Jumatatu, Julai 14, 2014

KUELEKEA UCHAGUZI 2015...Ridhiwani ataja 11 wanaotosha kugombea Urais

Miongoni mwa aliowataja kuwa wana sifa ni makada watano walio chini ya uangalizi wa CCM wa mwaka mmoja baada ya kubainika kuanza kampeni za urais mapema, mawaziri wawili waliopoteza nyadhifa zao katika kashfa ya Operesheni Tokomeza, mwanamke mmoja na Rais wa Zanzibar.
“Kutaja majina tu, naweza kuorodhesha wengi tu. Naweza kuorodhesha hata watu 500, kwa sababu tunaona wengi sana,” alisema mtoto huyo wa Rais Kikwete ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa muda mrefu akitokea umoja wa vijana wa chama hicho, UVCCM. “Kwa mfano, kwa upande wa Bara tunao Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, January Makamba, Bernard Membe, Steven Wassira, Edward Lowassa na Asha-Rose Migiro,” alisema.
Aliongeza: “Hawa ni kwa uchache zaidi… ni baadhi ya watu ambao wanatajwa kwa upande wa Bara, lakini jambo la msingi ni nani mwenye sifa za kuwa rais.”
Alisema pamoja na kwamba wanasiasa hao wote wanazo sifa za kuiwania nafasi hiyo ya juu, vikao vya chama ndivyo vitakuwa na nafasi ya kuwachuja ili kupata wanaotosha. “Kama wanatosha au la, vikao vya chama vitakaa kuamua licha ya kuwa hao wote niliowataja, kwa sifa za kugombea urais wote wanajitosheleza. Wana sifa, wana uwezo wa kugombea na wana uwezo wa kushinda, hao ni kwa upande wa Bara,” alisema.Hata hivyo, Ridhiwani alidokeza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa watakaokwama kufikia lengo hilo kutokana na kukabiliwa na kesi ndani ya chama, ambazo hakuzitaja wala kutaja wahusika. CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom