HAIKUWA kama nilivyodhani kuwa Nadia alitakiwa kupumzika ili
hasira zake zipungue, niliamua kuondoka kimyakimya bila kumuaga Nadia ambaye
bado alikuwa anatetemeka.
“Unaenda wapi Gerlad!!” kwa mara ya kwanza aliniita kwa jina
langu halisi. Nikakosa cha kujibu lakini sikuendelea zaidi nikalazimika
kugeuka.
“Unaondoka kwa chuki kisa nimekueleza ukweli sivyo? Kisa
nimesema kuwa nyie wote ni walewale. Kisa nimewasema sivyo!! Ulitaka nisiuseme
ukweli ama, mwandishi hutakiwi kuchukia eti kisa tu wewe ni mwanaume. Haya basi
tuseme kuwa nyinyi hamfanani, mbona nilipotoka pale nyumbani kwa Danny nikazidi
kukutana na akina nyie na matatizo yenu yaleyale. Hivi kwani nyie wanaume huwa
mnawaza nini? Ama labda niseme hivi nyie huwa mna cha huyu mbaya huyu mzuri!!
Hamna mashaka kabisa kuwa mwingine anaweza kuwa jini.
Hebu ‘imagine’ na hali
yangu ile ya kutokea rumande, nimechakaa haswa, nimekonda na nina kidonda
kibichi, jenga picha kuwa bado nikakutana na wanaume wanajifanya kunitamani.
Huruma yenu ipo wapi? Nilikwambia kuwa nakiri kuwa wema hufa mapema, Jadida na
Danny waliondoka mapema sana, ni hawa walikuwa wema kwangu na wakaondoka nikiwa
nawahitaji. Tazama Danny amekufa bila hata kuniambia kwa nini Desmund alikuwa
akiwachukia watu weupe, jibu ambalo nilikuwa nalitafuta siku zote” Nadia
akatabasamu kidogo kisha akaendelea,
“Ujue mwandishi labda nina hasira sana ama
labda ni kwa sababu nasema kweli nd’o maana wanishangaa, ndio lazima unishangae
maana si ndio zenu kuuchukia kweli, lakini amini kuwa hakuna kitu kizuri kama
ukweli katika maisha haya, ni kweli kabisa kuwa ukweli unaumiza sana lakini
unakuta mtu nimemwambia kabisa kuwa mimi sina cha kupoteza awe mkweli tu lakini
bado anadanganya. Baada ya kuwa nimeondoka nyumbani kwa Danny aliyekuwa
marehemu tayari huku sijui lolote kuhusu mama yake mzazi sikuwa na pa kwenda
mjini Musoma. Nilitamani kumkabili Desmnd lakini nikagundua kuwa sijajipanga na
mwisho wa siku nitarejea kulekule rumande na safari hii asingepatikana Danny
mwingine kuweza kunikomboa, nikaingia mtaani, nikapata pikipiki ambayo nilitaka
inipeleke moja kwa moja kituo cha mabasi.
“Unaenda kupanda basi muda huu dada ama!” mazoea yetu
yalianzia hapa na huyu bwana ambaye uso wake nilipoutazama alionyesha kuwa
mkarimu lakini sikutilia maanani maana hata Desmund alikuwa hivyo hivyo.
Nilikubali kuwa nahitaji kusafiri kuelekea Mwanza. Na hapa
akanipinga sana kuwa hakuna mabasi muda huo na kwa pale Musoma mabasi hayana
utaratibu wa kulazwa humo Stendi.
Kweli tulipofika hapakuwa na mabasi, na ni kama alinisoma
akili yangu kuwa nilikuwa nina hofu lakini kuna jambo kama alishindwa kuniambia
hata nilipomlipa pesa yake aliipokea kwa kinyongo. Alitamani sana kusema nami
zaidi lakini sikuwa nikimpa ushirikiano. Akawasha pikipiki yake na kutoweka.
Alipoondoka ndipo hofu ikazidi kunitawala maana niligundua
kuwa nimebaki katika upweke mwingine mpya. Katika kituo cha mabasi huku nyuma
nikiwa nimeacha maiti katika chumba cha Danny. Na ni Danny alikuwa ameuwawa.
Nikiwa bado katika tafakari, upepo ukipuliza na baridi
ikipenyeza katika mwili wangu nikapata wageni wa ghafla waliokuja kunighasi.
Huenda ni jambo hili lilimtia hofu yule dereva wa pikipiki. Walikuwa ni
vibaka!!
Wakanighasi huku na kule wakinilazimisha niwape pesa, katika
kunitikisa mara simu ikadondoka wakaitwaa, wakaendelea kunibughudhi na hapo
likatokea jambo jingine lililonifanya nistaajabu. Nilisikia kelele za mwanaume
akiwafukuza wezi wale huku, nilipogeuka alikuwa ni dereva wa pikipiki akiwa na
panga mkononi akielekea pale nilipokuwa, waler vibaka wakatoweka na ile simu.
Uzuri ni kwamba hawakunijeruhi.
“Nilijua nikikwambia mapema kuwa kuna vibaka maeneo haya
ungeweza kunihisi vibaya sana maana hukuwa na ushirikiano katika mazungumzo
yetu” aliniambia yule mwanaume huku akinishika mkono. Sasa nilifuata alichokuwa
akiniambia, hofu ilikuwa imetanda upya, alikuwa ameninusuru kutoka katika
mikono mibaya ya vibaka.
Akanipeleka katika pikipiki yake aliyokuwa ameiegesha mahali.
Akanichukua hadi nyumbani kwake!!!
Akalala chini akaniachia kitanda!!
Huu ukawa mwanzo wa kufahamiana na Christian.
Asubuhi aliniamsha mapema sana ili niwahi basi la kwenda
Mwanza!! Lakini sikuitamani ardhi ya Mwanza ambayo ilishuhudia nikilawitiwa na
haikusema chochote.
Chris akanisoma akili yangu na kuamua kuhoji! Lakini sikuwa
tayari kumweleza lolote kuhusiana na mimi, lakini sikuitaka safari ya Mwanza.
Nikahitaji hifadhi walau kwa siku mbili tatu niweze walau kumkabili Desmund ana
kwa ana tena, kwa silaha yoyote nimwondoe duniani kisha nikamatwe nifungwe ama
ninyongwe niende kumwomba msamaha mama yangu aliyeniachia laana hiyo.
Naam!! Sikutakiwa kuondoka katika mji huo!!
“Chriss…”
Alinitazama nami nikaendelea, “Sikufahamu hata kidogo nawe
haunifahamu na bado umekuwa mwema kwangu. Asante sana kwa yote…..”
“Lakini unaonekana unatawaliwa na hofu!!...halafu kama nakuja
vile” aliniambia huku akinitazama kwa makini.
“Sidhani kama unanijua lakini.”
“Ni kweli huenda mmefanana si unajua tena duniani
wawiliwawili.”
“Wewe ni mwenyeji sana hapa Musoma.”
“Mi mwenyeji nimekulia hapahapa na hata kielimu changu kidogo
nimechukulia hapahapa” alinijibu kwa ufasaha huku alkienda kuiwasha pikipiki
ili anipeleke stendi.
“Inapendeza sana unapofanana na mke wa mheshimiwa bwana.”
Alisema neno ambalo lilinishtua.
“Mheshimiwa gani tena jamani.”
“Diwani wetu aliwahi kuwa na mke kama wewe ila alitoweka
kimyakimya si unajua tena waheshimiwa huenda alimpeleka kusoma ulaya”
“Diwani yupi? Nami kidogo mwenyeji hapa.”
“Huyu aliyeingia baada ya Kenyigo kuuwawa kwa risasi wanamuita
Desmund!” alinijibu, moyo ukapasuka kusikia habari hiyo. Yaani Desmund ni
diwani?? Tena anaitwa mheshimiwa!!
Desmund alimuua Kenyigo!!! Niliwaza, maana sijui tu kwanini
niliwaza. Lakini nilihisi jambo hilo Desmund alimuua Kenyigo ili apate nafasi
ya udiwani, alaa!! Ni hivyo maana miaka mitano ilikuwa haijapita bado ya kuweza
kugombea udiwani.
“Vipi unamfahamu mheshimiwa?” aliniuliza huku akiendelea na
mambo yake.
“Chriss, hebu njoo kidogo. Namfahamu Desmund namfahamu vyema.”
“Kivipi?”
“Nilikuwa mkewe.” Nikamjibu, akaacha yote aliyokuwa anafanya
akanitazama kwa mshangao huku akiwa haamini hata kidogo.
“Chriss kama nilivyosema kuwa wewe hunijui nami sikujui na
hata unastaajabu kwa nini sihitaji tena hiyo safari ya Mwanza, kama nitakuwa
najipalia makaa ya moto na yaache yaniunguze lakini kama ni sahihi na iwe
hivyo. Chriss kwa uliyonitendea usiku wa jana naamini wewe ni mtu unayejali.
Naomba nikushirikishe kidogo juu yangu”….nikamuhadithia Chris dhuluma ambayo
ananifanyia huyo mtu wanayemuita mheshimiwa. Nikamweleza asilimia hamsini
kuhusu mimi, kisha nikamweleza juu ya mauaji yaliyofanyika usiku huo na
hatimaye nikakutana naye akanipeleka mjini.
Chriss alistushwa sana na habari hiyo niliyomsimulia lakini
sikuwa na namna nililazimika kutapatapa kama naweza kupata wa kuungana nami
katika harakati hizo. Chriss alionekana kuwa mwelewa sana jambo lililonifariji
sana.
Safari ikahairishwa, nikabaki nyumbani kwa Chriss huku nikiwa
nimejitoa mhanga kwa lolote litakalotokea, na kwa mara nyingine nikakumbuka
kumtukuza Mungu kwa yote anayonitendea huku nikiamini kuwa bado yupo upande
wangu. Licha ya magumu yote ambayo nilikuwa napitia bado aliniunganisha na watu
ambao walikuwa upande wangu.
Sikutakiwa kutoka nje kabisa wakati wa mchana, hivyo mambo
yangu yote ya faragha nilifanya katika kiza kinene.
Kwa muda wa juma moja kilitokea ambacho nilitaraji, nikageuka
kuwa mke wa Chriss kwa hiari yangu maana hakunibaka. Ni Chriss aliyekuwa
ananipa habari zote zilizokuwa zinaendelea mtaani, nia yangu ilikuwa hali
itulie ili niweze kutimiza azma yangu.
Usiku mmoja nilimuuliza Chriss swali moja tu ambalo
lilinifanya niendelee kuwaona wanaume kuwa wote hawapendi kuwa wakweli.
Nilimuuliza iwapo ana mke!! Akanijibu kuwa hajaoa na kama ikiwezekana atanioa
mimi. Nilirudia swali hilo mara tatu na jibu likabakia kuwa lile la mwanzo.
Macho yake yaling’ara kabisa kwa nuru ya upendo. Alikuwa
anaongea kwa hisia kali sana za kimapenzi.
Mwanzoni nilikuwa kama mtumwa tu wa mapenzi yake, yaani
nilikuwa nafanya ilimradi tu kwa kuwa nafanya. Lakini taratibu nikawa nakolea
na kujikuta nikimkaribisha Chriss katika moyo wangu.
Niliponyoa nywele zangu kichwani hakika nilibadilika, mavazi
ya baibui yakanifanya sasa niwe huru kuwa natoka nje mara moja moja. Chriss
ambaye alikuwa akifanya shughuli ya bodaboda alikuwa anatoka asubuhi akiwa
amenichemshia chai ya maziwa na kuniwekea katika chupa, mchana alileta aidha
chakula kikiwa tayari ama mboga nami ninapika akirudi jioni anapata chakula
nyumbani. Uzuri pale hapakuwa na majirani maeneo ya karibu ambao wangeweza
kuhoji chochote.
Licha ya kuwa anafanya shughuli za bodaboda alikuwa amejipanga
kiasi chake, chumba na sebule vilikuwa vimesheheni haswa. Nami nikawa mama
mwenye nyumba.
Mapenzi huondoa chuki, mapenzi hushinda vita, mapenjzi huweza
kuisimamisha dunia kwa dakika kadhaa. Mapenzi ni kitu cha ajabu sana!!
Nimtafutie nini Desmund iwapo Chriss alikuwa akinipa mapenzi
ya dhati, Desmund alinipenda kwa sababu nilikuwa nina pesa, lakini Chriss
alinipenda kama nilivyo!! Hiyo ilikuwa tofauti kubwa sana kati ya wanaume hao.
Moyo wangu ukajifunza kusamehe, nikaamini huenda mama yangu
ameifuta ile laana aliyonipa. Kama mama yangu amenifutia laana ni kwanini mimi
nakuwa na kisasi moyoni mwangu? Nilijiuliza siku ambayo nilijipanga rasmi
kwenda kumvamia mkewe Desmund katika mkutano wa kisiasa na kummaliza
ikiwezekana.
Nilihudhuria mkutano ule huku nikiwa na silaha ya kisu kikali.
Lakini moyo ukawa mzito, na nikahisi kuwa huyu mama hana kosa,
mbaya wangu mimi alikuwa ni Desmund. Ni huyo alifaa kuitumikia adhabu
niliyokuwa nimeipanga!!
Nikajiuliza kuwa iwapo nitamujeruhi yule mama na kisha
nikakamatwa, hiyo inamaanisha kuwa Desmund atabaki kuwa huru na akinicheka
nikiwa jele!!
Hapana!! Nikahairisha nikaamua kujipa moyo kuwa nitampata
Desmund! Ni huyu wa kunieleza jambo ambalo Danny alitaka kuniambia lakini
wakamuua kabla hajanieleza. Nilimuhitaji Desmund anipe jibu hilo kabla sijaamua
kumuua ama kumsamehe!!
Mwandishi katika haya maisha huwa tunapata shule kila siku na
masomo ni mapya kila leo na waalimu pia ni wapya. Nililokutana nalo kwa Chriss
ulikuwa mzigo hakika, mzigo mzito kutua….ewe moyo ulaaniwe!!
Ilikuwa saa sita usiku. Mimi sinahili wala lile nilikuwa
natazama tamthilia za kifilipino sikuwa na mashaka juu ya Chriss ambaye alikuwa
katika mihangaiko yake, haikuwa mara ya kwanza kwake kuchelewa nyumbani.
Nikasikia mlango ukigongwa, nikaendakufungua huku nikiamini kuwa ni Chris
ambaye nilikuwa namuita mume wangu kwa kipindi kile.
Mara!! Uso kwa uso kwa na mwnamke mnene mfupi rangi ya
chokleti.
Nikamkaribisha lakini akaonekana kusita, akamuulizia Chriss.
Nikamjibu kuwa hajatoka kazini na hapo pepo la wivu likanishawishi kumuuliza
swali kuwa yeye ni nani.
“Ni rafiki yake tu!! Nitarudi baadaye.” Alinijibu kisha
akaondoka akiniachia mchomo mkali wa wivu!! Ina maana Chriss ana wanawake nje!!
Nikazihifadhi hasira ili Chriss akirejea nimweleze.
Nilidhani atarejea Chriss kabla ya balaa lililotokea baada ya
nusu saa. Mlango uligongwa tena, nikatambua kuwa atakuwa Chriss nikaufungua
mlango kwa fujo!! Na hasira ikinitawala.
Uso wa uso na yule mama mfupi. Lakini sasa hakuwa mwenyewe
alikuwa na wengine wanne, wote wakiwa na miili iliyoshiba haswa.
“Kwani wewe ni nani yake?” aliniuliza, nami nikapata fursa ya
kumtambia kama yeye ni kimada basi mimi ni mke.
“Mimi ni mkewe…mama mwenye nyumba hii.” Niliwajibu.
Sikujua kama nimefanya kosa!! Nilisikia kauli moja
tu..’unamchelewesha huyu Malaya!!’..kauli ambayo Desmund aliwahi kunieleza. Na
hapo nikajikuta nimesukumwa nikaangukia katika kochi nikajigonga mgongo, nikiwa
sijayahimili maumivu yale, yule mwanamke kibonge mfupi akanirukia na
kuniangusha chini vizuri, akaanza kunikwangua na yale makucha yao marefu!! Neno
Malaya likijirudia mara kwa mara.
Hadi wakati Chriss anafika nilikuwa hoi nikivuja damu na bado
nilikuwa sijaelewa nini kinaendelea.
“We mpuuzi unataka upewe nini wewe…yaani kitanda changu,
unalala na changudoa anajiita mama mwenye nyumba. Christian sihitaji kujua wala
kusikia lolote kutoka kwako kabla hujafanya maamuzi kati ya haya mawili.
Nikabidhi pikipiki yangu, utoke katika nyumba hii na usinijue tena, ama huyu
Malaya wako aondoke hapa nd’o uzungumze na mimi vizuri.” Ilikuwa sauti ya amri
kutoka kwa yule mwanamke huku wenzake wakiishabikia.
Naam!! Chriss akawa mdogo, alikuwa anatetemeka…..Chriss ambaye
nilikuwa nimempa nafasi katika moyo wangu huku nikiamini ni kiumbe pekee
anayeweza kunipa faraja, sasa nasikia akiambiwa kufanya maamuzi. Chriss
hakunitazama nilivyokuwa navuja damu, Chriss hakukumbuka hata machungu yangu
yote niliyomweleza hapo kabla na mbaya zaidi hakukumbuka kuwa niliwahi
kumuuliza swali kama ana mke ama la!! Hivi hakujua maana yangu, angenambia tu
ukweli, kwani wanaume wangapi wamenitumia hovyohovyo, kwani wangapi
wamenidanganya?? Ni dunia nzima ilikuwa imenigeuka si mbaya naye angekuwa
muwazi kwani nilikuwa na thamani gani tena, eeh nilikuwa na jipya gani mimi.
Haya yote aliyapuuzia, kumbe alikuwa anacheza na hisia zangu tena!! Alikuwa
anacheza na moyo uliopondeka naye akazidi kuuponda….
Kisha akapiga nyundo ya mwisho….Chriss akatoa kauli kwa kinywa
chake, taa ikiwa inawaka na jicho langu likimtazama.
“Isabela mke wangu nisamehe!!” alitamka, nikasikia mapigo ya
moyo kama yanataka kukatisha safari yake.
“Chris baba nimekwambia chukua maamuzi kwanza.”
“Nadia chukua nguo zako na uiache nyuma hii. Huyu ni mke wangu
na kila kitu kwangu” alisema Chris kwa sauti yenye kitetemeshi, bila shaka moyo
ulikuwa unamsuta!!.
Wanawake wanne na mwanaume mmoja wakawa wananipinga mimi!!
Unadhani ningejiteteaje? Nilikuwa pake yangu katika hii dunia!!
Na hapo nikaulaani moyo wangu!! Moyo uliodanganyika,
uliodanganywa na mwanaume. Mwandishi bado nakuambia nyie wote ni sawa unakataa,
unapata chuki unataka kuondoka chumbani bila kuaga unaleta hasira kwa kuambiwa
ukweli. Unakataa nini sasa unakataa nini nakwambia nyie wote ni walewale!! Haya
ondoka, endelea na hasira hizohizo, endelea ondoka mlango upo wazi, niache
nilie mwenyewe, nenda hata Desmund alienda, hata Chriss aliniacha, Danny naye
aliniacha, Jadida aliniacha, mama alinikataa akanilaani, baba na ndugu zangu
wote walienda na wewe nenda…nenda si nd’o ulichoamua…niache!!.....ne…ee…”
hakuweza kuendelea Nadia. Maneno yake yakanichoma, sikuweza kujizuia kulia,
nikamkimbilia Nadia na nikaweka uandishi pembeni nikalazimika kumuomba msamaha
Nadia. Haikuwa kazi ndogo!!USIKOSE NINI KITAENDELEA
Maoni 1 :
Inasikitisha kwa kweli
Chapisha Maoni