Jumatatu, Oktoba 13, 2014

SIMULIZI FUPI "MBINAFSI"

NA ADELA D KAVISHE
Ilikuwa ni kazi ambayo nilijua kabisa rafiki yangu Joyce angeweza kuifanya, moja kwa moja nilimpigia simu na kumjulisha ili aweze kupeleka vyeti vyake. Ni muda mrefu Joyce alikuwa akihangaika huku na kule kutafuta ajira hivyo niliamua kumsaidia ili aweze kufanikiwa kupata kazi. Baada ya kumueleza Joyce alifurahi sana na haraka alikwenda kupeleka vyeti vyake na baadaye alifanyiwa usaili, na baada ya wiki mbili tu alifanikiwa kupata kazi katika kampuni ya Sigara. Maisha yaliendelea na sasa wote tulikuwa na kazi. Siku moja  nikiwa nyumbani nimepumzika Joyce alifika huku akionekana kuwa mwenye furaha sana "Mary rafiki yangu, sasa mambo yangu ni mazuri, yaani hapa nilipo ninafuraha sana, yaani hata sijui nianzie wapi kukueleza".

 Nilimtizama huku nikionyesha tabasamu zito nikiwa na shauku kubwa la kutaka kujua kwanini Joyce alikuwa amefurahi kiasi kile "Ehee niambie rafiki kuna nini tena" Aliguna kidogo kisha akasogea na kuketi karibu yangu huku akinionyesha karatasi ambayo ilikuwa na maandishi ambayo nilishindwa kuyasoma kwa haraka kwasababu Joyce alikuwa akihangaisha mikono yake bila kutulia, "Yaani Mary mwenzio naenda Marekani umeona hii barua ni kwamba kuna nafasi za kazi, zimetoka hivyo na mimi nimejaza fomu na hivyo nimechaguliwa kwaajili ya kwenda kusoma na kufanya kazi, hapa nilipo ninafuraha isiyo na kifani".

 Nilifurahi sana kusikia rafiki yangu kipenzi ndoto zake zinakamilika  "Hongera sana (my dear) mpendwa, Mungu akutangulie, katika kila jambo hiyo ni hatua kubwa sana, sasa mbona hukuniambia na mimi mapema ningejaribu bahati yangu?" Joyce alicheka na kusema "Unajua hizi nafasi zilikuwa chache na maalumu kwa wafanyakazi  wa kampuni ninayofanyia kazi hivyo hata ningekuambia usingeweza kufanikiwa" Tulizungumza sana siku hiyo na nilimtakia kila la heri baadaye aliondoka.


 Baada ya wiki chache kupita Joyce akiwa anajiandaa kusafiri, siku hiyo nilikutana na kaka mmoja anaitwa Roy ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya sigara kaka huyu tulikuwa tukifahamiana muda mrefu sana na ndiye aliyenisadia kumuunganishia Joyce kupata  ajira katika kampuni yao, tulisalimiana kisha akaanza kusema "Mary, mbona umepuuzia bahati ya kwenda kusoma Marekani, kwanini sasa ulikataa kujaza fomu na nilimpa Joyce akuletee.

 Nilistaajabu aliponiambia kuwa huna mpango wa kuendelea kusoma, na tena unataka kuolewa hivi karibuni, kimya kimya rafiki yangu hata kunifahamisha" Nilimsikiliza Roy kwa umakini maneno aliyokuwa anazungumza nikabaki nimepigwa na butwaa na kunyamaza kimya kidogo kisha nikamjibu "Ati nini, mimi kuolewa, wapi na nani? Halafu mbona Joyce hakuwahi kunieleza chochote kuhusu, kujaza fomu ya kwenda kusoma nje ya nchi, na pia nilimuuuliza siku aliyokuja kunipa taarifa kuwa anakwenda Marekani kusoma, akaniambia nafasi hizo ni kwaajili ya wafanyakazi wa kampuni yenu pekee, sasa nashangaa kuona wewe unaniambia mimi nimechezea bahati inamaana Joyce ni mbinafsi kiasi hicho,

 Ama kweli shukurani ya punda mateke, na katika maisha tenda wema uende zako usingoje shukurani,  yaani hakumbuki wema niliomtendea, kumtafutia kazi hadi kafanikiwa  leo hii anashindwa kunishirikisha katika jambo kama hili haya bwana kama ndivyo alivyoamua" Roy alinitizama kwa macho ya upole na kusema "Daah pole sana, Mary, ila yote maisha, wewe achana naye endelea na maisha yako kwani kuna leo na kesho, na katika maisha binadamu shida haziishi, leo unaweza kumsaidia mtu akafikiri ndiyo amemaliza kila kitu akakupotezea, na kukuona hauna msaada tena lakini ipo siku atarudi kuomba msaada wako tena huku akijuta kwa alichokutendea."

 Nilisikitika sana siku hiyo, nilitamani kumpigia simu kumueleza lakini niliamua kukaa kimya kutokana na ushauri wa Roy, na kweli Mungu alivyo wa ajabu safari yake haikufanikiwa kwani kuna vigezo alikuwa hajakamilisha, na baada ya miezi mitatu, alikuja akasimamishwa kazi kutokana na ukosefu wa nidhamu kazini, alinifuata na kunieleza, huku akiniomba nimsaidie kutafuta kazi, siku hiyo sikutaka kubaki na dukuduku nililokuwa nalo moyoni ilinibidi nimuweke wazi kwa kile alichonitendea kipindi cha nyuma, alinisikiliza huku akiniomba msamaha, bila hiyana nilimsamehe, lakini moyoni mwangu nilijua kabisa Joyce siyo rafiki mzuri kwani nimbinafsi anataka kufanikiwa yeye pekee na si vinginevyo, na akishafanikiwa hakumbuki alipotokea.Ubinafsi ni kitu kibaya sana kwani katika maisha ni vyema kusaidiana katika kila jambo kwani huwezi kujua kesho itakuwaje na nani atakayekusaidia.

Maoni 3 :

Amor alisema ...

Yaani hadithi yako imetulia dada na inatulenga sisi Watanzania kwa kweli maana ubinafsi wetu wengine unaturudisha nyuma. Safi sana! Yaani siku yangu imeanza vizuri kwa kusoma hadithi yako. Kazana mama!

ADELA KAVISHE alisema ...

pamoja sana Amor

Unknown alisema ...

Waweza nitumia kwa njia ya audio watsup 0769517313 mana zaninogeajeee...!!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom