Baada ya kumaliza chuo, Debora aliolewa ikiwa ni muda mfupi tu baada ya sherehe yake ya kumaliza stashahada ya uhasibu. Mume wake alikuwa ni mfanyakazi katika taasisi moja kubwa ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya watoto. Debora alikuwa ni Mama wa nyumbani kwa wakati huo kwani alikuwa hana kazi, kwa muda wote mume wake alikuwa akimpatia kila kitu alichokuwa anakihitaji, Lakini kwa upande wa Debora alitamani siku moja na yeye angefanikiwa kupata kazi na alikuwa akimueleza mume wake, kwani aliamini kuwa mume wake alikuwa akifahamiana na watu wengi ambao wangeweza kumsaidia katika kumuunganisha ili afanikiwe kupata kazi.Mume wake na Debora alikuwa hataki Debora afanye kazi, kitu ambacho kilikuwa kikimuumiza sana Debora.
Baada ya mwaka mmoja kupita walifanikiwa kupata watoto mapacha, hivyo Debora alikuwa katika majukukumu ya kulea watoto huku akiwa na wasaidizi wa kazi za pale nyumbani ambao walikuwa ni akina dada wawili.Maisha yaliendelea huku Debora akijipa matumaini kuwa watoto wakishakuwa na kufikia umri wa miezi sita ataendelea kutafuta kazi, na sasa alifikiria kuwa na kazi kuliko ilivyokuwa mwanzo kwani aliwaza kama angefanikiwa kupata kazi, wangesaidiana na mume wake katika majukumu mbalimbali ya pale nyumbani ikiwa ni pamoja na kuwaandalia watototo wao maisha bora.
Baada ya miezi sita kupita Debora aliandaa vyeti vyake pamoja na barua huku akizituma katika makampuni mbalimbali kutafuta kazi, wakati akiwa anafanya hivyo hakumshirikisha mume wake,lakini baadaye mume wake aligundua ndipo alipoamua kumweleza juu ya msimamo wake kuwa hataki afanye kazi "Nilishakuambia mke wangu, unapendeza sana ukiwa unakaa nyumbani na kuwalea watoto wetu, mimi nahangaika huku na kule ili tuwe na maisha mazuri, sasa wewe unahangaika kutafuta kazi ili iweje, kwani kuna kitu gani unakikosa, kama ni pesa nakupa,na kama haitoshi kadi yangu ya benki nimekupa ili utakapokuwa na shida utoe kiasi chochcote cha pesa unayotaka, sasa nashangaa kinachokusumbua ni kitu gani, unatakiwa utulie mke wangu mimi nipo kwaajili yako" Alikuwa akiongea huku akimtizama Debora ambaye alinyamaza kimya bila kujibu chochote. Kwani sikuzote amekuwa akimueleza mume wake umuhimu wa yeye kufanya kazi lakini anamkatalia.
Baada ya muda kupita Debora aliamua kumweleza Mama yake mzazi kuhusu tatizo lake la kazi, ndipo Mama yake alipoamua kumshauri afanye biashara yotote huku akiwekeza kidogo kwa kutumia pesa za mume wake anazompa. Debora alikaa na kutafakari na baadaye aliamua kuanza kufanya biashara kwa siri alifungua duka la vipodozi, na kumuweka mtu aliyekuwa akisimamia.Bila ya mume wake kujua na kutokana na pesa nyingi alizokuwa akipewa na mume wake pamoja na kadi ya benki aliyokuwa nayo aliamua kuchukua kiasi kidogo cha pesa na kuwekeza katika kununua viwanja.
Mume wake alikuwa ni mtu mwenye pesa nyingi sana kiasi kwamba alikuwa haulizi ni kiasi gani mke wake anatumia katika matumizi yake, na huwa anafanyia kazi gani. Maisha yaliendelea huku Debora akiendelea kufanya biashara na baadaye aliamua kuanza kujenga nyumba huku mume wake akiwa hana hili wala lile. wakati mwingine Debora alitamani kumueleza ukweli mume wake lakini alikuwa akihofu kuwa angekasirika na kumkataza kuendelea na biashara yake, ya maduka ya vipodozi.
Baada ya mwaka mmoja kupita katika ofisi aliyokuwa anafanya kazi mume wake na Debora, kulitokea matatizo ya kuibiwa kwa kiasi kikubwa cha pesa, ambapo ilipelekea baadhi ya wafanyakazi kusimamishwa kazi huku wakitakiwa kulipa kiasi cha shilingi bilioni moja iliyokuwa imepotea. Maisha yalikuwa magumu kwa upande wa mume wa Debora aliuza mali zake kama magari na nyumba mbili ili kuweza kulipa deni, hivyo walibakiwa na nyumba moja tu waliyokuwa wakiishi, Hali ilizidi kuwa ngumu kwani sasa Mume wa Debora alikuwa hana kazi na bado alikuwa na madeni ambayo anadaiwa, na rafiki yake ambaye alimkopesha kiasi cha shilingi milioni ishirini na tano.
Huku akiwa na matumaini ya kupata kazi, Mume wa Debora alionekana kuwa mwenye mawazo sana wakati wote, kwani alikuwa hajui nini hatima ya maisha yake. Ndipo siku hiyo mke wake aliamua kumkalisha na kumueleza ukweli kuhusu biashara alizokuwa anafanya, na jinsi alivyokuwa amewekeza kutokana na fedha alizokuwa akimpatia huku akifanya kwa siri kwasababu mume wake alikuwa hataki afanye kazi, Mume wake alibaki ameduwaa huku akisikitika na kusema "Nisamehe mke wangu, sikuwahi kufikiria kama ningekuja kuwa na maisha magumu, nilijua siku zote ningeweza kuhudumia familia yangu kwa hali na mali, Mke wangu wewe una akili sana Mungu akubariki." Walikumbatiana kwa furaha na sasa waliendelea kushirikiana katika kufanya biashara pamoja, na lile deni alilokuwa anadaiwa alilipa lote, na maisha yao yaliendelea kuwa na furaha na amani. Siku zote Debora alikuwa akisema NI LAZIMA NIFANYE KAZI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni