Pages

Jumatatu, Septemba 15, 2014

SIMULIZI FUPI 'Rafiki Adui"

MTUNZI-  ADELA DALLY KAVISHE
Siku moja nilikuwa nimekaa nyumbani ilikuwa ni majira ya saa moja jioni ambapo nilimuona kwa mbali Chipele akikimbia kuja nyumbani huku akiwa analia na kuniita kwa sauti kali "Wema, Wema .....Wemaaaaa, nisaidie rafiki yangu naomba unisaidie"Nilishtuka sana, na haraka nilimsogelea na kumuuliza "Chipele we Chipele una matatizo gani, mbona hivyo kunanini?".

 Nilipata hofu sana kumuona katika hali ile nilimsihi anyamaze ili aweze kunieleza nini kimemsibu alianza kuzungumza kwa sauti iliyo na kigugumizi " Wema , Mdogo wangu anaumwa sana, amedondoka ghafla na kuzimia, hapa nilipo sina  pesa yoyote sijui nafanyaje Wema nisaidie, kwani sina pakwenda, hapa nilipo sina Baba wala Mama, yaani nimebaki mimi na mdogo wangu na hali yake ni mbaya, mimi nachanganyikiwa Wema, nisaidie rafiki yangu" Aliongea Chipele kama mtu aliyechanganyikiwa huku akiwa ameweka mikono yake kichwani na akiendelea kububujikwa na machozi. 


Nilimuonea huruma sana, na haraka niliamua kumsaidia "Usijali Chipele, twende haraka, tumpeleke mtoto Hospitali, haina haja ya kuendelea kulia kwani kwa kufanya hivyo haitasaidia jambo la msingi nikuhakikisha mtoto anpelekwa haraka kupatiwa matibabu" Haraka tulienda kuchukua taksi na moja kwa moja tulimpeleka mdogo wake Chipele hospitali, hatimaye alipatiwa matibabu na hali yake iliendelea vizuri. Nililipia gharama zote, na kila kitu kilichohitajika, niliendelea kumuhudumia hadi mdogo wake alipona kabisa, pale mtaani watu walikuwa wakijua kwa namna tulivyokuwa  marafiki.

Nilikuwa nikiambiwa maneno mengi kuwa Chipele siyo rafiki mkweli, kwani ana tabia ya kunizungumzia vibaya kwa watu, nilihisi yalikuwa ni maneno ya watu kwani niliamini siku zote katika maisha kuna watu ambao hawapendi kuona watu wakipatana na kusaidiana katika shida na raha. Haikuwa rahisi kuamini maneno niliyokuwa naambiwa na watu kuhusu tabia ya Chipele, siku zote nilikuwa nikimuamini kama rafiki yangu wakaribu sana, Nilimpenda sana rafiki yangu, kiasi kwamba kila jambo langu nilikuwa nikimueleza, sikuwahi kumficha siri zangu, na hata ndugu na marafiki zangu wengine walikuwa wakimfahamu. 

Tulikuwa ni zaidi ya marafiki kwani nilimuona kama ndugu yangu, Maisha yetu sote tulikuwa tunafanya kazi ya kuajiriwa  mwenzangu alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha kusindika vyakula, na mimi nilikuwa nikifanya kazi katika kampuni kubwa ya vifaa vya ujenzi, ukweli ni kwamba mimi nilikuwa nikipokea mshahara mkubwa kuliko Chipele lakini siku zote nilikuwa nikimsaidia pale ambapo nilikuwa naweza kufanya hivyo. 

Ilikuwa ni siku moja ambapo nilifika kazini asubuhi na mapema kama ilivyokuwa kawaida, nilipofika kazini moja kwa moja bosi aliniita katika ofisi yake, nilifika alinikaribisha  na kutaka niketi kisha alianza kuzungumza "Wema, wewe ni mmoja kati ya wafanyakazi ambao nimefanya nao kazi vizuri sana, na pia nakuamini sana katika kazi, lakini kuna jambo ambalo linanishangaza, na sikutegemea kama na wewe unaweza kuniibia, katika kampuni yangu...na " Niliamua kumkatisha bosi  akiwa anazungumza na kusema "Bosi, kukuibia, mimi, wapi tena jamani" Bosi alinitizama kwa kunikazia macho na kusema.

 "Nisikilize nimalize kwanza kuzungumza, wewe unahusika katika kuuza nondo na sementi, kila mwezi, halafu hiyo pesa, huandiki katika mahesabu, unaichukua, sasa nimegundua ujanja wako, kwanini lakini unafanya hivi na mimi nimekuwa nikikulipa mshahara mzuri sana." NIlishtuka sana kusikia yale maneno kutoka kwa bosi, na kama haitoshi Bosi aliendelea kusema "Najua unashangaa haya maneno nimeyapata wapi, sasa sikiliza mwenyewe alichokisema huyu niliye mrekodi katika simu yangu halafu uniambie ukweli wa kila kitu".

 Bosi alichukua simu yake na alianza kunisikilizisha kile alichorekodi "Mimi nimeamua kukueleza yote haya kwasababu, sipendi kuona mtu anaibiwa, na vilevile ukizingatia mtu mwizi au muongo hafai katika jamii, halafu najua ulikuwa unamuamini sana Wema yaani yule mwanamke ni mnafki na ni mwizi mkubwa, hapo alipo ana mpango wa kufungua duka la vifaa vya ujenzi, na tena amesema atafungua duka hilo kwa kuiba vifaa kutoka katika kampuni yako, mimi nakueleza yote haya kwasababu namjua vizuri sana Wema nikiwa kama rafiki yake wa karibu. Mimi Chipele ni rafiki wa karibu sana, na Wema siwezi kukudanganya hata kidogo, ila usimuambie kama mimi ndiyo nimekuambia tabia yake ya wizi".

 Nilihisi kama mwili unakufa ganzi baada yakusikia  yale maneno tena aliyekuwa anazungumza ni rafiki yangu kipenzi Chipele ambaye nilimtabulisha kwa bosi wangu mara moja tu alipokuja kunitembelea katika sehemu ninayofanyia kazi, iliniuma sana kwani yale maneno yalikuwa ni ya uongo, ijapokuwa suala la kufungua duka la vifaa vya ujenzi ilikuwa ni ndoto yangu niliyomueleza, lakini siyo kufanya kwa kuiba katika kampuni ninayofanyia kazi nilisikitika sana.

 "Mungu wangu, inamaana Chipele ndiyo ananizungumzia maneno ya uongo kiasi hiki, nimemkosea nini mimi, yaani mema yote ninayomtendea, hapana ama kweli kikulacho ki nguoni mwako, kumbe Chipele ni rafiki adui inaniuma sana" Bosi aliendelea kunisikiliza na kwa wakati huo machozi yalikuwa yakinibubujika kwa uchungu, alinionea sana huruma baadaye alinitaka niondoke na kusema kuwa angeniita baadaye baada ya kufanya uchunguzi. Siku hiyo ilikuwa ni siku mbaya sana kwangu. Ila nashukuru Mungu baada ya uchunguzi Bosi aligundua kuwa sijawahi kuiba chochote hivyo aliniambia niendelee na kazi ila alinishauri niwe makini sana na marafiki wanaonizunguka kwani Chipele alimpigia simu na kumueleza mambo yote hayo. 

Nilifurahi kuendelea na kazi lakini sikusita kwenda kumueleza ukweli Chipele kuhusiana na kile alichonitendea aliona aibu sana na kubaki akiniomba msamaha huku akijiliza, Niliamua kumsamehe lakini urafiki wetu haukubaki kama ilivyokuwa zamani kwani sikutaka kumuamini tena niligundua kuwa alikuwa hapendi maendeleo yangu. KUWA MAKINI SANA siyo kila mtu anapenda mafanikio yako, hata kama unamsaidia kwa kiasi gani, watu wengine hawana shukurani.Unamtendea wema yeye anakutendea mabaya. MWISHO.

Maoni 2 :

Amor alisema ...

Asante dada yangu kwa ushauri maana wengine wetu ni rahisi sana kusahau kwamba shukrani ya punda ni mateke.

emu-three alisema ...

Mhh, simulizi tamu mpendwa, tupo pamoja, sitakata tamaa kukutembea

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom