ILIPOISHIA
Jonas atathubutu kutoa kilio niweze kumziba mdomo, hekaheka ziliendelea katika lile kochi bila shaka walikuwa wakibusiana, na walikuwa wamenogewa hadi pale honi ilipopigwa.
“Ndo hao
uliokuja nao.” Stephano aliuliza.
“Nimekuja naye
mmoja tu mbona, tumechukua teksi tu walishauri hivyo.” Alijibu mama Aswile sasa
niliweza kuisikia sauti yake vizuri.
“Mpenzi yaani
nd’o alikukwangua hivi?” mchungaji aliuliza.
“Mwendawazimu
sana yule mtoto, namfunga maisha haki ya Mungu!!” aliapa kwa hasira, nami
nikazidi kutetemeka lakini sikuhamisha macho kutoka machoni mwa Jonas. USIKOSE SEHEMU YA 23
INAPOENDELEA
“Kitu cha
msingi wewe muuzie kesi kuwa alimuua mzee wako, hapo tu utamaliza. Ushahidi wa
kutosha nitautoa mimi na Monica mtoto wako. Anafia jela huyu, na hapa ujue kitu
kimoja yaani akibaki tu ujue muda wowote ule tunaumbuka.” Mchungaji
alimsisitiza mama Aswile, na hapo wakasimama kisha wakatoka nje, kimya
kikatanda kidogo, nikatega sikio langu kwa makini kabisa na hapo nikasikia
vishindo kwa mbali. Wakaingia hadi sebuleni. Nikahesabu miguu iliyokuwa
inakatiza pale kupitia upenyo uliopoa chini ya kochi. Walikuwa watu wanne, wote
watu wazima.
“Kwa hiyo
yupo na mtoto sivyo.” Aliuliza mwanaume ambaye sauti yake niliitambua kuwa ipo
kiaskari.
“Yupo na
mtoto ndio, lakini mkorofi na ana nguvu ndo maana nataka tumshike wote yule…”
mama Aswile alisema kwa sauti ya uoga. Nikajisikia fahari kuwa kipigo
nilichokitoa kule nyumbani kiliacha heshima ya kutosha.
“Siwezi
kubabaishwa na msichana hata wakiwa kumi mimi.” Mchungaji Stephano alijitamba,
kisha akamalizia “Ila twende tu wote kama unavyosema.”
Wakatoweka
pale sebuleni, nami hapo nikafanya tukio la kutumia sekunde chache sana kuokoa
uhai na kuendelea na maisha yangu. Nikamkwapua Jonas, kisha nikanyata upesi na
kutokea mlango wa sebuleni, huko nikatimua mbio zaidi. Nikaikuta ile gari pale
nje, nikajifikiria kuingia ndani ya gari kisha niondoke nayo kwa sababu nilijua
kuendesha vyema lakini nikahofia kuzidisha kuyafanya mambo kuwa magumu zaidi.
Nikaamua kupita kona kadhaa hadi nikafika stendi, nikasimamisha gari, lilikuwa
lkimejaza sana na watu walinionea huruma sana kuwa nina mtoto sitaweza kupanda
lakini ni gari hilo nilikuwa nalihitaji.
Nikapanda
mwanaume mmoja akanisaidia kumbeba mtoto, gari likaondoka nikiwa nimebanwa
mlangoni.
Gari lilikuwa
linaelekea Mbalizi Mbeya, hapo mfukoni nikiwa na shilingi elfu mbili tu za
kitanzania. Sikuwahi kufika Mbalizi hapo kabla na wala hilo halikuwa lengo
langu. Kila kituo watu walikuwa wanashuka na hatimaye nikapata nafasi ya kukaa,
nikajipekua katika nguo zangu.
Alhamdulilah!!
Pesa haikuwepo, nikajipekua huku na kule, hakika pesa haikuwepo. Na katika
kipindi hicho yule kondakta alianza kudai nauli kwa watu wote ambao walikuwa
wamepandia njiani. Akili ilizunguka upesi sana nikijiuliza nafanya nini iliaweze
kunielewa kijana yule ambaye hakuwa na dalili zozote za huruma.
Hatimaye
akanifikia nikiwa nimempakata Jonas. Akanidai nauli yake. Nilimtazama kama
sijamsikia, na yeye akanidai tena nauli.
“Nimeibiwa
kaka yangu!!” hatimaye niliamua kuusema ukweli. Kondakta akaanza kucheka kwa
fedheha, ni kama hakuwa tayari kuniamini hata kwa mbali.
“Hadi kina
mama mnaanza kuwa wasanii siku hizi.” Akasema kauli hiyo, mimi sikusema lolote
lile.
“Haya bwana
sadaka yangu hiyo siku nyingi sijatoa sadaka wala sijaenda katika nyumba za
ibada.” Alisema kama anayetania kisha kweli akaniacha hadi niliposhuka Mbeya
mjini.
Nilijikuta tu
nikiona Mbalizi si mahali stahiki kwangu, hivyo nikaamua kuimalizia safari
yangu Mbeya mjini, walau hapo ningeweza kuwa karibu na huduma zozote za
dharula.
Ilikuwa ni
saa tano asubuhi wakati Jonas alipoanza kulia huku akilalamika njaa. Nilijaribu
kuitafuta tena na tena ile pesa ambayo awali niliikosa katika gari lakini
sikufanikiwa kuiona, nilitafuta kila mahali, nikajaribu kumbembeleza Jonas
lakini bado hakuonyesha dalili ya kunyamaza na alikuwa akihitaji chakula.
Ukimya wangu usingeweza kunisaidia kitu, nikatembea huku na kule hadi katika
mgahawa mmoja wa watu duni. Nikamkuta mwanaume akiwa ameketi na ni kama alikuwa
msimamizi wa mgahawa ule. Nikamwendea kwa heshima ya uoga.
Nikamsalimia
na kumweleza shida yangu.
“Baba mimi
nakuomba unisaidie, nioshe vyombo ama chochote ambacho naweza kusaidia hapa na
umpatie mwanangu chakula, mwanangu tu!! Mimi hakuna haja nitahimili lakini huyu
mtoto tangu asubuhi ya jana amekula wali kidogo tu!!” nilimsihi. Maneno
yakamgusa na bila shaka kilio cha Jonas kutoka mgongoni kiliam,sha hisia zake, wanawake waliokuwa
wafanyakazi pale wakawa wanamtazama ni maamuzi gani atachukua, nadhani hili
nalo lilimtia aibu zaidi.
Akafikia
hatua ya kunipa chakula bila kunifanyisha kazi yoyote, Jonas akala kwa fujo kabisa
kuonyesha kuwa alikuwa na njaa kali. Na mimi nikapewa sahani yangu nikala.
Hakika utu aliouonyesha yule baba ulikuwa wa aina yake. Nikamshukuru kwa utu
wake kisha nikamfunga mwanangu mgongoni tukaondoka nikiwa bado sijajua baada ya
kupata chakula mkile nini kinafuata?
Wazo kuu
nilitaka kujua nafika vipi katika mji wa Musoma tena kwa ajili ya kudai haki
yangu. Muda nao ulizidi kusogea kuikimbilia jioni nikiwa sina maamuzi thabiti, majira
ya jioni ya saa kumi na mbili na dakika kadhaa nilianza kuona hekaheka huku na
kule na baada ya dakika kadhaa nikaisikia adhana, hapa nikawaona watu wengi
wakiwa wamejikita katika kula na kunywa katika namna ya kuharakisha.
“Kuna nini
kwani?” nilimuuliza kijana mmoja muuza karanga aliyekuwa jirani nami.
“Mambo ya
kufuturu hayo.” Alijibu kwa ufupi. Ile kusikia neno futuru akili yangu nayo
ikapata uhai, si kwamba naweza kupata chakula cha bwelele jioni ile bali naweza
kupata na kitu kingine cha ziada cha kuniwezesha kufika ninapotaka. Sikuonyesha
mshtuko wowote na badala yake nilitabasamu tu lakini nilikuwa nimepata nguvu
mpya kabisa. Na hapo nikajihakikishia kuwa nitalala Mbeya kwa tabu usiku huo tu
lakini baada ya hapo nitaondoka na kufikia azma yangu vyema.
Nilikuwa
nimemuhoji maswali mengi sana yule kijana na alikuwa ameyajibu vyema, sasa
niliweza kuondoka na kutafuta mahali pa kufuturu. Kwa sababu nilikuwa muislamu
na niliijua miiko ya dini hiyo hata sikuhangaika sana, mwisho nikapata mahali
nikafuturu. Na kama bahati nyumba mbili baada ya mji ule kulikuwa na msiba,
nami nikajumuika katika msiba ule. Huko nikajishughulisha na shughuli mbili
tatu, lengo langu kuu likiwa ni kupata sehemu ya kulala, Jonas alipata fursa
nnyingine ya kucheza na watoto wenzake. Kweli nikalala na asubuhi kulipokucha
tu, nikaondoka na kuwa wa kwanza katika ofisi ya mabasi yaendayo jijini Dar es
salaam, nikavizia hadi nilipomuona mmiliki wa basi nililokuwa nalihitaji.
Alipoingia tu
na mimi nikaingia, nikazuiliwa mlangoni lakini nikajifanya kuwa ni abiria na nina
shida na bosi yule. Nikakubaliwa kuonana naye.
Nikaingia ana
kwa ana na mkurugenzi.
“Asalaamaleykum
Shehe…” nilimsalimia. Akanijibu na kunikaribisha.
Nikachukua
nafasi na moja kwa moja nikaingia katika mada iliyonileta.
“Mkuu, mimi
si ombaomba lakini nina shida. Nimelitafuta kimbilio sahihi katika jiji hili
nisilolijua na nimeona waweza kuwa mtatuzi sahihi. Shida yangu ni moja tu nisikupotezee
wakati wao kaka yangu. Nahitaji kufika jijini Dar es saam, nahitaji kufika
aidha kwa kusimama katika gari lako na kama ingekuwa inafaa hata kunihifadhi
katika sehemu ya kuhifadhia mizigo kwangu ni sawa. Nimetelekezwa jijini hapa,
naishi kwa kutangatanga, ukinisaidia tu kufika nyumbani sihitaji jambo lolote
lile jingine. Nahitaji tu kufika nyumbani, nikishushwa pale Ubungo tu mimi
nitakuwa nimefika, nitazame kwa jicho la huruma, kukataa kwako tu kunifikisha
huko basi kiumbe hiki mikononi mwangu kitalala nje tena kikipigwa baridi.
Usinionee huruma mimi na wala usitoe maamuzi yako kwa kunitazama mimi bali
kitazame kiumbe hiki mikononi mwangu. Sina hata senti tano ya kukinunulia
chakula, nisaidie ewe mkuu.” Nilimaliza kuzungumza nilichopanga kusema naye.
Maneno yale yakamgusa haswa. Akawa kama anayekosa kauli.
“Kama
haitawezekana nielekeze kwa wenzangu walio katika mfungo niwaeleze kama
watanisikiliza.” Nikauvunja ukimya. Kauli hiyo ikawa shabaha maana nilijua kuwa
amefunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, kukataa kwake jambo ambalo lipo ndani ya
uwezo wake ni kuiharibu funga yake, na kunielekeza kwenda kwa waislamu wengine
basi angekuwa anaikaribisha dhambi waziwazi na pia kuwa katika hatia kubwa.
“Sasa unajua
kusimamisha watu siku hizi hawaruhusu na basi langu haliruhusu kabisa…unaitwa
nani?” aliniuliza.
“Naitwa
Mariam bosi.” Nilimjibu kwa unyenyekevu mkuu.
“Mariam!! Mariam…haya
basi kesho njoo asubuhi tuangalie itakavyokuwa.” Aliniambia hatimaye, nikajua
kuwa tayari amenikubalia.
“Sijui
nikushukuru vipi kwa kunipa nafasi hii hadimu ya kunisikiliza, nitafika hapa
asubuhi sana” tuliagana akanipatia shilingi elfu tano.
Siku hiyo
sikucheza mbali na stendi kuu!! Na nililala msibani tena hadi alfajiri.
Yule
mkurugenzi akakutana nami asubuhi akampa maelekezo kondakta wake, kisha
akanieleza kuwa yule atanisimamia hadi nafika jijini.
“Funga yako
ni funga ya kweli!! Ubarikiwe sana” nilimweleza wakati naondoka kuingia ndani
ya gari na yeye akajibu ‘inshalah’ Wakati nilitegemea kuwa yule bwana
ameelekezwa kuwa nisimame ama nikae katika injini haikuwa hivyo, nilipatiwa
siti mbele kabisa. Nikakaa!!
Nikajishukuru
mwenyewe kwa ujasiri wangu kwani kama si hivyo aibu ingenikutia Mbeya.”
Kondakta
alikuwa karibu yangu na mara kwa mara alikuwa akinijulia hali, yeye pia alikuwa
mkarimu sana. Tuliingia Dar es salaam majira ya saa mbili usiku baada ya
kuharibikiwa gari maeneo ya Iringa.
“Njoo huku
dada.” Aliniongoza yule kondakta.
“Itabidi ukae
hapa mpaka nitakapokupa maelekezo zaidi aliyonipa.” Alimalizia nami
nikamsikiliza kwa makini na kumuelewa huku nikizidi kukumbuka ukarimu wa
mmiliki wa magari hayo.” Hapa Nadia akasita na kisha akapiga mwayo mrefu kabla
hajaketi vyema na kisha kuendelea.
“Mwandishi si
kila mtu anayekwambia amefunga ujue amefunga kweli kuna watu ni majambazi na
wenyewe unakuta wanajiita waumini safi kabisa mida ya mchana na wengine mchana
wananyenyekea lakini usiku ni wazinzi. Mtu unapoamua kufunga basi usifunge ili
fulani ajue wewe umefunga, maana utakuwa unajidanganya wewe mwenyewe, angalia
huyu Rama yaani tangu Mbeya hakutia kitu mfukoni na kila mara alidai kuwa
ameizoea swaumu tayari alizihesabu tasbihi mikononi na kila alipopata nafasi
alionekana kuwa katika tafakari nzito, hali iliyonipelekea kuamini kuwa bosi wa
kampuni ile alikuwa ameajiri watu makini na wacha Mungu sana, hata tulipofika
Ubungo bado niliendelea kuwa na imani juu ya kampuni hilo la usafirishaji.
Lakini
usilolijua ni sawa na usiku wa giza, kama Rama alikuwa vile kwangu bila shaka
kwa mtu yeyote yule angeweza kuwa vile na bado akaonekana mtiifu.
Rama
aliniweka pale hadi majira ya saa nne na nusu usiku, nilikula chakula kizuri na
Jonas alifurahia chakula alichokuwa anakitaka, mwisho Rama alifika na kunitaka
radhi kuwa alikuwa anafunga mahesabu kwa magari yote ya kampuni hiyo hapo ndipo
nikatambua kuwa yeye ni kondakta mkuu ama la alikuwa ndiye anayeaminiwa zaidi
na alipewa cheo fulani.
“Ujue
muheshimiwa akisikia upo hapa hadi muda huu atachachamaa sana.” Alisema tena katika
namna ya hofu kiasi, na hapo akanichukua na kuniongoza katika taksi. Mimi
nikiwa kama kondoo nafuata kile ninachoambiwa, taksi ilienda kwa mwendo mfupi
tukashuka na kuingia katika katika hoteli jirani tu na stendi ya Ubungo. Hapo tukaingia
katika hoteli hiyo ambayo nilihisi kuwa amelipia chumba tayari, akanipeleka
moja kwa moja hadi katika chumba hicho.
“Hii ndiyo
hoteli ya bosi, akiwa na wageni wake huwa wanafikia hapa na gharama zote juu
yake.” Alisema kauli ambayo ilinitoa hofu kabisa na kurejesha tumaini tena. Ukarimu
wa mkurugenzi ule ulikuwa wa aina yake.
Chumba
kilikuwa kikubwa!! Ramadhani akanielekeza kila kitu mle ndani na kisha yeye
akatoka na kuahidi kurejea baadaye iwapo itabidi.
Kauli yake
ikanitia utata, tayari ametukabidhi chumba sasa kwa namna gani tena anasema
atarejea wakati ni usiku mnene ule?
Nikaipuuza
kauli ile nikiamini ameitoa kimakosa, kwanza likuwa katika mfungo wa Ramadhani
kama lilivyo jina lake sikutegemea kama atataka kuwa karibu na msichana yeyote
yule kwani kwa kufanya hivyo ni kujikaribishia majaribu.
Kukumbuka
kuwa huo ulikuwa mwezi wa toba kukanitia nguvu!! Nikapanda kitandani na kulala,
niliangaza funguo niweze kufunga chumba sikuziona, nikajisahihisha kuwa huenda
ni ushamba wangu labda mlango ule haufungwi kwa funguo.
Baada ya hapo
nikajitupa kitandani na kujaribu kuutafuta usingizi huku nikiwa na maswali kuwa
kesho yangu itakuwa vipi………hapo nikamsahau Ramadhani..” Nadia akapiga tena
mwayo mrefu.
“Vipi ni njaa
ama!!!”
:Yaani kama
vile upo katika akili yangu, nina njaa kali kwakweli. Leo waambie walete chai
ya maziwa na chapatti maana siku nyingi sana sijala halafu nd’o zitatibu njaa
yangu.” Akanielekeza, nikanyanyua simu na kupiga kwa wahudumu. Nikasikilizwa,
kisha nikaambiwa muda si mrefu tutakidhiwa haja zetu.
Hapo sasa
maongezi yakawa juu ya vyakula mara Nadia aseme anapenda hiki nami namwambia
napenda kile, mara aseme hiki anajua kukipika mimi nijigambe najua kupika zaidi
yake. Mambo yalienda hivyo hadi muhudumu mnene alipokigonga chumba. Nikaenda
kukifungua nikampokea alichokuwa amebeba. Alikuwa anathema juu juu. Nadia akauliza
kulikoni.
“Nimepanda
ngazi aisee leo lifti mbovu.” Alilalamika huku akitweta. Mimi nikampa pole,
Nadia akaguna huku akibetua midomo.
Muhudumu
alipoondoka nikamuuliza Nadia kulikoni mbona anaguna.
“Si
namshangaa huyo kaka, yaani hivi vingazi sijui vingapi vinamtoa jasho hivyo,
dah kuna watu wamezoea raha duniani jamani. Hivi mwandishi hizo chai na mtoto
wa miaka miwili kipi kizito.’ Aliniuliza.
“Mtoto hata
kama ni wa mwaka mmoja atakuwa mzito kupita chai.” Nilimjibu.
“Na ghorofa
mbili na kumi na moja wapi kuna ngazi nyingi?” akauliza tena.
“We Nadia
nawe, ghorofa kumi na moja kuna ngazi nyingi mbona..”
“Sasa huyu
mkaka anavyolalamika hizi ngazi ngapi sijui je ingekuwa ngazi mia angeweza huyu
kweli ama ndo angefia njiani!!!”
“Sio yeye tu
hata mimi na wewe hakuna wa kupenya pale kirahisi bila kukomea njiani ama
kuchoka sana.” Nilimpinga Nadia. Hapa sasa badala ya kukaa vyema kunywa chai
akakaa vyema kusimulia ilimradi tu anithibitishie jambo analotaka kuniambia.
“G nitake
radhi, yaani hizo ngazi zinishinde…labda kama hujafikwa na matatizo wewe na
unaenda tu kwa starehe, lakini mimi niliziona chache sana siku hiyo. Tena ni
siku ile ambayo Rama alitupeleka katika kile chumba akidai kuwa ni bosi wake
amemwambia atuchukulie, mimi nikalala nimebweteka mara nasikia mpapaso, nakuja
kustuka nakutana na Rama. Akanifanyia ishara ya kukaa kimya. Nikaamka na
kuketi. Rama akataka kuendelea kunipapasa nikamzuia, hapo usingizi wote
ukaisha.
“Rama wewe si
umefunga wewe!!” nilimuhoji.
“Kufunga
mchana bwana muda huu nimefungua lakini.” Lijibu kwa kujiamini, nikamlaani yeye
na wengine wote ambao wanajifanya watakatifu mbele za watu wakati wakiwa
mafichoni wanafanya mambo yao ya hovyo kwa sababu tu hakuna awaonaye.
“Rama
hapana….” Nilikataa. Akaendelea kunipapasa.
“Sikia Mariam,
mimi ni kondakta mkuu hapo, na hiki chumba wala si bosi nimekuchukulia mimi
hapa upumzike mtoto mzuri, sasa wewe kigumu kwako nini eeh!! Wewe tufanye kisha
nitaongeza pesa utaishi hapa na mtoto wako mambo mengine tutaangalia
yanakuwaje.” Aliniongelesha katika maudhui ya kihuni, jambo ambalo sikupenda
kabisa. Rama alionekana kuzichukulia shida zangu kama mtaji, hivyo kwa
kuniambia tambo zile alijua kuwa lazima nitaingia mtegoni. Hakujua mimi ni wa
aina gani, hakujua kuwa kama isingekuwa kudhulumiwa ningekuwa na pesa na mali
nyingi tu na huenda tusingeweza kukutana katika mazingira yale katika namna
yoyote ile.
“Rama naomba
mimi nilale na kesho uniache tu nitaenda ninapojua kaka yangu.” Nikamsihi tena
lakini Rama hakuonekana kuwa tayari kuniacha wakati amegharamia chumba.
“Mariam eeh
acha utoto basi, kwani wewe bikra hadi ujifanye kubana, wamekuzalisha huko
wamekukimbia watu tunataka kukuweka mjini wewe unaleta pozi za kishamba hapa??”
sasa aliongea kama anayegombeza na wakati huohuo analazimisha.
“Rama
nakuomba ujiheshimu basi….ona aibu mwanangu huyu hapa unataka kunifanyia mambo
ya dharau kiasi hicho, acha Rama naomba utoke humu chumbani ama mimi na
mwanangu tutoke twende tunapojua.” Nilimsihi huku nikihisi jazba ikianza kunipanda,
Rama alikuwa ananikera na hapo hapo nikamkumbuka Ramso yule mwanaume
aliyenilawiti jijini Mwanza. Nikawachukia Rama wote, hakika nilijiaminisha kuwa
akina Rama wote ni walewale. Hasira ikanipanda maradufu, sasa nikawa najisikia
kutetemeka. Sikutaka aniguse tena, lakini alionekana kutojali.
“Kwani bila
haya mambo huyu mtoto ungempata mbona unaleta mambo ya kitoto kama umezaliwa
jana.” Aliniambia kwa jazba. Sasa alikuwa akinizongazonga kama anayelazimisha.
“Sikia
Mariam, kwani wewe unataka shilingi ngapi? Sema nikupe!!!”
“Rama
sihitaji chochote kutoka kwako, mimi sio changudoa, sijiuzi Rama.” Nilijitahidi
kuwa mstaarabu lakini bado haikuwezekana.USIKOSE SEHEMU YA 24
Maoni 1 :
tunaomba adella uendelee na simulizi ya kosa langu nini? au imwesha ili tujue mwisho wa joyce na fredi.asante
Chapisha Maoni