Jumatatu, Mei 19, 2014

SIMULIZI FUPI MDHARAU MWIBA..............

Siku hiyo Joanita alipigiwa simu na rafiki yake wa kiume ambaye alimwelekeza kuwa amfuate maeneo ya Kimara ili waweze kuonana, ilikuwa ni majira ya saa moja jioni ambapo Joanita alipanda daladala hadi kufika eneo hilo ambapo alichukua simu yake na kumpigia simu mwenza wake  ili amwelekeze alipo, maeneo yale kulikuwa na kona nyingi za kupita hivyo Joanita alikuwa hajui aanzia wapi kwani siku hiyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika maeneo yale, pembeni kulikuwa na vijana wamekaa maskani huku wakizungumza na kumtizama Joanita aliyeonekana kuwa bize na simu yake na hata alipofika karibu na wale vijana aliwapita bila ya kuwasalimia.

 Aliendelea kutembea na kisha aliamua kupiga simu tena ili aelekezwe vizuri, ndipo mchumba wake huyo alipomuambia ni vyema angewauliza watu hapo jirani ili wamwelekeze hadi kwenye bar hiyo iliyokuwa inaitwa Kituka Bar, ndipo Joanita alirudi nyuma na kwenda kuwasalimia wale vijana aliowapipa mara ya kwanza, aliwasalimia na kisha aliwaomba wamwelekeze kwenye ile bar, Wale vijana walionekana kukasirika na mmoja wao akasema "Yaani wewe umetupita hapa, haujatusalimia, halafu umefika huko mbele ukaona unahitaji msaada ndiyo unakuja kutusalimia? Kwenda zako nenda kawaulize watu wengine, mwanamke gani una dharau, kwenda zako toka hapa".


 Joanita alibaki akiwa amejiinamia kwa aibu, waliendelea kumbwatukia lakini mmoja wao alisimama na kusema "Mwacheni bwana ngoja mimi nimuelekeze, sasa dada inabidi uwe makini kwasababu mida hii ukipita njia nyingine unaweza kukabwa pita njia ile pale mkono wa kulia moja kwa moja utafika kwenye hiyo bar" Joanita aliondoka huku wale vijana wakiendelea kumrushia maneno, Akiwa anaelekea ile njia aliyoelekezwa moyoni mwake aliwaza "Hawa vijana lazima watakuwa vibaka, mmh wala sipiti njia hiyo ngoja nitafute mtu mwingine nimuulize" Hivyo Joanita aliondoka na alipofika mbele alimuona kijana mmoja aliyekuwa amesimama akiwa anavuta sigara alisogea na kumsalimia kisha kumuomba amuelekeze, kijana yule alimtizama Joanita na kisha akamwambia.

"Hapo mbona karibu sana, dada, twende nikupeleke wala siyo mbali" Joanita alitabasamu na kumshukuru yule kaka hivyo waliongozana na kupita njia ya upande wa kushoto tofauti na ile aliyoelekezwa na wale vijana waliendelea kutembea hadi walipofika eneo moja ambapo kulikwa na giza sana yule kijana alipiga filimbi, na ghafla wimbi la vijana kama watano walifika na kumzunguka Joanita kisha kuchukua simu na mkoba wake aliokuwa ameushika , vijana wale walikuwa wameshikilia mapanga Joanita alitetemeka sana na kuwaomba wasimdhuru, lakini mmoja wao akasema "Haiwezekani tukiachie kifaa kama hiki, msichana mrembo sana huyu au mnasemaje wakuu" Walitizamana na mmoja wao alimbeba Joanita juu juu kama mzigo hadi kwenye kichochoro kimoja ambapo waliamua kumfanyia ukatili mkubwa na hatimaye walimbaka, masikini Joanita alilia kwa uchungu baadaye sauti ilisikika na wale vijana waliokuwa kule maskani ya mwanzo walikuja kumokoa ambapo walimkuta akiwa hajitambui kwa maumivu makali, "Jamani huyu dada si tulimwambia asipite njia hii, daah tizama sasa kilichomkuta duuh tumsaidie jamani kumpeleka hospitali. Walimpeleka hospitali na baadaye ndugu zake walifika ili kumuhudumia. Joanita alibaki akijutia "Yalaiti ningewasikiliza wale vijana wa mara ya kwanza, inaniuma sana, ama kweli asiyesikia la mkuu huvunjika guu, na mdharau mwiba mguu huota tende.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom