Pages

Jumamosi, Julai 20, 2013

SIMULIZI...KOSA LANGU NI LIPI....?...SEHEMU YA ....17........ILIPOISHIA
Fredy alishangaa kusikia hivyo na kusema “Embu mkaribishe ndani”  Sukari ambaye muda wote alikuwa amenyamaza kimya aliingia ndani Fredy alimtizama huku akijiuliza maswali na nafsi yake "Mbona mimi huyu mtu simfahamu, na anamfahamu vipi mke wangu." Aliwaza na kumsalimia Sukari "Habari  yako, karibu sana, sijui ulikuwa na shida gani" Aliuliza Fredy huku Sukari akiwa anamtizama bila ya kuzungumza chochote. Je nini kitaendelea usikose ...SEHEMU ....YA 17.....

 INAPOENDELEA

Fredy kuona Sukari amenyamaza kimya, aliamua kuuliza tena “Vipi ndugu ulikuwa na shida gani?” Sukari alimtazama Fredy huku akionyesha tabasamu la kinafki “Sijui nianzie wapi ili unielewe nadhani Joyce angekuwepo ingekuwa vizuri zaidi, nafikiri wewe utakuwa ni mume wake." Aliuliza Sukari “ Ndiyo, Unaweza kuongea tu mimi ni mume wa Joyce, kwani ulikuwa unashida gani?Mbona unazungusha maneno, kama kuna jambo lolote unaweza kuniambia bila tatizo, karibu sana, tunaweza kusogea na kwenda kuketi sebuleni" Waliongozana na Fredy alimkaribisha vizuri Sukari.

Wakiwa pale sebuleni walianza mazungumzo "Karibu sana kaka, sijui nikusaidie kinywagi aina gani kuna soda, maji na juisi" Alisema Fredy huku akiwa anamtizama Sukari "Asante sana, ila sihitaji kinywaji chochote, jambo kubwa lililonileta hapa, ni kuonana na Joyce, ili..." Kabla hajamaliza kuzungumza Fredy alimkatisha na kusema "Joyce hayupo, lakini kama nilivyokueleza, mimi ni mume wake unaweza kunieleza jambo lolote na akirudi nitamfikishia ujumbe, kwani wewe ulikuwa na shida gani na mke wangu?".


 Aliuliza Fredy huku akimtizama kwa kumkazia macho,  Sukari akamjibu “Kwasababu umenisisitiza nitakueleza, mimi naitwa Sukari, nimefahamiana na mke wako miaka mitatu iliyopita, na alikuwa ni mpenzi wangu...."Fredy aliguna kidogo na kusema "Ati unasema miaka mitatu iliyopita Mama James alikuwa mpenzi wako? Una uhakika na unachokizungumza wewe, unajua huyo unayemzungumzia hiyo miaka mitatu iliyopita tayari alikuwa ni mke wangu" Alihamaki Fredy huku akimshangaa Sukari ambaye hakujali kumuona katika hali ile na kuendelea kusema "Sikiliza nikuambie kaka mimi sikuwahi kujua kama Joyce alikuwa ni mke wa mtu, na pia nimekuja hapa kwa lengo moja tu nahitaji mtoto wangu”.

 Fredy akamjibu kana kwamba alikuwa hajamsikia vizuri “Eti umesema nini wewe,  unahitaji mtoto wako?au sijakuelewa vizuri” Sukari akamwambia “Katika kipindi ambacho nilikuwa na Joyce  alifanikiwa kupata ujauzito lakini alinificha, sikufahamu lolote kwa kipindi hicho.Kumbe Joyce alikuwa  na nia  ya kuwa na mimi ili abebe ujauzito.Kwani baada ya kujigundua kuwa ni mjamzito alianza kunionyesha vituko, na tuliachana bila sababu yoyote ya msingi, na kwa wakati wote huo sikujua yeye alikuwa na lengo gani."

  Lakini namshukuru sana  Lina rafiki yake kipenzi  na Joyce, ambaye mwanzoni ndiye aliyetukutanisha ameniambia kila kitu. kuwa Joyce anaye mtoto na ni wakwangu na vilevile...” Kabla hajamaliza kuzungumza  Fredy aliyekuwa akimsikiliza kwa umakini  alimkatisha na kusema “Hivi wewe una kichaa,  au umetumwa, nahisi wewe ni mwendawazimu. Hivii unamzungumzia mke wangu huyuhuyu Joyce au umekosea njia?” Sukari akahamaki “Samahani sana mimi siyo kichaa nina akili zangu zote timamu. Sasa ni vyema  huyo mkeo angekuwepo ili  azungumze ukweli mimi ninachotaka ni mtoto wangu. Mimi baba yake nipo hawezi kulelewa na mwanamume mwingine”.


Fredy alikuwa kama haamini anayosikia alizunguka pale sebuleni bila kujua wapi anaelekea huku akijisemea “Inamaana James si mtoto wangu? Joyce alikuwa na mwanamume mwingine siamini kwakweli” Sukari akajibu “ Wewe uamini usiamini hiyo ndiyo hali halisi” Wakiwa wanaendelea kuzungumza ghafla Joyce aliingia akiwa hana wazo lolote nini kinaendelea ghafla alishtuka kumuona Sukari alishindwa hata kutoa salamu akabaki ameduwaa , Fredy alimuangalia na kusema “Habari za kazi mke wangu” Joyce huku akitetemeka mithili ya mtu aliyeona kitu cha kutisha akasema “Ni kwema na za hapa”.

 Fredy akaguna na kusema “Mgeni wako huyo hapo” huku akimuangalia Sukari Joyce alinyamaza kimya huku akiwa ameinama chini Sukari akasema “Nimekuja kumchukua mtoto wangu mueleze kila kitu mume wako kwasababu ananiona mimi ni kichaa” 

 Joyce alianza kulia huku akimungalia Fredy na kusema “Nisamemehe mume wangu nimekosa nisamehe sikudhamiria kutenda yote haya’ Fredy kuona vile alisogea karibu na kumsukuma Joyce kwa nguvu huku akimpiga na kutoa maneno makali “Yaani  nilifikiri haya maneno hayana ukweli kumbe wewe mwanamke ni muuaji kweli unaamua kunifanyia mimi yote haya. Aibu gani hii jamani sikutaki tena Joyce, mchukue na mtoto wako muondoke na huyo baba yake. Nakuambia ondoka sitaki kukuona”.

 Joyce alilia sana huku akijaribu kuomba msamaha bila ya mafanikio. baadaye msichana wa Kazi alikuja akiwa na mtoto James. Sukari alimchukua mtoto akambeba, Jame alikuwa ni mtoto asiyeogopa watu.Sukari alimwacha Joyce  na kuondoka na mtoto.  Joyce alikuwa akilia huku akiomba msamaha lakini Fredy hakutaka kumsikiliza na kusema “Toka mjinga mkubwa wewe, Nafikiri  hata hiyo mimba uliyonayo siyo yangu. Kahaba mkubwa wewe toka nakwambia sitaki kukuona” Yaani ilikuwa ni purukushani ya patashika nguo kuchanika.  Fredy alimtupia Joyce baadhi ya vitu vyake nje ambapo ilimbidi Joyce aondoke na kuelekea katika hoteli. Huku mtoto akiwa amechukuliwa na Sukari . James alikuwa hana tabia ya kuogopa watu, kwani alikuwa akipendelea sana michezo. Hivyo ilikuwa ni rahisi kwa sukari kuishi naye.
 Joyce alikuwa katika wakati mgumu sana, akiwa Hoteli aliwaza sana  “Eeeh Mungu naomba unisaidie, nisamehe kosa langu, sijui nitafanyaje, yaani nahisi kuchanganyikiwa, nyumbani wakigundua baba mkubwa na mama watanifikiriaje najuta sana kukubali ushauri wa Lina. Hapa nilipo nina nina ujauzito wa Fredy, yalaiti ningevuta subira kipindi kile yote haya yasingetokea.Sasa maji yameshamwagika na hayazoleki. nimeharibu kila kitu na Fredy hanitaki tena. Sijui nitaificha wapi sura yangu.eeh Mungu nisaidie" aliendelea kuwaza Joyce huku machozi yakimtoka.JE NINI KITAENDELEA...USIKOSE... SEHEMU YA  18. SIMULIZI YA BADO MIMI ITAKUWEPO JUMATATU

         


Maoni 4 :

Bila jina alisema ...

mhhhh maskin sasa lina atafurai,ila usijl yataisha tu joy.

Bila jina alisema ...

Mamaaaaaaa,! hivi ni kweli ninachokisoma au ni miujiza,! maskini joice ameanza maisha ya kutangatanga tena. ukiomba ushauri kwa mu2 jaribu kuchanganya na akili zako,!

Bila jina alisema ...

Heeeeeee! jamani joyce pole sana! na hiyo ndo faida na hasara ya kutokuwa mwaminifu na kuwa muongo ktk ndoa yako. cha msingi omba mungu ili fred akurudishe kwake

Bila jina alisema ...

Ooh! Maskini Joyce. Fred msamehe mkeo kwani anakupenda.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom