Jumatano, Agosti 27, 2014

UMRI WA KUOLEWA UWE MIAKA 18 ASEMA GRACA MICHAEL

Watanzania wameaswa kukitumia kipindi hiki cha kuundwa kwa Katiba mpya kuwa na kifungu kwenye katiba kinachoeleza umri wa ndoa kuwa miaka 18 na kuendelea, ili kuondoa tatizo la ndoa za utotoni.


Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na mwanzilishi wa mfuko wa Graca Machel Trust, Grace Machel, alipokuwa akizundua kampeni ya kitaifa dhidi ya ndoa za utotoni inayoanzia katika wilaya ya Tarime mkoa wa Mara.

Machel ambaye ni mjane marais wa kwanza wa Msumbiji na Afrika Kusini, Samora Machel na Nelson Mandela, alisema ni muhimu kwa wadau wote wa haki za watoto wakashinikiza wajumbe wa Bunge Maalumu na watunga sheria wote wahakikishe kipengele hicho kinaingia ndani ya katiba.

“Ninajua katika suala hili kuna upinzani kutoka kwa makundi mbalimbali, kama ya wakereketwa wa jadi, wahafidhina au wanaolalia mrengo wa kidini ambao wanaweza wakatumia mwanya wa ukereketwa wao kupinga juhudi zetu hizi,” alisema.

Alisema ni juu ya wadau wote serikali, asasi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini na wananchi wenye mapenzi mema kuyaelimisha makundi haya yakubali uwepo wa sheria ndani ya katiba inayotamka kuwa mtoto ni mwenye umri chini ya miaka 18.

Alisema wanaanzia kampeni ya kupinga ndoa za watoto katika mkoa wa Mara, kwa kuwa ndiko kuliko na changamoto nyingi hasa ya ndoa za utotoni, ukatili dhidi ya watoto na wanawake pamoja na ukeketaji wa wanawake (FGM).

Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, pamoja na kuunga mkono kampeni hiyo, alitoa wito kwa watoto kujitokeza hadharani na kutumia fursa zote wanazozipata kupaza sauti dhidi ya mbinyo wa haki zao, likiwamo suala la ndoa za utotoni. 

Naye Mwakilishi wa kanisa kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania  (CCT), Askofu Peter Kitula, alisema ni muhimu kwa wadau kuwa na sauti moja ya kupinga vitendo vinavyokiuka haki za watoto ikiwamo hii ya ndoa za utotoni.

“Vitendo vya aina hii ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu, hivyo ni bora tukaungana dhidi ya madhira yote yanayohatarisha fursa za watoto kupata elimu na kulitumikia taifa kwa ufanisi hapo baadaye,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza Kuu wa Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoa wa Mara, Sheikh Zuberi Saidi, alisema, uislamu unahimiza waumini wake kuitafuta elimu kwa nguvu zao zote.

“Na kwa hali hiyo, tunahimiza watoto waachwe wasome kwanza kwani ni vigumu kusoma ikiwa watakuwa wameshaolewa,” alisema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, kipengere cha umri wa ndoa, inaelekeza mwanaume awe na walau miaka 18 na mwanamke walau miaka 15 wakati wa kuoa na kuolewa.

Aidha sheria hiyo inasema, kwa mwanamke ambaye hajafikisha umri  wa miaka 18, kabla hajaolewa atatakiwa apate idhini ya baba, au mama ikiwa baba amefariki au kama wote wamefariki idhini ya yule anayemlea.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom