Pages

Jumanne, Juni 24, 2014

Flora mbasha na mume wake watafuta suluhu kurudiana.

Dar es Salaam. Kuna kila dalili kwamba mwimbaji maarufu wa muziki wa Injili nchini, Flora Mbasha na mumewe Emmanuel Mbasha wanatamani kurudiana, baada ya kuwapo mgogoro katika uhusiano wao wa ndoa, ulioingia katika vyombo vya habari yapata mwezi mmoja sasa.
Kwa nyakati tofauti jana, kila mmoja wao alimwambia mwandishi wetu kwamba yupo tayari kurudiana na mwenzake, hatua ambayo inaweza kuondoa mgogoro huo ambao umefifisha taswira yao ya kiutumishi.
Akizungumza nyumbani kwake Tabata Kimanga, Dar es Salaam, Mbasha alisema ameshamsamehe mkewe na kwamba anamsubiri muda wowote arudi nyumbani kusuluhisha mgogoro wao.
“Nawapenda Watanzania wote wazidi kutuombea ili mimi na mke wangu turudiane.”
Kauli hiyo ni sawa na ile aliyoitoa Flora wiki iliyopita pale aliposema: “Ninawaomba Watanzania waendelee kuniombea ili niweze kushinda majaribu haya, kilichotokea ni sehemu tu ya kupimwa imani yangu”.
Jana, Flora alirudia kauli hiyo kupitia kwa wakili wake, Addo Mwasongwe ambaye alisema mwimbaji huyo yupo tayari kukutana na mumewe na ndugu ili waondoe tofauti zao.
Maelezo ya MbashaKwa upande wake Mbasha alisema: “Mi namwomba Flora ajishushe akubali, aje home (nyumbani) tuyamalize na maisha yaendelee. Yeye ni mke wangu namtaka. Kama ananipenda arudi, tuite wazazi tutatue mgogoro huu.”
Aliongeza kuwa hakuna binadamu yeyote asiyesamehewa na kwamba kilichotokea katika ndoa yao ni sehemu ya maisha ambayo wengi hupitia.
“Siku zote naamini tunachotakiwa ni kujenga na siyo kubomoa… Flora asing’ang’anie kwa watu arudi hapa… apige hodi… ‘mume wangu’ nimerudi …na mimi nitampokea tuendelee kulea watoto.”
Mbasha anakabiliwa na tuhuma za kumbaka shemejiye wa miaka 17 na kesi yake inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na sasa yupo nje kwa dhamana.
Kauli ya FloraWakili Mwasongwe alisema: “Flora amesema ameshayatoa rohoni masuala yote ya mgogoro na mumewe na leo (jana) aliniambia anataka kusuluhishwa hata kesho (leo) lakini nimeshindwa kuwakutanisha kwa sababu nipo ‘busy’.
“Ila nilimwambia Ijumaa hii nitafanya hivyo kwa kuwakutanisha yeye (Flora), Mbasha na wazazi wake ili kumaliza tofauti hizo.”
Wakili huyo alisema awali alikutana na wazazi wa Mbasha lakini hawakufikia mwafaka, lakini kwa sasa anaamini mambo yatakwenda vizuri.CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom