifukuzwa kutokana na kushindwa kulipa kodi. Baada
ya kufukuzwa walijikuta wakirandaranda
mitaani kutafuta kipato."Dada njaa inaniuma" James alikuwa akimwambia Dada yake aliyekuwa amejiinamia huku akiwaza siku hiyo walikuwa hawajapata pesa kabisa kwani kila walipokuwa wanaomba hakuna aliyewapa pesa Joyce alimtizama mdogo wake na kusema "Usijali James nitakunulia chakula, ngoja niende nikaombe kwenye magari yanayopita barabara ya upande wa pili".
Alinyanyuka huku akiwa ameweka mikono yake kichwani alijaribu kumuomba kaka mmoja "Samahani kaka naomba unisaidie hela nikamnunulie mdogo wangu chakula" Yule kaka alimtizama Joyce kuanzia chini hadi juu na kusema "Unawazimu wewe msichana, mimi nikusaidie hela umeambiwa mimi benki halafu mabinti wa sikuhizi mnajifanya ombaomba kumbe makahaba tu wa mitaani kwenda zako." Yule kaka alimtukana Joyce ambaye alinyamaza kimya na kuondoka taratibu aliendelea kuomba hatimaye alifanikiwa kupata shilingi elfu moja na mia tano ambapo alienda moja kwa moja kumnunulia chakula mdogo wake. Maisha ya Joyce na James yamebadilika na sasa wamekuwa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu huku wakikutana na changamoto nyingi sana wakiwa mitaani. JE NINI KITAENDELEA ....USIKOSE SURA YA...4.....
Maoni 2 :
Duh maskin.ila mungu ni mwema hamtupi mja wake
Ooh! Jamani nna imani maisha yatakuja kubadilika hapo badae inshallah.
Chapisha Maoni