Mtoto Erick Emmanuel (6)mkazi wa Kijiji cha Bwizanduru Kata ya Maruku, Wilaya ya Bukoba Vijijini, akiwa na makovu na majeraha mapya yanayodaiwa kutokana na kipigo cha viboko kutoka kwa baba yake. Picha na Phinias Bashaya
Matukio ya ukatili yameendelea kuibuka nchini baada ya kugundulika kwa mtoto mwenye umri wa miaka sita katika Kijiji cha Bwizanduru Kata ya Maruku Wilaya ya Bukoba Vijijini akiwa amefungiwa ndani kwa miezi saba huku makalio yake yakiwa yamechanika kutokana na adhabu ya viboko.
Mtoto huyo aitwaye Erick Emmanuel anatembea kwa shida huku akiwa na makovu mengi mwilini na sehemu ya makalio yake kuharibika vibaya. Amekuwa akipewa adhabu hiyo na baba yake mzazi.
Kwa mujibu wa majirani wa mtoto huyo ambaye anaishi na mama yake wa kambo aitwaye Fidea Emmanuel, anayedaiwa kumtesa mtoto huyo ni baba yake mzazi aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Justinian.
Chanzo cha mateso hayo inadaiwa kuwa mtoto huyo hujisaidia ndani na hivyo baba yake mzazi kuamua kumfungia kwa kipindi chote cha miezi saba bila kutoka nje huku kila siku mtoto huyo akipata adhabu kali ya viboko.
Mama wa kambo wa mtoto huyo Fidea Emmanuel aliiambia Mwananchi kuwa mume wake alikuwa akimpa adhabu mtoto huyo mara kwa mara hasa alipojisaidia au kukojoa ndani kwa kutumia fimbo ya mti wa m’buni.
Hata hivyo mama huyo wa kambo na Erick alisema kutokana na hali mbaya ya mtoto huyo iliyotokana na adhabu ya viboko,amekuwa akimtibu kwa kutumia dawa za mitishamba bila ya kufanyiwa vipimo au kupelekwa hospitalini.
Pia, mtoto huyo anaonekana kuwa na michirizi mikubwa katika sehemu ya kifua na tumbo pamoja na makovu makubwa mwilini mwake, alama ambazo zinahusishwa na viboko alivyokuwa akicharazwa na baba yake mzazi.
Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maiga Audax Bayon, alisema kuwa ilikuwa ni vigumu kumuona mtoto huyo kwa kuwa kila aliyemuulizia aliambiwa yuko ndani akijifunza kusoma na watoto wengine jambo ambalo halikuwa kweli.
Mama mzazi wa mtoto huyo Aneth Brand ambaye anaishi Kijiji cha Bugabo wilayani humo alisema miezi saba iliyopita alimpeleka mtoto huyo kwa baba yake na kudai hakuwa na matatizo makubwa yanayomkabili mtoto wake, lakini sasa ana matatizo ikiwamo upungufu wa damu.
Akizungumzia tukio hilo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bwizanduru, Edward Mwemezi alisema pamoja na mtoto huyo kufanyiwa ukatili mkubwa kwa muda mrefu alisema familia ilijitahidi kuficha taarifa hizo hata kwa majirani.
Alisema baada ya kuendelea kuenea kwa uvumi wa kuwepo kwa mtoto aliyefungiwa kwa muda mrefu na kupewa mateso katika familia hiyo waliamua kufuatilia na tayari mtuhumiwa amewekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.CHANZO MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni