Jumatano, Februari 19, 2014

SIMULIZI FUPI "MAMA MWENYE NYUMBA"

Baada ya kumaliza chuo James alifanikiwa kupata kazi jijini Dar es salaam, Kwa kipindi chote kabla ya kupata kazi James alikuwa akiishi nje ya mji wa Dar es salaam huko Bagamoyo, baada ya kupata kazi aliamua kutafuta nyumba ya kupanga ili aweze kuishi karibu na maeneo ya ofisi aliyokuwa anafanyia kazi, ambapo ilikuwa ni maeneo ya Sinza madukani. alifanikiwa kupata nyumba nzuri, na kupangisha chumba na sebule, katika ile nyumba mwenye nyumba alikuwa ni Mama mmoja wa makamo ambaye alikuwa akiishi peke yake Mama huyu alikuwa na watoto wa kike wawili wote walikuwa wameolewa hivyo walikuwa wakiishi katika makazi yao.

Ilikuwa ni nyumba kubwa, ambapo palikuwa na wapangaji wengine watatu, na James alikuwa ni mpangaji wa nne.Mama mwenye nyumba alimpokea kwa ukarimu sana James.Baada ya siku mbili tatu alihamia katika ile nyumba.Maisha ya James katika ile nyumba alikuwa akiondoka saa kumi na mbili asubuhi na kurudi saa moja jioni, kutokana na uchovu wa kazi nyingi mara nyingi James alikuwa akipendelea kula  chipsi, kwani alishindwa kupika mara kwa mara ijapokuwa James alipenda sana kujipikia,Baada ya mwezi mmoja kupita Mama mwenye nyumba alianza kuonyesha ukaribu na James kwani alianza kuwa anapika chakula na kumuachia James. Kutokana na uchovu wa kazi James alifurahi sana na siku zote alikuwa akimuheshimu sana Mama huyu.


 Maisha yaliendelea huku James akionekana kumzoea zaidi Mama mwenye nyumba,mara nyingi walikuwa wakikaa na kuzungumza pamoja, Ilifikia kipindi Mama mwenye nyumba alianza  kuchukua  nguo za James na kufua kila siku ya jumamosi, ijapokuwa mwanzoni James alionekana kukataa lakini baadaye alikubali kutokana na Mama mwenye nyumba kuonekana kumsisitiza kuwa asiwe na shaka kwani yeye huwa anamuonea huruma akirudi kutoka kazini anakuwa amechoka sana.

Siku zilivyozidi kwenda Mama mwenye nyumba alionyesha kumpenda zaidi James, siku moja akiwa amepumzika chumbani kwake huku moyoni akifikiria "Huyu James, ni kijana mcheshi sana, yaani nampenda sana, lakini nashindwa nitawezaje kumueleza hisia nilizonazo moyoni mwangu, namuhitaji awe wangu peke yangu" Mama mwenye nyuma alikuwa akiwaza moyoni mwake. Baada ya siku mbili tatu kupita siku hiyo ilikuwa ni siku ya Jumamosi ambapo James alirudi nyumbani akiwa ameongozana na dada mmoja ambaye anaitwa Tunu, alipofika nyumbani alimkuta Mama mwenye nyumba anamsubiri, Mama huyu alipomuona James ameongozana na msichana mrembo alishtuka  huku akionekana kushangaa kana kwamba mtu aliyepigwa na butwaa.

 James alisogea karibu na kumsalimia kisha alianza kumtambulisha yule dada. "Tunu huyu ni Mama mwenye nyumba yangu, yule ambaye nilikuambia kuwa naishi naye vizuri sana yaani ni kama Mama yangu mzazi" Mama mwenye nyumba alikuwa anamtazama James huku akionyesha tabasamu la kinafki. 

James aliendelea kuongea "Mama, huyu ni mkwe wako anaitwa Tunu,alikuwa anahamu sana ya kukuona nadhani leo imekuwa vizuri mmefahamiana, nampenda sana huyu mrembo Mama nataka kuoa kabisa nimuweke ndani ili usipate shida ya kunipikia tena" Huku akiwa anatabasamu na kuweka utani kidogo James alikuwa amemshika mkono Tunu. Mama mwenye nyumba aliguna kidogo na kusema "Karibu sana Tunu" Bila kuongeza neno lolote aliingia chumbani kwake kupumzika na kumuacha James akiwa na Tunu.

Siku hiyo ilikuwa ni siku mbaya sana kwa Mama mwenye nyumba kwani alionekana kukerwa sana na kitendo cha James kumtambulisha mchumba wake, "Yaani huyu James anajifanya mjanja sana, anakuja na hicho kikahaba chake, kunionyesha mimi ili iweje, na sasa ngoja atanijua mimi ni nani."Alikuwa akiwaza Mama mwenye nyumba huku James akiwa hana hili wala lile.Baada ya wiki moja kupita Mama mwenye nyumba aliamua kumueleza ukweli James kuwa anamuhitaji kimapenzi, hali ambayo ilimshangaza sana James kwani alikuwa akimuheshimu Mama huyu kama Mama yake mzazi.Moja kwa moja James alimkatalia Mama mwenye nyumba ombi lake, kitendo ambacho kilimfanya Mama mwenye nyumba amchukie sana na wakati huu alianza kumfanyia visa ili James aondoke katika nyumba yake.

 James alikuwa katika wakati mgumu sana ndipo alipoamua kufanya utaratibu wa kuhama katika nyumba ile. Alifanikiwa kupata nyumba maeneo ya jirani. Baada ya kuhamia pale ndipo alipopata taarifa za yule Mama mwenye nyumba ya kwanza aliyokuwa anaishi kuwa Mume wake alifariki na ugonjwa wa Ukimwi na yule Mama ni tabia yake, kutaka kuwa kimapenzi na vijana wadogo na pia huwaambukiza virusi vya Ukimwi kwa makusudi. James alihuzunika sana baada ya kupata taarifa hizo "Nashukuru sana Mungu niliweza kumkataa Mama mwenye nyumba ama kweli duniani kuna watu wabaya inabidi kuwa makini kwani huwezi kumjua mtu mwema kwa kumuangalia."

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom