Pages

Jumatano, Septemba 24, 2014

SIMULIZI YA BADO MIMI SEHEMU YA 33


ILIPOISHIA
Baada ya kutafakari niliamua kukubali ombi la Renata, na sasa tuliongozana na mchungaji hadi nyumbani, hatimaye tulifika na kwa wakati huo Tumaini alikuwa yupo shule, na  mume wangu Charito alikuwa amekwenda kazini. Nilimkaribisha mchungaji James alipoingia tu pale sebuleni alisimama mlangoni na kusema "Mungu wangu, naomba uniongoze niweze kumtokomeza mtu huyu" Nilishtuka na kumtizama mchungaji ambaye alinisogelea na kunishika mkono mimi pamoja na Renata na kuanza kufanya maombi, alisali sana, baadaye nilihisi kama naishiwa nguvu wakati mchungaji akiwa anaomba hatimaye nilianguka chini, baadaye nilikuja kushtuka nikiwa nimeketi kwenye kochi na mchungaji James alikuwa amesimama na Renata wakiwa wananitizama. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 33.

INAPOENDELEA
Nilikuwa nimeishiwa nguvu, kwani miguu na mikono ilikuwa imelegea sana, nilimtizama mchungaji James nakusema "Mbona najisikia kuchoka sana, viungo vyote vinaniuma, kwanini, nimekuwa katika hali hii, najisikia vibaya sana" Mchungaji alinitizama na kisha alinishika mikono yote miwili huku akisema "Kandida,umezungukwa na nguvu kali sana za giza katika maisha yako, na sasa ni wakati wako wa kumrudia mwenyezi Mungu, na kuvunja vunja nguvu zote za giza zilizo ndani yako wewe pamoja na familia yako.  Katika nyumba yako kumezingirwa na nguvu za giza, na wewe umefumbwa macho usione kile kinachoendelea”.

Nilikuwa namsikiliza Yule mchungaji huku nikimtizama Renata aliyekuwa ametulia huku akitizama kwa makini. “Mchungaji naomba utusaidie, mfungue macho dada yangu aone yale mabaya yanayotendeka katika hii nyumba, kwani nimekuwa nikimueleza lakini haniamini kabisa,tusaidie mchungaji” Aliongea Rena na kwa wakati huo huo kabla hata mchungaji hajazungumza chochote, mlango wa pale sebuleni ulifunguliwa ghafla na alikuwa ni mdogo wangu Tumaini akiwa ameongozana na mume wangu Charito. 


Baada ya kuingia tu ndani Charito alimtizama mchungaji, aliyekuwa amesimama karibu yangu na kusema “Huyu ni nani? na ni nani aliyemkaribisha humu ndani, naomba aondoke mara moja, tena kabla sijamaliza kuzungumza naomba atoke nje, sasa hivi, atoke nje sitaki kumuona” Aliongea Charito kwa sauti ya ukali kiasi kwamba nilishindwa kuelewa kwanini amebadilika kiasi kile.

 kwani sikuwahi kuona hata sikumoja akiongea vile, Tumaini alikuwa amesimama pembeni bila ya kuzungumza chochote, Mdogo wangu Renata alimtizama shemeji yake na bila kusita akasema “Shemeji, huyu ni mchungaji James, amefika hapa kuiombea familia yetu, sizani kama upo sahihi kumfukuza” Charito alimtizama Renata kwa macho makali  sana kisha akasema “Funga bakuli lako, mjinga mkubwa wewe, sitaki kumuona huyo mtu hapa, takataka mkubwa, nimesema atoke nje sasa hivi, mimi namtambua mchungaji mmoja tu ambaye ni mchungaji Mkombozi, na pia wewe Renata ni mtoto mdogo sana kuanza kujibizana na mimi, na ukiendelea kuongea nitakupiga vibaya sana”  Wakati wote huo nilikuwa kama nimepigwa butwaa, kwani hali ya Charito kuwa mkali kiasi kile ilinishangaza.

 Mchungaji alikuwa ameshika Biblia, alisogea karibu huku akimkazia macho Charito kisha alisema“Wewe ni nani, ambaye unauwezo wa kunifukuza nikiwa nafanya kazi niliyotumwa na Mwenyezi Mungu, sikiliza nikuambie, wewe ndiye utakayeondoka, kwani kwa Mungu hakuna linaloshindikana” Aliongea mchungaji kwa kujiamini, na sasa Charito alishindwa kumjibu chochote, na haraka alifungua mlango na kutoka nje. Mchungaji alimsogelea Tumaini na kuanza kusali “Mungu wangu, wewe ni kila kitu katika maisha yetu, nakuomba ukamsaidie mtoto, Nguvu zako zikamsaidie awe huru ewe  Mungu nakuomba umsaidie, ni nguvu kali sana zimezingira maisha yake, lakini wewe pekee ndiye unayeweza kuoko maisha ya mtoto huyu”.

 Aliomba mchungaji ghafla Tumaini alianguka na kuanza kutapatapa chini kama mtu aliyekuwa anaugua ugonjwa wa kifafa, na kasha sauti kali nzito ilianza kuzungumza kutoka katika kinywa cha Tumaini na kusema “Niache nimalize, kazi yangu, siwezi kuachia huru, kwani siwezi kurudi kwa Bibi Bilionea nikiwa sijakamilisha alichonitu, nimesema sitoki niache nimalize kazi yangu” Ilikuwa ni sauti nzito sana ikiongea, nilibaki nikiwa nashangaa baada ya kusikia jina la Bibi Bilionea, moyoni mwangu niliwaza “Inamaana Bibi bilionea bado ananifuatilia, tena ndiyo amemfanya mdogo wangu kuwa katika hali hii, eeh Mungu wangu naomba utusimamie, wewe pekee ndiyo unaweza msaidie mdogo wangu.

 Wakati huo mchungaji alikuwa akiendelea kusali sana “Nasema utatoka tu, muachie huyu mtoto uondoke zako, sasa hivi natuma moto, ukutokomeze kabisa toka kwenda zako, huu ndiyo mwisho wako nimesema toka katika jina la Mungu Baba muumba Mbingu na Nchi. Tumaini aliendelea kutapatapa na mara ghafla alinyamaza na kutulia kimya kabisa, nilikuwa na hofu sana huku nikitetemeka lakini mchungaji James alinisihi nisiwe na hofu na kunitaka niketi, kwani kuna mambo ambayo alikuwa akitaka kuniuliza kuhusu maisha yangu. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA  34


Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Umeifanya fupi sana na inachelewa sana kutoka.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom