Pages

Jumanne, Julai 08, 2014

NI MUHIMU KUWA MAKINI "Binti asimulia Watanzania wanavyotumikishwa kwenye madanguro China"

Wakati wanawake kwa wanaume wengi huenda barani Asia, hasa China kununua bidhaa kwa ajili ya kuja kuzichuuza, hali sasa ni tofauti kwa kuwa kuna wasichana ambao huenda huko kwa ahadi za ajira, lakini huishia kufanya ukahaba kwenye madanguro, gazeti hili linaweza kukuthibitishia.
Wasichana hao hutafutwa na mawakala wa hapa nchini ambao kazi yao huwa ni kutafuta wasichana wazuri na baadaye kuwashawishi kwa kuwaeleza fursa za ajira za hotelini zilizo barani Asia.
Msichana akikubali, wakala huchukua jukumu la kumtafutia viza ya kuingia China na baadaye kuwasiliana na mwenyeji wake, maarufu kama Lady Boss, ambaye hutuma tiketi ya ndege kwa ajili ya kumsafirisha ‘mwajiriwa’ mpya.
Hata hivyo, hali hubadilika mara wafikapo huko kwa kuwa ‘mwajiri’ huyo humpokonya hati ya kusafiria na baadaye kumpa maelekezo kuwa atatakiwa kulipa Dola 200 kila siku ambazo atakuwa akizipata kwa kufanya umalaya kwenye klabu na maeneo ya biashara.
Tayari wasichana kadhaa wa Kitanzania wamenaswa katika mtego huo na kujikuta wakilazimika kuuza miili yao ili wamudu ada ya Dola 200 pamoja na fedha za kujikimu, akiwemo Munira Mathias mwenye umri wa miaka 23 ambaye alimudu kuvaa ujasiri wa kuweka bayana uovu huo katika mazungumzo yake na gazeti hili.
Binti huyo Mtanzania aliyesafiri kwa saa 18 kwenda Guangzou, China alitakiwa kupumzika kwa saa mbili tu kabla ya kupelekwa kuanza ‘kazi’ ambayo hakuitarajia.
 “Baada ya kupumzika kwa saa mbili tu, nilipelekwa kwenye klabu,” anasema Munira wakati akisimulia mkasa wake.
 “Sikuwa na kazi nyingine zaidi ya kucheza muziki na wanaume ambao licha ya kwamba sikuwahi kuwaona, walinichangamkia kama vile wananifahamu.”
Munira aliondoka Januari mwaka huu kwenda China ambako aliahidiwa kuwa angeajiriwa hotelini, lakini alikutana na ‘ajira’ ya ukahaba, huku akilazimika kuwalipa ‘waajiri’ wake Dola za Marekani 200 kila siku.
 Binti huyo, ambaye alifanikiwa kuchomoka mikononi mwa waajiri hao baada ya viza yake kuisha, alisema kwa siku 91 alizokaa China, alipata mateso ambayo hatayasahau ikiwamo kupigwa, kubakwa na kundi la wanaume raia wa Nigeria, pia kulazimika kutoa mimba aliyoipata kwa kubakwa.
 “Nilifika Guangzhou kama saa 9.00 alasiri za China na kulikuwa na baridi sana,” anasema Munira akisimulia jinsi alivyokanyaga kwa mara ya kwanza ardhi ya nchi hiyo akiwa na matumaini ya kuanza maisha mapya.
“Wakati huo nilikuwa nikijaribu kupata mawasiliano na mwenyeji wangu ambaye niliagizwa kutoka Magomeni, Dar es Salaam.Alisema alipotoka Dar es Salaam aliambiwa angepokewa na mtu anayeitwa Jacky ambaye hakumkuta kwa kuwa alikuwa safarini Malaysia, lakini alikuwa ameacha maagizo apokewe na mwanamke mwingine.
 “Nilielekezwa nikodi taksi hadi kwenye hoteli inayoitwa Nairobian. Kutoka hapo uwanja wa ndege hadi  kwenye hiyo hoteli ni sawa na umbali wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam hadi Bagamoyo,” anasema Munira.
 Anasema alitakiwa kulipa Yuan 200 (Sh60,000) na alipofika katika hoteli hiyo alipokewa, akaoga na kupewa chakula.
 “Nilipomaliza kula nilipumzika kwa saa mbili hivi. Jacky alikuwa amesharudi na alinifuata chumbani na kuniambia natakiwa kwenda saluni. Hivyo tuliondoka pamoja hadi kwenye jengo kubwa lenye maduka makubwa linaloitwa Tin- shu,” anasimulia Munira.
Watanzania lukuki
Katika jengo hilo alishangaa kuwaona Watanzania wengi, wakiwamo wanawake kadhaa ambao aliwahi kukutana nao Magomeni wakati akifuatilia safari yake.
Munira anasema miongoni mwa watu aliowaona ni binti mmoja ambaye wanafahamiana ambaye alistaajabu kumwona sehemu hiyo.
 “Aliniuliza kwa mshangao, ‘mbona umekuja huku? Umekuja kufanya nini?’ Wakaanza kunishangaa. Yule msichana akaniambia ‘huku msala ndugu yangu, umekuja kufanya nini?” alimnukuu na kuongeza kuwa kabla hawajamaliza mazungumzo yao, mwenyeji wake alitokea hivyo waliyakatisha.
Anasema waliingia saluni ambako aliwakuta Watanzania na Wakenya wakifanya kazi humo na wakati yeye akiendelea kusukwa nywele kwa umaridadi, Jacky alikwenda kumnunulia nguo na viatu dukani.
 “Baada ya hapo niliambiwa nivae nguo niende klabu kwa sababu huo ni msimu wa sikukuu za mwaka mpya wa Kichina,” alisema Munira. 
Anasema alishangaa kuambiwa aende klabu usiku huo wakati alikuwa amechoka kwa safari ndefu.
 “Kilichokuwa kinanipa moyo usiku ule ni kuwa niliwaona wasichana wa Magomeni, lakini nilihisi wameambiwa wasiwe karibu na mimi.”Anasema alipoingia klabu, pia alishangaa zaidi kukutana na Watanzania wengi wa rika tofauti ambao baadhi yao aliwatambua kwa sura na pia kulikuwa na raia wengi wa Nigeria.
 “Kiasi fulani nilifarijika kuwaona Watanzania na nilijisikia kukua kiakili baada ya kuwaona Wanigeria ambao nilizoea kuwaona kwenye filamu peke yake,” anasema.
Hata hivyo, alishangaa kuona pale klabu alichangamkiwa na watu wengi, lakini hakutaka kudadisi zaidi bali alidhani ndiyo hali halisi au alikuwa na bahati ya kupendwa.
 “Baada ya kumaliza kucheza muziki kwenye klabu hiyo, walipelekwa kwenye klabu nyingine ya asubuhi.
“Tuliporudi hotelini, nilijitupa kitandani na kulala kwa sababu ya uchovu mwingi. Miguu ilikuwa imevimba kwa sababu nilikuwa nimevalishwa viatu virefu na kucheza muziki mfululizo. Nikalala bila ya hata kuoga,” anasema.
Mwanzo wa mateso
Baada ya saa moja kupita na akiwa amelala fofofo mchana ule, mara aliamshwa na Jacky, ambaye alimwamuru amkabidhi pasipoti yake.
 “Nikampa, pasipoti yangu nilikuwa nimeiambatanisha na tiketi na kila kitu. Akanishangaza kuniambia kuwa kuanzia siku hiyo niwe nampelekea Dola 200 mezani kila siku. Nilishangaa na nikaanza kulia,” anasema.
 Kwa hasira na mshtuko alioupata, Munira anasema alitoka nje na kuanza kulia na wenzake walipomuuliza kinachomliza, aliwaeleza. Waliamua kumwambia ukweli kwamba hata wao walipelekwa kwa miadi ya kupata ajira za hoteli, lakini hawafanyi hivyo.
 “Waliniambia kuwa nao walirubuniwa na wakanyang’anywa hati za kusafiria kama mimi na wakaishia kuambiwa wafanye biashara ya kuuza miili ili watafute fedha,” anasema Munira.
 Munira anasema alichanganyikiwa, hasa pale alipoambiwa na wenzake kwamba kazi kubwa ni kwenda klabu kujiuza au kuzurura eneo la Chambu Chambu.
Chambu Chambu  ni soko la bidhaa ambako wasichana hujifanya wananunua vitu, lakini kimsingi huwa wanakwenda kutafuta wateja wa ngono.“Kule wanaume wameshajijengea picha kuwa wanawake wa Kitanzania wapo kwa ajili ya kujiuza, basi wakikuona tu wanakufuata na mnaongea biashara, mnakwenda kumalizana,” anasimulia.
 Wasichana wenzake wa Kitanzania walimwambia kuwa hayo ndiyo maisha yenyewe, hivyo aliporejea ndani, mwenyeji wake (Jacky) alimwambia ajiandae kuanza kazi mara moja na Munira akawa hana budi kufuata maelekezo.
Baada ya hapo aliingia bafuni akaoga, kisha akaenda eneo la Chambu Chambu kutafuta wateja.
  “Nikakubaliana na hali halisi nikawa nafanya kazi kama nilivyoambiwa. Niliona nikubali lakini akili kichwani mwangu ilikuwa nifanye mbinu ili nirudi nyumbani,” anasema.
Simulizi ya Munira itaendelea kesho kwenye kijarida cha Ndani ya Habari.
* Munira Mathias si jina halisi-Mhariri CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom