Pages

Jumatano, Agosti 13, 2014

SIMULIZI YA BADO MIMI SEHEMU YA 29 ENDELEA KUPATA UHONDO


Mdau unaweza kujikumbusha 
ILIPOISHIA
Baadaye Charito alirudi na nilimsimulia hali halisi na kile alichokiona Tumaini. Alibaki akiwa anashangaa "Haiwezekani mmmh mambo gani haya itabidi tuende kuonana na mchungaji" Alisema Charito huku akiwa ananitizama.Tulikubaliana ni vyema kwenda kuonana na Mchungaji Mkombozi ili aweze kutusaidia. Binafsi nilikuwa na hofu zaidi kutokana na  ujauzito niliokuwa nao. Baada ya mwezi mmoja tukiwa tunaendelea na maisha. Siku moja mume wangu alikuja akiwa amebeba chupa ya juisi amabapo alifika na kunimiminia kwenye kikombe kisha alinipa "Mke wangu hii juisi ni nzuri sana  kwa hali yako kwani inasaidia kuongeza damu mwili, si unajua, Mama mjamzito anatakiwa kuwa na damu nyingi"Charito alizungumza huku akitabasamu.Nilikunywa ile juisi yote ilikuwa na harufu nzuri sana ya zabibu. Kila siku Charito alikuwa akiniletea juisi.

Ilipita kama wiki moja, siku hiyo nilikuwa nimepumzika peke yangu, huku nikiwa natizama tamthilia. Ghafla tumbo lilianza kuniuma sana "Mama yangu, uwiiii, aaaah aaaah , Mamaaaaa, mbona tumbo linauma hivi. Eeeh Mungu wangu, maumivu yanzidi." Yaani nilikuwa nasikia maumivu makali sana, pale nyumbani kulikuwa hakuna mtu zaidi ya mdogo wangu Renata. Maumivu yalinizidi hatimaye damu zikaanza kunitoka kwa wingi, niliogopa huku nikilia kwa uchungu. Renata alikuja na kunishika huku akipiga kelele kuomba msaada. Majirani walikuja na kunibeba haraka kunikimbiza hospitalini. JE ...NINI KITAENDELEA USIKOSE...SEHEMU YA ...29...

INAPOENDELEA
Nilihangaika sana kumtafuta Tumaini siku hiyo, bila mafanikio na Charito alizunguka huku na kule lakini hakumpata Tumaini, Nilikosa amani kabisa na sasa tuliamua kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi ambacho kilikuwa karibu na maeneo yale. Usiku ulikuwa mrefu sana kwani nilikuwa nawaza mdogo wangu atakuwa ameelekea wapi “Siwezi kuamini naona kama ni ndoto siamini kama Tumaini ametoweka kusikojulikana, sijui atakuwa wapi eeh Mungu Tusaidie”.

 Nikiwa naendelea kuwaza usingizi mzito ulinipitia, nikiwa usingizini nilisikia sauti ya mtoto ikiniita “Dada Kandida, njoo, Dada Kandida njooooooo” Nilishtuka sana huku jasho likinitoka kwa wingi niligeuka huku na kule na kumtizama Charito ambaye alionekana kulala fofofo, nilinyanyuka pale kitandani na kuanza kuifuata sauti niliyokuwa naisikia ikiniita, kwani nilijua atakuwa ni Tumaini, nilikuwa natembea huku nikitetemeka kwa hofu. Baada ya kufika sebuleni, ghafla alitokea Renata nilishtuka sana na kumtizama, alionekana kuwa na hofu "Dada, dada nimesikia sauti ya Tumaini, yuko wapi Tumaini".


 Nilibaki nikiwa namtizama Renata bila ya kujibu chochote huku moyoni mwangu nikijisemea "Inamaana Renata ameota ndoto niliyoiota mimi, Mungu wangu  Tumaini atakuwa amepatwa na kitu gani?" Tukiwa tumesimama pale sebuleni ghafla ilisikika sauti ya Tumaini akicheka kwa sauti kali, Rena alisogea na kunikumbatia kwa nguvu, kisha akasema "Dada Kandida Tumaini atakuwa amejificha kwenye kabati mimi naisikia sauti inatoka kule kwenye kabati" Taratibu nilitembea huku nikiwa na hofu kuelekea kwenye kabati, Renata alikuwa anaogopa na kwa wakati huo ilikuwa ni majira ya saa nane za usiku, nilipofika pale kwenye kabati nilifungua mlango lakini sikumuona Tumaini." Nilibaki nimepigwa butwaa kwani sasa nilikuwa nawaza ile sauti inatokea wapi na kama ni Tumaini kwanini amejificha, yaani nilikuwa nawaza na kujiuliza maswali bila kupata majibu. Wakati tukiwa tunaendelea kusubiri pale sebuleni,Ulisikika mlango wa kutokea nje ukifunguliwa, nilipata hofu na kumshika mkono Renata na sasa nilitaka kutimua mbio, Kabla hata sijageuka ule mlango ulifunguliwa na aliingia Tumaini  akiwa ameongozana na Charito. 

Nilishtuka sana na kusema "Eeeh Charito si ulikuwa umelala, mbona umetoka nje na Tumaini umempatia wapi? Nilikuwa naongea kama mtu aliyechanganyikiwa, "Charito alisogea na kunishika mkono huku akiniondoa wasiwasi "Usiwe na hofu mke wangu, wakati wewe unatoka nje na mimi nilikufuata, na nilipoisikia sauti ya Tumaini ilinibidi nimfuate nje haraka kwa kupitia mlango wa nyuma"Alisema Charito huku akionyesha tabasamu pana usoni mwake, Renata alinitizama na kumtizama Charito kisha aligeuka na kumshika mkono Tumaini "Ulikuwa wapi Tumaini? Mbona umetusumbua sana, kwani tumekuwa na wasiwasi mwingi hatukujua tutakupata wapi?".

Tumaini alinyamaza kimya bila kujibu chochote, na ghafla akaanza kulia "Dada nisamehe sintorudia tena, nilienda kucheza na watoto nikapotea hivyo nikashindwa kurudi nyumbani, Nisamehe dada" Nimtizama na kumkumbatia kwa nguvu "Usijali mdogo wangu, Nimefurahi sana umerudi nyumbani, tafadhali usiwe unaenda kucheza mbali na nyumbani" Baadaye wote tuliondoka na kuelekea chumbani kupumzika kwani tayari ilikuwa ni usiku wa manane. Kesho yake asubuhi na mapema, Charito aliamka na kuniaga kuwa anakwenda kazini. 

Baada ya Charito kuondoka, Renata alinifuata huku akionekana kama kuna jambo anataka kunieleza. Alinisalimia na kisha akawa anaendelea kunitizama, kutokana na hali ile ilinibidi nimuulize "Vipi, Renata mbona unanitizama kama vile kuna jambo unataka kusema" Renata aliguna kidogo na kusema "Unajua Dada, siku zote nasema "Jambo usilolijua ni sawasawa na usiku wa kiza kinene, na inanisikitisha sana kuona wewe dada yangu hutaki kuniamini kile ninachokuambia...na" 

Kabla hajamaliza kuzungumza nilimkatisha na kusema "Wewe mtoto, umekuwa ni mtu wa kunifundisha methali mimi, khaa, na pia usitake kuzungusha sana maneno, sema ulichokuwa unataka kunieleza " Rena alinitizama na uso uliokosa furaha na kusema "Dada Kandida hivi tukio la kupotea Tumaini, na hadi alivyopatikana, umelionaje, na pia hufikirii kuwa shemeji Charito anahusika katika kupotea kwa Tumaini, Dada tafadhali nakuomba fungua macho yako uone, mimi nakueleza ukweli shemeji siyo mtu mzuri, fikiria dada yangu mambo yote niliyokueleza" Nilinyamaza kimya kidogo na kutafakari jambo moyoni mwangu "Hivi inawezekana kweli, Charito akawa siyo mtu mzuri, yaani ni mchawi, mmmh lakini mbona kumekuwa na mambo ya ajabu sana".

 Nikiwa nawaza moyoni bila kuongea chochote Renata alinishika mkono na kusema "Dada dada, hivi unanisikia kweli?" Nimtizama na  kwa sauti ya upole nikasema "Nakuelewa mdogo wangu, itabidi niwe makini sana, lakini nakuomba usifanye jambo lolote litakalomkera shemeji yako, mimi bado natafakari na kuchunguza yote uliyonieleza sawa mdogo wangu" Renata alinitizama na sasa alionyesha tabasamu katika paji la uso wake. Wakati tukiwa tunaendelea na mazungumzo Tumaini alikuwa bado amelala.

Maisha yaliendelea lakini sasa niligundua kuwa tabia ya Tumaini ilikuwa imebadilika, kwani alikuwa mkimya sana, asiyezungumza jambo lolote na hata ukimuuliza kuwa anamtatizo gali alikuwa hasemi na pale ulipokuwa unamuuliza sana, alianza kulia.Siku moja nikiwa chumbani nimepumzika nilisikia Renata na Tumaini wakigombana, nilisimama na kwenda hadi chumbani kwao, taratibu nilisimama mlangoni bila wao kuniona na sasa nilimuona  Tumaini akiwa amemkalia dada yake huku akimpiga na kumn'gata hadi kumtoa  damu kwenye paji la uso.

Nilisogea haraka na kumshika kwa nguvu. "Mungu wangu yaani Tumaini unampiga dada yako, wewe mtoto umechanganyikiwa" Nilimtizama katika midomo yake alikuwa amebaki na damu wakati nikiwa nataka kumfuta ile damu nilishangaa alinitoa mkono wangu huku akiilamba ile damu na kuimeza, Renata alikuwa analia sana nilibaki nimepigwa na butwaa nikimshangaa Tumaini kile alichokifanya kwani alionekana kama mtoto tofauti kabisa na Tumaini ambaye tulikuwa tumemzoea. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 30. Endelea kufuatilia sasa utaipata hadi mwisho wake.
Maoni 1 :

emu-three alisema ...

Mhh, umeachia patamu, tupo pamoja nasubiri tuone ni nini kitaendelea tupo pamoja kky

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom