Pages

Jumatatu, Septemba 23, 2013

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA


MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE
KITABU MALIPO NI HAPAHAPA

Hii ni moja ya simulizi iliyopo katika KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA, IFUATILIE HAPA MWANZO HADI MWISHO WAKE.


Katika Mji wa Arusha Mtaa wa Kaloleni ni eneo ambalo wakazi
mbalimbali walipendelea sana kuishi kutokana na mazingira yake kuwa
tulivu na yenye mandhari nzuri. Katika mtaa huo aliishi mzee mmoja
aiitwaye Magesa. Mzee huyo alikuwa na mke na watoto watatu, watoto
wawili wakiume ambao waliitwa Joseph na Peter na mtoto mmoja wa kike
aliyeitwa Julieth.

Mzee Magesa hakuwa na uwezo mkubwa sana kifedha. Maisha ya Mzee
huyo na famila yake yalitegemea sana kipato kidogo kilichotokana na
biashara ya kuuza mboga sokoni ambayo alikuwa anaifanya siku zote za
maisha yake hadi akapewa jina la ‘Muuza mboga’. Mke wake alikuwa ni
mama wa nyumbani akijishughulisha na kupika chapati na kuuza ili
kuongeza kipato kwa ajili ya mahitaji ya pale nyumbani.

Maisha yalikuwa magumu sana lakini familia ilikuwa na furaha na upendo
kwani waliishi kwa kupendana na kuheshimiana. Mzee Magesa aliwapenda
sana watoto wake, kwani mara nyingi alikuwa akiwafundisha mambo
mbalimbali kuhusu maisha ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza kusoma. Julieth
alikuwa Darasa la Tano na mdogo wake Joseph alikuwa Darasa la Pili,
Peter yeye alikuwa hajaanza shule.


Siku moja yapata saa mbili usiku Mzee Magesa akiwa amekaa kwenye
sebule karibu na chumba chake cha kulala alimwita Julieth kwa ajili ya
mazungumzo.
“Julieth!” Mzee Magesa aliita kwa nguvu.
“Abee baba!” Aliitikia Julieth aliyekuwa anaosha vyombo huku
akimwendea baba yake.
“Unafanya nini saa hizi?” Mzee Magesa aliuliza kwa sauti ya upole.
“Naosha vyombo baba.” Alijibu Julieth kwa adabu.
“Umemaliza?” Aliuliza tena Mzee Magesa.
“Hapana baba, bado sufuria mbili.” Alijibu Julieth.
“Acha utamalizia kesho kaa hapo nina maongezi na wewe.” Aliongea Mzee
Magesa huku akinyoosha kidole kwenye kiti cha miguu mitatu.
“Nimekuita ili kukwambia maneno machache kuhusu hali ya maisha yetu
hapa nyumbani.” Mzee Magesa alianza kueleza sababu ya wito huku
Julieth akimwangalia na kumsikiliza baba yake kwa makini.

“Kama unavyoona hali yetu ya maisha tunayoishi ni ngumu sana. Na hii
inatokana na kipato chetu kuwa kidogo. Namna pekee ya kujikwamua na
hali hii ni wewe mtoto wetu mkubwa kusoma kwa bidii ili uje utusaidie
sisi wazazi wako pamoja na wadogo zako. Na pia …” Mzee Magesa
alikatisha ghafla huku akiwa kama amekumbuka kitu fulani muhimu.

“Mama yako yuko wapi?” Aliuliza Mzee Magesa.
“Yupo chumbani.” Alijibu haraka Julieth.
“Mama Julieth!” Aliita Mzee Magesa.
“Abee!” Aliitikia mama Julieth kutokea chumbani huku akitoka.
“Mama Julieth nina maongezi kidogo na Julieth naomba na wewe
ushiriki.” Alitamka Mzee Magesa.
“Maongezi gani hayo?” Aliuliza mama Julieth.
“Wewe kaa usikilize ndio maana nimekuita”. Mzee Magesa alijibu kisha
akaendelea kuongea na Julieth huku mama yake akiwa amekaa pembeni
mwa Mzee Magesa.

“Julieth kama nilivyoanza kukwambia maisha yetu ni magumu sana
kutokana na kipato kidogo tunachopata. Tumejaribu kufanya bidii lakini
hakuna mabadiliko. Njia pekee ya kujikwamua kiuchumi katika siku zijazo
ni elimu. Hivyo wewe kama mtoto wetu mkubwa unatakiwa usome kwa
bidii sana ili uje utusaidie sisi na wadogo zako pia. Sisi wazazi wenu
tutakazana kuhangaika kutafuta fedha ili wewe usome. Angalia Mzee
Mtokambali alisomesha mtoto wake wa kwanza hadi Chuo Kikuu, leo hii
wadogo zake mmoja yupo Kidato cha Sita na mwingine Chuo Kikuu.
Maisha ya Mzee Mtokambali ni mazuri. Ninaimani hata sisi hili
linawezekana ilimradi tu kama wewe una nia ya kusoma.”

“Ni kweli angalia mke wake anavyobadilisha kanga na vitenge, ni kutokana
na kijana wao mwenye kazi nzuri. Baba Julieth, hili linawezekana mbona
binti yetu ana nia sana ya kusoma na uwezo anao.” Alidakia mama Julieth
bila hata kusubiri Mzee Magesa amalize.

“Baba na mama nimesikia sana mawazo yenu mazuri ninapenda sana
kusoma. Nitasoma!” Alisisitiza Julieth.
“Julieth wewe ndiye binti yetu wa kwanza, kumbuka wadogo zako bado
ni wadogo sana nakuomba mwanangu siku zote za maisha yako mtu
asikudanganye ukawachukia wadogo zako. Uwapende ndugu zako na
kuwaheshimu watu wote wanaokuzunguka wakubwa kwa wodogo, kwani
mwanangu kuna leo na kesho leo mimi na mama yako hatutakuwepo
mshikamano na upendo ndiyo silaya yenu. Hata ukisoma sana kama
hutawapenda na kuwaheshimu wadogo zako na watu wote itakuwa ni
bure.” Aliongeza Mzee Magesa.

Julieth aliinamisha kichwa chini kama vile anatafakari kitu halafu
akawaangalia baba na mama yake kwa uso wenye maswali.
“Baba mbona mnaongea hivi? Mimi nawapenda wadogo zangu na watu
wote, hata siku moja haitatokea nikawachukia wadogo zangu. Lakini
mbona leo mnaongea hivi?” Aliuliza Julieth kutaka kudadisi zaidi.

“Huu ni mwendelezo tu wa maongezi ambayo mara kwa mara mimi na
mama yako tumekuwa tukifanya. Ila leo tumeongea kwa msisitizo zaidi
kwani maisha ni magumu kupita siku zilizopita. Lakini pia kumbuka sasa
umekuwa mkubwa hivyo lazima tukwambie msimamo wetu juu ya maisha
yetu, yako na ya wadogo zako, au siyo mama Julieth!” Alifafanua Mzee
Magesa huku akimgeukia mama Julieth.

“Ni kweli wewe ndo mkubwa lazima uyajue haya kuanzia sasa ili
kukujengea uwezo wa kuishi vizuri na watu.” Aliongeza mama Julieth.
“Sawa wazazi wangu nimewaelewa.” Alisema Julieth.
“Baba Julieth naona tumalize maongezi kwani kesho asubuhi na mapema
unatakiwa uwahi sokoni kufungua biashara. Na wewe Julieth kesho ni
shule, hebu tukalale.” Alishauri mama Julieth.

“Haya Julieth nenda kapumzike ila ukae nayo kichwani yote
tuliyozungumza leo.” Alisisitiza Mzee Magesa huku akisimama kuelekea
chumbani.
“Sawa baba.” Alijibu Julieth.
Kesho yake asubuhi waliamka mapema sana. Julieth alijiandaa haraka na
kunywa uji na kuwahi shuleni. Mzee Magesa aliweka mboga zake kwenye
mkokoteni na kuelekea sokoni. Mama Julieth tayari alikwishaanza kupika
chapati kama kawaida yake.

“Mke wangu leo nitachelewa kurudi kwani nikifunga tu biashara itabidi
niende kuchukua vitunguu na nyanya. Ninaomba leo usiku unipikie ugali
na matembele.” Aliomba Mzee Magesa huku akiondoka na toroli lake
kuelekea sokoni.
“Haya baba kazi njema ila sio ndiyo uchelewe sana, halafu usisahau kuleta
matunda.” Aliongea mama Julieth huku akimsindikiza kwa macho.
***********
Mzee Magesa alipofika karibu na sokoni akiwa anavuka barabara, ghafla
lilitokea gari likiwa katika mwendo wa kasi ya ajabu na kumgonga. Mzee
Magesa aliumia sana sehemu za kichwani na sehemu mbalimbali na
kusababisha kutoka damu nyingi mdomoni, puani na masikioni.
Wasamalia wema walimkimbilia Mzee Magesa ili kumwahisha Hospitali
ya Mkoa lakini alikufa palepale hata kabla ya kuondoka.

Mashuhuda wa ajali walijaribu kuchukua namba za gari lakini haikuwa
rahisi kwani halikusimama. Walipiga simu polisi na askari walifika baada
ya muda wa kama dakika ishirini hivi. Baada ya kuwahoji walioshuhudia
ajali ile waliuchukua mwili wa Mzee Magesa na kuondoka.
Baada ya askari kuupeleka mwili wa marehemu Hospitali ya Mkoa askari
wawili walikwenda kutoa taarifa nyumbani kwake. Walipofika walimkuta
mama Julieth katika biashara yake ya chapati.

“Habari yako mama.” Askari mmoja alisalimia.
“Nzuri tu karibuni.” Alijibu mama Julieth na kuwakaribisha akidhani ni
wateja wake wa chapati.
“Asante mama sisi ni maofisa usalama tumekuja kukupa taarifa kwamba
mume wako amepata ajali.” Wale askari walizungumza moja kwa moja
kitu ambacho kilimpa mshtuko mama Julieth na kushindwa kuamini
alichoambiwa na kabla hawajaendelea mama Julieth aliwakatisha.
“Nini? Jamani mbona siwaelewi, mume wangu amepata ajali wapi? Na ya
nini? Je, hali yake inaendeleaje?” Aliongea mama Julieth maneno mengi
kama mtu aliyechanganyikiwa.

“Amegongwa na gari na kwa bahati mbaya gari halikusimama.” Askari
alifafanua.
“Mbona mnazunguka nimeuliza hali yake iko vipi?” Mama Julieth
aliendelea kuhoji zaidi huku ametoa macho mithili ya panya aliyebanwa
kwenye mtego wa chuma.
Wale askari wakatazamana kwa sekunde chache kisha mmoja wao
akatamka.
“Wewe ni mwanamke lakini tunakusihi ujikaze kiume.” Akamwangalia
usoni mama Julieth kisha akaendelea.

Mume wako yupo katika Hospitali ya Mkoa katika chumba cha …”
“Wagonjwa mahututi?” Mama Julieth alimalizia sentensi akiwa kama
aliyechanganyikiwa.
Askari kuona hali ya kuchanganyikiwa kwa mama Julieth akaamua
kumdanganya.
“Ndiyo mama yupo ICU. (Intensive Care Unit)” Alifafanua Askari.
“ICU? Ndo wapi huko mbona unanichanganya.” Alihoji mama Julieth.
Samahani mama ninamaanisha yupo chumba cha wagonjwa mahututi
anafanyiwa uchunguzi wa kina.

Kisha mama Julieth aliwaomba wale askari ajitayarishe ili aongozane nao.
Baada ya dakika kama tano hivi mama Julieth alikuwa tayari kuelekea
hospitali kumwona Mzee Magesa. Walipofika askari mmoja aliwaambia
wasubiri kidogo nje ili akamwombe daktari ruhusa ya kumwona mgonjwa.
Askari mmoja alibaki na mama Julieth katika chumba cha mapokezi huku
yule mwenzie akiingia katika chumba cha daktari ambaye ndiye aliyepokea
mwili wa Mzee Magesa na kuthibitisha kitaalamu kwamba kweli Mzee
Magesa alikuwa amekufa.

Daktari aliposikia kutoka kwa askari kwamba mke wa marehemu amekuja
alimwambia akamwite. Haraka askari alitoka nje na kuwakuta wakimsubiri
kwa hamu na kutoa ishara ya kumfuata. Wote walielekea ofisini kwa
daktari.
“Karibuni mkae kwenye viti”. Daktari alitamka kisha akaendelea huku
akimwangalia kwa makini yule mama. Kwa bahati mbaya alifikiri wale
askari walikwisha mwambia kuhusu kifo cha Mzee Magesa.
“Pole sana mama mwili wa mumeo upo katika chumba cha …..? Kabla
ya kumaliza kusema mama Julieth alianguka chini na kupoteza fahamu.
Haraka wale askari walimbeba Mama Julieth na kumwingiza katika
chumba maalumu ambako alipata huduma na kupata fahamu baada ya saa
3. 

Kisha daktari aliwaomba wale askari kumsindikiza mama Julieth
nyumbani kwake.
Majirani zake mama Julieth walikwisha kusanyika nyumbani huku mmoja
wao akienda shuleni kuwafuata watoto. Baada ya kufika mama Julieth vilio
na kelele za kila aina vilitawala huku mama Julieth akianguka chini na
kukosa nguvu kabisa. Mipango ya mazishi ilifanyika na kuamua kuzika
siku iliyofuata.

Siku ya mazishi watu walijaa sana huku simanzi na masikitiko vikitawala
katika eneo lote la Kaloleni kwani Mzee Magesa alikuwa maarufu sana.
Mwili wa Mzee Magesa ulizikwa kwa taratibu zote huku viongozi wa dini
na serikali kutoka Kaloleni wakihudhuria na kutoa nasaha zao. Huo ndio
ulikuwa mwisho wa maisha ya Mzee Magesa ‘Muuza mboga’ sokoni.

Wiki mbili baada ya mazishi Mama Julieth alikuwa bado hajapata nguvu
za kuanza kufanya chochote. Siku moja alikuwa amekaa katika ngazi
amejiinamia kama mtu ambaye amekata tam       aa ya maisha, akiendelea kulia
kwa uchungu. Julieth alitoka ndani akiwa ameshika kikombe cha chai na
kumpa mama yake huku akimfariji.
“Mama usilie, sisi tupo na wewe Mungu atatusaidia.” Julieth alimfariji
mama yake huku akimpa chai.

“Mwanangu baba yenu alikuwa nguzo ya familia na sasa hayupo tena.
Kumbuka mnatakiwa msome nani atawasomesha? Hivi ni kwa nini
Mungu amemchukua mapema hivi?” Alijibu mama Julieth huku
akibubujikwa na machozi.

“Mama tusikate tamaa hata baba kabla hajafariki alisema tuwe na
mshikamano na upendo katika familia yetu. Mama mimi nitakuwa nawe
bega kwa bega kukusaidia.” Julieth aliendelea kumfariji mama yake.
Mama Julieth alimwangalia Julieth kwa macho ya matumaini kisha
akamkumbatia mwanawe.

“Sawa mwanangu kwani yote haya ni mapenzi ya Mungu.” Alijibu mama
Julieth na kuanza kunywa chai.
Basi Julieth aliendelea na kazi za ndani na kumwacha mama yake akiwa
amepumzika.

*************
Baada ya mwaka mmoja kupita tangu Mzee Magesa afariki mama Julieth
aliugua ugonjwa wa moyo, kwa hiyo akashindwa kuendelea kufanya kazi
zake za kila siku na hata biashara ya sokoni aliyokuwa akiifanya baba
Julieth hakukuwa na mtu wa kuwasaidia kuiendeleza. Hali ya kipato ilizidi
kuwa ngumu kutokana na kuugua kwa mama Julieth kwani hata kazi ya
kupika chapati hakuweza kuendelea nayo tena.

Kutokana na hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu Julieth aliamua kuacha
shule akiwa Darasa la Sita ili kumsaidia mama yake kazi za pale nyumbani
na ikiwa ni pamoja na kuuza chapati.
Julieth alianza kuuza chapati biashara ambayo haikuwapa kipato kikubwa
kuweza kujikimu kutokana na wateja kuwa wachache. Kutokana na maisha
kuwa magumu walilazimika kula mlo mmoja kwa siku ili kukusanya kodi
ya vyumba viwili walivyokuwa wanaishi. Julieth aliendelea kuvumilia bila
kukata tamaa kwani mbali na kuwa ni binti mdogo lakini alikuwa na
majukumu makubwa ya kutunza familia.

Katika kuuza chapati Julieth alikutana na watu mbalimbali waliozipenda
sana chapati alizokuwa akipika. Siku moja asubuhi alikuja kaka mmoja
kununua chapati akatokea kumpenda sana Julieth.
“Habari yako mrembo!” Yule kijana alimsalimia Julieth huku akitabasabu.
“Nzuri kaka karibu.” Alijibu Julieth huku akimwangalia usoni.
“Mimi naitwa John sijui mwenzangu unaitwa nani?”Alijitambulisha yule
kijana.

Julieth alisita kidogo halafu akajibu;
“Naitwa Julieth karibu kaka chapati shilingi mia moja na hamsini nikupe
chapati ngapi?” Alijibu Julieth.
“Naomba chapati mbili.” Alitamka John huku akimpa noti ya shilingi elfu
kumi.
“Mmh jamani huna hela ndogo kaka au kuna kitu kingine unataka
kununua dukani nikakuchukulie, asubuhi hii chenchi zinasumbua kweli.”
Alisema Julieth kwa kulalamika.
“Usijali Julieth nipe hizo chapati na fedha inayobaki ni zawadi yako.”
Alijibu John.
“Mh we kaka, hela yote hii nibaki nayo kuna usalama kweli? Hapana kaka
ngoja nikutafutie tu chenchi.” Alisema Julieth huku akinyanyuka kwenda
dukani.
“Julieth usiogope mimi sina nia mbaya na wewe chukua tu hiyo hela
itakusaidia usijali.” Alitamka John huku akimzuia kuondoka.
Julieth aliamua kukaa chini na kumsikiliza John hatimaye wakafahamiana.
John alikuwa ni mkazi wa Mwanza na alikuwa ni mfanyabiashara wa
samaki. Julieth alimweleza hali halisi ya maisha yao. Baada ya kufahamiana
kwa siku kadhaa walianza kuwa marafiki na baadaye John alimtaka Julieth
awe mpenzi wake. Mwanzoni Julieth alikataa sana kuhusu urafiki wa
kimapenzi na John. Lakini baadaye alikubali wakawa marafiki. siku moja
Julieth akiwa amekaa nje ya nyumba yao John alipita pale na kufanya
maongezi na Julieth.
“Julieth tumekuwa marafiki kwa muda wa wiki tatu sasa naona nikwambie
ukweli. Kutoka siku ya kwanza nilipokuona nilitamani sana uwe mpenzi
wangu. Naomba unipe nafasi ndani ya moyo wako. Nakupenda Julieth
zaidi ya urafiki tulionao.” John alimwambia Julieth.
“Haiwezekani John! Mimi ni masikini sana unaiona familia yetu
inanitegemea sana mimi, halafu nianze tena mapenzi! Hapana! Tena sitaki!
Wewe tafuta tu mwanamke atakayekufaa anayeendana na wewe.” Alikataa
Julieth kwa msisitizo mkubwa.
“Sikiliza nikwambie Julieth, mimi na wewe tukiwa pamoja hata familia
yako itakuwa yangu pia, tutasaidiana sana katika maisha. Mama yako
atakuwa hana matatizo tena. Wewe nipe nafasi amini hutajuta maishani
kwa kunikubali mimi.” John aliendelea kubembeleza.
Julieth alinyamaza kimya kwa muda huku akichimba chini na kidole gumba
cha mguu wa kushoto.
“Huyu kaka tumefahamiana kwa muda mfupi sana lakini ni mtu mwenye
heshima na amekuwa karibu na mimi kwa wakati wote. Lakini zaidi ya
yote hata mimi pia nimempenda. Nikimkubali naamni hata mama
atampenda pia. Lakini je, mama atakubali niolewe katika umri huu?”
Aliwaza Julieth huku John akimwangalia kwa macho na uso wa
kumtamani.
“Nimekubali ombi lako.” Julieth hatimaye alikubali huku akiendelea
kuchimba chini na kuangalia pembeni akijaribu kuyakwepa macho ya
John.
“Nimefurahi sana Julieth nakupenda sana tutakwenda kuishi wote
Mwanza.” Aliongea John huku akimkumbatia, kumbusu na kumnyanyua
Julieth juu kama mtoto mdogo.
“Wewe! Mimi niende Mwanza nimwache mama na nani? Hapana kwanza
inabidi nikupeleke ukamwone mama umwambie lakini hilo la kwenda
Mwanza sahau.” Julieth Alimaka na Kuhamaki.
Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa wote na bila kupoteza muda wote
wawili walianza safari ya kwenda nyumbani kwa kina Julieth ili kuonana
na mama. Walipofika walimkuta mama Julieth akiwa amekaa sebuleni.
Julieth aliongoza kuingia ndani huku akifuatiwa na John. Julieth alimweleza
mama yake juu ya uhusiano wao na John.
Mama Julieth alichukia sana kusikia eti Julieth kapata rafiki wa kumwoa.
Kimsingi mama yake hakuwa tayari kumruhusu Julieth kuolewa katika
umri mdogo. Vilevile, mama yake Julieth alikuwa bado ana ndoto ya
kwamba Julieth atasoma hadi chuo kikuu.
“Julieth usijidanganye kabisa umri wako bado ni mdogo kuhimili
mikikimikiki ya ndoa. Lakini pia mimi bado napenda ukasome ili ndoto
yako ya kuwa daktari itimie.”Alitahadharisha mama Julieth juu ya urafiki
alionao na John.
“Hapana mama kama ni kusoma atasoma tu, na kuhusu kwamba Julieth
ana umri mdogo si tatizo kwani kuna wengine wanaolewa wakiwa na umri
chini ya umri wa Julieth, lakini wanahimili vishindo vya maisha ya ndoa.”
Alifafanua zaidi John.
“Na wewe mwenyewe muolewaji unasemaji mbona umenyamaza kimya?”
Aliuliza mama Julieth.
“Mimi mama nipo tayari kuolewa naye kwani kwa kipindi cha wiki tatu
tangu nimfahamu ameonyesha moyo wa kutusaidia.” Alijibu Julieth huku
akimwangalia John kwa macho ya kusisitiza.
“Sawa! Kwa sababu yeye ameridhia hata nikimkatalia ni kazi bure. Ila
nawaomba mfuate taratibu zote za kimila na kufunga ndoa rasmi ili mpate
baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa wazazi pia.” Alishauri mama
Julieth.
“Huo ni ushauri mzuri mama, lakini namwomba niende naye Mwanza
nikamtambulishe kwa wazazi wangu halafu atarudi ili tufanye taratibu hizo
kama ulivyoshauri.” Aliomba John.
“Kumbe kwenu ni Mwanza?” Aliuliza Mama Julieth.
“Ndiyo mama.” Alijibu John.
“Na je maisha yenu yatakuwa wapi?” Aliuliza mama Julieth.
“Baada ya taratibu zote za kufunga ndoa kukamilika tutakwenda kuisha
Mwanza.” Alijibu John.
“Sasa baba kama mtaishi mbali na mimi nani atanihudumia, maana Julieth
ndiyo alikuwa akinisaidia. Mimi mwenyewe hali yangu si nzuri sana
naumwa mara kwa mara na Julieth anajua.” Alihoji mama Julieth.
“Hapana mama usijali mimi na mwenzangu tumekwisha jipanga namna
ya kukusaidia. Kwanza nataka uondoke hapa uhamie kwenye nyumba
nzuri nitakayokupangishia. Pia nitakuachia pesa ili uweke msichana wa
kazi ambaye atakusaidia kazi mbalimbali. Kuhusu pesa isiwe tatizo kabisa
mambo yote yatakaa sawa.” John aliongea na kuahidi kwa kujiamini huku
akimwangalia Julieth ambaye alikuwa akitabasamu muda wote wa
maongezi.
“Sawa mimi nashukuru kama mmejipanga hivyo. Mungu akubariki sana
mimi sina kipingamizi tena alimradi mmependana na kufuata taratibu za
kufunga ndoa ili mpate baraka za Mungu. Pia ninaomba mkishaanza
maisha muwe mnakuja huku kutusalimia mara kwa mara.” Mama Julieth
alishauri huku akimkazia macho Julieth na baadaye John.
“Hilo halina tatizo kabisa mama hapa ni nyumbani tutakuja bila shaka
kwani nyumbani ni nyumbani, hata hivyo kwa sasa akishawaona wazazi
wangu tu atarudi ili kukamilisha mambo ya ndoa kama ulivyoshauri.”
Alijibu John.
 ITAENDELEA USIKOSE KUFUATILIA HADI MWISHO WAKE.
****************


Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom