Pages

Ijumaa, Juni 27, 2014

Kuwa mjasiriamali fahamu namna gani unaweza kuanzisha biashara ya vipodozi

Moja ya biashara zinazovutia watu wengi ni biashara ya vipodozi. Hata hivyo wafanyabiashara wa vipodozi wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali. Baadhi ya changamoto hizi ni baadhi ya wafanyabiashara kutofahamu taratibu za kufanya biashara hii.Katika makala ya leo nitaeleza namna ya kujihusisha na biashara ya vipodozi kuanzia kusajili jengo, kuagiza bidhaa za vipodozi kutoka nje ya nchi na kusajili vipodozi.
Vipodozi ni wingi wa bidhaa kipodozi. Kipodozi ni kitu chochote kinachoweza kutumika kwenye mwili au sehemu ya mwili kwa njia ya kujipaka, kuosha, kunyunyuzia, kujipulizia, kwa ajili ya kusafisha, kujiremba, kujipamba, kuongeza uzuri wa ngozi au muonekano wa sura.
Kwa mujibu wa sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, TFDA ndiyo yenye kudhibiti ubora na usalama wa bidhaa za vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya ya jamii.
Sheria hii pia inakataza kuuza, kuhifadhi au kutengeneza chakula, dawa na vifaa vya tiba isipokuwa katika maeneo yaliyosajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na mtengenezaji bidhaa awe na leseni ya bidhaa iliyotolewa na mamlaka.
Ni marufuku mtu kutengeneza kwa kuuza, kusambaza au kuhifadhi bidhaa zinazosimamiwa kwa mujibu wa Fungu la 18 la sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya Mwaka 2003, isipokuwa kwenye maeneo yaliyosajiliwa na TFDA.
Ili uweze kufanya biashara ya vipodozi unapaswa kuhakikisha kuwa vipodozi unavyotaka kuuza vimesajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). TFDA imeweka utaratibu unaomwezesha mtu yeyote kusajili bidhaa za vipodozi. Tangu mwaka 2003 mpaka Juni 2013 TFDA imesajili jumla ya vipodozi 3,968.
Usajili wa vipodozi unajumuisha utathimini wa taarifa za ubora na usalama wa viambata vilivyotumika, uchunguzi wa kimaabara wa sampuli za vipodozi husika na tathimini ya taarifa za kwenye lebo.
Taratibu za kusajili vipodozi
Kama unataka kusajili vipodozi unatakiwa kuomba Usajili wa Vipodozi TFDA.
Wasilisha maombi yako kwa kujaza Fomu ya Maombi ukamilifu pamoja na sampuli mbili za bidhaa. Fomu hizi zinapatikana katika ofisi za TFDA na tovuti ya mamlaka. Wasilisha nakala ya kawaida na ya kielektroni kwenye CD-ROM kwa muundo wa PDF, fonti 12 mtindo wa zamani wa “bookman”. Kama unasajili bidhaa zaidi ya moja, wasilisha fomu ya maombi iliyojazwa kwa ukamilifu tofauti kwa kila bidhaa au bidhaa mbadala.
Katika maombi ya usajili wa vipodozi lipa pia ada ya tathmini na usajili ya dola za Marekani 75.00 kwa kipodozi cha kilichotengenezwa nje ya nchi au dola za marekani 45.00 kwa kipodozi kilichotengenezwa nchini. Iwapo mamlaka itaridhika, itatoa usajili wa kipodozi. TFDA itakataa kusajili wa vipodozi kama itakugundua kama kuna ukiukwaji wa utaratibu katika usajili au bidhaa inayotarajiwa kusajiliwa ina viambato vyenye sumu ambavyo ni hatari kwa matumizi ya binadamu. Baadhi ya viambata hivi ni Hydroquinone, Mercury na steroids.Masharti ya kusajili vipodozi
Anayesajili vipodozi anatakiwa kuwa mkazi wa Tanzania au kampuni iliyoandikishwa/kusajiliwa nchini Tanzania. Nyaraka zote za maombi zinatakiwa kuwa zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili. Muombaji wa usajili wa vipodozi anatakiwa kuwasilisha sampuli, nyaraka na taarifa nyingine kadri atakavyoelekezwa au kutoa ufafanuzi kutegemea hali halisi ya bidhaa anayotaka kusajili. Martin Malima ni mtaalamu wa masoko kutoka TFDA. CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom