SEHEMU YA TISA
Nadia alivuta pumzi kidogo kisha akanitazama….
“Mwandishi, hivi wanadamu wana roho za aina gani?
Yaani watendwe na watu wengine halafu hasira zao wamalizie kwangu….ama hakika
walipata pa kupoozea hasira zao. Alianza kijana mmoja kulaumu kuwa mimi ndiye
nilikuwa chanzo cha mikosi.
Mara mwingine akaunga mkono. Wakaanza kunizonga
zonga hapo nikiwa sina walau nguo moja mwilini. Nikajaribu kujihami, hapo
nikiwa nawaza kitu kimoja tu kuipata nguo yangu, hasahasa ile blauzi yenye pesa
zangu ambazo nilipanga kuzitumia katika mchakato mzima wa hapo Musoma mjini
nilipokuwa naelekea.
Nilijaribu kumkaba yule msichana aweze kunipatia
blauzi yangu, kweli nilifanikiwa kumwangusha chini, sasa nikawa juu yake
nikifanya jitihada za kuiondoa nguo.
Mara nikasikia sauti moja ikidai kuwa mimi ni
kichaa na nikiachwa naweza kumuua yule binti, hapo sasa kundi la watu shupavu
likanivamia. Nilipojifanya mkomavu sana nikaanza kupokea kichapo huku nikiwa
uchi wa mnyama. Nilijaribu kujitetea lakini sauti yangu moja haikuwa chochote
kwenye umati ule. Nikasukumiwa kichakani, huko napo kipigo kikaendelea,
hatimaye sauti haikutoka tena, nikabaki kutazama tu jinsi walimwengu
walivyoamua kuikatisha safari yangu hapa duniani katika namna ya kipekee.
Ninakufa nikiwa sijapata haki yangu!!
Iliniuma sana!!
Nilichoweza kukiona kwa uhakika wakati jicho langu
likiwa na uhai bado ni mwanaume akija mbio huku akiwa amenyanyua kitu mfano wa
jiwe juu juu. Nilifanikiwa kupiga kelele lakini sijui kama ile kelele
niliisikia mimi peke yangu ama kila mmoja aliweza kuiskia. Na kama waliisikia
mbona wasinisaidie.
Nilipofumba macho kukwepa kumtazama yule mtu,
sikuyafumbua tena hadi nilipojikuta mikononi mwa mzee mwenye ndevu nyingi
anayezungumza Kiswahili kwa shida sana.
Watoto wake hawakuweza kabisa kuzungumza Kiswahili.
Kitu cha kwanza baada ya fahamu kunirejea ni
kuutazama mguu wangu, mguu ambao niliusikia ukiwa mzito sana na sikuweza
kuunyanyua.
“Porepore..porepore mona wane.” Aliyasema maneno
haya katika lafudhi ambayo nilikuwa naifahamu, lafudhi ya kikurya.
Nilipojitazama, mguu ulikuwa umeunganishwa na vifaa
visivyokuwa vya kitaalamu sana. Na hogo lililofungwa lilikuwa limechafuka sana.
“Mama Marwaa uuuuuuh!!” aliita yule mzee,
akaitikiwa na sauti ya kike kutoka mbali kiasi fulani. Kisha baada ya sekunde
kadhaa akafika mwanamke imara kabisa mbele yangu.
Wakaanza kuongea kikabila!!
Sikujua nini wana maanisha!!
Lakini baadaye mzee yule aliyejitambulisha kwangu
kama Marwa kwa kulazimisha Kiswahili alinisimulia jinsi nilivyookotwa hali
yangu ikiwa mbaya sana wakidhani nimekufa.
Katika kusimuliwa ndipo nikaikumbuka taswira
niliyoiona mara ya mwisho kabla ya kuzimia. Kumbe yule mtu aliniponda na jiwe
katika ugoko wa mguu wangu na hapo nikapoteza fahamu huku nikiuacha mguu
ukivunjika.
Mzee Marwa katika kuchunga mifugo yake ndipo
akakutana na mwili wangu ukiwa katika hali mbaya, lakini akabaini kuwa bado
nilikuwa napumua. Hakuweza kujua nilikaa pale kwa siku ngapi nami pia sikujua
lolote kwa sababu sikumbuki ilikuwa siku gani niliyozimia.
Nikayaanza maisha mapya katika familia ya mzee
Marwa.
Mwandishi kuna watu wana maisha magumu sana.
Wanaishi bila kuijua kesho yao lakini bado wanapata nafasi ya kuonyesha upendo
wao wa dhati.
Sijui kwa nini familia ya akina Desmund haikupewa
mioyo ya aina ile maana ni kama walilaaniwa wale binadamu. Mwanzoni nilidhani
labda ni kila mtu katika kabila lao alikuwa na tabia kama zile lakini sasa
nilikuwa nayapata majibu kuwa sikuwa sahihi hata kidogo. Tabia ya mtu hutegemea
na mtu mwenyewe na wala sio kabila lake.
Mwandishi, nikikuambia kuwa zamani nilikuwa nakula
sana basi huu ulikuwa mwisho, asubuhi tulitazamana tu na kama ikitokea bahati
tunapata uji usiokuwa na sukari nilisikia wakiuita ‘litaghata’, mchana tulikula
ugali wa mtama, na usiku tulikula ama usiku ulipita hivyo hivyo, nilihangaika
sana kuizoea hali ile lakini sikuwa na pa kulalamika, mguu wangu ulikuwa mbovu.
Niliishi pale kwa miezi mine ya mateso, lakini
afadhali mateso yale nilikuwa nimeyazoea, baada ya muda fulani nikiwa
ninatembea vyema japo nilichechemea kidogo alikuja mtoto wa mzee Marwa, alikuwa
ametokea mjini Musoma ambapo alikuwa anasoma. Nilimtambua kwa jina la Mwita
japo alipenda sana kujiita ama kuitwa David. Aliichukia asili yake na hakupenda
kuzungumza kabila lake, mara zote alipoongeleshwa kikabila alijibu Kiswahili.
Elimu yake ilikuwa imemfanya mtumwa wa mambo ya kizungu. Kuingia kwa Mwita
kukaanza kunikosesha amani kutokana na tabia zake za kupenda kunitazama kwa
macho fulani yaliyoonyesha matamanio, na mara nyingine alikuwa akinikonyeza.
Nilimkanya kuwa sitaki hicho anachokitaka lakini hakutaka kujirekebisha,
nilitamani kumshtaki kwa baba na mama yake lakini niliona kuwa haina haja mimi
ni wa kupita tu pale.
Wakati huo nilikuwa naweza kuhudhuria shambani na
kulima kwa bidii. Iliniwia ngumu sana kuamini kuwa Desmund na penzi lake haramu
wameniharibia maisha yangu kiasi kile. Lakini yote sikutaka yaendelee kujikita katika
kichwa change nikaacha maisha yaendelee.
Ulipotokea msiba, mzee Marwa na mkewe wakahudhuria
ni hapa nilipoianza safari nyingine ya kuhaha kuitafuta amani bila kusahau haki
yangu. Nyumbani tulibaki mimi, Mwita na watoto wengine
wawili wadogo. Majira ya saa tatu usiku Mwita anayejiita David alinifuata
katika nyumba ya majani ambayo nilikuwa naishi kwa wakati huo.
Hapakuwa na umeme katika mji ule wala majirani
hivyo kiza kilikuwa kimetanda haswa. Mwita alikuwa peke yake mwanzoni. Alianza kunieleza
mambo ambayo ninayaita ya kipuuzi, alilalamika kuwa kulikuwa na baridi sana,
sikumjibu niliendelea na shughuli yangu ya kushona nguo yangu iliyokuwa
imechanika.
Aliongea mengi lakini nilimweleza kuwa sipo tayari
kwa jambo lolote lilena iwapo akiendelea kunilazimisha nitamshitaki kwa baba
yake.
Huenda jibu hili lilimkera sana Mwita, akaondoka na
kisha baada ya nusu saa hivi akarejea akiwa na kikundi cha wanaume wanne wote
walikuwa wanaongea kikabila na sikuweza kuwaelewa walichomaanisha.
“We demu unajifanya mjanja sio.” Alinikoromea
kijana mmoja, lafudhi yake ikifanana kabisa na ile ya Desmund kabla
hajajanjaruka.
Niliwatazama sikusema neno, wakasemezana kikabila
tena. Mara mmoja wao akanishika mkono nakutaka kuninyanyua. Mwandishi wale watu
wana nguvu balaa!! Nilijaribu kujitoa lakini haikuwezekana, wakaanza kunivuta
kuelekea walipojua wao. Giza lilikuwa limetanda haswa. Niliendelea kupambana
lakini hali haikuwa shwari. Hatari mbele yangu.
“Mwita nipo katika siku zangu!!!” nilimlilia yeye
ambaye nilikuwa nikimfahamu kwa jina, lakini hakutaka kunisikiliza alikuwa
amekasirika.
“Acha ujanja wa kizamani we demu, mbona hukusema
mapema.” Alinikaripia kijana mwingine.
Sasa tulikuwa tumekifikia kichaka fulani,
wakanisukuma huku na kule, wakafanikiwa kuitoa kanga yangu.
Nikaiona dalili ya kubakwa. Sikuwa tayari kwa jambo
lile. Nikafurukuta hukuna kule lakini ushindi ulikuwa upande wao.
“Haya nimekubali naomba nilale mimi mwenyewe.”
Niliwasihi, wakanielewa. Nikajilaza chali, wakaitoa nguo yangu ya mwisho.
Hakika nilikuwa katika siku zangu na ndio kwanza
nilikuwa nimeanza, lakini wale vijana walionekana mshipa unaosaidia kuona
kinyaa kwao haukuwepo. Hawakujali ile damu!!!
Mwita akajiteua kuwa wa kwanza. Mimi nilikuwa
nikiombea wafanye kosa lolote niweze kutimua mbio. Lakini wakati huo huo
nikajiuliza iwapo nitakimbia ni wapi naelekea sasa, kulikuwa na giza nene sana.
Mwita akaondoa nguo zake na kunivamia pale chini
tayari kwa kuniingilia kimwili.
Wakafanya kosa!!
Kosa ambalo walipaswa kujutiana hawakuupata muda
huo wa kujutia.
Kijana mmoja aliyekuwa ameshika panga kali kabisa
alilichomeka chini. Akaanza naye kuvua nguo zake ili zamu yake ikifika imkute
akiwa tayari tayari.
Hilo likawa kosa ambalo nililisubiri bila kujua
kama litatokea.
Mwita alikuwa amejiweka kimjini mjini na hakuwa
shupavu kama wenzake. Hata mimi kukaa kwangu kijijini kwa muda mfupi niliweza
kumuhimili. Alipokuwa juu ya kifua changu akitaka kunibaka, nilimuhesabia mara
tano tu kuwa atakuwa katika ulimwengu mwingine.
Kweli nikahesabu kisha kwa nguvu zangu na kujitetea
kwangu kwa mara ya mwisho, chuki ikinitawala juu ya wanaume, nilimrusha mbali
nami, kisha upesi nikasimama na kukimbilia lile panga, nikalitia mkononi.
Nikashukuru kwa sababu nilikuwa mzoefu tayari
katika kukata kuni kila kukicha hivyo nililimudu panga.
Nikaanza na yule aliyekuwa uchi nikamfyeka mgongoni
akaangukia pembeni huku akipiga yowe kikabila, nikamrukia Mwita, sikutarajia
kama nitamkata shingoni lakini panga lile kali lilitua shingoni.
Mwita hakupiga kelele, kijana mmoja aliyebakia
akawahi kutimua mbio. nami nikatimua mbio baada ya kuikwapua kanga yangu ,
panga mkononi, mbio kuelekea popote penye njia.
Kwa sababu nilikuwa nakuja kukata kuni mara kwa
mara nilijikuta naizoea njia!!!
Nilijua tayari nimezua balaa na sitakiwi tena hapo
kijijini.
Nikaendelea kukimbia hadi nilipoifikia barabara ya
lami…..
Lami ya kuelekea Musoma!!!
Musoma kwa akina Desmund.
Nilikuwa na panga langu bado kwa ajili ya kukabiliana
na hatari yoyote usiku ule.
Mvua kali ilinikuta barabarani!! Nikiwa sijui
lolote la kufanya kujiepusha na balaa ambalo lilikuwa linanikabili.
Mvua ilinipiga, nikaanza kujiuliza kuwa mimi
nanyeshewa, Desmund aliyenidhulumu mali zangu na kisha kuupondaponda moyo wangu
alikuwa amelala ndani, amemkumbatia mkewe na wamejifunika blangeti….tena bila
shaka walikuwa wameahidiana kuamshana asubuhi wawahi kazini.
Kazi ambayo ni jasho langu mimi Nadia, nikapandwa
na hasira kisha hapo nikaikumbuka simulizi marehemu Jadida baada ya kuja Musoma
katika kunisaidia kudai haki yangu!!! USIKOSE SEHEMU YA KUMI
Maoni 1 :
Jamani..haya maisha haya. Ahsante da Adela lkn unachelewa kuweka.
Chapisha Maoni