SEHEMU YA PILI
Baada ya kumlaza mapajani kwangu huku akilia kwa
uchungu mkuu, nami nikifanya jitihada za kuyafuta machozi yake. Hatimaye Nadia
alitulia. Nilipomtazama alikuwa amepitiwa na usingizi, nikamfunika na upande wa
kanga yake. Kisha nikaiweka mikono yangu vyema aweze kuegemea vizuri.
Ukimya uliotanda ukanifanya nami nianze kusukwa
sukwa na usingizi, nilijitahidi kuukabiri lakini sikuweza. Nikajiegesha vyema
katika kiti, nikasinzia pia.
SAUTI nzito ya mpiga debe ndo ilitukurupua.
“Oyooo mwisho wa gari hapa!!”
Nadia naye alisikia sanjari na mimi, tukatazamana
na kutabasamu kama kwamba tuliambiana kufanya hivyo. Nadia akajinyoosha huku
akipekecha macho yake, mimi nikajishughulisha katika kuweka sawa mabegi yetu.
Tukatoka ndani ya gari tukiwa abiria wa mwisho kabisa. Tukaikanyaga stendi ya
Buzuluga jijini Mwanza, safari yetu fupi kutoka Musoma kwenda Mwanza ikawa
imekamilika.
Nadia alilalamika njaa inamuuma. Nilitazama huku na
kule nikauona mgahawa ng’ambo ya pili ya barabara. Nikamshika kiganja cha mkono
wake, tukavuka barabara kama hatuzisikii kelele za madereva taksi waliokuwa
wakitupigia kelele ili tukodi mojawapo ya teksi kwa ajili ya safari yetu.
Hakika tulikuwa na haja na teksi lakini matumbo
yalikuwa matupu, tulihitaji chochote kitu hasahasa cha moto.
Tulisfutahi kimya kimya bila mazungumzo baina yetu.
Kila mmoja alionekana kuwa na uchovu wake.
Baada ya hapo nd’o tulihitaji taksi, ikatuchukua
hadi G & G Hotels, ni huku nilipendekeza. Teksi ilipotoweka, Nadia
aliniuliza swali.
“Umeifahamu vipi hii hoteli kaka.”
Kwanza nilimtazama huku nikitafakari nini cha
kujibu.
“Hi ndo hoteli yangu mara kwa mara nikitembelea
jiji hili.” Nilimjibu, kisha nikaongezea kidadisi, “Kwani kuna tatizo?”
Hakujibu kitu nami sikuuliza tena, nilitambua kwa
nini hakujibu, bila shaka ni uwepo wa watu kadhaa mahali tulipokuwa,
nikajisogeza mapokezi nikafanya malipo ya vyumba viwili tofauti vyenye hadhi ya
‘Deluxe’ kisha nikamfanyia ishara Nadia akanifuata. Nikamwongoza hadi katika
chumba ambacho angelala siku ile.
Alipokiona chumba alishusha pumzi kwa nguvu,
nikakifungua akaingia, hapa akafika na kusimama katikati ya chumba akiwa anatazama
dirishani. Upesi nikachukua vifaa vyangu. Bila shaka Nadia alitaka kujibu lile
swali dogo nililomuuliza na kutarajia majibu ya kawaida.
“Kila moyo huwa na shukrani, lakini mwanadamu hana
shukrani. Naamini kabisa mwanadamu hana shukrani, Afadhali Punda aliyejiweka
wazi na shukrani yake ya mateke kuliko mwanadamu. yaani angekuwa mlemavu Yule.
Huduma mbovu za kule Musoma wakadai anatakiwa akatwe mguu. Nikamdanganya mzee
wangu kuwa nimepoteza Laptop ya rafiki yangu yenye thamani ya milioni nyingi.
Mzee wangu mimi na upendo wote anaonionyesha lakini bado nikamdanganya eti kisa
Desmund.
Tukakodisha usafiri akaletwa Bugando, naikumbuka siku aliyofika kwa
mara ya kwanza tulifikia hoteli hii, laiti ningeyajua ambayo yangekuja kutokea
nisingepoteza pesa zangu wala nisingemlaghai baba, Desmund bila ndugu yeyote
mimi nikawa kila kitu. Alifikia hatua ya kuniita Mungu wake, akanililia siku
ambayo aliweza kusimama kwa mara ya kwanza, nikamshika mkono akiwa anafanya
mazoezi ya kuimarisha miguu, nikaacha kuingia darasani hadi alipopona.
Nilipomrudisha Musoma kwao ndo hapo niliposikitika
zaidi, kile chumba alichokuwa akiishi Desmund tulimkuta mtu mwingine,
alipoulizia samani zake akapewa mkeka na sufuria ndogo mbili. Nilishangaa
lakini yale nd’o yalikuwa maisha yake halisi.
Sitaisahau siku ambayo tulilala wote ili nimtazame
afya yake, sikutaka awe mbali nami. Moyoni nilianza kukumbwa na pepo mchafu,
pepo wa maajabu aliyesema eti siwezi kukaa mbali na Desmund. Nikalala naye
katika hoteli ya Grand Villa huko Musoma. Ni usiku huo ambapo nilianza rasmi
mahusiano na Desmund, vishawishi vya kimwili, tamaa ya muda mfupi nikajikuta
kwa hiari yangu nafanya mapenzi na Desmund. Siwezi kusema alinilaghai la! Hata
yeye hakutegemea kama jambo hilo litatokea, hakika siwezi kujuta maana ni
upendo wa dhati ulinituma.
Desmund akatumia neno hilo ‘nakupenda’
nililomtamkia kuanza kunisulubu. Alijua nampenda sana hilo alilijua hadi siku
ya mwisho na ataendelea kulijua. Nikampangia chumba kikubwa na kumnunulia
baadhi ya vifaa vya ndani, hii nyumba ikaja kuwa chungu kwangu kile kitanda,
lile godoro na mashuka niliyonunua mimi ikafikia kipindi akawa jasiri kuingiza
wasichana pale ndani. Alimuingiza hadi yule msichana ambaye alisababisha
anitegue mguu kwa mpini wa jembe.
Desmund alikuwa mshamba wakati naanza naye
mahusiano, hakuna chakula cha kifahari alichokitambua zaidi ya Chipsi kuku.
Nikamwonyesha dunia ilivyo, hakujua hata mkanda wa ndege unafungwa vipi?
Nikampandisha ndege….hakujua nini maana ya ‘body exercise’ yote haya
nikamwonyesha mimi, akatanua kifua na kuvaa vizuri hatimaye akapendeza.
Kweli yule Desmund ambaye hata hakuwa akijua nini
maana ya ‘Piza na Baga’ ikafikia kipindi akanipiga mateke akisema mimi ni
mshamba sana, nimekalia kukuza matiti tu kila kukicha, sijui kuoga. Na mbaya zaidi
akafikia hatua ya kusema eti ninanuka sana hawezi kuishi na mimi
anajilazimisha. Nilitamani sana kuondoka lakini ningeenda wapi mimi
ningekimbilia kwa nani? Kila mtu anayeitwa ndugu yangu alikuwa amenitenga.”
Safari hii Nadia hakulia bali alifanya tabasamu hafifu…lakini alikuwa
amechukia. Nikaaga na kuelekea chumbani kwangu. Majibu yake ya sasa yakiwa
yanaongeza giza mbele yangu. Sikupata jibu kabisa alikuwa ana maanisha nini.
Nikavuta subira nikaenda chumbani kwangu. Nikaoga
na kubadili nguo kisha nikarejea chumbani kwa Nadia.
Nilimkuta akiwa analia, nilipoufungua mlango
akazidi kulia, japo kwa sauti ya chini. Luninga ilikuwa ikipiga kelele na
hakuonekana kama alikuwa anaitazama.
Nikaketi pembeni yake mara akasimama ghafla.
“Hivi wanaume mnataka mfanyiwe nini hasa, mnataka
mliliwe vipi ndipo mjue kuwa mnapendwa eeh….hivi mnataka roho zetu eeeh
nakuuliza ..nakuuliza wewe na wewe ni mwanaume ujue nasema na wewe …” Hapa
akanikamata ukosi wa shati langu kwa ghadhabu, akaanza kunitikisa,
sikujishughulisha kuitoa mikono yake nilitaka aseme kitu akiwa na hasira. Kweli
akaendelea.
“Yaani wakaona kuninyoa nywele zangu haitoishi,
wakanifanyta mtumishi wao wa ndani nayo pia haikutosha. Kweli Desmund
akawaangalia dada zake wananimwagia maji mimi, maji machafu…Desmund ulishindwa
kuwakaripia waache kunionea.
Mama yake naye niliyedhani kuwa anaweza kunionea
huruma akapigilia nyundo ya mwisho katika kidonda change. Eti hakuna ndoa wala
ndoano mpaka….yaani mpaka nifanyiwe tohara. Nilishtuka nikataka kukimbia lakini
nani angenipokea kama ningekimbia kila mtu alikuwa ananiona mimi adui. Mbaya
zaidi baba na mama yangu hawakutaka kunisikia na kubwa zaidi walijikusanya na
kurejea Doha Saudi Arabia. Nikabaki Tanzania nikiwa peke yangu. Licha ya upweke
ule mwanaume na mwanadamu pekee niliyetegemea atasimama upande wangu kila siku
akaniacha nikakamatwa kwa nguvu. Naikumbuka siku hiyo nililia lakini
hawakuniachia, wakanifikisha mahali ambapo ni kama machinjioni, looh!! Kuna
makabila yana roho mbaya namna hii, kumbe kabila la Desmund lina mambo haya.
Wakanifanyia ukeketaji, Desmund akiwa mkimya
kabisa, lakini kumbe haya yote yalifanyika ili mimi nikate tamaa ya kuolewa na
Desmund, walijua kuwa nitakataa lakini mimi nikakubali kumbe Desmund
hakunipenda alikuwa na mchumba aliyechaguliwa na mama yake. Lakini mchumba wa
kupewa na mama mimi sina tatizo, mbona sasa akaanza kulewa, mbona sasa akaanza
kuwabadili wasichana hovyo, au kwa sababu …au kwa sababu nilikuwa
sizaiiii….eeeh au kwa sababu sikumzalia mtoto mimiii……Desmund hivi sio wewe uliyenisindikiza
kutoa mimba mara tatuw tofauti. Si wewe Desmund uliyesema kondomu huwa
zinakuwasha na hauzipendi hata kidogo.
Nikakusihi tuwe makini ukanikaripia
nikakusikiliza usemayo mume wangu. Kama mimba tulienda kutoa wote mbona
nilipopata tatizo la kizazi ukanitenga, ukanitupia katika midomo ya mawifi
zangu. Nikatukanwa nikasemwa kikabila chenu, wakanitukana kikabila chenu wewe
naye ukasema nao kikabila chenu ili nisiweze kuwasikia. Kumbe nawe ulinitenga
Desmund…..Desmund….
Wakanilaza jikoni huku wewe ukilala chumbani kwa
raha zako, ukaridhika kuniona nasulubika, asubuhi ukaondoka bila
kunisalimia..na ukatoweka kwa siku ishirini.
Desmund nilikunong’oneza kuwa siyajui maisha ya
kijijini, nawe ukasema hutaniacha pekee kamwe, lakini ukatoweka, nikawa mtumwa
rasmi, nikaosha vyombo nikafua hadi nguo za mawifi. Nikakamua ng’ombe maziwa,
mara nikaambiwa niwe naenda kuwapeleka malishoni.
Ni lini mimi nimejua kuchunga ng’ombe…lini
nimejifunza kitu hiki. Nilikwambia Desmund kuwa maisha niliyotoka mimi ni ya
kudekezwa sana, sawa sikatai kuchunga ng’ombe lakini walau basi ningefundishwa
taratibu.
Nikaenda malishoni, ng’ombe wakapandwa mori zao
mmoja akanitupa mbali kwa pembe zake, nikavunjika kiuno. Desmund ukanipa pole
kwa njia ya simu…..kweli kiuno kimevunjiaka ukatumia simu …Desmund….simu!!!!!
aaaargh Des…De…..Desmu…..Desmuuu…….” hapa uvumilivu ukashindikana akaangua
kilio, hiki cha sasa kilikuwa kilio kitakatifu, akajirusharusha kitandani,
akaruka huku na kule. Hapa nikashtuka kuwa anaweza kujizuru, nikamkamata mabega
yake nikamgandamiza kitandani. Akashindwa kufurukuta lakini hakika alikuwa
amechachamaa sana.
Niliendelea kumgandamiza huku nikimchukia Desmund.
MOJA. Yaani mkeo anavunjika kiuno hufiki kumwona
unapiga simu.
MBILI: Mwanamke aliyeweka masomo kando akakupigania
unashindwa kumpigania mbele ya ndugu zako.
TATU: Yani kumbe Desmund mpuuzi bado anaendekeza
mila za kizamani za tohara.
“MASKINI NADIA ……USILIE NADIA……jikaze jikaze ndo
wanadamu hawa…..jikaze usilie…” nilimsihi……..USIKOSE NINI KITAENDELEA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni