Pages

Alhamisi, Julai 17, 2014

Ugomvi wa mipaka ya Mashamba "Mwanamke auawa kwa kucharangwa mapanga"Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Milembe Masanja (50), ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Muhida, Kijiji na Kata ya Busangi, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, ameuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga kichwani na mikononi na watu wawili, wanaodaiwa kukodiwa kufanya mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Julai 14, mwaka huu, saa 2.00 usiku.

Aliwataja waliofanya mauaji hayo kuwa ni Chuchu Lugodisha na mwenzake, Ngeja Kugodisha, ambao wote ni wakazi wa Kijiji cha Izumba, Kata ya Luguya, mkoani Tabora.

Alisema watu hao walikodiwa na Madaha Luhemeja ili kufanya mauaji hayo.Ilielezwa kuwa familia ya marehemu ilikuwa na ugomvi wa mipaka ya mashamba na familia ya Luhemeja.

Hata hivyo, Kamanda Kamugisha alisema watuhumiwa wote watatu walikimbia baada ya mauaji hayo na Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali kuwakamata.

Alisema kufuatia mauaji hayo polisi mkoa wa Shinyanga inawashikilia watu watatu kwa mahojiano.

Watu hao ni Pili Paulo(37), Juma Paulo (19) na Daudi Ngassa (57), ambao ni wote wakazi wa Busangi, Wilaya ya Kahama.

Kamanda Kamugisha aliwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watu wanaofanya vitendo vya mauaji kwa kukata mapanga baada ya kukodiwa.
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom