Pages

Alhamisi, Agosti 28, 2014

SIMULIZI YA MAISHA "USILIE NADIA SEHEMU YA 10"

SEHEMU YA KUMI
Nikakumbuka jinsi Jadida alivyoyumbishwa na kuambiwa kuwa mimi nilikuwa msichana wao wa kazi na waliniokota nikiwa chokoraa mjini Mwanza familia yangu ikiwa ina maisha magumu sana. Hapo tu alipoelezea kuwa alikuwa ni dada yangu na alikuja kudai mali zangu walau nusu tu!!
Jadida akajazwa mneno kuwa nilipokuwa msichana wao wa kazi nilipata mimba na nilipojaribu kuitoa nikapata kichaa cha mimba!! 

Wazimu wangu ukazua utata baada ya kuanza kuwapiga watoto mtaani. Nikawa nusu siku nakuwa mzima na nusu nyingine nakuwa na wazimu!! Polisi walipotaka kuniweka ndani ndipo wakanirudisha nyumbani kwetu Mwanza. Huko wakaikuta familia yangu yote ikiwa imetekete kwa ugonjwa hatari wa kipindupindu. Kabla hawajajua nini cha kufanya nikapandwa na wazimu na kuanza kufanya vurugu kisha nikakimbia na kutoweka. Kama hiyo haitoshi wakamueleza Jadida kuwa yeye sio wa kwanza kudanganywa na mimi juu ya mali zile kuwa nahusika nazo.

Mwandishi!! Kwa maelezo yale Jadida akaanza kuamini kuwa huenda kuna ukweli kwani mwanamke aliyemkuta hapo nyumbani alikuwa mama haswaa mwenye heshima zake. Na alipokuaja Desmund mwenyewe ambaye ni baba mwenye nyumba ndipo Jadida alizidi kunywea, Desmund hakuonekana kuwa mwanaume wa ajabu kama nilivyomzungumzia mimi kwa Jadida hapo kabla, Jadida akabakiza imani kidogo sana kwangu na kuamini kuwa huenda nilikuwa na wazimu kweli.

Lakini alipokutana na kimbembe cha kukamatwa ghafla na polisi wakati akitaka kutoka katika nyumba ya Desmund ndipo akili yake ikafunguka kuwa maneno aliyoambiwa yote ni uongo na kuna kila dalili ya dhuluma imefanywa na Desmund na mkewe. Jadida akawekwa mahabusu kwa siku tano kwa kosa la kutaka kufanya utapeli, baadaye akaachiwa huru.

Jadida akatumia ujanja wa mjini kuwaweka sawa makondakta wakampakia katika gari kuja jijini Mwanza. Jadida alikuwa na hasira sana, huenda hata ni hasira hizi zilimuua, Jadida akaamua kujiingiza katika umalaya uliokubuhu kuliko ule w awali ilimradi aweze kuzisaka pesa nyingi kisha aandamane nami mjini Musoma katika kudai haki yangu. Lakini haikuwa kama tulivyopanga!! Jadida akabakwa na kuuwawa katika nyumba ya kulala wageni!!!
Nilichoamini hadi dakika ile ni kwamba Jadida aliniachia kitu kimoja kikuu na muhimu. Jadida aliniachia roho yake!! Nilibadilika na kuwa jasiri sana!! Hakuna nilichokuwa nahofia.

Sasa ni kiza kinene na nilikuwa nipo peke yangu katika eneo tata, panga langu mkononi. Mvua kali ikiwa imenipiga na kunifanya nitetemeke haswa.Kuendelea kunyeshewa nikiwa nimekaa sehemu moja niliona si jambo sahihi, nikikumbuka kuwa nimefanya balaa kwa kutumia panga huko nilipotoka. Nikaanza kutembea kuelekea nisipopajua lakini nikiifuata lami, nilitembea bila kuchoka, mvua nayo iliendelea kunimwagikia. Kadri nilivyojihakikishia kuwa ile sio ndoto bali nipo katika maisha halisi nikazidi kumwona Desmund kama mnyama hatari asiyestahili kuishi tena.

Nilitembea sana hadi nikafikia sehemu nikakutana na vibao vinavyoelezea juu ya njia ya kwenda Tarime, Sirari ….na kibao kingine kilionyesha mahali nilipokuwa napahitaji. Musoma!!!
Hii sehemu niliikumbuka vyema kabisa, ni huku alikuwa akiishi mama yake Desmund!!
Walipaita Makutano, haswaa nilikuwa sijakosea hata kidogo.
Wazo la kwenda Musoma likaishia pale kwa muda kwa sababu hata ningeendelea bado nilikuwa sijaweka mikakati yangu vizuri. Nikaamua kufanya kitu ambacho roho ilikuwa imenituma!!!

Nikachepuka katika njia ambayo niliikumbuka vizuri panga langu sasa nilikuwa nimelichomeka kiunoni. Nikaruka matuta katika shamba la mihogo. Hatimaye usiku huo huo nikaifikia nyumba ambayo ilikuwa ngeni sana machoni mwangu!! Lakini mti mkubwa wa mwembe ulinikumbusha kuwa sijapotea.

Sikujali kama ule ulikuwa ni usiku ama la!! Nikajikongoja hadi mlangoni kisha nikagonga hodi!! Niligonga hodi bila kupata majibu yoyote…lakini mara nilisikia hatua za mtu akisogea pale mlangoni, nguvu zikaanza kuniishia mwilini lakini nikajikaza. Akauliza kikabila kuwa mimi ni nani? Nikamjibu kwa kumtajia jina la Wankuru!! Akafungua mlango huku akionekana kuwa na wasiwasi.

Akafanya kosa moja tu kuacha mkon wake nje, mara moja nikamvuta!! Akapiga yowe moja lakini nikawa nimemkamata tayari. Hakuna nilichokuwa naogopa.
“Wewe ni nani?” nilimuuliza nikiwa nimemshikia panga.”
“Bhooke!” alijibu.
“Desmund ni nani yako?”
“Mjomba wangu!!”
Alipojibu hivyo tu, nikaamua kumtumia huyu kama sadaka.
Na damu yao yote ilikuwa halali yangu!!! Ni neno aliwahi kusema Jadida kabla hajafa. Nami nikaona lipo sahihi sana.
“Kama alinitukania familia yangu!! Kama aliudhalilisha utu wangu, kwa nini nimuonee huruma YEYE na kizazi chake.” Nilijiuliza. Kisha nikamfyeka yule mtoto na panga begani, akapiga yowe moja, nikamfyeka tena mkono. Kisha kama ifanyavyo kuku, nikamkanyaga asirukeruke. Nikahakikisha kuwa anatulia tuli.
Nikaitimiza azma yangu ya ghafla kuwa ili nimpate Desmund vizuri lazima niweke huruma yangu kando!!! Nimpe adabu kimya kimya kisha nikumbane naye….nikaanza na huyo mjomba wake.
Nilitarajia litatokea nililokuwa nahitaji!!
Desmund alikuja kuhudhuria msiba ule. Nami sikulaza damu siku ya kuaga mwili nikiwa naishi maisha ya kula msibani hapo kwa kubangaiza na kulala palepale msibani. Msiba ambao nilikuwa nahusika nao kwa asilimia zote! Sasa niliamua kumkabili Desmund.
Nilisubiri amalize kumwaga mchanga katika kaburi la mjomba wake niliyemuondoa maksudi. Sasa nilihitaji kuzungumza naye kistaarabu.
Baada ya maziko macho yangu yakiwa makini kabisa kumtazama hatimaye nilimuona kwa uzuri kabisa.
Mwandishi, Desmund alikuwa amebadilika sana. Alikuwa na afya nzuri sana na alikuwa ameng’aa haswa.
Hatua kwa hatua nikapiga moyo konde, bila viatu miguuni nikajikongoja kwenda kukutana na yule. Litakalokuwa na liwe….

Mwandishi, nilikutana na Desmund. Nikaziba njia nikasimama mbele yake. Macho yetu yakatazamana ana kwa ana. Desmund alikosa neno la kusema kwa ghafla ile. Nami sikusema kitu niliendelea kumtazama tu. Jinsi alivyong’aa na jinsi mimi nilivyopauka!!
“Ni pete yako hii kidoleni mwangu Desmund!! Pete uliyonivika mbele ya wanafunzi wenzangu, ni jeraha hili Desmund ulilonipa kwa kupigania penzi langu. Sijaivua pete yako mpaka leo na sitaivua hata mpaka unieleze tu nilikukosea nini mimi hadi ukanitenda hivi. Hongera kwa kufunga ndoa naona pete yangu ulishaitupa mbali. Desmund sina hadhi ya kuzungumza na wewe nadhani hata watu wanatushangaa. Naomba unipe changu niendelee na maisha yangu. Nipe walau nusu tu ya mali zangu nijiondokee zangu. Nahitaji kuishi kwa amani. Desmund ni mazito umenifanyia, nadhani unajua ni kiasi gani nimeishi maisha yasiyokuwa na tofauti na jehnamu kama kweli jehanamu ipo kama wanavyosema wenyewe. Unajua umeniharibia kiasi gani. Ok kwa kifupi Desmund, kama ni njaa nimelala njaa, kama ni kutukanwa nimetukanwa, familia imenitenga, uchangudoa nimefanya sana tu…nimebakwa sana, nimelawitiwa mimi sana tu!!. Desmund huoni kama yanatosha yaliyonitokea. Halafu by the way, yule dada yangu uliyemwambia kuwa mimi ni mwendawazimu amekufa tayari. Sina pa kuegemea. Desmund nipatie walau nusu nasema nusu tu!! Nikayamalizie maisha yangu nikiwa na amani.NAKUOMBA!!” Nilimweleza Desmund kwa kirefu kabisa. Bado tukiwa tunatazamana na wapita njia wasijue lolote linaloendelea. Zaidi ya kutushangaa
“Wewe ni nani binti?” hatimaye aliniuliza swali la ajabu sana ambalo lilinishangaza. Desmund anajifanya hanijui mimi!! Desmund hanijui wakati amesababisha niwe katika hali ile.Hapo ndipo ulizuka utata… utata juu ya utata.”USIKOSE SEHEMU YA KUMI NA MOJA

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Ooh! Jamani...nakupendaje sasa da Adela. Nasubir kwa hamu nisome Nadia itakuwaje anatia huruma.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom