SEHEMU YA NNE
Kama ni kulia hakika Nadia alikuwa Amelia haswa, na
kama ni majuto hapakuwa na shaka alikuwa amejutia mengi sana ambayo aliyafanya
kisha kutumbukia katika mdomo mbaya wa Desmund. Bado nilikuwa katika fumbo gumu
sana la kuweza kujua nini kilijiri hadi binti huyu yakamsibu mazito kiasi kile.
Alikuwa amekonda na hakuonekana kujali kuhusu hilo. Hakika alikuwa katika
majuto makuu.
Sikutaka kusema neno lolote la ziada maana
nilihofia kumtibua na kuanza kusimulia mkasa mwingine mpya ambao ungekiamsha
kilio chake upya tena.
Lakini ni neno gani nilipaswa kusema na lipi
sikupaswa kusema. Maana kama neno dogo la kiingereza nililosema lilimtibua
Nadia na kujikuta akinieleza mambo mengine mengi. Ni neno gani lilikuwa sahihi
kwa wakati ule. Nilifumba macho yangu na kumkabidhi Mungu wakati ule ili
aniongoze vyema katika matamshi yangu.
Ni kweli nilihitaji kuandika kitabu cha
kusisimua kutoka katika simulizi ya kweli ya Nadia lakini bado sikupenda
kumwona binti yule wa kiarabu akilia kilio cha uchungu, sikupenda Nadia
alivyokuwa anajuta mbele yangu. Niliumia sana hakika. Lakini nilijionya kuwa
kama nikiendel,ea na huruma ile nitajikuta siifanyi kazi yangu.
“Nadia mama….” Nilimuita, akageuka kunitazama.
Ebana eeee!!! Jicho jekunduuu!! Msichana alikuwa
Amelia sana, kuwa jekundu pekee hakukutosha. Lilikuwa limevimba haswa.
“Abee!” aliitika, nikawahi kukwepesha macho maana
nilihisi muda wowote naweza kutokwa machozi pia.
“Nenda ukaoge dadangu….nenda ukaoge….”
Alinitazama kiasi kwamba nikahisia ameijiwa na
kumbukumbu nyingine, jambo ambalo sikuwa tayari kuliona likitokea.
“Kuna maji ya moto…” aliniuliza kwa sauti ya chini
ambayo ilikuwa inakwaruza.
Upesi nikairukia simu nikapiga mapokezi na kuomba
huduma hiyo.
Acha hoteli za kitalii ziitwe hivyo hivyo.
Hazikupita dakika nyingi simu ikaita, nikapewa maelekezo kuwa tayari mambo
yamesetiwa kitaalamu ni mimi tgu kama nataka kuoga.
Laiti kama ningekuwa na mahusiano na Nadia, siku
hiyo ningemsaidia kumwogesha. Hakika alikuwa amechoka sana, alikuwa amechoka
Nadia. Alistahili kusaidiwa lakini mimi nilibakia kuwa mwandishi tu. Alipoingia
bafuni name nikaenda chumbani kwangu. Nikajimwagia maji.
Baada ya muda tulikuwa tunatelemsha ngazi kuelekea
katika mgahawa mpana wa hoteli ya G & G. tukatafuta mahali tulivu
tukajiweka hapo.
Mara muhudumu akafika tukiwa tunapitia karatasi ya
orodha ya vyakula.
“Tutakuita” nilimweleza akajiondokea huku akiwa
anaendelea kutabasamu kama ilivyo kawaida ya wahudumu.
“Hivi hawa Capuccino (soma: kapuchino) yao itakuwa
murua.” Nilimuuliza Nadia ambaye alikuwa mwenyeji wa jiji la Mwanza.
Cappuccino ni kinywaji mchanganyiko wa kahawa na
maziwa na madikodiko mengine, mara nyingi kinapatikana katika hoteli za wazito.
Kwa mara nyingine Nadia akatabasamu, kisha kwa mara
ya kwanza kabisa Nadia akacheka, Nadia alicheka vyema na kwa mara ya kwanza
nikafanikiwa kutambua kuwa kabla ya matatizo Nadia alikuwa mrembo haswaa. Kubwa
zaidi alikuwa na mwanya katikati ya meno yake ya mbele.
Ebwanaa eee! Kilichofuata hapo ni kingine. Alianza
kwa furaha….
“Ina maana unanicheka Nadia au haitamkwi hivyo
jamani, hivi ni kapuchino ama kapusino…mi sijuagi hata” nilimweleza huku nikiwa
katika kufurahia tabasamu lake.
“Hamna inaitwa hivyo hivyo ila umenikumbusha dada
yake Desmund, mwenzangu!! mara yake ya kwanza kuiona hiyo Kapuchino sasa,
kwanza alikuwa haijui, hata Desmund mwenyewe alikuwa haijui lakini eti siku
hiyo akajifanya anaijua sana akamwambia dada yake aitamke, he! Akasema
kafufinyo wacha tucheke hadi nikapaliwa, maskini wifi yangu akawa amekodoa
macho tu. Sie tunacheka na Desmund wangu.
Mambo yanabadilika kweli jamani, wifi yangu Janeth
yaani alikuja huku mjini miguu imepasuka wewe sijui nd’o wanaita magwambala,
imepasuka haswaa, yaani dah! Mimi hata sikujali, alikuwa hajui kutamka maneno
mengine ya Kiswahili lakini yote mi nasema Mungu atanilipia, kweli Janeth mimi
nilimpatia nguo zangu, sikuona aibu kumfunza mambo mengi ya mjini hatimaye
nikamtafutia kazi akaanza kujitegemea kwa mshahara wake mkubwa tu. Mshahara
ambao kwa darasa lake la pili aliloishia angelipwa kwa mwaka mzima ama miwili.
Janeth hakuyakumbuka haya, Janeth akasimama kidete kabisa anamweleza kaka yake
eti mimi ni mchawi nimemwendea kwa mganga nimemwekea dawa, Janeth jamani yaani
nilipokosa kanga ya kujifunika huko kijijini kwao nikachukua kanga yake
akanikwapua na kudai nitaiwekea chawa kanga yake. Janeth ambaye alikuja mjini
akiwa ananuka mbuzi na ng’ombe nikampulizia marashi nikamkumbatia bila kujali
harufu yake, na yeye akasimama kunipinga, Janeth kweli nikaugua Malaria
akashangilia eti madawa ya mganga yamenirudia, mwandishi yaani mimi sijui
lolote kuhusu waganga , sijawahi kwenda Mungu aliye hai ananiona, sasa
nilimkosea nini mimi Janeth., na Desmund akanyanyua kinywa chake akadai dada
yake huwa hasemi uongo hata kidogo. Amakweli mfadhili mbuzi akikukera umle
nyama si mwanadamu, si mwanadamu nasema.
Mwandishi yaani kumbe kumtunza kote huko huyo
Janeth wala hakuwa dada yake na Desmund, eti kumbe ndiye yule mke ambaye alichaguliwa
na mama yake, kwa hiyo Desmund kumbe hakunipenda tangu zamani yule. Alinitumia
tu, sitaki kukumbuka pesa zangu alizotumia lakini kwa nini ameivuruga akili
yangu kwa kiasi kile. Desmund na Janeth ni wanadamu wa aina gani sasa hawa,
eeh!! Wanadamu gani msiojali kuwa Nadia hana ndugu mwingine katika dunia hii
mnaitwaa Roho yake mnaitwangatwanga. Si mngechukua pesa zangu zote, si
mnenidhulumu hata viungo vyangu iwapo vinafaa mkaniachia moyo na roho yenye
amani, mbona mkanitenda vile.
Yaani Desmund kweli ukamwachia huyo mwanamke wako
duka langu kubwa la nguo kisha ukanipeleka mimi huko kwenu mimi nikawe mvuvi wa
samaki, Desmund ukanikabidhi katika kundi la wanaume eti nijifunze uvuvi.
Desmund saa nane usiku mtoto wa kike ukaniacha ziwa Viktoria, desmund si heri
ungenipiga risasi mimi Nadia nife mara moja kuliko kuniua taratibu.
Nikayavumilia hayo yote hukujali, ukanikomaza mikono Desmund kwa kushika nyavu
na kuwavua samaki. Wewe na hawara yako mnatesa na mali zangu unaniambia ni dada
yako, shenzi kabisa Desmund, shenzi nasema. Na laiti ningejua mapema Desmund
wallah ningekufanyia kitu kibaya ujue, Desmund nilikustahi sana we mwanaume.
Ujue sitakiwi kulaumiwa mimi sitakiwi kabisa kulaumiwa basi tu lakini yaani
basi….
Unanikabidhi kwa wavuvi kisha wananitaka kimapenzi
ukaniita mimi Malaya eti ni mimi nawataka. Hivi Desmund nani alikudanganya kuwa
wewe na hao ndugu zako kuwa mlikuwa na mvuto wa kupagawisha msichana?? Basi tu
nilikupenda mimi Nadia, haukuwa na hadhi walau ya kunisimamisha na kuanza
kunitongoza hakika.
Lakini nafasi niliyokupa ukaamua uitumie vyema, eti
huyo unayemuita dada yako, na mama yako ambaye sipendi kutukana lakini ni mama
mjinga kupita wote duniani mnaniweka kikao na kunishutumu kuwa ninafanya umala
katika mtumbwi. Hivi mlikuwa na akili ninyi viumbe mlikuwa na akili Desmund.
Nakuomba nirejee kuuza dukani kwa sababu upepo wa
bahari unaniumiza kifua unanieleza kuwq mahesabu yatanichanganya hapo dukani
labda Janeth akipata muda anielekeze, Desmund ulikuwa umelewa siku hiyo ama?
Yaani Janeth aliyekuja na miguu imepasuika mjini wewe na yeye kwa pamoja hamjui
kapuchino wakati huo mnatumia pesa yangu, leo hii unaniambia eti sijui mahesabu
yatanichanganya. Hakika ulipitiwa na dharau ya hali ya juu. Na kama hiyo
haitoshi ndugu mwandishi Desmund, mama yake na huyo Janeth siku moja wa…….”
Kabla hajamaliza muhudumu alikuwa amefika,
tukamuagizia kapuchino mbili. Moja ya kwangu na nyingine ya Nadia.
Nadia akasitisha mazungumzo yake, akainama kwa
muda. Mimi nikjapiga funda moja la kapuchino kisha nikamsihi Nadia naye apate
kapuchino kabla haijapoa.
Akainua uso wake nikampatia kitambaa akajifuta
machozi kabla hayajatiririka.
Kisha akapiga funda moja kubwa.
“Si nilikwambia yaani hawa jamaa kapuchino yao
wanatumia maziwa freshi kabisha sijui wanayatolea kwa akina Desmund maana wana
mang’ombe mengi hao duh halafu yana afya kama nini…..” hapa alisema huku
akitabasamu.
Nilimtazama kidogo nikamjibu kwa tabasamu pia kisha
nikainama.
Nikajiwekea maswali na majibu mapya.
MOJA; Yaani Desmund na Janeth kumbe ni wapenzi
wakahudumiwa na NADIA jijini Mwanza….UNYAMA NA USHAMBA MKUBWA….
MBILI: NADIA binti wa kiarabu akapelekwa kuvua
samaki…HATARI hii lazima kulikuwa na kitu hapa.
TATU: NADIA alipogundua Janeth ni mke mwenza nini
kilitokea???
NNE: Mbona NADIA anadai hatakiwi kulaumiwa???
TANO: DESMUND, MAMA YAKE NA JANETH wapo wapi??
Nikapiga funda jingine kubwa la kinywaji kile cha
moto huku nikikiri kuwa hakika kapuchino yao ilikuwa maridadi kuliko baadhi ya
maeneo jijini Dar es salaam.
Nikamtazama Nadia naye alikuwa amejikita katika
kukifurahia kinywaji kile.
Kimya kikatanda…. USIKOSE NINI KITAENDELEA
Maoni 1 :
Maskini Nadia...mmh pole
Chapisha Maoni