Jumapili, Julai 14, 2013

" WAHESHIMU BABA NA MAMA UPATE MIAKA MINGI NA HERI DUNIANI" LAKINI MAAJABU HAYA MISS TANZANIA AMTESA MAMA YAKE...

Amlazimisha kusafisha mbwa 12 anaowafuga
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mshiriki wa Miss Tanzania 2002, Samia Khan (26) anadaiwa kumfanyia vitendo vya kitumwa mama yake mzazi ikiwa ni pamoja na kumpiga na kumfungia ndani bila kula.

Inadaiwa Samia mkazi wa Ungindoni, Kigamboni jijini Dar es Salaam, alifanya unyama huo kwa kipindi cha mwezi Juni mwaka huu kwa kushirikiana na mchumba wake mwenye uraia wa nchi ya Uingereza.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, mama mzazi wa Samia, Anitha Charles (39), mwenyeji wa Lushoto mkoani Tanga, alisema binti yake alimfungia ndani kama mfungwa, kumtukana na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali ya mwili kwa kipigo.
Akiwa ndani ya nyumba moja isiyokamilika ujenzi wake alipohifadhiwa kwa muda, alisema chanzo cha kufanyiwa unyama huo ni madai ya mtoto wake kuwa anamuibia mchumba wake pesa wakati wao wakiwa hawapo.
Alidai tangu afike jijini Dar es Salaam, maisha yake yamekuwa magumu kila siku baada ya binti yake huyo kumfanyisha kazi za kitumwa kwa kumlazimisha kufua nguo za ndani za mchumba wake pamoja na kusafisha mbwa 12 anaowafuga.


KUHAMA LUSHOTO KUJA DAR
Anitha alisema Samia ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu aliowazaa na mumewe Hakim Khan, ambaye alifariki mwaka 2009.
Alisema wakati akiwa na mumewe, waliweka makazi yao Mjini Iringa, lakini baada ya kifo chake aliamua kwenda kuishi Lushoto karibu na familia yake iliyopo mkoani Arusha.
Hata hivyo, alipokuwa Lushoto, binti yake huyo alikuwa akimshawishi kuhamia jijini Dar es Salaam ili wawe karibu naye.
"Alinishawishi sana kuja huku, hapo mwanzo nilikataa kwa sababu kule nilikuwa nina biashara zangu na hali ya hewa ya joto sipatani nayo," alisema.
Baada ya kuona mama yake ameng'ang'ania na msimamo huo, Samia alimuongopea kwamba amepata nyumba kubwa, hivyo hawezi kuishi peke yake na anahitaji kuwa na familia ili waweze kuimilki.
"Baada ya kujadiliana na ndugu zake, nilikubali kwa shingo upande kuja, siku ya pili mwanangu akiwa na mchumba wake walikuja na kutuhamisha," aliongeza kusema.
NYUMBA ZA MATESO
Alisema baada ya kufika jijini Dar es Salaam, walifikia eneo la Msasani na kukuta wanaingia katika nyumba ya vyumba vitatu na sio katika nyumba kama alivyoambiwa awali. Kutokana na kuwa na vitu vingi, baadhi ya vifaa vilikuwa vimewekwa nje ya nyumba kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka huu walifanikiwa kupata nyumba eneo la Bunju, ambapo huko ndipo mateso yalianza taratibu, ambapo binti huyo alianza kumtukana na kumlazimisha kumfulia nguo na kusafisha mbwa.
"Kutokana na hali yangu nilikataa kusafisha mbwa, nilichokuwa nafanya ni kufua nguo tu, wakati mwingine napewa hata nguo za ndani za mkwe wangu, ni matusi makubwa kwangu," alisema mama huyo huku akilia.
Alisema kutokana na hali hiyo kuwa ngumu, aliomba arudishwe nyumbani kwake Lushoto kwa kuchoshwa na manyanyaso.
"Alipoona nazidi kung'ang'ania kuondoka, mwanangu alitunga uongo mwingine kuwa amenitafutia nyumba ya kuishi peke yangu pamoja na eneo la biashara, ndipo nilipoletwa huku Ungindoni lakini hali ilikuwa ile ile," alisema.
Alidai hali mbaya ilianza wiki ya kwanza ya mwezi Juni, ambapo binti yake baada ya kurudi kwenye matembezi yake na mchumba wake, alimfuata na kumueleza kuna wizi umetokea wa pesa za kimarekani Dola 400 za mchumba wake.
Licha ya kukataa kuhusika na jambo hilo, mwanawe alianza kumtukana matusi ya nguoni na kumuita mbwa.
Baada ya kutukana, alimchukua na kumuingiza chumbani, kisha alifunga mlango na funguo na kuondoka kusikojulikana.
"Aliporudi aliniuliza kama nimezirudisha hizo pesa, niliposema sifahamu wizi huo, alianza kunipiga mfululizo na kuniumiza vibaya tumboni na mdomoni," alizidi kusema.

AMKOSEA RADHI
Baada ya kuona kichapo kinazidi, mwanamke huyo kwa hasira aliamua kuvua nguo zote kama ishara ya kumkosea radhi, kitu ambacho kilisababisha mtoto wake kuacha kumpiga na kuendelea kumpatia vitisho.
"Ni vibaya kwa mzazi kuchukua hatua kama ile, lakini ilinibidi baada ya kuona damu zinanitoka huku yeye akionekana hanionei huruma, inaniuma sana," alisema.
Kwa kupata mwanya huo, alikimbilia serikali ya mitaa kwa ajili ya kuomba msaada wa hifadhi na ofisi hiyo ilimlazimishe mtoto wake amrudishe Lushoto akaendelee kuishi kama awali.
Alisema, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ungindoni, Aisha Mohamed, alijaribu kuwasuluhisha na kumuomba Samia amrudishe mama Lushoto lakini ampatie hifadhi katika nyumba hiyo hadi hapo atakapopata pesa ya kumsafirisha.

MWENYEKITI ANENA
Mwenyekiti huyo alipozungumza na Gazeti hili, alikiri kulifahamu suala hilo na kusikitishwa kwa kitendo cha polisi kuingilia kati na kumuondoa kwa nguvu mama huyo ndani ya nyumba.
Alisema jambo hilo lilipata ufumbuzi baada ya kukutana na pande zote mbili, ambapo kwenye maamuzi ya jumla walikubaliana mwanamke huyo pamoja na mtoto wake wa miaka 10 waendelee kuishi kwenye nyumba hiyo hadi hapo atakapopewa nauli ya kumsafirishia yeye na mizigo yake.
"Nilimwambia yule binti kwamba pamoja na kukosana, lakini nazi haishindani na jiwe, lazima amuheshimu mama yake na ampatie hifadhi hadi hapo nauli itakapopatikana," alisema Aisha.
Wakiwa wanasubiri utekelezwaji wa ahadi hiyo, alisema siku ya pili yake nyakati za usiku, polisi kwa kushirikiana na mtoto wake walivamia nyumba hiyo na kumtoa kwa nguvu na kumpeleka kituo cha Kigamboni.
Aisha, alisema kitu cha kushangaza siku ya pili yake aliachiliwa, lakini aliamriwa kuondoka haraka ndani ya nyumba hiyo.
"Hana sehemu ya kwenda, tumeamua kumsaidia hadi hapo utakapopatikana uwezo wa kumsaidia kurejea nyumbani kwake," alisema.
Hata hivyo, alipotafutwa Samia kwa kutumia simu yake ya mkononi, kwa ajili kuzungumzia tuhuma hizo simu ilionekana kuzimwa muda wote.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

Maoni 9 :

Bila jina alisema ...

jmn jmn wengne tunawasaka hta wakuwaita mama hatupati yy anamfanyia hivyo?????????????ila htambue malipo ni duniani,tuwekee pic yke tumuone uyo mdada jmn mbna ana roho mbya kbsa kha! mama ako umpige?????????hii kali ya mwaka.

Bila jina alisema ...

kitu kizuri duniani hakuna kama Mama hata kama anakukosea vipi mimi naomba serikali imchukulie hatua kali sana huyo mdada

Bila jina alisema ...

Jamani dunia hii haya ni majanga.
Watu wanawatafuta mpaka mama wa badnia leo unamyanysa mama yako.
OOo mwenyezi mungu atanusuru na vizazi vyetu kiulweli huyu binti amenikela sana

Bila jina alisema ...

Mwenye miaka 39 ni mtoto ni mama?Kama ni mama alimzaa lini huyo bibie?na huyo mtoto ana umri gani?

Bila jina alisema ...

Mama ana miaka 39, mtoto miaka 26! wametofautiana miaka 13?!!!!!

Unknown alisema ...

Mama n mama

Bila jina alisema ...

Ndio maama hamuheshimu kwa sababu mtoto kazaa mtoto.Kwa tofauti ya umri huo sidhani kama kuna haja ya kuumiza kichwa kwa nini hamheshimu mamaye maana anaona wako sawa tu.

Bila jina alisema ...

hiyo wala sio sababu mama ni mama hata akiwaje

Bila jina alisema ...

naye huyu dada (the so called mama) kwa nini anaendekeza kuteswa? from huko msasani inaonyesha wazi alipata mateso, kwa nini asingeenda polisi kuripoti, then angeomba msada wa pesa za kumfikisha kwao..at the age of 39 she seems helpless & desperate why? nayeye wala sio mtu mzima wa hivyo in fact she is still very young. na huyo mtesaji??!!!! ni ulimbukeni ama? alihitaji maid wa kumtesa akamchagua mama? yani roho inaniuma utadhani mtu kamfanyia mama yangu..dunia hii??! tunavyojipendekeza kwa wazazi hata akukwaze unajitahidi usimwonyeshe hasira unatafuta njia ya upole kusema naye, yeye anamgeuza maid, na dharau juu..ama kweli...NAOMBA MKONO WA MWENYEZI MUNGU UMFIKIE. SISI WAKRISTU KUNA AMRI ALIYOTOA MWENYEZI MUNGU KWAMBA WAHESHIMU BABA NA MAMA UPATE MIAKA MINGI NA HERI DUNIANI. SIDIRIKI KUSEMA ASAMHEWE ILA NASEMA AONJE JOTO YA JIWE JAPO KIDOGO THEN NDO ASIMAME

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom