Jumatano, Julai 03, 2013

KOSA LANGU NI LIPI....? SEHEMU YA ...12....



 ILIPOISHIA
“Hee leo umepotea njia” Joyce alicheka kidogo na kusema “Lina na wewe hata salamu” Lina akamjibu “Mwenzangu nimeshangaa kukuona. hatujaonana siku nyingi au ndiyo shemeji anakuficha” Baadaye alimkaribisha ndani na kumpatia kinywaji, na waliendelea kuzungumza “Eeh rafiki yangu, niambie za huko kwako vipi shemeji mzima” Alisema Lina.Joyce alinyamaza kimya kidogo na kujibu “Mzima lakini huko si kwema sana, nina tatizo kidogo”. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE ....SURA YA.....12.......

INAPOENDELEA 
“Tatizo gani tena wewe mwanamke una mume anakupenda. kila kitu unapata  sasa una matatizo gani” Alisema Lina huku akiguna kidogo. Joyce alimjibu “Tatizo ni kupata ujauzito,hapa nilipo sijui nifanyeje natamani kweli kupata mtoto na Fredy jana alipofika tu baada ya kutoka kazini amelizungumzia hilo na kusema anataka mtoto” Lina alimsikiliza kwa umakini na kusema  “Sasa hapo kuna tatizo gani, ni kwenda  tu Hospitali. mkaangalie kama kuna tatizo. Mshauri mume wako ili muende kwa wataalamu watawasaidia, mbona kuna watu wanakaa hata miaka kumi ndiyo wanakuja kupata mtoto”  Joyce akamjibu “lakini kweli rafiki nitafanya hivyo”. Waliendelea kuzungumza baadaye Joyce aliondoka na kurudi nyumbani.



Huko nyumbani siku zilivyozidi kwenda Fredy aliendelea na nia ya kutaka kupata mtoto. Ndipo Joyce alipoamua kumuambia kuhusu kwenda Hospitalini. Siku hiyo Joyce alifika nyumbani na kufanya kazi zake za  nyumbani kama kawaida kisha aliketi sebuleni akimsubiri Fredy ili amshauri kuhusu kwenda hospitalini. Akiwa pale sebuleni moyoni mwake aliwaza akisema “Eeeh Mungu naomba unisaidie nipate mtoto, hivi  inawezekana labda kizazi changu  kiliharibika nilipokuwa natoa mimba, kipindi nipo kwa Maliki sijui nitafanyaje kama mimi ndiye mwenye tatizo na Fredy hafahamu kama mimi nilishawahi kutoa mimba naogopa sana kumpoteza Fredy”.

 Akiwa anaendela kuwaza alishtuka Fredy yupo karibu yake. Fredy alimshangaa na kusema “Vipi mke wangu mbona una mawazo sana yaani mimi hadi naingia ndani hunioni unawaza nini?” Joyce aliamua kutabasamu kisha kusema “Samahani mume wangu nilikuwa nimepitiwa kidogo ila pia nilikuwa nawaza kuhusu wazo la kupata mtoto” Kabla hajamaliza kuzungumza  Fredy akasema “ Vipi kuna dalili ya ujauzito mke wangu” 




Joyce akasema “Hapana nilikuwa napendekeza tuende Hospitalini kuangalia kama kuna tatizo naamini watatusaidia” Fredy alicheka kidogo na kusema “Unajua mke wangu nilijua ipo siku utaniambia hivyo, mimi sina tatizo na kwanza nilipoona tumekaa muda mrefu bila ya kupata mtoto. Niliwahi kumuomba Daktari aniangalie kama nina uwezo wa kumpa mimba mwanamke. Na majibu ninayo kwamba sina tatizo. Kwahiyo wa kwenda Hospitali ni wewe na si mimi”

Joyce alishangaa  na kusema “Lakini Fredy, haujanitendea haki mume wangu. Kwanini hukunishirikisha” Fredy alinyamaza kimya kidogo na kusema “Naomba unisamehe mke wangu, kwani niliogopa nikahisi isije ikawa mimi ni tatizo. nilitamani kujua mapema samahani kwa hilo” Joyce aliinama chini kidogo kisha akamwangalia mume wake na kumuahidi ataenda kuangalia nini tatizo. Ilipita kama wiki moja tokea Joyce na Fredy wazungumze juu ya kupata mtoto mambo yalizidi kuwa mabaya kwa upande wa Joyce kwani  hata ndugu wa Fredy walianza kuhoji kuhusu mtoto.



 Siku moja Mama yake mzazi na Fredy alienda kuwajulia hali Joyce na Fredy. Siku hiyo alimkuta Joyce kwani Fredy alikuwa hayupo kwa wakati huo."Habari za hapa Joyce, binti yangu naona unazidi kupendeza" Alisema Mama Fredy. Joyce alijibu huku akionyenya tabasamu pana "Asante mama jamani nimefurahi umekuja kutusabahi, nikuletee kinywaji gani Mama yangu" Mama Fredy akamjibu "Hapana Joyce usiniletee chochote embu keti kwenye sofa kwanza tuzungumze".



 Joyce alijisogeza huku akisema "Lakini mama si ningekuletea angalau hata soda" Mama Fredy akasema "Hapana Joyce hizo soda nakunywa kila siku, mimi kilichonileta hapa nataka kujua hivi unawaza nini kuhusu kupata mtoto jamani" Joyce alinyamaza kimya kidogo bila kujibu chochote kana kwamba kuna kitu anatafakari "Hivi si nazungumza na wewe Joyce inamaana hunisikii" Alihoji Mama Fredy "Hapana Mama, Mimi na mume wangu tumeshalizungumzia suala hilo la kupata mtoto.Kwani  muda bado upo Mama mtoto atakuja tu" Alisema Joyce huku akimtizama mkwe wake, ambaye hakuridhika na majibu ya Joyce  "Muda upo! muda gani huo? Wakati  ndiyo huu, natamani sana kumuona mjukuu wangu, au wewe binti ni mgumba?" Aliuliza mama Fredy.



 Joyce alionekana kukosa amani na kusema "Jamani Mama kupata mtoto ni mipango ya Mungu. Naamini Mungu atatusaidia tu...."Kabla hajamalizia kuzungumza Mama Fredy alimkatisha na kusema "Sikiliza nikuambie binti mimi naona hapa kuna tatizo. Sasa kama mwanangu ameoa mwanamke mgumba, itabidi atafute mwanamke mwingine ili azae naye. siwezi kukubali mwanangu asiwe na mtoto wakati wanawake wapo wengi" Joyce alimsikiliza Mama Fredy kwa umakini na kusema "Lakini mama mbona unafika huko" Alilalama Joyce Mama Fredy akamjibu kwa sauti iliyojaa jazba "Huko wapi?Ahera au, tena sikiliza nikuambie fanya ufanyalo mimi nahitaji mjukuu. alaah! Hivi unafikiri hili jambo ni dogo eeh, mimi naondoka lakini tuliyoyazungumza hapa ukae nayo kichwani na uyafanyie kazi" Aliongea huku akiondoka na kumuacha Joyce akiwa ameketi pale sebuleni. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA ......13..... NA KESHO USIKOSE SIMULIZI YA ,,,,,,,BADO MIMI.....

Maoni 3 :

Bila jina alisema ...

mhhhhhhhhhh majanga yameanza,mungu msaidie joyce jmn awe mzma.

Bila jina alisema ...

Heeeeeey! ndo yamekuwa hayo tena,! hilo ndio tatizo la kuoa na kukaa karibu na wazazi, ni vurugu 2pu, lkn jaman hayo yote matatizo kwa joyce ni kwa 7bu ya maliki. cha msingi joyce awe mvumilivu mola atakuwa naye na atapata mtoto 2

emuthree alisema ...

“Tatizo gani tena wewe mwanamke una mume anakupenda. kila kitu unapata sasa una matatizo gani”
Tupo pamoja mpendwa

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom