Pages

Jumatatu, Mei 19, 2014

HABARI ZILIZOCHUKUA UZITO KATIKA MAGAZETI YA LEO

GAZETI MWANANCHI
Dar/Dodoma. Meneja Biashara wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) amekutwa amekufa hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitoka Dodoma ambako alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Meneja huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na jukumu la kupanga bei za mafuta za kila mwezi, alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili; Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na Ewura kwenda kuhudumia umeme vijijini (Rea) na fedha za mfuko wa barabara.
Jeshi la Polisi, Mkoa wa Temeke limethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa meneja huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo Vituka wilayani Temeke.
***************************************************************************************************
Dodoma. Mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya CUF, Amina Abdallah Amour amemjia juu katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwa kuufananisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kundi la Boko Haramu na kutaka alaaniwe.
Ukawa iliundwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba na unahusisha wajumbe kutoka vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma juzi, mbunge huyo alisema kauli ya Nnauye ni ya uchochezi na inapaswa kulaaniwa.
Mbunge huyo alikuwa akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Wanawake, Jinsia na Watoto kwa mwaka 2014/2015 iliyowasilishwa na waziri wake, Sophia Simba.
*****************************************************************************************************Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuongoza mkutano wa mashauriano ya awamu ya kwanza ya uwekezaji katika mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) utakaowakutanisha wawekezaji wa ndani na nje Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa DART, Asteria Mlambo alisema mwishoni mwa wiki kuwa mkutano huo utakaofanyika mapema mwezi ujao utatoa nafasi kwa wawekezaji kuzijua fursa za uwekezaji zitakazopatika kwenye mradi huo.
Washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa kutoka katika benki na taasisi mbalimbali za kifedha, kampuni za kutengeneza mabasi, kampuni za mawasiliano, mifuko ya kijamii na wengine.
Mada kuhusu mradi wenyewe wa DART itatolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Jumanne Sagini.
Kabla ya mkutano huo, DART imeandaa mkutano wa wamiliki wa daladala Dar es Salaam, Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) na wadau wengine ili kuwafahamisha jinsi gani wanaweza kunufaika na mfumo huo mpya.
*********************************************************************************************************
GAZETI NIPASHE
Bunge linaendelea na vikao vyake leo kwa Kambi Rasmi ya Upinzania, kuwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/15 kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Jumamosi iliyopita Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliwasilisha hotuba yake na Kamati ya Huduma za Jamii.

Baada ya maswali na majibu, Bunge litaanza kujadili bajeti ya wizara hiyo elimu kesho na keshokutwa itakuwa zamu ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Ujenzi.

Mei 22 hadi 23, mwaka huu ni Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati Mei 24 na 26 ni Wizara ya Kazi na Ajira na Wizara ya Uchukuzi.

Mei 27 hadi 30, Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Nishati na Madini.

Mei 31 hadi Juni 02 ni Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia pamoja na Maji wakati Juni 03 hadi Juni 04 ni Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Fedha.
**********************************************************************************************************Vyama vitatu vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimesema havitasusia uchaguzi mkuu wa 2015 hata kama kama Chama cha Mapinduzi (CCM) na wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wataamua kupitisha rasimu ya katiba mpya iliyochakachuliwa.

Vyama hivyo vimesema kwamba vitashiriki katika uchaguzi huo kupambana na chama tawala.

Viongozi wa Ukawa walisema kususia uchaguzi mkuu ambao utamchagua rais, wabunge na madiwani na kuiachia CCM pekee yake itakuwa ni sawa na kumuachia fisi bucha ambaye ataweza kula nyama yote.

Ukawa unaundwa na vyama vya CUF, NCCR- Mageuzi na Chadema ambavyo viliamua kususia Bunge la Katiba kupinga uendeshaji wa Bunge hilo hususani kupuuzwa kwa mapendekezo ya Tume ya Warioba kuhusu muundo wa Muungano.

Vyama hivyo pia kwa kufanya mikutano nchi nzima kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.

******************************************************************************************************

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amesema njia pekee ya kushinikiza serikali kuwasilisha muswada wa mabadiliko wa sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari ni vyombo hivyo kugoma nchi nzima.

Amesema vyombo vya habari vimekuwa vikilalamikia kwa muda mrefu sheria hizo kandamizi kutofikishwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa mabadiliko wakati wana uwezo wa kuungana na kugoma nchini na serikali ikapeleka muswaada huo bungeni.

“Nyinyi vyombo vya habari mna nguvu kubwa sana, kila siku mnalalamikia kwetu sisi wabunge kuhusu muswada wenu wa habari ambao unakaliwa na serikali kuwa haufiki bungeni, kwanini msiungane na kugoma nchi nzima tuone kama hautaletwa bungeni na serikali, tatizo mimi naona hamjaweka nguvu ya pamoja,” alisema Lema.

 Lema alisema hayo wakati akichangia mada kuhusu changamoto zinazowakabili vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari katika kuripoti habari za Bunge iliyoandaliwa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom