Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal akimsikiliza msanii maarufu nchini, Rehema Chalamila, ‘Ray C’, jana, wakati akipata ushuhuda kutoka kwa msanii huyo jinsi dawa za kulevya zilivyomwathiri alipotembelea banda lake la asasi ya Ray C Foundation kwenye maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani ambayo kitaifa yalifanyika Mbeya. Picha na Godfrey Kahango
Juni 26 ya kila mwaka, dunia inaadhimisha siku ya kupiga vita matumizi na kusafirisha dawa za kulevya. Mwaka huu, maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa mkoani Mbeya kwenye Uwanja wa Ruanda Nzovwe ambako Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alikuwa mgeni rasmi.
Pamoja na mambo mengine kwenye eneo hilo, walikuwapo watu wawili ambao walitoa ushuhuda wa madhara ya dawa za kulevya kwa binadamu na jamii kwa ujumla na kusababisha watu waliokuwapo kukumbwa na baridi ya woga kama mbwa aliyeona chatu.
Mashuhuda hao ambao walisafirisha, walitumia kwa njia mbalimbali dawa za kulevya na hatimaye kujinusuru ni Very Fidelis Kunambi na Rehema Chalamila maarufu kwa jina la Ray C.
Hata hivyo aliyewaliza wengi na kuwafanya wafikirie mengi ni Ray C ambaye leo tunalazimika kukuleta kauli yake yote akianza hivi,
“Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa hapa leo nikiwa mzima mwenye afya na moyo wa ujasiri. Natumia fursa hii pia kuwashukuru Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya kwa kunialika kutoa ushuhuda wangu. Nafurahi kwa mahudhurio haya ya viongozi na wananchi, Nawapenda wote.
Naitwa Rehema Chalamila, wengi wananifahamu kwa jina la Kisanii la “Ray C”. Mungu alinibariki na kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa kwani nikiwa na umri wa miaka 17 nilifanikiwa kupata kazi ya utangazaji katika Radio East Africa, mwaka 1999, mwaka 2000 nilijiunga na Radio Clouds. Mafanikio yangu hayakuishia hapo, nikiwa Radio Clouds mwaka 2002 nilianza muziki na kupata mafanikio makubwa sana. Mafanikio ambayo yaliniwezesha kujenga nyumba nzuri na kubwa nikiwa na umri wa miaka 19, baadaye kununua magari na kufungua maduka makubwa jijini Dar es Salaam na hatimaye kuwa msaada mkubwa wa familia yetu.
Aidha, nilitembelea Marekani, Dubai, Sweden, Hongkong, Uganda, Kenya, Afrika Kusini, , Uingereza, China, Oman, Australia, China, Norway, Msumbiji, Afrika Kusini, India, na Nigeria kufanya muziki.
Dawa zamgeuza miguu juu kichwa chini
Ghafla ujana ulionipaisha na kunipeleka juu ukanigeuza kichwa chini miguu juu. Nuru na nyota yangu ikafifia, Nikawa sionekani kiasi cha watu wakafikia kusema nimekufa.
Uwezo wangu wa kufanya muziki ulitoweka, nilianza kuuza vitu vyangu kimoja baada ya kingine nikianza na vidogo vidogo, mwisho nikauza magari yangu, Nyumba nayo ikaenda, Maduka nayo nikayafilisi nikafunga, nikaanza kuwa mtu wa kujificha huku nikendelea kudhoofika.
Ilifika wakati nililazimika kutembea nimevaa “kininja”. Mungu wangu! Nilikuwa nimenasa kwenye mdomo wa mamba, dawa za kulevya zilikuwa zinanimaliza! Nilipokuja kushtuka nilikuwa tayari nimenasa, Maisha yangu yakawa si starehe tena bali mateso na aibu!
Nilipokuwa katika uteja nilikwenda mbali zaidi ya kuuza vitu vyangu vya thamani. Roho inaniuma sana ninapokumbuka nilipomshikia kisu mama yangu mzazi kumlazimisha anipe hela nikanunue dawa. Roho inaniuma sana ninapokumbuka nilipomnyonga mkono mama kumpokonya simu.. ninapokumbuka haya roho huwa inaniuma kuliko hata kupoteza vitu vyangu vya thamani nilivyopoteza.Namshukuru mama alitambua sikuwa mimi, hakunikatia tamaa aliendelea kunihangaikia na kufanya maombi sana. Samahani kwa mateso niliyokupa na asante sana mama yangu, Mungu azidi kukubariki. Nawaomba wazazi Chonde Chonde wasaidieni vijana wenu.
Mheshimiwa, nakumbuka nilivyofukuzwa kama mbwa kwa muuza dawa kwa sababu nilikuwa sina hela, naumia sana ninapokumbuka siku nilizokuwa nalala kwenye boksi, siwezi kurudi nyumbani nikiwa arosto. Kwa sababu ya kukosa dawa kwa kukosa hela nikalazimika kulala kwenye boksi kusubiri labda itatokea “kampani” ininunulie dawa nipone. Yalikuwa ni mateso ya ajabu ambayo hayana mfano.
Azungumzia familia nzima ilivyoteseka kwake
Mateso na dharau nilizopata hazikuwa zangu peke yangu. Familia yangu pia ilikuwa katika dimbwi la mateso, Familia yote iliumwa, mama yangu alilia sana na kuhaangaika... mwanangu...nini hiki... umerogwa na nani mwanangu? ... ee Mungu nisaidie. Kilikuwa ndiyo kilio cha mama kila wakati. Mtu aliyekuwa akitegemewa na familia nilikuwa natoweka taratibu .. sasa nikawa mzigo mkubwa kwa familia.
Nilikuwa naumia sana na nataka kuacha lakini nimenasa kwenye meno makali ya mamba sina ujanja. Mama alihangaika sana na ndugu zangu pia walikosa raha. Mama alikuwa ni mtu wa kwenda kwenye maombi kila wakati. Alikuwa na fedha lakini naye uchumi wake uliporomoka na kutoweka kwa sababu yangu mimi.
Mungu ameonyesha nguvu zake
Hatimaye Mungu alimwinua Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na kunisaidia kwa kunipa matibabu na kwa sababu nilikuwa na dhamira ya kuacha, kwangu ilikuwa ni jambo rahisi kuachana na dawa za kulevya.
Nitumie fursa hii kwa mara nyingine kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa nyingine ya kuwa Ray C, lakini siyo tu kuwa Ray C yuleyule wa zamani, bali kuwa Ray C mwenye akili na mitazamo mipya kabisa ya maisha na ambaye Watanzania na taifa litanufaika naye sana!
Ampigia magoti JK
Kwa namna ya kipekee kwa mara nyingine namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete kwa kunisaidia Mungu azidi kumbariki. Ninaahidi leo, kwa kunisaidia mimi wengi watapona!
Na najua hiyo ndiyo ilikuwa dhamira yake, niwe mfano ili wengi waokoke na janga hili. Na Ninaamini Mungu alikuwa na mpango na mimi, lazima nimtumikie kwa njia hii.
Ataja siri za kutumia dawa za kulevyaKilichoniingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya ilikuwa ni marafiki wabaya na mahusiano mabaya ya kimapenzi, ambapo kupitia mtu niliyempenda na kumwamini sana katika mazingira ambayo hayakuwa wazi nilijikuta nimeshanasa kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Nilipokuwa katika tatizo hilo nilijifunza mambo makubwa matatu, jambo la kwanza ni kuwa siyo wote wanaotumia dawa za kulevya wameingia huko wakijielewa.
Pili kuna unyanyapaa mkubwa wanaofanyiwa waathirika wa dawa za kulevya kutoka kwa jamii na vyombo vya dola, na kwa asilimia kubwa unyanyapaa huo unatokana na uelewa mdogo wa jamii na vyombo vya dola juu ya hali halisi ya tatizo.
Tatu, nilijifunza kuwa watu kuendelea kutumia dawa hizi na tabia nyingi hatarishi wanazokuwa nazo hakutokani na wao kupenda bali mateso makali ambayo mtu anayapata anapokosa dawa hizo.
Roho inaniuma sana ninapowaona waathirika wa dawa kwenye maskani zao au popote, najua mateso mazito waliyonayo tofauti na jamii inavyofikiri.
Sasa kuongoza vita dhidi ya dawa za kulevya
Kutokana na Mungu kunisaidia kwa kumtumia Dk Jakaya Mrisho Kikwete, na jinsi mimi mwenyewe ninavyoguswa na tatizo hili, shukrani yangu kubwa kwa Mwenyezi Mungu na Mheshimiwa
Rais Kikwete ni kufanya juhudi kuelimisha jamii juu ya athari za dawa za kulevya. na pia kuwasaidia waliokwishaingia watoke na ambao hawajaingia wasithubutu.
Kwa kufanikisha hilo nimeamua kuanzisha asasi inayoitwa Ray C Foundation, asasi hii ina lengo la kufanya uelimishaji mkubwa kwa jamii kupitia makundi yake mbalimbali pamoja na kusaidia walioathirika warudi kuwa watu wa kawaida,
Kwa kupitia Ray C Foundation tayari tumeanza kampeni ya shule kwa shule tukitembelea baadhi ya shule za sekondari za jijini Dar es Salaam, na tuna lengo la kuzitembelea shule zote za sekondari katika mikoa yote ya Tanzania hasa ile iliyoathirika zaidi na dawa za kulevya.
Vile vile tumeanza kutembelea vijana watumiaji dawa za kulevya kwenye maskani zao na kuwaelemisha waache na katika miezi miwili tu ya kampeni hiyo vijana 25 wameamua kuacha na sasa wanapata matibabu ya Methodone.
Aidha, tunakusudia kufanya uelimishaji kwa makundi mbali mbali ya kijamii kwa kutumia njia mbalimbali.CHANZO MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni