Mmoja kati ya wale kidada aliyekuwa anaitwa Subira alisimama nakusema "Lakini jamani pamoja na yote twendeni tukamsaidie mwenzetu" Wote walimcheka na kunyanyuka huku wakiondoka na kumuacha Subira akielekea katika kile chumba alichokuwa akisikia sauti ya Mwanadodo Aligonga mlango bila ya mafanikio, akiwa ameendelea kusimama pale mlango ulifunguliwa na mume wake Mwanadodo alitoka bila ya kuzungumza chochote na kubamiza mlango kisha kuondoka na kumuacha Subira akiwa ameduwaa.
Akiwa chumbani Mwanadodo alikuwa akiendelea kulia kwa uchungu kutokana
na maumivu aliyokuwa akiyasikia, Subira alifungua mlango na kuingia ndani “Pole
sana Mwanadodo, yaani huyu mume wako hana hata huruma jamani, kwani umefanya
kosa gani?” Aliuliza Subira huku akimtizama Mwanadodo ambaye kwa sauti ya
unyonge akasema “Sijamkosea chochote, amekuja na kuanza kunilaumu kuwa mimi
nina mdharau, kwasababu akirudi nyumbani usiku nachelewa kumfungulia mlango,
sasa nilipomuhoji kwanini anarudi usiku, muda ambao unakuta mimi na watoto
tumekwishalala fofofo, alikasirika na kuanza kunipiga yaani nateseka sana
rafiki yangu”. Subira alisikitika sana huku akimsihi kama ataendelea na tabia
hiyo ni vyema akawashirikisha na wazazi.
Maisha yaliendelea huku Mwanadodo akiwa anavumilia matatizo yote
anayoyapata kutoka kwa mume wake anayeitwa Bundala , akiamini ipo siku
atabadilika na kuacha tabia ya kumpiga.Siku moja akiwa nyumbani baada ya
kumaliza kupika chakula cha usiku alikuwa ameketi mezani na kumuita mume wake
ili wajumuike na kula chakula pamoja. Alipofika mezani alifunua bakuli la mboga
na kupakua huku Mwanadodo akiwa anamtizama. Akiwa anaaanza kula ghafla
alisimama na kuanza kusema “Wewe mwanamke umeniwekea nini kwenye hiki chakula?”
Mwanadodo alibaki akishangaa na kusema hee! Kwani kuna nini? Mbona umekuwa
mkali hivyo mume wangu?”
Bundala alisimama akiwa ameshikilia bakuli la mboga “Wewe mwanamke ni mchawi yaani unataka kuniloga
mimi? Sasa leo nitakuonyesha”
Alizungumza Bundala na kisha alichukua lile bakuli lilokuwa na mboga na kumwagia
mke wake kwa bahati ilimwagikia kwenye nguo, hakuishia hapo aliendelea kumpiga
huku akisema “Leo nitakuua mchawi mkumbwa wewe” Mwanadodo alikuwa akilia kwa
uchungu alijaribu kujitoa mikononi mwa Bundala na haraka alifungua mlango na
kukimbilia kwa jirani ambapo aliwakuta akina dada wawili waliokuwa wakimfahamu
mmoja wao akamuuliza “Haya tena kulikoni, mbona mbio mbio kama mtu
aliyechanganyikiwa” Mwanadodo huku akiwa ameweka mikono yake kichwani akasema
“Naombeni mnisaidie mume wangu ananiua jamani, ananipiga bila sababu”.
Wale
wanawake walicheka na kugonganisha mikono yao “Hee, ni maajabu mtu kukupiga
bila sababu, na wewe hata ukipigwa ni sawa kabisa, mara ngapi watu wanakushauri
uachane na huyo bwana lakini wewe bado upo naye, halafu unataka tukuasaidie
embu kwenda zako huko. Aliongea Yule mwanamke huku akimtizama Mwanadodo kwa
dharau, Bundala alitoka nje na kumkuta akiwa amesimama maeneo yale aliendelea
kumtukana “Wewe mchawi, njoo hapa yaani unataka kuniloga mimi, leo
nitakumaliza” Wale kinadada wakawa wanasemeshana “Makubwa haya, inawezekana
kweli huyu mwanamke ni mchawi” Mwanadodo alikuwa anatetemeka kwa hofu lakini
wale kina dada walimuacha na kuondoka Bundala alimvuta hadi chumbani huku
akiendelea kumpiga”
Maisha ya Mwanadodo yalikuwa ni magumu sana pale mtaani, kwani wale
kinadada walianza kumtangaza kuwa ni mchawi ndiyo maana mume wake anampiga kila
siku, hali hiyo ilimpelekea Mwanadodo kuanza kutengwa na baadhi ya watu alikuwa
akijisikia vibaya sana, kwani mume wake alikuwa akimfanyia ukatili huku akiwa hana msaada wowote.Pale mtaani
Mwanadodo alikuwa na rafiki mmoja tu ambaye ni Subira na alikuwa akimsikiliza
na kumuone huruma sana. Sikumoja Subira aliamua kuwaalika wanawake wa pale
mtaani nyumbani kwakwe kwaajili ya chakula cha mchana, walifika wanawawake
wengi sana, na Mwanadodo naye alifika huku taratibu akiwa anaelekea kuketi,
mmoja kati ya wale wanawake alisimama na kusema “Hee! Na huyu mchawi amealikwa?
Sasa si tunalogana tu hapa, mimi naondoka zangu”.
Mwanadodo alikuwa amejiinamia kimya
huku machozi yakiwa yanamlenga lenga, Subira alisimama na kumfuata huku
akimshika mkono na kusema “Jamani wanawake wenzangu, acheni kumtenga mwanamke
mwenzetu, huyu ni rafiki yetu, hivi hata mmoja wenu alishawahi kufikiria mateso
anayoyapata Mwanadodo, kama ingelikuwa ni wewe ungefanyaje, huyu mwanamke
anahitaji msaada wetu, mume wake anamfanyia ukatili kila siku anampiga na sasa
amemtangaza kuwa ni mchawi ili watu wamchukie, lakini chakushangaza hata nyinyi
wanawake ambao mngeweza kumsaidia kupambana na huu ukatili mnamdharau na
kumcheka na zaidi ya yote mnamtenga.Kumbukeni hakuna anayefurahi kuishi maisha
ya namna hii, wanawake tupendane na tuungane kumsaidia mwenzetu” Wanawake wote
walikuwa makini sana huku wakimsikiliza Subira, kila mmoja alianza kuingiwa na
moyo wa imani na kwa pamoja walimuomba msamaha Mwanadodo na sasa alijumuika nao
pamoja.
Kesho yake kama kawadia mume wake
alirudi nyumbani na kuanza kumtukana na kumpiga mke wake huku akimuita mchawi,
wale majirani wanawake siku hiyo walijikusanya pamoja na kwenda hadi nyumbani
kwa Mwanadodo kumsaidia, Walimsukuma Bundala na kumchukua Mwanadodo. Mama Mmoja kwa ujasiri mkubwa akasema “Wewe
Bundala, kwanini unamtesa mke wako kiasi hiki? Wewe ni binadamu gani ambaye
hauna huruma, sasa sikiliza wanawake wote tumeungana kupambana na ukatili huu
wa kijinsia tutakupeleka polisi, jichunge sana, ukirudia tabia yako lazima
tukupeleke katika mkono wa sheria” Siku hiyo ilikuwa ni patashika nguo
kuchanika.
Bundala alibaki ameduwaa kuona umoja ule wa wanawake, Alikuwa mpole
sana, na sasa alimtizama mkewe na wale wanawake walimwambia aombe msamaha, na
kama ilivyo kawaida umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, Bundala aliomba msamaha na kuahidi hatorudia
kosa lile. Baada ya hapo Mwanadodo alirudi nyumbani huku akiendelea kuishi
vizuri na mume wake. Bundala alibadilika na sasa alimuheshimu na kumsikiliza
mkewe. Subira alikwenda kumjulia hali Mwanadodo walizungumza sana na kufurahi
pamoja huku Subira akisema Ama kweli “Rafiki wa mwanamke ni mwanamke,
tukiungana pamoja tunaweza kuteteana katika kila jambo siku zote wanawake
tupendane.
.********************MWISHO*************
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni