Pages

Jumatano, Aprili 30, 2014

SIMULIZI FUPI "NAJUTA KUMPENDA JOANITA"


Ben alikuwa anampenda sana Joanita siku zote alikuwa tayari kumsaidia katika kila jambo, Kijana huyu alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa ambaye alikuwa akijiweza katika mambo mbalimbali yaani pesa kwake ilikuwa siyo tatizo. Joanita alikuwa ni mwanafunzi wa chuo cha uhasibu na kwa wakati huo alikuwa akimalizia mwaka wa mwisho wa masomo yake. Baada ya kumaliza chuo Joanita alitamani kwenda kusoma nchini Marekani, ambapo alifikiria kumuomba mpenzi wake amsaidie kwani wazazi wa Joanita walikuwa hawana uwezo na hata chuo miaka miwili ya mwisho Ben ndiye aliyekuwa akimlipia ada. Baada ya kumueleza Ben nia yake ya kutaka kwenda kusoma Marekani, mwanzoni Ben alikuwa akisita na kumtaka aendelee kusoma hapahapa Tanzania.

 Lakini Joanita aliendelea kumbembeleza hadi Ben alikubali kwani alitakiwa kwenda kusoma kwa mwaka mmoja na baada ya hapo arudi nchini Tanzania.Taratibu za safari zilianza na Ben alijipanga kumuandalia kila kitu kipenzi chake Joanita, alifanya mipango yote hadi sehemu ambayo Joanita angefikia huko Marekani alikuwa na ndugu yake ambaye alimjulisha kuhusu safari ya Joanita. Siku zote Ben alimsihi Joanita akasome kwa bidii, na asisahau kuwa anampenda sana katika maisha yake na pindi tu atakapomaliza wangefunga pingu za maisha. 

Hatimaye siku ya safari ilifika na sasa Joanita aliondoka na kumuacha Ben akiwa mpweke, Kwa upande wa wazazi wa Joanita walimshukuru sana Ben, kwa kumjali mtoto wao. Baada ya wiki moja Ben alikuwa akiwasiliana na Joanita kila siku huku akimtaka asome kwa bidii, Maisha yaliendelea ikapita kama miezi saba tokea Joanita aondoke taratibu mawasiliano yakaanza kupungua na hata namba aliyokuwa akiwasiliana na Joanita ilikuwa haipatikani.

Ben alipata hofu nakuhisi labda Joanita atakuwa amepatwa na matatizo  kwani siku zilienda na hatimaye mwaka uliisha ambao Joanita ndiyo alikuwa amemaliza masomo yake , lakini kwa kipindi cha miezi mitatu kulikuwa hakuna mawasiliano kati ya Joanita na Ben, Baadaye Ben aliamua kumpigia simu yule ndugu yake wa Marekani aende katika chuo alichokuwa anasoma Joanita kumuangalia labda atakuwa na matatizo, Yule ndugu yake alienda moja kwa moja hadi kule chuoni ambapo palikuwa na umbali kama kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine takribani masaa kama saba, kwa usafiri wa basi.

 Alipofika pale chuoni alimuulizia, na ndipo alipokutana na baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wakimfahamu, mmoja kati ya wale wanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Eli akasema "Joanita si ameenda Tanzania kumtambulisha mume wake, kwani walifunga ndoa na kaka mmoja wa kizungu, lakini baadaye Joanita alisema atampeleka mume wake Tanzania halafu atarudi kuendelea kuishi Marekani" Kaka yule aliyetumwa kwenda kumuulizia alibaki ameduwaa asiamini maneno aliyokuwa anaambiwa ilibidi aulize mara mbimbili "Ati Joanita kaolewa? Na mzungu? Halafu wameenda Tanzania? Lini? mmmh haiwezekani".

Eli alimtizama na kuchukua simu yake kisha akaanza kumuonyesha picha mbalimbali ambazo zilimuonyesha Joanita akiwa na mzungu katika siku yake ya ndoa. Kaka yule alimuomba yule dada amtumie zile picha katika simu yake ya mkononi, na baada ya hapo aliondoka huku akiwaza ni namna gani anaweza kumjulisha Ben kile alichokutana nacho. Baadaye alifikiria na kuamua kumueleza ukweli Ben kuwa Joanita ameolewa na mzungu Ben hakumuamini ndipo alipoamua kumtumia picha za Joanita akiwa anafunga ndoa. 

Masikini Ben alikuwa kama amechanganyikiwa moja kwa moja aliamua kwenda nyUmbani kwa kina Joanita. Alipofika aliwakuta wazazi wa Joanita ambao walimweleza kuwa Joanita alikuwa ameondoka siku hiyo asubuhi Ben alikuwa akilia kama mtoto mdogo huku akiwalaumu wazazi wa Joanita ambao walimfahamisha kuwa walikuwa hawajui chochote kinachoendelea kwani mtoto wao amewashangaza pia kwa uamuzi aliouchukua. Baada ya muda kidogo Baba yake Joanita alinyanyuka na kuingia chumbani ambapo alirudi na kumletea barua aliyoiandika Joanita kwa Ben.

 "Asante sana kwa kila jambo uliloweza kunisaidia katika maisha yangu, najua ulinipenda sana, nashindwa namna ya kujielezea lakini naomba unisamehe Ben, Moyo wangu umeamua kuwa na mwanaume mwingine ambaye naamini nampenda sana, nakutakia maisha mema naamini utampata mwanamke atakayekupenda maisha yako yote. Naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea. Kila la heri katika maisha yako Ni mimi Joanita."

Baada ya Ben kumaliza kuisoma ile barua aliichana na kuondoka bila ya kuaga. Huku akiwa kama amechanganyikiwa alizungumza mwenyewe"Najuta kumpenda Jonita, ameniumiza sana moyo wangu, siamini kama amesahau yale yote niliyomtendea roho inaniuma sana". Katika maisha kuna atakaye kupenda kutoka moyoni ambaye hawezi kukuacha kwa wakati wowote ule lakini pia yupo yule atakayekuonyesha mapenzi ya usoni, huku moyoni akiwa anajua anachokitaka kutoka kwako ni mali tu na si vinginevyo kuwa makini.. 

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom