Alhamisi, Januari 30, 2014

SIMULIZI FUPI "KULIPA MATANGA"


Siku hiyo Kasebo alionekana kukosa furaha, kutokana na kupungukiwa na pesa ya kulipa kodi ya nyumba aliyokuwa amepanga. Akiwa amejiinamia huku akiendelea kuwaza nini cha kufanya wazo lilimjia aende kumuomba msaada rafiki yake kipenzi anaitwa Roby. Haraka alinyanyuka na kuelekea nyumbani kwa Roby ambapo alikaribishwa vizuri na moja kwa moja alielezea shida yake. Roby alimsikiliza kwa umakini sana na alimuonea huruma hivyo aliamua kumsaidia kwa kumkopesha kiasi cha shilingi laki tano.

 Kasebo alifurahi sana huku akimshukuru rafiki yake na kuahidi kuwa atarudisha pesa hiyo baada ya wiki nne. Maisha yaliendelea, baada ya wiki nne kupita Kasebo hakumrudishia ile pesa Roby kama alivyomuahidi, ijapokuwa kwa kipindi hicho mambo yake yalikuwa mazuri kwani alionekana kutumia pesa nyingi katika starehe lakini Roby alipokuwa akimkumbusha kuhusu kulipa deni alikuwa akinyamaza kimya na kuendelea kutoa ahadi kuwa atamlipa, lakini siku zilizidi kwenda bila ya kulipa deni hatimaye miezi mitatu ilipita.Roby alikuwa ni kijana mpole sana, baada ya kuona Kasebo anamzungusha kumlipa deni lake aliamua kunyamaza kimya.


Katika maisha unaambiwa shida haishi mara moja siku zote unaweza kusaidiwa leo lakini zikapita siku  mbili tatu ukaomba msaada tena. Siku moja Kasebo alipata matatizo katika sehemu aliyokuwa anafanya kazi na hivyo alisimamishwa kazi kwa muda, kutokana na hali hiyo maisha yake yalikuwa magumu sana, ndipo siku moja aliamua kwenda kwa Roby kumuelezea matatizo yake. Kama kawaida Roby alimsikiliza na kumuonea huruma sana kutokana na hali aliyokuwa nayo, aliamua kumsaidia ijapokuwa alikuwa bado hajamlipa deni la kwanza lakini alimkopesha tena kiasi cha shilingi laki tatu.

 Kasebo alifurahi sana na kuahidi kuwa atamrudishia pesa zote baada ya miezi miwili. Siku zilienda hatimaye baada ya wiki tatu Kasebo alirudishwa kazini, na sasa aliwekwa katika kitengo kizuri ambapo alikuwa akilipwa pesa nyingi zaidi. Baada ya miezi miwili kupita Roby alienda nyumbani kwa Kasebo kumsalimia na kumkuta akiwa mwenye furaha sana lakini alipomkumbushia tu deni lake alibadilika na kuanza kulalamika "Yaani Roby shilingi laki nane ndiyo unanidai, kana kwamba umenikopesha milioni mia moja, nitakulipa hivyo vihela vyako usijali" Aliongea Kasebo huku akimuangalia Roby ambaye alibaki akimshangaa "Eti unasema vihela? Ama kweli binadamu tunajisahau, ulikuja mpole sana wakati ukiwa na shida sasa hivi umepata mafanikio unaonyesha dharau, sasa sikiliza mimi ninchotaka unilipe pesa zangu tena sasa hivi vinginevyo tutaonana wabaya".

 Roby alikasirika sana siku hiyo lakini Kasebo hakujali na hakumlipa pesa yoyote siku hiyo. Baada ya wiki moja kupita hatimaye Roby aliamua kumshtaki Kasebo ili aweze kulipwa deni lake, ijapokuwa walikuwa ni marafiki wa siku nyingi lakini Roby aliksirika kutokana na Kasebo kumtolea majibu ya kashfa. Baada ya Roby kumshtaki Kasebo hatimaye alilipwa pesa zake huku Kasebo akionekana kukasirika kana kwamba ameonewa lakini baadaye alikuja kugundua kuwa yeye ndiye mwenye makosa na kumuomba msamaha Roby na sasa wanaishi kwa furaha kama zamani. Kumbuka dawa ya deni ni kulipa na siyo unaenda kuopa huku mikono ikiwa nyuma lakini kulipa ina kuwa matanga.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom