Pages

Alhamisi, Julai 31, 2014

PONGEZI NYINGI KWA "Rais Kikwete kutunukiwa Tuzo ya Nyota wa Demokrasia Afrika"Rais Jakaya Kikwete kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo la kimataifa ya Nyota wa Demokrasia Afrika kwa mwaka huu. Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete, amekuwa mshindi wa kwanza na kuwaacha wenzake mbali katika mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia mwisho mchuano wa kuwania tuzo hiyo.

Katika barua iliyochapishwa na  Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida la The Voice, Pastor Elvis Iruh, akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, alisema uongozi wa Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio katika Bara la Afrika ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.

Tuzo hiyo hutolewa na Jarida la The Voice na mwaka jana mshindi alikuwa ni Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye alikuwa ni mshindi wa pili wa tuzo hiyo ambayo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwa Rais wa Kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.

Sherehe maalum ya kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika Oktoba 17, mwaka huu, katika Hoteli ya Van der Valk, iliyoko Almere, nchini Uholanzi.

Miongoni mwa sifa zilizopelekea Rais Kikwete kutunukiwa tuzo hiyo ni, kwa sababu ya kuwa msimamizi mzuri wa demokrasia, kuendelea kuhakikisha kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana katika eneo la Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na matatizo.

Aidha, gazeti hilo limesema Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa mfano kimataifa na kikanda na linatoa mfano wa mchango wake katika kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Kenya kufuatia uchaguzi mkuu wa 2007.

Rais Kikwete pia anasifiwa kwa mchango wake katika kusimamia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbali mbali kama kilimo, elimu, miundombinu, maendeleo ya viwanda, utalii na pia mchango wake katika kuendeleza vijana na kutoa nafasi nyingi kwa akinamama kushika nafasi nyingi za uongozi.

Jarida la The Voice pia limempongeza Rais Kikwete kwa kuimarisha umoja na Muungano wa Tanzania na kutoa nafasi kwa wananchi kujadili na kukubaliana kuhusu Katiba mpya ya Tanzania.

Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alitunukiwa tuzo la kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Afrika kwa mwaka 2013.
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom