Ilipoishia
Nikavaa makubadhi yangu na yeye akajitanda kiremba chake tukafunga chumba na kutelemka chini!!! Huku nikiwa nina wahka wa kujua nini kilijiri??? USIKOSE SEHEMU YA 16
Inapoendelea
Nilimshika mkono Nadia tukakiacha chumba na kuteremsha chini
ambapo nia yetu ilikuwa kununua maji ya kunywa. Nadia alikuwa mchangamfu sana
tofauti na siku nyingine. Tukakifikia kibanda kidogo maalumu kwa huduma hizo
tukanunua chupa mbili za maji ya baridi. Nikafanya malipo tukarejea tena juu.
“Hivi keshokutwa nd’o safari eeh.” Aliniuliza. “Duh unakumbukumbu wewe, mi nilishaanza kunogewa na kanda ya
ziwa. Yah! Keshokutwa ndani ya basi tena Dar es salaam hiyo, umepamis eeh!!”
nilimjibu huku nikimtazama usoni ataipokea vipi ile hali. Niliamini anatamani
sana kufika Dar es salaam maana mazungumzo yetu ya awali kabisa hadi kufikia
hapo Mwanza kulikuwa na mazuri mengi sana tuliyoyataegemea jijini Dar es
salaam. Jiji hilo ungekuwa mwanzo wa kuungana tena na familia yake iliyobakia.
Nilikuwa nimemuhakikishia hilo, nami nilikuwa nimehakikishiwa na watu waliokuwa
wameniagiza.
“Dar es salaam, Dar es salaam, Dar Dar es salaam.” Nadia akawa
kama anayeimba kwa sauti ya chini, furaha ikapotea usoni mwake na macho yake
yakabadilika na kuwa mekundu tena, yakang’ara kwa ishara ya machozi muda
wowote.
Tukaufikia mlango wa chumba changu nikaufungua, Nadia
akatangulia kuingia na kujirusha kitandani. Mimi nikaweka vifaa vyangu vya
kurekodia sawasawia ili kama lipo neno kuhusiana na Dar es saalam ama chochote
kile aweze kunieleza nami nirekodi.
“Dar es salaam, dah marafiki zangu enzi hizo wal;ikuwa
wananitamani sana nilipowaambia kuwa naishi Dar es saalam, mimi pamoja na wao
tuliiona Dar kama paradise na mahali ambapo pana kila aina ya starehe.
Lakini tukasahau kuwa hata mateso pia yanaweza kuwepo, lakini
utayafahamu vipi mateso kama wewe mwenyewe hujawahi kuteseka. Shida ikukumbe
wewe nd’o utaweza kuhadithia vizuri, hata wewe mwandishi najua unanisikiliza
lakini huwezi kujua uchungu nilionao nikikwambia niliteseka.
Dar es salaam si mahali sahihi na niliingia huko nikiitwa
Mariam. Jina hili sijui kama lilikuwa sahihi kutoka kwa Jesca maana
liliniiingiza pabaya. Baada ya kutekwa na watu nisiowajua na kisha kutupwa
katika kile chumba cha watu ambao ni sahihi kuwaita wafu, aah!! Mzee Mwaijande
jamani…” alisita akaanza kulia kidogo kisha akaendelea.
“Kila wema upande wa Nadia hawadumu, yaani yule mzee angeishi
walau siku mbili hakika yasingenikuta yale yaliyonikuta, mzee wa watu
akajifia!! Na walimuua kwa mateso wale. Ni mzee Mwaijande alikuwa walau na
uwezo kidogo wa kuzungumza akanieleza kuwa nijipe pole kwani nipo katika tundu
baya tayari, tundu la kifo!! Sikumuelewa nikaendelea kumuhoji, akanieleza kuwa
kwa sababu mimi nina nguvu ningeweza kulikwepa japo ni hatari kuthubutu kutoroka.
Akaendelea kwa shida kuzungumza akaniambia kuwa yeye alikuwa katika ugomvi na
mtu akajikuta yumo humo ndani baada ya kuonekana ule ugomvi wa kuwania kiwanja
alikuwa akielekea kuushinda. Nayeye akawa kama mimi akashindwa kukiri kuwa yule
mpinzani wake ndiye aliyemtupa humo ndani.
“Kwani wewe uligombana na nani.”
“Na mzee Makorani wa hapo hivi Area C”
“Area C wapi tena mzee wangu.”
“Si hapa Dodoma ama wewe si mwenyeji!!” alinijibu bila
wasiwasi. Hapo sasa nikapagawa, mimi nilikuwa Mwanza, sasa naambiwa Dodoma.
Nikiwa katika hamaniko mara mwanamke mwingine akadai hapo tulipokuwa ni
Singida, mwingine akajikaza kazungumza kuwa tupo Mugumu Serengeti. Hapo sasa
nikatambua fika kuwa hakuna ajuaye ni wapi tulipo kila mmoja aliletwa bila
kujitambua.
Mzee Mwaijande akaendelea kuniambia kuwa humo kuna mawili ama
matatu kama yapo, lakini kubwa zaidi ni biashara ya madawa ya kulevya.
“Watakupasua tumbo lako na kuweka madawa yao, si unawaona
wenzako hao wote wamesafiri mara kadhaa.” Mwili ukanisisimka kusikia jambo lile.
Nilikuwa naona tu katika luninga mambo kama hayo ya mtu kupasuliwa tumbo na
kisha kuhifadhi madawa ya kulevya, sasa naambiwa kuwa na mimi nitakuwa mmoja
wao.
“Kama wewe ni mrembo wataanza na wewe kwanza kuwafurahisha na
baada ya hapo utawatumikia katika biashara yao. Wenzako hao wamekuja humu ndani
wakiwa warembo sasa wamejiishia. Mwingine anasema alikuwa Miss wapi sijui, miss
Upareni.” Aliposema hivyo nikazifdi kusisimka, kumbe miss Upareni hakufa
mwandishi, wala hakupotea katika mazingira ya kutatanisha alitekwa na kisha
nafasi yake ikachukuliwa na mtu mwingine. Niliduwaa kwa sababu niliwahi kusoma
katika gazeti tukio hilo.
“Lakini wewe unaweza kutoka hai humu ndani. Zipo njia zao mimi
kama mkongwe ninazifahamu. Hivi huu ni mwaka gani kwani?” aliniuliza.
Nikamtajia mwaka ambao nilifahamu tupo.
“Doh! Nimekaa miaka mitano humu sasa. Jitahidi utoke binti,
ukitoka wewe unaweza kutukomboa na sisi.” Alinisihi na mara milango
ikafunguliwa. Wakavutwa watu kadhaa wenye nguvu kiasi. Mimi wakaniacha, nikiwa
naduwaa mara wakarejea mara ya pili wakanichukua.
Nikakutana na mwili wa mzee Mwaijande ukiwa mfu tayari.
Niliwasikia wakipiga simu na kuwaeleza watu wao kuwa mzee alikuwa amechoka
tayari.
Naam simulizi yake ikaishia pale huku akiniacha bila kuijua
njia.
Kutoijua njia kukanisababisha nifike Dar es salaam,
walinisafirisha katika namna ileile ya kwanza. Sijui sasa kutoka katika nyumba
ile hadi Dar ni muda gani lakini pale Dar nikafikishwa katika hospitali ambayo
nimeisahau jina lakini inajulikana tu. Tukifika Dar nitakuonyesha. Mwandishi
nikiisikia Dar najisikia uchungu, yaani natamani isingekuwepo ama nisingefahamu
pale nilipokuwa ni wapi, lakini nilipafahamu na huyo Daktari niliwahi kumwona
hapo kabla. Daktari akanichoma sindano ya ganzi hapo nikiwa namuona, wamenifunga
kamba ngumu. Bora wangefanya hivyo nikiwa najaribu kujifungua mtoto lakini wao
walifanya vile kwa lengo lao la kunibebesha madawa ya kulevya.
Sijui ni kitu gani nilikuwa nimewakosea, nakumbuka nilipiga
kelele sana, lakini macho na midomo ikawa mizito. Nikasinzia.
Nilizindukia katika hospitali nyingine, huku sasa walikuwa ni
madaktari wengine wazungu. Nikajikuta nimeshonwa tumboni.
Bila shaka walikuwa wamenitumia tayari.
Nilijilaani na kukitamani kifo, lakini kila nilipotamani kufa
nikawa namkumbuka Desmund!! Sikutakiwa kufa, nikaamini hivyo.
Baada ya hapo nilipoteza fahamu tena na nikaibukia tena katika
kile chumba katika mji tusioujua wote kwa pamoja.
Ule usemi wa kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza ulichukua
nafasi yake baadaye kidogo. Nilikuwa napewa huduma nzuri sana, nikafanyishwa
mazoezi na mara nikawa nalazwa kitandani, sikuchanganyika tena na wale
wenzangu, sikujua wana nia gani mpya, nikaendelea kuvumilia. Hadi nilipopona
kabisa ndipo nikakutana na mzee wa kiarabu.
Mkutano wetu wa kwanza ulikuwa chumbani tukiwa wawili pekee.
Nikiwa uchi wa mnyama. Yeye alikuwa na taulo tu.
Mara akanisemesha kiarabu, nikaambulia baadhi ya maneno maana
nilijifunza kutoka kwa baba yangu enzi hizo lakini sikumjibu. Mara akanisogelea
na kuanza kunipapasa. Nikajua yale maneno ya Mwaijande yanatimia. Unadhani
ningefanya nini na ningekimbilia wapi? Akazidi kunipapasa. Hapo nikanyanyua
kinywa changu nikasema nisamehe kwa kiarabu. Akashtuka akaniangalia na kukoma
kunipapasa.
“Wewe unatoka wapi?” aliniuliza kwa kiarabu, hilo nalo
nikalinasa lakini kujibu ikawa kazi ngumu. Lakini nikajikakamua na kumjibu
niwezavyo, “Familia ya Barghash.” Nikajibu
Akaendelea kuzungumza harakaharaka nikamwambia simwelewi,
akajaribu kusema Kiswahili, naam Kiswahili kibovu kabisa.
Lakini afadhali nilinasa mawili matatu.
Akanieleza kuwa kama nikiwa mpenzi wake atanisaidia. Ningeanza
vipi kumkatalia wakati nilimkatalia mzee Matata na sasa nipo katika matata.
Uhusiano ukaanza siku ile!!
Uhusiano wa kujilazimisha ilimradi kama kweli ataweza anisaidie
nitoroke. Nilifanikiwa kujua kuwa yeye hakuwa na sauti ya mwisho, kwani kuna
mzee mmoja alikuwa akiamrisha na yeye anatii. Hapo nikajua kuwa kazi ipo.
Jicho la yule mzee mkuu zaidi sijui kama lilikuwa halijawahi
kuniona ama vipi, maana siku ambayo nilonana naye alikuwa kama zezeta
anayetazama nzi arukavyo na kutua. Akanipandiosha na kunishusha.
Baadaye akahitaji kuonana nami tukiwa wawili tu. Bahati nzuri
alikuwa anajua kiingereza na mimi hapo palikuwa nyumbani.
Tulizungumza mengi, na baada ya kutoka hapo nilikuwa na cheo.
Cheo katika taasisi nisiyoijua na mbaya zaidi hata sikujua ni nani amesababisha
nitupwe hapo na sikujua hata ni nchi gani.
Nikaanza kukitumikia kile cheo, jukumu langu likiwa kuhesabu
kila siku ni akina nani wapo hai na wangapi wamekufa! Hivyo tu, kila mmoja
alikuwa amefungwa namba mkononi ambayo ilikuwa haivuliwi hadi pale unapofariki.
Mwanzoni nilikuwa muoga sana kushuhudia mtu anavyokufa lakini
baadaye na hata sasa ua mtu mbele yangu na wala sitatikisa hata mkono.
Nilibadilishwa roho yangu na kuwa ya kinyama sana. Nikawa nawahesabu wenzangu,
kila siku lazima mmoja alikufa nikiwa naona. Kila walivyokuwa wanakufa nikawa
natamani kushuhudia kifo cha Desmund kwa macho yangu kwa mambo haya magumu
aliyonisababishia.
Lakini sikujua hata nilipokuwa.
Baadaye mkuu akanitaka kimapenzi na wakati huo Barakat alikuwa
mpenzi wangu. Sikumkataa na yeye nikamwachia anachotaka, sikuwa na thamani
mwandishi, thamani yangu ipo wapi? Kama sina uhuru ni kitu gani cha kunilinda?
Hakikuwepo….
Nilidhani mkuu yule waliyezoea kumuita masta alinitaka
kimapenzi tu kisha basi ajiondokee zake lakini mara akaniganda, kila baada ya
juma moja ananivamia na kunitaka kimapenzi.
Siku ya siku ambayo sikuwa naijua hata jina lake baada ya
kuishi kwa muda katika mazingira yale. Siku iliyonihamishia katika ukimbizi
mwingine.
Mwandishi yule masta alinifumania na Barakat, tulikuwa
tumekumbatiana tu kimahaba. Aisee mimi nilijifanya nimezoea kuona watu wakiwa
wafu ama wamekufa, kumbe kuna wenzangu wanajua kuua.
Masta alirusha sijui kitu gani kile kikauparaza mkono wa
Barakati ukawa kama unataka kukatika, Barakati naye akajitutumua akachomoa
jambia akarusha likapasua bega la masta. Hapo sasa wakavaana kimya kimya, mimi
nikajua yeyote yule atakayepona ataniua mimi..hapo nikaamua kutimua mbio,
kuelekea popote pale ambapo ningeweza kufikia tamati yangu.
Nilikimbia sana na huku nyuma nikasikia sauti ikiita jina
langu kwa namna, maana walizoea kuniita 105 (one zero Five)…nikaibaini ile
sauti kuwa ni ya yule masta, sikutaka kugeka maana kwa vyovyote vile nilikuwa
nakufa. Asingenipa muda wa kujieleza. Mara taa zikazimwa, giza kali na sikujua
naelekea wapi tena, lakini sikuacha kukimbia, nilizidi kupenya huku na kule,
mara nianguke nasimama tena, sikuwa na uhakika hata asilimia moja kuwa huko mbele
kuna njia maana sikuwahi kufika huko. Sauti ya masta sasa niliisikia kwa mbali
sana. Nikaendelea mbele, nikafikia vyuma nikajibamiza nakuanguka chini,
nikaisikia damu ikivuja kutoka katika midomo yangu.
Nikatulia pale huku nikikisikia kifua changu kikipiga filimbi
kila nilivyokuwa napumua. Giza tu ndo macho yangu yaliweza kuona. Nilibaki
kushika vyuma vile nikisubiri wafike na kuniua. Maana miguu ilikuwa inavuta
sana na sikuwa na nguvu za kuendelea kukimbia na hata ningekuwanazo ningekimbia
kwenda wapi??
Nikakumbuka kufanya sala ili Mungu anichukue kabla
hawajanifikia ikibidi. Wakati nasali sauti ya masta nayo ikazidi kusogea karibu
na masikio yangu.
Alikuwa anatukana matusi ya kiingereza, hakika alikuwa
amekasirika maana aliweka na kiapo kuwa akinikamata ananikata vipandevipande.
Mwandishi hata sala sikuweza kuimaliza, nikakisubiri kifo changu.
“Nakulaani Desmund na damu hii inayoenda kumwagika, roho hii
inayohukumiwa bila hatia Desmund popote ulipo, isiondoke roho hii kabla
haijakusulubisha wewe na ukoo wote na kizazi chako chote, Desmund nakufa
mimi…nakufa d’o kitu ulichokuwa unataka, lakini nakuaminisha kuwa upendo wangu
ulioulipa kwa mabaya haya utakusulubu maisha yako yote, na damu hii haitakauaka
kabla haujajutia….” Nilizungumza huku nikiisikia sauti yangu ikijirudiarudia.
Badala ya kusikia jibu kutoka kwa Desmund mara nikasikia
nikikamatwa mguu wangu!!
“Mpumbavu, Malaya mkubwa wewe.” Masta alikoroma kiingereza.Nadia nilikuwa nimekamatika.
Hilo likawa neno lake la mwisho kwa kiingereza akaanza kuzungumza
kiarabu cha ndani kabisa. Alinivuta lakini sikutaka kumfuata. Niliendelea
kung’ang’ania vyuma nilivyokuwa nimeshikilia. Lakini nilijua tu ni mfa maji
haishi kutapatapa…….” Akasita kisha akaendelea, “Yaani nimesema maji nd’o
nakumbuka tumenunua maji na hadi sasa hatujanywa!! Duh yasije yakawa ya moto
tena.” Alisema Nadia kisha akachukua maji nami nikatwaa yangu, hakika makoo
yalikuwa yamekaua haswaa!!USIKOSE SEHEMU YA 17
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni