SEHEMU YA KWANZA
Mwendo wa kutoka nyumba ya kulala wageni tuliyolal
usiku uliopita haukuwa mkubwa sana hadi kuifikia staendi kuu ya mjini Musoma
ambayo ujenzi wake ulikuwa unaendelea bado licha ya kwamba ilikuwa imeanza
kutumika. Mara yangu ya mwisho kuingia katika mji huo ambao ni makao makuu ya
mkoa wa Mara kituo cha mabasi bado kilikuwa kipo katikati ya mji.
TULIPOFIKA kituo cha mabasi tuliangaza huku na kule
huku tukikwepa usumbufu wa ‘wapiga debe’ wa kutuchagulia gari la kupanda huku
wakitoa sifa kedekede kuhusu gari wanalolipigia debe.
“Tupande Zacharia Coach” alininong’oneza binti yule
huku akinielekeza mahali zilipo ofisi zao. Tukajongea huku kila mmoja akiwa
ametundika begi lake mgongoni. Nilimsaidia kubeba kifurushi kimojawapo.
Baada ya kupata tikiti zetu mbili ambazo
zilituruhusu kuketi pamoja katika basi lenye hadhi ya V.IP, tulijongea upesi
garini japo muda wa kuondoka ulikuwa haujafika. Lakini hatukuwa na jambo lolote
la kutufanya tukae nje.
“Naomba nikae dirishani kaka” aliniomba,
nikamruhusu nami nikaketi mkono wake wa kushoto, hapa sasa niliweza kumchunguza
kidogo kwa macho ya kuibia ibia nywele zake jinsi zilivyokuwa zimenyonyoka,
huenda ni kwa sababu ya kukosa matunzo. Uso wake ulikuwa umechujuka na ile
rangi yake ya asili ilikuwa imetoweka. Alikuwa na mabaka mabaka yasiyokuwa
rasmi na ambayo nilikuwa sijajua sababu yake.
Nikiwa katika kumchunguza mara alinigeukia huku
macho yake yakiwa yanalengwa lengwa na machozi. Midomo ikimtetemeka, bila shaka
alikuwa anataka kusema kitu, ama la kuna kumbukumbu ilimjia. Ni hicho ambacho
nilikuwa nataka kutoka kwake.
Upesi nikafungua begi langu, nikatoa kijitabu
changu kidogo na kalamu kisha niitegesha na simu yangu upande wa kunakili
sauti. (sound recording).
Badala ya kusema neno alitazama nje pale dirishani,
nami nikachungulia na kukutana na wauzaji wa bidhaa ndogo ndogo, sikujua hii
inamaaanisha nini.
Binti yule akageuza kichwa na kunitazama sasa
alianza kuzungumza
AKAANZIA HAPA. Nami nikamrekodi huku kiuandishi
nikinukuu mazingira na muonekano wake ili nisipoteze uhalisia.“Mara ya kwanza kabisa nilikutana naye hapa,
alikuwa anauza maji na soda za kopo pamoja na biskuti. Sikuwa na mpango wa
kununua chochote lakini ucheshi wake ukanifanya ninunue soda ya kopo, huwa
sipendi kula nikiwa safarini. Sipendi kabisa. Sijui nini kilinivuta kwake,
nikanunua. Akatabasamu baada ya kuona amefanikiwa kunishawishi, wakati anataka
kunipatia chenchi yangu mara gari likaanza kuondoka, nilikuwa nimempatia
shilingi elfu mbili tu na alitakiwa kunirudishia shilingi elfu moja.
Nikamsikia
anapiga mayowe ya kuzuia basi lisiende anipatie pesa yangu, nilitamani kupiga
kelele kumwambia abaki na ile pesa lakini sikubarikiwa uwezo wa kupiga kelele.
Nilikuwa siti ya dirishani kama leo hii hapa, nikachungulia anapotokea ili kama
nikifanikiwa kumuona nimpungie mkono na kumuashiria kuwa sihitaji pesa ile. Na
kweli sikuwa na haja na pesa ndogo kama ile, nilikuwa na nyingine nyingi.
Lakini mara macho yangu yakashuhudia kitu kibaya sana kijana yule alijibamiza
katika basi jingine akapiga mweleka chini, maji na juisi zake zikatapakaa huku
na huko. Hapo sasa niliweza kupiga kelele huku nikiwa nimetaharuki. Yule kijana
alikuwa amepata ajali.
Safari yangu ikaharibika, nikawa namlilia mwanaume
nisiyemjua hata jina na ilikuwa mara ya kwanza kuonana naye. Nililia sana bila
kukoma, hakuna aliyeweza kunibembeleza maana ni moyo wangu ulikuwa unalia.
Walionitazama nje hawakujua lolote.
Laiti kama ningejua lijalo, nisingethubutu kununua
maji yake mwanahizaya mkubwa yule, nisingethubutu kusema naye na
nisingedanganyika na ucheshi wake hata kidogo. Yaani nikamlilia nikiwa hat
simjui lakini yeye akaja kuniliza huku akiwa ananijua kila kitu nje na ndani.
Akiwa anaijua historia yangu, ile siku analifukuza gari ili anipe chenchi yangu
kisha akagongwa na gari akaibadilisha na kuja kunifukuza mimi ili anipige.
Desmund! Desmund!! Hakufanikiwa kulipata gari alilokuwa akilifukuzia ili anipe
chenchi yangu lakini alifanikiwa kunipata Desmund akanipiga, tazama
alichonifanya (Hapa akajifunua kidogo blauzi yake upande wa bega…kidonda!!
Sijui niite jeraha…nikachukua kamera yangu nikampiga picha.)…..kisha akaendelea
tena “Desmund kweli aaargh!.....akanikanyagia chini bila huruma hata kidogo.
Siku alipogongwa na gari nilitoa kelele kidogo lakini siku hii nilitoa kelele
kubwa, hakukithamini kilio changu Desmund.
Akanitemea mate kisha akaniita
Malaya ninamtia kichefuchefu. Akaenda ndani ya nyumba, akaufunga mlango.
Nikalala nje kwa mara ya kwanza. Mvua kali ilinyesha yote ikatua katika mwili
wangu. Asubuhi alipoamka aaargh Desmund….hivi hakutosheka kunilaza nje ya
nyumba yangu. Hakuridhika kwa mimi kunyeshewa mvua, akaniamkia asubuhi na
kipigo, eti namdhalilisha na sikupaswa kuwa katika historia ya maisha yake!!
Yaani mimi…mimi niliyeibadili historia mbaya ya maisha yake leo hii anasema
sikustahili kuwa katika maisha yake…yaani kwa mambo yote niliyomfaanyia
mimi…akaniita mbwa ninayefaa kuishi na kula jalalani.” Hapa akashindwa
kuendelea alikuwa anatetemeka sana, uso wake ukawa mwekundu sana, mikono ikawa
inatetemeka na kisha akawa anatokwa jasho. Bila shaka alikuwa na hasira
iliyopitiliza. Upesi upesi nikahifadhi kamera yangu, ‘kinasa sauti’ na daftari
langu vyote pamoja na kalamu nikahifadhi katika begi.
“Usilie Nadia jamani!!” nikamchukua kichwa chake,
nikakilaza katika bega langu. Machozi yake yakawa yanatua katika shati langu.
Alipokuwa amenilalia niliweza kuyahisi mapigo yake ya moyo. Yalikuwa yanaenda
kasi sana. Na midomo ikizidi kumcheza cheza, nikajipapasa na kutoka na leso,
nikamfuta machozi yake huku nikikumbuka kuwa binti huyu ana kilio moyoni haya
machozi ya nje kwake si tatizo. Nikajikaza sana nisionyeshe udhaifu nami
nikatokwa machozi.
Maswali na majibu yalishaanza kurindima katika
kichwa changu.
MOJA. Kumbe jamaa anayehusika na hali niliyomkuta
nayo anaitwa Desmund!!
MBILI. Kumbe alikutana naye stendi akiwa masikini
wa kutupwa. Nini kikajiri sasa?
TATU. Baadaye wakaunda mahusiano? Waliunda vipi
sasa mahusiano wakati walionana na kuachana pale stendi?.
NNE. Jamaa aliwahi kumpiga? Kisa nini sasa. Tena
akamwita mbwa!!!
BAADAYE binti akanyamaza, sikutaka kuwa na papara
za kumuuliza maswali katika mfumo wa ‘Swali na jibu la papo hapo’ nilihitaji
zaidi maelezo ili nikiandika kitabu kiwe na mashiko ndani yake. Na ili kitabu
kiwe hivyo basi ni vyema msimuliaji aamue mwenyewe kusema bila kuulizwa. Ama la
mwandishi atumie mbinu zake ili msimuliaji ajibu bila kujua kama ameulizwa.
“Hii barabara yenu imenyooka sana….” Nilimgusia ili
asikumbuke machungu ya alichokuwa anasimulia awali juu ya jinsi alivyokutana na
Desmund.
Alinijibu huku akiwa amechangamka, lakini sikujua
kama swali langu linaweza kuleta athari kwake!!
“Ndio ni nzuri lakini zamani sasa dah! Palikuwa na
mashimo mashimo, sikudhani kuwahi kutegemea nitakuja kupita barabara kama hii.
Mwaka ule ninakuja huku palikuwa hapapitiki, mimi nilidhani kuwa nilipoondoka
kuwa sitarudi tena huku hata rafiki zangu niliosafiri nao kipindi kile
walinambia ‘Nadia hutaweza wewe mtoto mayai’ …nilicheka tu huku nikilazimisha
kuwa nitaweza. Ilikuwa haki yao kusema kuwa sitaweza, mimi mzee wangu amenidekeza,
sio mimi pekee hata dada na kaka zangu wote walidekezwa sana yaani, sijui hata
pale nyumbani nilikuwa nakosa nini. Shuleni napelekwa na gari na kurudishwa
hivyo hivyo, nilipoingia chuo na kuchaguliwa kusomea Mwanza, sikuwahi kupanda
basi kila likizo ni ndege kila likizo ndege tu. Si kwamba sikuyafurahia maisha
yale la! Ila kwa kiasi fulani yaliwafanya rafiki zangu wanione mimi mzembe na
ndo maana hata rafiki yetu alipofiwa na baba yake huko Mugumu Serengeti nami
niliposema kuwa naenda kumsindikiza walinambia kuwa ‘Nadia huko hakuna ndege
wala uwanja wa ndege’ baki tu.
Sikukubaliana nao kirahisi, ule ulikuwa msiba.
Nikalazimisha nikaenda, huko Dar es salaam, baba na mama hawajui lolote. Nd’o
nikaujua uchungu wa kupanda basi tena barabara mbovu. Kutoka Mwanza hadi Musoma
hapakuwa na tatizo lakini kutoka Musoma kuelekea Serengeti, nilifika nikiwa
mgonjwa lakini sikutaka kudeka ule ulikuwa msiba nilikunywa dawa za kutuliza
maumivu kisha nikalala, nilikuwa msichana pekee mwenye asili ya kiarabu katika
msiba ule.
Maisha ya kule yalinishinda lakini nilivumilia,
ukarimu wa watu niliowakuta kule ulinipa faraja nikayasahau machungu. Siku
tuliyoondoka ndo niliapa kuwa sitakanyaga kule tena kwa namna yoyote. Rafiki
zangu walinitania kuwa naweza kupata mchumba kutoka huko itakuwaje niliwajibu
kuwa ni heri nisolewe kabisa. Lakini cha ajabu sasa ambacho hadi leo
ninakishangaa nilipofika Mwanza nilirudi peke yangu tena kule Musoma, kwa lengo
ambalo hadi wakati huu sijui shetani gani alilileta kwangu, nikarudi Musoma kwa
ajili ya Desmund.
Desmund kijana aliyeniuzia maji kisha akapata
ajali. Nilishuka pale Musoma na kuanza kuulizia huku na kule, lilikuwa limepita
juma moja tu tangu ajali ile itokee, hivyo taarifa zilikuwa zimezagaa.
Nikafanikiwa kumwona tena.
Alhamdulilah!! Alivunjika miguu yote miwili, na
mwajiri wake alikuwa hayupo tayari kumuhudumia, na tayari alikuwa ametafuta
kijana mwingine kwa kazi ileile. Alikuwa amedhoofu sana, na matusi kutoka kwa
madaktari kuwa watamfukuza pale hospitali kwa sababu hakuna ndugu anayefanya
malipo yoyote. Sikungoja zaidi, nilifanya malipo kama yalivyohitajika, bado
alikuwa akinishangaa kuwa mimi ni nani. Huduma ikaboreshwa, nilikesha pale
wodini nikizungumza na naye na ni siku hiyo aliponiambia jina lake. Desmund!!
Nilikesha nikiumwa na mbu mimi, nikajitoa kwa moyo
wote japo ajali sikuipanga mimi, lakini yeye aliponipiga na na mpini wa jembe
akanivunja mguu aliniacha nikilia peke yangu barabarani, yaani kweli Desmund
mimi kukuuliza tu yule mwanamke ni nani ukanipiga hadharani aah. Wema wote
niliouonyesha kwake, uvumilivu wote nilioufanya kweli akaishia kunikana
hadharani kwamba nilikuwaga demu wake tu lakini tumeachana tayari. Watu
nisiowafahamu wakaniokota na kunipeleka hospitali nikiwa sina hili wala lile
Desmund hakuja kunisalimia, hakuja kulipa bili nilizokuwa nadaiwa. Kale kasimu
kangu nikaamua kukauza ili nipate tiba kwa mguu wangu uliokwisha teguka.
Nilisaidiwa kurudi nyumbani baada ya kupata nafuu huku nikitumia mpini wa jembe
kujikongoja…yaani Nadia mimi nikafikia kumkufuru Mungu sasa. Ndani ya chumba
changu kitanda changu ninacholalia na Desmund wangu..nikakuta chupi na sidiria
..havikuwa vya kwangu. Kwa hiyo kumbe Desmund….De…De…” akashindwa kusimulia
kilio kikaanza tena wakati huu safari ilikuwa inaendelea. Upesi nikahifadhi vifaa
vyangu. Nikamchukua na kumlaza katika mapaja yangu, nikausikia mwili wake wa
moto ukizidi kuchemka.
“Usilie Nadia…yamepita hayo mpendwa wangu…USILIE
NADIA….USILIE” nilimsihi kwa upole na sauti ya chini…….
Wakati huo kichwani yakifuata maswali kadhaa na
majibu.
MOJA. Kumbe Nadia alikuwa mtoto wa familia bora?
Sasa kulikoni mbona kachakaa kiasi kile.
MBILI. Kumbe Desmund alikosa wa kumuhudumia
akatunzwa na Nadia, sasa mbona akamvunja mguu? Nadia alikuwa na kasoro gani
kwani.
TATU. Halafu Desmund akaleta msichana nyumbani
kwake? Hivi ilikuwa maksudi? Mpuuzi sana huyu. Halafu kumbe nd’o chanzo cha
kumpiga kisa kuulizwa yule msichana ni nani? Au huyu alikuwa mwingine?
NNE. Hivi Nadia na kuchakaa kote huku kumbe ana
elimu ya chuo kikuu tena chuo chenyewe kikuu kwelikweli!!! Sasa mbona hafanyi
kazi!!
TANO. Familia yake ilikuwa wapi huyu bwege
anamnyanyasa hivi? Na ni mkoa upi huo waliishi?? USIKOSE SEHEMU YA PILI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni