Jumatatu, Aprili 28, 2014

SIMULIZI FUPI "WIFI NIMEKUCHOKA"

NA.Adela D. Kavishe
Katika maisha unaambiwa mvumilivu hula mbivu, kwani siku zote hakuna safari ya maisha isiyokukuwa na changamoto,Monalisa aliolewa na Jerome na kufanikiwa kupata watoto wawili walikuwa wakiishi katika nyumba ya kupanga na kutokana na hali ya maisha walikuwa wamepanga vyumba viwili, Watoto walikuwa wakilala sebuleni.Wakiwa wanaendelea kuishi huku wakihangaika kutafuta pesa ya kujikimu katika maisha, Siku moja wakiwa nyumbani majira ya saa moja jioni walisikia mlango ukibishwa hodi.

 Monalisa alinyanyuka na kufungua mlango kumbe alikuwa amekuja wifi yake ambaye alikuwa ambeba begi lake kubwa na mfuko wa Rambo, Alimkaribisha ndani na kumsaidia kubeba begi. Wifi huyu alikuwa ametokea Kijijini  Morogoro na alifika kwa kaka yake ili aweze kutafutiwa shule, Basi alikaribishwa  vizuri bila matatizo yoyote, Kutokana na nyumba kuwa ndogo ilimbidi ajumuike kulala pamoja na watoto pale sebuleni ambapo walikuwa wakitandika godoro na kulala pamoja. Maisha yaliendelea, huku wifi akiwa anaishi pale nyumbani, siku zote alikuwa akiamka asubuhi lakini asimsaidie Monalisa kufanya kazi yoyote.


Hivyo Monalisa alikuwa akimka mapema nakuandaa kifungua kinywa na wakati mwingine ilimbidi apike chakula asubuhi kwaajili ya kuwaachia watoto halafu ndiyo aondoke kwenda kwenye biashara yake ya kuuza samaki.Maisha yaliendelea hivyo hivyo ndipo sikumoja Monalisa aliamua kumueleza mume wake tabia za mdogo wake kukaa bila ya kufanya kazi yoyote na ukizingatia alikuwa ni msichana mkubwa, Jerome alijaribu kumwelekeza mdogo wake bila mafanikio kwani sasa ndiyo alileta mtafaruku zaidi kati ya Monalisa na wifi yake, sasa Wifi alianza kununa bila sababu na kumchukia sana wifi yake. 

Hali ile ilikuwa inamuumiza sana Monalisa ambaye alikuwa akihangaika siku zote ili nyumbani watoto waweze kupata chakula, na Mume wake alikuwa ni fundi seremala, na hata alipokuwa akipata pesa mara zote alikuwa akimpa mdogo wake kwahiyo ilimbidi Monalisa, ajibane sana katika kutafuta pesa kwaajili ya matumizi ya pale nyumbani. Baada ya miezi sita kupita wifi yake Monalisa vituko ndiyo vilizidi sasa alianza kuleta wanaume pale nyumbani. Siku zote alikuwa akisubiri watoto wakiwa wameenda shule, na Baba na Mama wakiwa wameenda kazini, na kutumia muda huo kuingiza wanaume, na huku akitumia kitanda cha kaka yake bila ya kujali chochote, tabia hiyo iliendelea hadi siku ambayo Monalisa aligundua kuwa shuka lilikuwa limechafuka na kumuuliza wifi yake ambaye alikasirika sana.

 Huku akiwasingizia watoto walikuwa wakicheza kitandani, lakini watoto walikanusha huku wakilia kuwa wamesingiziwa. Baadaye Monalisa alipuuzia lakini wifi yake hakuacha hiyo tabia, ndipo siku moja jirani aliamua kumueleza Monalisa kile kinachoendelea akiwa hayupo.Monalisa alisikitika sana na sasa aliwaza namna ya kumfumania wifi yake. 

Siku hiyo alikwenda kazini kama kawaida lakini hakukaa muda mrefu akawa anawasiliana na yule jirani ambaye alimwambia kuwa muda huo kuna mwanaume amefika pale nyumbani. Moja kwa moja Monalisa aliondoka kijiweni na kurudi nyumbani ambapo alimkuta wifi yake akiwa amejipumzisha kitandani kwake na mwanaume huku wakifanya starehe zao, Alishtuka sana na kuanza kumfokea huku akimtaka aondoke."Wifi nimekuchoka, naomba uondoke, aibu gani hii jamani, unawafundisha nini watoto wangu naomba uondoke sitaki kukuona kabisa"

 Wifi kwa hofu alianza kulia na kuomba msamaha kwa Monalisa asimueleze kaka yake.Lakini Monalisa alimuambia haiwezekani amekwisha mvumilia vya kutosha lazima aondoke, Baadaye Jerome aliporudi kutoka kazini Monalisa alimweleza kila kitu ndipo kaka mtu alipoamua kumrudisha mdogo wake kijijini kwa kuchoshwa na tabia za mdogo wake.Wifi aliomba msamaha, na Monalisa alimsamehe lakini alimwambia ni vyema angerudi nyumbani Morogoro.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom