Pages

Jumatatu, Desemba 01, 2014

SIMULIZI FUPI "NAISHI KWA MATUMAINI NIPENDE KAMA NILIVYO" maalumu kwa SIKU YA UKIMWI DUNIANI. MTUNZI - ADELA D KAVISHE.
Haikuwa rahisi kukabilia na kila mwanaume aliyekuwa akieleza hisia zake juu yangu, ukweli ni kwamba wakati mwingine nilikuwa nikishindwa namna gani ya kuweza kukabiliana na hali ya kutongozwa na wanaume mbalimbali, siyo kwamba sikupenda kuwa na mpenzi, bali ilinibidi nisiwe katika mahusiano ya kimapenzi kwa wakati huo.

 Siku moja nikiwa njiani kuelekea shuleni ambapo nilikuwa nasoma katika chuo cha uhasibu, nikiwa njiani nilikutana na kaka mmoja anayeitwa Majaliwa, ambaye siku zote alikuwa hakati tamaa kuniambia kuwa ananipenda, aliponiona tu aliniita "Nyamboga wewe Nyamboga, tafadhali nakuomba unisubiri, kuna jambo nataka nikueleze" Nilisimama na kumsubiri, alisogea karibu huku akionyesha tabasamu pana katika paji la uso wake akasema "Nyamboga tafadhali nakuomba unipe nafasi katika moyo wako, nakupenda Nyamboga  tafadhali nikubalie ombi langu".


 Nilimtizama kwa umakini sana na kisha niliguna kidogo nakusema "Lakini Majaliwa, mimi nashindwa kukuelewa, unajua nilishakueleza wazi kuwa siwezi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wewe, na wala sihitaji mpenzi sasa nashangaa bado unanifuatilia, yaani labda nikueleze jambo moja kuwa mimi sikutaki na kamwe siwezi kuwa na wewe, nafikiri tumeelewana na pia nakuomba sana usiendelee kunisumbua" Nilimwambia kwa msisitizo kwani sasa nilikuwa nimechoka na porojo zake za kila siku.

 Majaliwa alinitizama kwa macho ya upole na kisha akasema "Yalaiti ungelijua ni kwa kiasi gani nakupenda, usingenijibu hivyo Nyamboga, unaniumiza moyo wangu, tafadhali naomba unifikirie, mimi nipo tayari kwa lolote juu yako, natamani uwe wa kwangu tuishi maisha mazuri iwe ni katika shida au raha milele tuweze kupendana, naomba ukanifikirie mpenzi".

 Sikutaka kuendelea kumsikiliza niliamua kuendelea na safari yangu, ya kwenda chuo.zilipita kama siku mbili tatu Majaliwa aliendelea kunifuatilia bila ya kukata tamaa. Siku moja nilikuwa nimekaa chumbani huku nikifikiria "Majaliwa ni kijana mzuri na pia anaonekana anaheshima sana, nahisi kumpenda pia ila hali yangu hairuhusu kuwa na mpenzi, mimi nilizaliwa na virusi vya Ukimwi na wazazi wangu walifariki nikiwa bado mdogo sana, pia malezi ya mama yangu mdogo siku zote amekuwa akinieleza ukweli kuhusu hali yangu, na kwamba nisije kuwa kama Baba yangu mzazi ambaye alijijua kuwa ni muathirika, lakini aliweza kumuambukiza Mama kwa makusudi, na kusababisha mimi kuzaliwa nikiwa na virusi vya Ukimwi.

 Siku zote nimekuwa nikiishi kwa kutumia dawa za kurefusha maisha (ARV), siri hii naijua mimi lakini watu wanaonizunguka marafiki zangu hawajui chochote kuhusu hali yangu, na hata mtu akinitizama hawezi kujua kama naishi na virusi vya Ukimwi, namshukuru Mungu amenijalia kuwa na sura nzuri na umbo zuri la kuvutia, lakini nikifikiria umri wangu unazidi kwenda na kila siku nazidi kuwa mrembo, na wanaume wamekuwa wakirusha ndoano zao kila mmoja kujaribu bahati yake, lakini mimi najua siwezi kuwa na mpenzi kwani hawa wanaume wanaonitongoza ikitokea wakagundua kuwa naishi na virusi vya ukimwi wote watanikimbia".

 Nilikuwa nikiwaza nakujiuliza mambo mengi sana, Maisha yangu nilikuwa nimejikubali kwa hali yangu niliyonayo, Maisha yaliendelea Majaliwa aliendelea kunifuatilia ilifikia kipindi tukawa marafiki, ijapokuwa alikuwa akitaka urafiki wetu uwe zaidi na kuwa wapenzi, lakini mimi niliendelea kuwa na  msimamo hivyo tulibaki kuwa marafiki wa kushirikiana katika mambo mbalimbali.

 Moyo wangu ulikuwa ukivutiwa sana na Majaliwa lakini nilijitahidi sana kuzuia hisia zangu lisitokee jambo lolote, tuliendelea hivyohivyo hadi siku moja ambapo tulikuwa tumetoka na kwenda katika mgahawa mmoja tulivu maeneo ya mikocheni, Majaliwa alikuwa akinitizama sana na kisha akaanza kuzungumza "Unajua Nyamboga tumekuwa marafiki kwa muda mrefu sana, kuna jambo ningependa nikueleze" Nilimtizama na kisha nikasema "Hapana Majaliwa kama unataka kuzungumzia suala la mapenzi, mimi nitaondoka, nafikiri unalijua hilo mimi na wewe ni marafiki tu ibaki kuwa hivyo".

 Majaliwa alinitizama na kisha alishusha pumzi na kusema "Nimekuelewa Nyamboga, jambo nililokuwa nataka kusema ni kuwa mimi hapa nilipo ni.....yaani sijui hata nisemeje na sijui utanielewaje ila....mimi..." Alikuwa akizungumza kwa sauti iliyojaa wasiwasi sana, nilishindwa kuelewa ni kitu gani kilichokuwa kinamsumbua. "Vipi una nini Majaliwa? Sema tu usiwe na wasiwasi naweza kukusaidia katika ushauri".

 Majaliwa alijisogeza na kisha aliinamisha kichwa chini nakusema "Nyamboga, nakupenda sana, wewe ni kila kitu kwangu ijapokuwa najua huwezi kuwa mpenzi wangu, ila naomba niwe muwazi kwako mimi naishi na virusi vya Ukimwi kwa muda mrefu sasa, niliambukizwa na dada mmoja ambaye kwasasa amekwisha fariki, na hapa nilipo naishi kwa kutumia dawa za kurefusha maisha, huku ndugu zangu wakiwa wananifariji na kunifanya niishi maisha ya kawaida. Kwani nimejikubali na najipenda, siku zote katika maisha yangu niliapa kuwa sintoweza kumuambukiza mtu kwa makusudi, naongea yote haya kutoka moyoni kwasababu nakupenda na wewe ukiwa ni rafiki yangu ambaye nakupenda sana".

 Nilihisi kuishiwa nguvu baada ya Majaliwa kuzungumza maneno yale nilimtizama kama takribani dakika moja na kisha nikasema "Usihofu Majaliwa, nimekusikiliza kwa makini sana, najua sikuzote ulikuwa ukijiuliza kwanini mimi nilikuwa nikikataa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wewe, naomba niwe muwazi kwako mimi pia nilizaliwa nikiwa na virusi vya Ukimwi na siku zote nilisema siwezi kuambukiza Ukimwi kwa makusudi, nimefurahi na nakupongeza kwa ujasiri wako wa kuwa muwazi kwangu, yaani umenipa ujasiri na mimi pia kwani nilikuwa na hofu sana kumueleza mtu juu ya hali yangu asante sana Majaliwa"

 Tulikumbatiana kwa faraja kubwa na kupeana matumaini, siku zote tulikuwa marafiki, na hatimaye tuliamua kuanzisha kikundi cha kusaidia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi. huku tukishirikiana na baadhi ya taasisi ambazo zilitusaidia kwa kiasi kikubwa hivyo tulikuwa tukitembelea vituo mbalimbali vya watoto na kadhalika huku tukitoa misaada mbalimbali, kama nguo,sabuni,mafuta ya kupikia na vitu vingine vingi. Nilikuwa huru kujielezea hali yangu bila wasiwasi na kuwatia watu moyo namna ya kuishi kwa matumaini, Maisha yaliendelea hatimaye tulikuja kufunga pingu za maisha na Majaliwa, na huku tukiendelea kuishi kwa matumaini.

KAULI MBIU YA SIKU YA UKIMWI MWAKA 2014
 "Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, Vifo vitokanavyo na Ukimwi, Ubaguzi na Unyanyapaa inawezekana"

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom