SEHEMU YA NANE
Mlo unaoitwa ‘mlo kamili’ uliletwa katika meza yetu
ambayo kwa maksudi kabisa tuliiacha izungukwe na viti viwili ili tuwe na uhuru
wa kufanya mambo yetu. Hasahasa mazungumzo maana tulihitaji kuwa na faragha kwa
kila kitu tulichokuwa tunafanya. Nadia alipitia orodha ya chakula, safari hii
tuliagiza chakula cha kufanana.
Sato na ugali wa dona!!
Hakika Nadia alikuwa na njaa!!
Mbaya zaidi hatukuwa tumepata kifungua kinywa
asubuhi ya siku hiyo. Kila mmoja akajikita katika sahani yake na
kushambulia awezavyo, mara kwa mara nikimtupia jicho Nadia niweze kupata kitu
cha kuandika hasahasa katika muonekano. Sikutaka kupitwa na tukio hata moja,
hata jinsi anavyomeza chakula nilitaka kufahamu ili nikiandika kitu niwe
nimeandika kitu chenye uhalisia na safari yangu hii iwaridhishe waliokuwa
wanaifahamu na hata pesa zao waone zimeenda kiusahihi kabisa.
Nikiwa nimefikisha ugali wangu nusu ya safari huku
samaki aina ya sato akiwa ameteketea upande mzima na macho ya samaki huyo
yakiwa wazi yakinitazama. Niligutuka kuwa Nadia alikuwa amesita kula na alikuwa
akiangaza macho huku na kule.Nilimtazama kwa kwa sekunde kadhaa kisha akaonekana
kupata kitu alichokuwa akikihitaji, akanyanyua mkono wake akapunga hewani.
“Nini tena Nadia…mbonaa….” Nilimuuliza huku
nikiitazama sahani yake. “Mwenzangu, nimeshiba kama nini?” “Nadia umeshiba, yaani hivyo vitonge viwili tu
Nadia hebu acha utani wewe.” Nilijaribu kubishana naye, wakati huo yule mtu wa
kunawisha alikuwa amefika tayari akaanza kunawa mikono.
Nikakosa la kusema!!
“We acha huyo samaki hapo bwana!” nikamzuia yule
muhudumu,tamaa zilikuwa zimeniingia tayari, na pia ubahili wa kumlipia samaki
yule mkubwa kisha Nadia hata upande mmoja hakuwa amemaliza.
Muhudumu akanitazama kwa jicho la chuki lakini
midomoni akatoa tabasamu lao la kawaida. Sikujali kuhusu hilo.
“Lakini Nadia..yaani samaki ndo umedonoa hivyo?”
nilimuhoji, kisha nikaendelea,”Au waifungashe tukaisonsomole chumbani”
Nadia akalipuka kwa kicheko baada ya mimi kutumia
neno lile maarufu sana kwa wasukuma jijini Mwanza na mkoani Shinyanga.
Wakimaanisha ‘kula katika namna ya kufurahia’
“Ujue zamani nilikuwa nakula sana, huyo samaki huyo
mbona hata robo tatu ningeweza kumfikisha mimi mwenyewe,unadhani mi huwa nina
aibu katika kula, nakula sana tu lakini huwezi amini zamani niliambiwa kuwa mtu
ukiwa umezoea kula chakula kidogo sana pasi na matakwa yako basi unajikuta bila
kujua tumbo linajibana na kuwa dogo siku ukijaribu kula chakula kingi
haiwezekani.
Sikuwahi kuamini, lakini maisha niliyoishi Musoma
Vijijini huko yalinifanya niamini kuwa haya mambo yapo. Ile familia ya mzee
Marwa ile, basi tu Mungu hakuwapa utajiri. Hakuwapa mali na dhiki zote
akaziacha juu yao sijui kwaninihata. Ujue bila wao Nadia mimi ningekuwa
nishakufa zamani sana, yaani zamani sana mwandishi. Sawa walikuwepo wanafamilia
na mapungufu yao lakini hakika mzee Marwa ni mtu mwema sana japo najua
ananichukia sana!!!
Dah! Safari ikiwa una nia mbaya nayo hakika unaweza
kuwavurugia hata wengine ambao hawana nia mbaya, yaani jinsi nilivyokuwa
nakereketwa hapa kooni, jinsi nilivyokuwa nina hasira nikiwa ndani ya basi.
Yaani ilikuwa sawa kabisa mwandishi, yaani kila mtu nilikuwa na hasira naye
ndani ya gari. Kila mwanaume nilimuona kama Desmund ama Ramso Rama, na kila
mwanamke alifanana na mama yake Desmund huku wasichana wakimfanania yule wifi
feki mwanaharamu kabisa. Aliyenigusa nilijikuta natoa tusi zito, kondakta akiwa
wa kwanza kisha akafuata abiria ambaye alinigonga bahati mbaya, nikamtapikia
matusi ilhali nikijishangaa japo sikuweza kujizuia.
Abiria niliyekaa naye siti moja pia aliipata moto
moto ya matusi huku nikitishia kupigana. Watu wakadhani huenda
nimechanganyikiwa. Wakaamua kunisusia!!
Safari za usiku sijui kama zina raha yake, lakini
nililazimika kusafiri usiku,niliondoka Mwanza na gari ya mwisho kabisa kuelekea
Musoma. Sikutaka hata mtu mmoja auone uso wangu. Hofu ilinitawala sana, hofu ya
kukamatwa kwa kesi ya mauaji jijini Mwanza hivyo niliamua kusafiri usiku.
Baada ya basi zima kuwa limenichukia mimi naye
niliendelea kuchukia zaidi.
Ni basi kuwa Mungu alituzibia namna ya mtu kuweza
kuona mambo yaliyo katika moyo wa mwenzako. Lakini abiria wangeuona moyo wangu
jinsi ulivyobeba uchungu mzito hakika wangelia na kusaga meno, wanaume
wangejilaani huku wanawake wakiinama kwa aibu.
Lakini hawakujua haya yote, nilipoanza kulia ghafla
ndani ya gari, wakatambua kuwa ukichaa unaanza kunipanda, nikiongea peke yangu
jirani yangu anasogea pembeni kidogo ili nisimdhuru. Hali hii haikuwa njema
hata kidogo!!
Hatimaye jirani alipopata upenyo wa kupita
akatoweka asirejee tena, siti ya watu wawili nikabaki peke yangu.
Nililia sana, kila mmoja alinitafsiri alivyojua ye
mwenyewe mi sikujali tena hayo.
Hatimaye ukafika ule muda wa kutengwa, muda ambao
ulinikutanisha na familia nyingine kiajabu ajabu.
Familia ya mzee Marwa!!
Mwendo wa basi ulianza kupungua, kisha waliokuwa
mbele wakaanza kutishia amani kwa , maneno yao.
“Tumetekwa…..tumetekwa jamani. Majambazi weeee!!”
Alilalamika mwanaume mmoja.
“Mwanaume wewe acha hofu za kijinga jinga nani
kasema tume…” kondakta alibwata lakini hakuimaliza kauli yake. Mara kweli
tukawa tumetekwa.
Kwanza ikapigwa risasi, bila shaka hewani, lakini
kwa wakati ule kila mmoja angeweza kuisikia ikiwa imelia katika sikio lake na
labda kujihisi amekufa.
Hata mimi nilihisi nimekufa lakini nikajishangaa
kuwa nipo hai katika kiti kilekile, cha ajabu sasa wale abiria waliokuwa
wamenikimbia kwa kuhisi mimi nina wazimu, wengi walikuwa wamenikumbatia bila
uoga. Wanadamu bwana, hapa huja ile kauli kuwa panapo matatizo wengi
watakukimbilia wewe lakini uwapo na tatizo basi watakukimbia wao na usiwakamate
katu!!
Mimi sikuwakimbia, na ningeweza vipi kuwakimbia
iwapo walikuwa wameniegemea? Basi ukawa mshike mshike!!
Kwangu mimi kidogo ilikuwa salama, mara ghafla
msukumo ukazidi kisha nikaanza kusikia milio ya ajabu ajabu akina mama wakilia
na wanaume wakilalamika kwa maumivu. Jicho langu likafanikiwa kuona panga si
panga jambia si jambia.
Kaka, usiombe kuona ninachokuhadithia mara
likanyanyuliwa likashushwa, waaa!! Damu pwaa!! Mkono chini!! Abiria kanyofolewa
mkono!!” Nadia akasita akanitazama machoni, bila shaka alitaka kutambua kama
nimeguswa na kipengele kile, wacha wee alichokiona anajua yeye, maana mimi kama
mimi japo sijioni nilijua kuwa nimekodoa macho sana. Inatisha msomaji!! Mkono
kuondolewa!! Eti panga si panga jambia si jambia!! Nadia bwana!! Akaendelea!!
“Watu wakapiga mayowe mimi nikiwa hata uwezo
kufungua mdomo sina, wakinamama wakazidi kunilalia, mara jicho langu likaiona
panga si panga jambia si jambia likinyanyuliwa tena, mara likatua. Safari hii
mlio uliotoka ni paa!! Mwanamama akapiga mayowe alikuwa amepigwa na ubapa wa
maana!! Uzito ukaanza kupungua mimi nikiwa sijui nitafanya nini, kumbe ni mmoja
baada ya mmoja anatolewa nje.
Nami nikafikiwa, kabla ya kuvutwa nikatoka
mwenyewe, nikaenda nje upesi, maana wale waliojichelewesha walipigwa na ile
panga si panga jambia si jambia. Niliposhuka ndani ya gari nikavutwa, kushoto.
Ndani ya sekunde kadhaa nilikuwa uchi wa mnyama.
Nikasukumwa huku nikiona aibu huku aibu ikaniisha,
kila abiria alikuwa uchi wa mnyama.
Kilikuwa kizaazaa. Wakati huo sasa wimbo wa mtaji
wa masikini ule wa msanii gani sijui ulikuwa upo bado.
Wale majambazi au watekaji walikuwa wanao,
wakawasha redio, Banza Stone…eheee!! Nimemkumbuka Banza anaimba kwenye redio
sisi tunacheza uchi. Tena tulitakiwa kucheza kwa bidii huku kila mara mmoja
wetu akiingia katikati kunengua mauno. Wakati tunaendelea kucheza ikafika zamu
ya dereva kukata mauno, kama ingekuwa filamu hakika ningecheka maana dereva
alikuwa kibonge na ana tumbo kubwa!!.
Dereva kibonge, akagoma. Mwandishi ujue alikuwa
jirani yangu sana, nilimsihi, nilimsihi akubali yaishe, sijui kama alidhani
bado nina wazimu wa kwenye gari lakini mimi nilikuwa nimeona kitu. Mwandishi
niliona macho yanayofanana na ya marehemu Jaduda. Macho yasiyokuwa na utani na
yanayomaanisha yanachosema. Yule jambazi hakuwa katika utani!!!
Kilikuwa kitendo cha sekunde kadhaa yule mwanaume
jambazi ambaye alikuwa akionekana macho tu, aliruka na panga si panga, jambia
sijambia.
Ohooo!! Damu ya mwanadamu ni ya moto sana aisee!!,
damu ya dereva ikanirukia, alikuwa amechomwa bisu la tumboni.
Wacha watu waanze kupiga mayowe wakilia huku Banza
Stone akizidi kuimba mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe…..nasi tukitakiwa
kucheza. Huku mwenzetu mmoja akipigania uhai bila dalili yoyote ya
kufanikiwa!!!
Ilitisha kutazama!!!
Baadaye tukaamriwa kulala chini kifudi fudi, sasa
hakuna aliyebisha kila mtu alilala hivyo. Kimya kikatanda, redio ikiendelea
kuimba kuwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe. Sisi tumelala kifudifudi.
Uchi wa mnyama….tochi mbili zikitumulika. Tuakendelea kutambua kuwa wale
majambazi wapo nasi!! Nusu saa ikakatika.
Mbwa waliokuja kutubwekea na kisha kumng’ata mmoja
wetu akapiga mayowe ndio walitukurupua tena……
Kila mmoja akaanza kuhaha akitafuta namna ya
kujistiri na hali ile.. Wengine walikuwa na watoto wao, wengine na wake zao,
huenda na wengine na baba mkwe zao.
Kizaazaa!! Nani atajali katika hali hii???
Huyu avae ya huyu mara huyu avae ya huyu. Hapakuwa
na umoja, huenda hicho kitu ndio kilisababisha hata tukashindwa kuelewana, mtu
mmoja akavaa nguo yangu nilipomshika akanitukana akidai mimi ni kichaa.
Umoja ukajengeka, wakamuunga mkono kuwa mimi ni
kichaa na sijui ninachokiongea, wengine wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa ni
mimi nimewazulia balaa lile la aina yake.
Mara nikatengwa maneno yakawa maneno!! Mara
nisukumwe mara nitukanwe!! Hakuna aliyekuwa nani mwandishi!! Hakuna hata
mmoja!!
Ile nguo aliyoing’ang’ania yule dada ndio nguo
ambayo ilikuwa ndani yake nimeishonea ile pesa yangu niliyomuibia marehemu bosi
wa Mwanza….na niliamini kuwa lazima itakuwemo, nilishona kwa ustadi mkubwa
sana. Wale majambazi wasingeweza kuiona!!
Mwandishi Ni heri ningekaa kimya tu nisijibizane na
umati ule …..ni heri ningekubaliana na usemi wa mwenye nguvu ndo mwenye haki.
Nilikosea sana kuthubutu kuongea….nilikosea sana
kuidai haki yangu……” kilichotokea ……JE NINI KITAENDELA USIKOSE.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni