Pages

Jumatano, Agosti 06, 2014

Kasi hii ya maambukizi ya ukimwi bado tishioUgonjwa wa ukimwi bado ni tishio kubwa nchini na kwingineko duniani. Kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu imeendelea kuwa kubwa na hili linadhihirishwa na takwimu mpya kuonyesha kuwa hadi sasa, watu milioni 75 duniani kote wameshapata maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa huo.

Taarifa za kitaalamu zilizotolewa katika mkutano wa 20 wa kimataifa wa ukimwi duniani uliofanyika hivi karibuni nchini Australia zinaonyesha kuwa miongoni mwa makundi ya watu walio katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo ni wafanyakazi wa migodini, wavuvi na watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Wengine waliotajwa kuwa hatarini zaidi ni pamoja na wafungwa, watu wanaojidunga dawa za kulevya, wafanyabiashara na madereva.

Faraja pekee kwa Watanzania ni kuwapo kwa taarifa kuwa taifa lao ni miongoni mwa nchi 26 duniani zilizoonyesha kupiga hatua katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo baada ya Tanzania kutajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye mwelekeo mzuri kwa kuwa na maambukizi yaliyopungua na kufikia kiwango cha asilimia 33. Inaelezwa zaidi kuwa karibu watu milioni 13 kutoka nchi zinazoendelea wamepata dawa za kupunguza makali ya ukimwi (ARVs), hivyo kuokoa maisha ya watu milioni 53 duniani.

Kwa takwimu hizi, NIPASHE tunaona kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Ni kweli kwamba uelewa kuhusu ukimwi umeongezeka kwa kiasi kikubwa kulinganisha na mwanzoni mwa miaka ya 1980 wakati ugonjwa huo ulipogundulika. Hata hivyo, idadi ya watu wanaoambukizwa na pia wale ambao tayari wangali wakitumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huu inaonyesha kuwa mapambano dhidi ya ukimwi yanapaswa kuendelezwa kwa kasi kubwa zaidi.

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapaswa kushirikiana zaidi na wadau wake mbalimbali katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huu.

Kwa mfano, mpango wa kuendelea kutoa elimu juu ya namna uambukizwaji wa ukimwi unavyotokea na pia mbinu sahihi za kuepukana na maradhi hayo unapaswa kuwa endelevu. Wananchi, hasa wale wanaotajwa kuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi haya wanapaswa kukumbushwa juu ya athari zitokanazo na ugonjwa huu, kwa kuamini kuwa baada ya hapo watakuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukimwi.

Kuugua kwa muda mrefu ni baadhi ya athari za ugonjwa huu. Vifo pia huletwa na ugonjwa huu na hivyo, mwisho wa siku hupunguza nguvu kazi ya taifa. Isitoshe, serikali hujikuta ikitumia kiasi kikubwa cha fedha katika kukabiliana na ukimwi. Matokeo yake, jitihada za kukuza uchumi hupata pigo.

Athari hizi za kiuchumi hugusa pia ngazi ya familia kwani baada ya vifo vitokanavyo na ukimwi kuongezeka, ni wazi kuwa watoto wengi hukosa malezi ya wazazi wao. Wanaachwa wakiwa yatima.

Yote haya yanapaswa kuepukwa kwa kuhakikisha kuwa vita dhidi ya ukimwi inaendelezwa kwa ari zaidi, kasi kubwa na nguvu ya ziada itakayofanikisha ushindi dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu.

Pamoja na kuwapo kwa taarifa za kutia moyo kuwa kasi ya maambukizi ya ukimwi imeanza kupungua, NIPASHE tunaona kuwa hili peke yake halitoshi kupunguza kasi ya mapambano.

Aidha, sisi tunaaminin kuwa matendo ya baadhi ya watu yanadhihirisha vilevile kuwa bado kuna haja ya kuzidisha mapambano katika vita dhidi ya ukimwi.

Kwa mfano, ni kawaida kuona kuwa katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, hasa nyakati za usiku, kuna watu huweka kando ubinadamu wao na kujiuza miili kwa minajili ya kujiingizia kipato. Hawa hugeuza ngono kuwa biashara. 

Kuna kundi jingine kubwa pia la watu wasiojali tahadhari nyingi zinazotolewa kila uchao kuhusiana na ukimwi. Wanajihusisha na uhusiano wa kimapenzi na watu zaidi ya mmoja.

Hii ni hatari. Watu wa aina hii huhitaji kukumbushwa zaidi juu ya madhara wanayoweza kuyapata. 

Na kama takwimu zinavyoonyesha, hali huwa mbaya zaidi kwa watu wanaotumia muda mwingi wakiwa kwenye maeneo ya mbali na familia zao, hasa wavuvi, madereva, wachimba madini na madereva.

Jitihada zaidi ziendelee kutolewa kwa watu wa aina hii wanaojitwalia wapenzi wapya kila uchao. Kwa ufupi, taarifa hizi za kuendelea vyema kwa Tanzania katika vita dhidi ya ukimwi zinapaswa kuwa chachu ya mapambano zaidi. Kamwe tusibweteke.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom