Pages

Alhamisi, Septemba 18, 2014

SIMULIZI YA MAISHA "USILIE NADIA" SEHEMU YA 13

HAIKUWA kama nilivyodhani kuwa Nadia alitakiwa kupumzika ili hasira zake zipungue, niliamua kuondoka kimyakimya bila kumuaga Nadia ambaye bado alikuwa anatetemeka.
“Unaenda wapi Gerlad!!” kwa mara ya kwanza aliniita kwa jina langu halisi. Nikakosa cha kujibu lakini sikuendelea zaidi nikalazimika kugeuka.

“Unaondoka kwa chuki kisa nimekueleza ukweli sivyo? Kisa nimesema kuwa nyie wote ni walewale. Kisa nimewasema sivyo!! Ulitaka nisiuseme ukweli ama, mwandishi hutakiwi kuchukia eti kisa tu wewe ni mwanaume. Haya basi tuseme kuwa nyinyi hamfanani, mbona nilipotoka pale nyumbani kwa Danny nikazidi kukutana na akina nyie na matatizo yenu yaleyale. Hivi kwani nyie wanaume huwa mnawaza nini? Ama labda niseme hivi nyie huwa mna cha huyu mbaya huyu mzuri!! Hamna mashaka kabisa kuwa mwingine anaweza kuwa jini. 

Hebu ‘imagine’ na hali yangu ile ya kutokea rumande, nimechakaa haswa, nimekonda na nina kidonda kibichi, jenga picha kuwa bado nikakutana na wanaume wanajifanya kunitamani. Huruma yenu ipo wapi? Nilikwambia kuwa nakiri kuwa wema hufa mapema, Jadida na Danny waliondoka mapema sana, ni hawa walikuwa wema kwangu na wakaondoka nikiwa nawahitaji. Tazama Danny amekufa bila hata kuniambia kwa nini Desmund alikuwa akiwachukia watu weupe, jibu ambalo nilikuwa nalitafuta siku zote” Nadia akatabasamu kidogo kisha akaendelea,


 “Ujue mwandishi labda nina hasira sana ama labda ni kwa sababu nasema kweli nd’o maana wanishangaa, ndio lazima unishangae maana si ndio zenu kuuchukia kweli, lakini amini kuwa hakuna kitu kizuri kama ukweli katika maisha haya, ni kweli kabisa kuwa ukweli unaumiza sana lakini unakuta mtu nimemwambia kabisa kuwa mimi sina cha kupoteza awe mkweli tu lakini bado anadanganya. Baada ya kuwa nimeondoka nyumbani kwa Danny aliyekuwa marehemu tayari huku sijui lolote kuhusu mama yake mzazi sikuwa na pa kwenda mjini Musoma. Nilitamani kumkabili Desmnd lakini nikagundua kuwa sijajipanga na mwisho wa siku nitarejea kulekule rumande na safari hii asingepatikana Danny mwingine kuweza kunikomboa, nikaingia mtaani, nikapata pikipiki ambayo nilitaka inipeleke moja kwa moja kituo cha mabasi.

“Unaenda kupanda basi muda huu dada ama!” mazoea yetu yalianzia hapa na huyu bwana ambaye uso wake nilipoutazama alionyesha kuwa mkarimu lakini sikutilia maanani maana hata Desmund alikuwa hivyo hivyo.
Nilikubali kuwa nahitaji kusafiri kuelekea Mwanza. Na hapa akanipinga sana kuwa hakuna mabasi muda huo na kwa pale Musoma mabasi hayana utaratibu wa kulazwa humo Stendi.
Kweli tulipofika hapakuwa na mabasi, na ni kama alinisoma akili yangu kuwa nilikuwa nina hofu lakini kuna jambo kama alishindwa kuniambia hata nilipomlipa pesa yake aliipokea kwa kinyongo. Alitamani sana kusema nami zaidi lakini sikuwa nikimpa ushirikiano. Akawasha pikipiki yake na kutoweka.
Alipoondoka ndipo hofu ikazidi kunitawala maana niligundua kuwa nimebaki katika upweke mwingine mpya. Katika kituo cha mabasi huku nyuma nikiwa nimeacha maiti katika chumba cha Danny. Na ni Danny alikuwa ameuwawa.
Nikiwa bado katika tafakari, upepo ukipuliza na baridi ikipenyeza katika mwili wangu nikapata wageni wa ghafla waliokuja kunighasi. Huenda ni jambo hili lilimtia hofu yule dereva wa pikipiki. Walikuwa ni vibaka!!

Wakanighasi huku na kule wakinilazimisha niwape pesa, katika kunitikisa mara simu ikadondoka wakaitwaa, wakaendelea kunibughudhi na hapo likatokea jambo jingine lililonifanya nistaajabu. Nilisikia kelele za mwanaume akiwafukuza wezi wale huku, nilipogeuka alikuwa ni dereva wa pikipiki akiwa na panga mkononi akielekea pale nilipokuwa, waler vibaka wakatoweka na ile simu.
Uzuri ni kwamba hawakunijeruhi.

“Nilijua nikikwambia mapema kuwa kuna vibaka maeneo haya ungeweza kunihisi vibaya sana maana hukuwa na ushirikiano katika mazungumzo yetu” aliniambia yule mwanaume huku akinishika mkono. Sasa nilifuata alichokuwa akiniambia, hofu ilikuwa imetanda upya, alikuwa ameninusuru kutoka katika mikono mibaya ya vibaka.

Akanipeleka katika pikipiki yake aliyokuwa ameiegesha mahali.
Akanichukua hadi nyumbani kwake!!!
Akalala chini akaniachia kitanda!!
Huu ukawa mwanzo wa kufahamiana na Christian.
Asubuhi aliniamsha mapema sana ili niwahi basi la kwenda Mwanza!! Lakini sikuitamani ardhi ya Mwanza ambayo ilishuhudia nikilawitiwa na haikusema chochote.
Chris akanisoma akili yangu na kuamua kuhoji! Lakini sikuwa tayari kumweleza lolote kuhusiana na mimi, lakini sikuitaka safari ya Mwanza. Nikahitaji hifadhi walau kwa siku mbili tatu niweze walau kumkabili Desmund ana kwa ana tena, kwa silaha yoyote nimwondoe duniani kisha nikamatwe nifungwe ama ninyongwe niende kumwomba msamaha mama yangu aliyeniachia laana hiyo.
Naam!! Sikutakiwa kuondoka katika mji huo!!

“Chriss…”
Alinitazama nami nikaendelea, “Sikufahamu hata kidogo nawe haunifahamu na bado umekuwa mwema kwangu. Asante sana kwa yote…..”
“Lakini unaonekana unatawaliwa na hofu!!...halafu kama nakuja vile” aliniambia huku akinitazama kwa makini.
“Sidhani kama unanijua lakini.”
“Ni kweli huenda mmefanana si unajua tena duniani wawiliwawili.”

“Wewe ni mwenyeji sana hapa Musoma.”
“Mi mwenyeji nimekulia hapahapa na hata kielimu changu kidogo nimechukulia hapahapa” alinijibu kwa ufasaha huku alkienda kuiwasha pikipiki ili anipeleke stendi.
“Inapendeza sana unapofanana na mke wa mheshimiwa bwana.” Alisema neno ambalo lilinishtua.
“Mheshimiwa gani tena jamani.”
“Diwani wetu aliwahi kuwa na mke kama wewe ila alitoweka kimyakimya si unajua tena waheshimiwa huenda alimpeleka kusoma ulaya”
“Diwani yupi? Nami kidogo mwenyeji hapa.”
“Huyu aliyeingia baada ya Kenyigo kuuwawa kwa risasi wanamuita Desmund!” alinijibu, moyo ukapasuka kusikia habari hiyo. Yaani Desmund ni diwani?? Tena anaitwa mheshimiwa!!
Desmund alimuua Kenyigo!!! Niliwaza, maana sijui tu kwanini niliwaza. Lakini nilihisi jambo hilo Desmund alimuua Kenyigo ili apate nafasi ya udiwani, alaa!! Ni hivyo maana miaka mitano ilikuwa haijapita bado ya kuweza kugombea udiwani.
“Vipi unamfahamu mheshimiwa?” aliniuliza huku akiendelea na mambo yake.
“Chriss, hebu njoo kidogo. Namfahamu Desmund namfahamu vyema.”
“Kivipi?”
“Nilikuwa mkewe.” Nikamjibu, akaacha yote aliyokuwa anafanya akanitazama kwa mshangao huku akiwa haamini hata kidogo.

“Chriss kama nilivyosema kuwa wewe hunijui nami sikujui na hata unastaajabu kwa nini sihitaji tena hiyo safari ya Mwanza, kama nitakuwa najipalia makaa ya moto na yaache yaniunguze lakini kama ni sahihi na iwe hivyo. Chriss kwa uliyonitendea usiku wa jana naamini wewe ni mtu unayejali. Naomba nikushirikishe kidogo juu yangu”….nikamuhadithia Chris dhuluma ambayo ananifanyia huyo mtu wanayemuita mheshimiwa. Nikamweleza asilimia hamsini kuhusu mimi, kisha nikamweleza juu ya mauaji yaliyofanyika usiku huo na hatimaye nikakutana naye akanipeleka mjini.

Chriss alistushwa sana na habari hiyo niliyomsimulia lakini sikuwa na namna nililazimika kutapatapa kama naweza kupata wa kuungana nami katika harakati hizo. Chriss alionekana kuwa mwelewa sana jambo lililonifariji sana.
Safari ikahairishwa, nikabaki nyumbani kwa Chriss huku nikiwa nimejitoa mhanga kwa lolote litakalotokea, na kwa mara nyingine nikakumbuka kumtukuza Mungu kwa yote anayonitendea huku nikiamini kuwa bado yupo upande wangu. Licha ya magumu yote ambayo nilikuwa napitia bado aliniunganisha na watu ambao walikuwa upande wangu.

Sikutakiwa kutoka nje kabisa wakati wa mchana, hivyo mambo yangu yote ya faragha nilifanya katika kiza kinene.
Kwa muda wa juma moja kilitokea ambacho nilitaraji, nikageuka kuwa mke wa Chriss kwa hiari yangu maana hakunibaka. Ni Chriss aliyekuwa ananipa habari zote zilizokuwa zinaendelea mtaani, nia yangu ilikuwa hali itulie ili niweze kutimiza azma yangu.
Usiku mmoja nilimuuliza Chriss swali moja tu ambalo lilinifanya niendelee kuwaona wanaume kuwa wote hawapendi kuwa wakweli. Nilimuuliza iwapo ana mke!! Akanijibu kuwa hajaoa na kama ikiwezekana atanioa mimi. Nilirudia swali hilo mara tatu na jibu likabakia kuwa lile la mwanzo.

Macho yake yaling’ara kabisa kwa nuru ya upendo. Alikuwa anaongea kwa hisia kali sana za kimapenzi.
Mwanzoni nilikuwa kama mtumwa tu wa mapenzi yake, yaani nilikuwa nafanya ilimradi tu kwa kuwa nafanya. Lakini taratibu nikawa nakolea na kujikuta nikimkaribisha Chriss katika moyo wangu.
Niliponyoa nywele zangu kichwani hakika nilibadilika, mavazi ya baibui yakanifanya sasa niwe huru kuwa natoka nje mara moja moja. Chriss ambaye alikuwa akifanya shughuli ya bodaboda alikuwa anatoka asubuhi akiwa amenichemshia chai ya maziwa na kuniwekea katika chupa, mchana alileta aidha chakula kikiwa tayari ama mboga nami ninapika akirudi jioni anapata chakula nyumbani. Uzuri pale hapakuwa na majirani maeneo ya karibu ambao wangeweza kuhoji chochote.

Licha ya kuwa anafanya shughuli za bodaboda alikuwa amejipanga kiasi chake, chumba na sebule vilikuwa vimesheheni haswa. Nami nikawa mama mwenye nyumba.
Mapenzi huondoa chuki, mapenzi hushinda vita, mapenjzi huweza kuisimamisha dunia kwa dakika kadhaa. Mapenzi ni kitu cha ajabu sana!!

Nimtafutie nini Desmund iwapo Chriss alikuwa akinipa mapenzi ya dhati, Desmund alinipenda kwa sababu nilikuwa nina pesa, lakini Chriss alinipenda kama nilivyo!! Hiyo ilikuwa tofauti kubwa sana kati ya wanaume hao.
Moyo wangu ukajifunza kusamehe, nikaamini huenda mama yangu ameifuta ile laana aliyonipa. Kama mama yangu amenifutia laana ni kwanini mimi nakuwa na kisasi moyoni mwangu? Nilijiuliza siku ambayo nilijipanga rasmi kwenda kumvamia mkewe Desmund katika mkutano wa kisiasa na kummaliza ikiwezekana.
Nilihudhuria mkutano ule huku nikiwa na silaha ya kisu kikali.

Lakini moyo ukawa mzito, na nikahisi kuwa huyu mama hana kosa, mbaya wangu mimi alikuwa ni Desmund. Ni huyo alifaa kuitumikia adhabu niliyokuwa nimeipanga!!
Nikajiuliza kuwa iwapo nitamujeruhi yule mama na kisha nikakamatwa, hiyo inamaanisha kuwa Desmund atabaki kuwa huru na akinicheka nikiwa jele!!
Hapana!! Nikahairisha nikaamua kujipa moyo kuwa nitampata Desmund! Ni huyu wa kunieleza jambo ambalo Danny alitaka kuniambia lakini wakamuua kabla hajanieleza. Nilimuhitaji Desmund anipe jibu hilo kabla sijaamua kumuua ama kumsamehe!!

Mwandishi katika haya maisha huwa tunapata shule kila siku na masomo ni mapya kila leo na waalimu pia ni wapya. Nililokutana nalo kwa Chriss ulikuwa mzigo hakika, mzigo mzito kutua….ewe moyo ulaaniwe!!
Ilikuwa saa sita usiku. Mimi sinahili wala lile nilikuwa natazama tamthilia za kifilipino sikuwa na mashaka juu ya Chriss ambaye alikuwa katika mihangaiko yake, haikuwa mara ya kwanza kwake kuchelewa nyumbani. Nikasikia mlango ukigongwa, nikaendakufungua huku nikiamini kuwa ni Chris ambaye nilikuwa namuita mume wangu kwa kipindi kile.
Mara!! Uso kwa uso kwa na mwnamke mnene mfupi rangi ya chokleti.
Nikamkaribisha lakini akaonekana kusita, akamuulizia Chriss. Nikamjibu kuwa hajatoka kazini na hapo pepo la wivu likanishawishi kumuuliza swali kuwa yeye ni nani.
“Ni rafiki yake tu!! Nitarudi baadaye.” Alinijibu kisha akaondoka akiniachia mchomo mkali wa wivu!! Ina maana Chriss ana wanawake nje!!
Nikazihifadhi hasira ili Chriss akirejea nimweleze.
Nilidhani atarejea Chriss kabla ya balaa lililotokea baada ya nusu saa. Mlango uligongwa tena, nikatambua kuwa atakuwa Chriss nikaufungua mlango kwa fujo!! Na hasira ikinitawala.
Uso wa uso na yule mama mfupi. Lakini sasa hakuwa mwenyewe alikuwa na wengine wanne, wote wakiwa na miili iliyoshiba haswa.
“Kwani wewe ni nani yake?” aliniuliza, nami nikapata fursa ya kumtambia kama yeye ni kimada basi mimi ni mke.
“Mimi ni mkewe…mama mwenye nyumba hii.” Niliwajibu.
Sikujua kama nimefanya kosa!! Nilisikia kauli moja tu..’unamchelewesha huyu Malaya!!’..kauli ambayo Desmund aliwahi kunieleza. Na hapo nikajikuta nimesukumwa nikaangukia katika kochi nikajigonga mgongo, nikiwa sijayahimili maumivu yale, yule mwanamke kibonge mfupi akanirukia na kuniangusha chini vizuri, akaanza kunikwangua na yale makucha yao marefu!! Neno Malaya likijirudia mara kwa mara.
Hadi wakati Chriss anafika nilikuwa hoi nikivuja damu na bado nilikuwa sijaelewa nini kinaendelea.
“We mpuuzi unataka upewe nini wewe…yaani kitanda changu, unalala na changudoa anajiita mama mwenye nyumba. Christian sihitaji kujua wala kusikia lolote kutoka kwako kabla hujafanya maamuzi kati ya haya mawili. Nikabidhi pikipiki yangu, utoke katika nyumba hii na usinijue tena, ama huyu Malaya wako aondoke hapa nd’o uzungumze na mimi vizuri.” Ilikuwa sauti ya amri kutoka kwa yule mwanamke huku wenzake wakiishabikia.
Naam!! Chriss akawa mdogo, alikuwa anatetemeka…..Chriss ambaye nilikuwa nimempa nafasi katika moyo wangu huku nikiamini ni kiumbe pekee anayeweza kunipa faraja, sasa nasikia akiambiwa kufanya maamuzi. Chriss hakunitazama nilivyokuwa navuja damu, Chriss hakukumbuka hata machungu yangu yote niliyomweleza hapo kabla na mbaya zaidi hakukumbuka kuwa niliwahi kumuuliza swali kama ana mke ama la!! Hivi hakujua maana yangu, angenambia tu ukweli, kwani wanaume wangapi wamenitumia hovyohovyo, kwani wangapi wamenidanganya?? Ni dunia nzima ilikuwa imenigeuka si mbaya naye angekuwa muwazi kwani nilikuwa na thamani gani tena, eeh nilikuwa na jipya gani mimi. Haya yote aliyapuuzia, kumbe alikuwa anacheza na hisia zangu tena!! Alikuwa anacheza na moyo uliopondeka naye akazidi kuuponda….

Kisha akapiga nyundo ya mwisho….Chriss akatoa kauli kwa kinywa chake, taa ikiwa inawaka na jicho langu likimtazama.
“Isabela mke wangu nisamehe!!” alitamka, nikasikia mapigo ya moyo kama yanataka kukatisha safari yake.
“Chris baba nimekwambia chukua maamuzi kwanza.”
“Nadia chukua nguo zako na uiache nyuma hii. Huyu ni mke wangu na kila kitu kwangu” alisema Chris kwa sauti yenye kitetemeshi, bila shaka moyo ulikuwa unamsuta!!.
Wanawake wanne na mwanaume mmoja wakawa wananipinga mimi!! Unadhani ningejiteteaje? Nilikuwa pake yangu katika hii dunia!!


Na hapo nikaulaani moyo wangu!! Moyo uliodanganyika, uliodanganywa na mwanaume. Mwandishi bado nakuambia nyie wote ni sawa unakataa, unapata chuki unataka kuondoka chumbani bila kuaga unaleta hasira kwa kuambiwa ukweli. Unakataa nini sasa unakataa nini nakwambia nyie wote ni walewale!! Haya ondoka, endelea na hasira hizohizo, endelea ondoka mlango upo wazi, niache nilie mwenyewe, nenda hata Desmund alienda, hata Chriss aliniacha, Danny naye aliniacha, Jadida aliniacha, mama alinikataa akanilaani, baba na ndugu zangu wote walienda na wewe nenda…nenda si nd’o ulichoamua…niache!!.....ne…ee…” hakuweza kuendelea Nadia. Maneno yake yakanichoma, sikuweza kujizuia kulia, nikamkimbilia Nadia na nikaweka uandishi pembeni nikalazimika kumuomba msamaha Nadia. Haikuwa kazi ndogo!!USIKOSE NINI KITAENDELEA

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Inasikitisha kwa kweli

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom