ILIPOISHIA
“Kwani bila
haya mambo huyu mtoto ungempata mbona unaleta mambo ya kitoto kama umezaliwa
jana.” Aliniambia kwa jazba. Sasa alikuwa akinizongazonga kama anayelazimisha.
“Sikia
Mariam, kwani wewe unataka shilingi ngapi? Sema nikupe!!!”
INAPOENDELEA
Mara Rama akaniachia, akaenda katika kiti kilichokuwa wazi pale chumbani, chini ya kiti akatoka na kibegi kidogo, akakifungua. Akatoka na mabulungutu ya pesa.
“Tatizo
unanichukulia poa sana Mariam, haya sema unataka shilingi ngapi unipe.”
Aliniambia huku akitoa noti nyingi na kunirushia pale kitandani.
Ni kweli
nilikuwa nahitaji sana pesa lakini sikuwa tayari kuwa mwepesi kiasi nkile, Rama
alitaka kunidhalilisha na alikuwa anataka kuyafanya hayo katika mwezi mtukufu.
Hakika nilikuwa na dhambi nyingi lakini sikutaka kumwingiza Rama katika dhambi
ile ya kuzini katika mwezi mtukufu.
“Rama
….SITAKI!!” sasa nilimwambia kwa ukali.
“UTATAKA!!”
alinikaripia na sasa alinikamata kwa nguvu. Rama alikuwa na nia ya kuniingilia
kwa nguvu. Sikuwa na msaada zaidi ya mwanangu pale kitandani. Rama alikuwa na
nguvu sana lakini nilijilazimisha nikafurukuta huku na kule kumwepuka, mbaya
zaidi nilikuwa nimelala na nguo ya ndani pekee.
Mara Rama
akaruka chini na kutua katika kibegi kile akakipapasa huku na kule, akachomoka na bisibisi.
“Ukijifanya
mjanja Mariam nakuchomachoma tumboni.” Alinitisha na hakuonekana kutania, karipio
lake likamshtua Jonas, akagutuka kutoka usingizini, akabaki kushangashangaa.
Rama hakuonyesha kushtuka wala, akaendelea kunisogelea. Hakika alikuwa amenuia
kunifanyia kitu kibaya.
“Haya Rama
nimekubali.” Nilisalimu amri, nikanyanyua mikono juu. Na hapa Rama akafanya
kosa ambalo wanaume wewngi hulifanya na kisha kuukosa hata muda wa kujuta.
Kosa la
kumwamini msichana upesiupesi!! Rama akaweka bisibisi chini kisha akatoa nguo
zake, akabaki kama alivyozaliwa, akanisogelea na mimi ili aweze kunitoa nguo
yangu iliyobakia, nikamruhusu akanisogelea. Lakini akili ikiwa haijakubali
kudhalilishwa mbele ya mtoto wangu JONAS……
Rama akawa
ananivua huku akininong’oneza maneno ya kimapenzi. Alipopanda kitandani
nikapata fursa ya kufanya nilichokiota. Kabla ya kukifanya nikamshukuru Mungu
kwa sababu ananipa akili mara kwa mara na huku akinipa nafasi moja tu ya
kufanya maajabu.
Upesi
nikamkumbatia Rama kimahaba, akajua nimekolea halafu sekunde hizohizo
nikamgeuza yeye chini mimi juu. Halafu mwisho nikamrusha kwenda sakafuni nikiwa
juu yake. Kichwa chake kilitua katika marumaru ya pale chumbani. Rama hakupiga
kelele na ule ulikuwa mwisho wa ile jeuri yake, na hapo nikashuhudia damu
zikimchuruzika kutoka katika kichwa chake na kutapaka kwa haraka sana.
Nikamnyakua
mwanangu na kuanza kushuka ngazi kuelekea chini. Nilishuka kwa mwendo wa kasi
na sikukumbuka kama ile ilikuwa ghorofa ya kumi juu, ajabu sasa sikuchoka wala
kupata dalili ya kuchoka.
Nilipofiuka ghorofa ya pili kwenda chini nikakumbuka
jambo la msingi zaidi.
Pesa!! Yule
mtu niliyemuacha anavuja damu pale chini alikuwa na pesa. Hapo hapo nikageuza
na kupanda kazi, Jonas alikuwa analalamika lakini sikujali. Nikarejea kule
chumba kwa tahadhari kubwa, nikaingia na kuchukua lile begi. Kwa mwendo wa
haraka tena nikaanza kushuka zile ngazi, G nikikwambia kuwa huyu muhudumu
aliyekuja kutuhudumia ni mzembe naomba uniamini, sawa baadaye niligundua kuwa
nilichoka sana lakini cha muhimu ni kwamba nilishusha nikapandisha na
nikashusha tena.
Mapokezi
nilimkuta yule msichana wa mapokezi amelala, mlango ulikuwa umefungwa.
Nikamwamsha
akaamka na kuniuliza kulikoni saa tisa usiku nahitaji kutoka.
“Nimegomaba
na mpenzi wangu…hivyo tu..sitaki kuwa hapa tena.” Nilijibu kiujasiri.
Akajizoazoa taratibu, nilitamani kumtusi lakini ningezua mengine na kumjengea
wasiwasi, mwisho akanifungulia mlango nikatoka nikiwa na Jonas wangu mikononi.
Na begi la pesa likiwa pamoja nasi.
Nikachukua
taksi na kumuamuru dereva atupeleke Mbezi ya Kimara. Nikapekua lile begi
nikavuta noti ya shilingi elfu kumi.
Nikampa
dereva akakanyaga mafuta gari ikatoweka. Barabara ilikuwa tupu hadi tunafika
Mbezi mwisho. Nikashuka bila kuonyesha wasiwasi wowote, na hapo nikaangaza huku
na kule nikaona kibao kinachoonyesha nyumba ya kulala wageni, nikajongea huku
nikitembea kijasiri sana.
Bahati ikawa
upande wetu tena tukapata chumba, nikawalipa tukakabidhiwa chumba chetu. Humo
ndani hata Jonas naye hakutaka kulala alikuwa na furaha sana na alikuwa
akichekacheka, amakweli pesa sabuni ya roho.
Nikahesabu
mafungumafungu yote ya pesa na kufanikiwa kiwepesi kugundua kuwa jumla ilikuwa
takribani milioni moja na laki tano.
Katika
mahesabu hayo juu palikuwa na kikaratasi, kilikuwa na namba ya akaunti.
Jina lilikuwa
la kampuni ya yule mfadhili wangu wa kutoka Mbeya!! Nilijisikia vibaya sana kwa
kuwa zile pesa zilikuwa mikononi mwangu na ikiwa ni hasara kwa mtu
aliyenifadhili, hapohapo nikajisafisha na kudai kuwa mimi si mkosefu wa
kulaumiwa ni Rama.
Nililala
nikiwa nimelikumbatia lile begi imara kabisa mikononi mwangu.
Asubuhi saa
kumi na mbili nilimchukua Jonas mgongoni mwangu na kuondoka kuelekea barabarani
ambapo tulisubiri mabasi yaendayo Mwanza yenye utaratibu wa kuchukua abiria
barabarani.
Naam!
Nikapata basi mimi na Jonas tukaingia humo na bahati nzuri zaidi tukapata
nafasi ya kuketi. Nilikuwa nimeandaa pesa ya nauli tayari tayari hivyo
sikulifungua tena lile begi.
Safari
ikaendelea ya kuliacha jiji la Dar es salaam. Nilifumba macho yangu na kuduwaa
ni kwa namna gani maisha yanaenda kasi namna ile, ndani ya juma moja tu yalikuwa
yametokea mambo mengi sana katika maisha yangu. Nilikuwa nimepigana na familia
ya mzee Aswile, nilikuwa nimekutana na mchungaji mnafiki Stephano, nilikuwa
nimeponea tundu la sindano kukamatwana polisi, nililala nje jijini Mbeya,
nilikutana na mkurugenzi wa mabasi na nilisafirishwa kuja Dar, nimekutana na
Rama na tumefarakana nikamsukuma chini, sasa nina pesa nyingi na nipo safarini
kuelekea jijini Mwanza. Safari ambayo sijui kwa nini naenda huko lakini ndo mji
pekee ambao ulikuja ghafla katika kichwa changu. Wewe G wewe hivi unataka shida
yako nisile chapatti zangu ama, mwee!! Nina njaa mwenzio tena nina njaa kweli.”
Nadia alisema haya huku akifungua chupa ya chai, kisha akamimina katika vikombe
vyote viwili, na hapo tukaanza kushughulika na mambo ya chai. Simulizi ile
ikakaa kando.
****
“Kuna
wanadamu wenyewe wameumbwa wakiwa na huruma tu, wameumbwa wakiwa na mioyo ya
kujitolea tu, wana maisha magumu lakini wanapoweza kujitolea wanajitolea. Wanadamu
kama hawa ni wachache sana, yaani wenyewe hali haziwabadili maana walipewa
mioyo ya uaminifu, hakika uaminifu unaweza kumponza na kumpoteza kabisa mtu
lakini hawa hawataki kujua kuhusu hayo kabisa.” Nadia alianza tena kusimulia
baada ya kumaliza kunywa chai.
“Nilipofika
Mwanza niliuhesabu kuwa mkoa ambao ulikuwa mbaya sana kwangu na mkoa ulionipa
machungu mengi, lakini bado ilikuwa lazima nipite hapo ili niweze kufika mkoani
Mara, wilaya ya Musoma. Kama kawaida tena nililala nyumba ya wageni, asubuni
sana nilikuwa macho, kutazama saa ukutani ilikuwa ni saa kumi na moja na nusu.
Kuna mtu
nilimuwaza kabla sijalal usiku uliopita hivyo nikaamua kwenda kumtafuta.
Nilipenya huku na kule hadi nikaifikia nyumba aliyokuwa amepanga wakati ule.
Nilikuwa na mashaka sana kuwa huenda aliwahi kuhama hivyo nilifanya kama
kubahatisha.
Ajabu
nilimkuta akiwa anaishi pale pale, niligonga mlango wake akaufungua, mwanzoni
hakunitambua lakini baada ya sekunde kadhaa akanitambua. Akanirukia kwa nguvu
na kunikumbatia, hakuamini hata kidogo kama ni mimi nilikuwa mbele yake. Huyu
alikuwa ni yule dada ambaye wakati nikiwa baamedi niliwahi kuishi kwake, na ni
huyu aliyekuwa wa mwisho kuniona jijini Mwanza wakati ule nikikabiliwa na kesi
ya kumuua bosi wangu. Hata nilipoishi na Jesca kwa wiki kadhaa kabla
hajanisaliti na kujikuta akiingia safari nyingine nami nyingine sikupata nafasi
ya kwenda kuonana na dada yule. Lakini sasa alikuwa mtu wa muhimu sana kwangu.
Akanisikiliza
vyema nikamueleza juu juu shida zangu, kubwa zaidi ilikuwa juu ya Jonas,
nikamweleza kuwa nahitaji kuwa huru kiasi fulani katika kuzikabili changamoto
kadhaa za maisha yangu kwa takribani siku kumi tu hivyo nilihitaji sana Jonas
abaki naye pale halafu nikirejea nitamchukua. Yule dada hakupinga japo
alijaribu kunieleza ugumu wa maisha alionao kwa kipindi kile, alikuwa hana kazi
na aliishi kwa kubangaiza bangaiza hivyo hofu yake kuu ilikuwa ni kwa namna
gani ataishi na Jonas. Nikakumbuka ile siku ananipatia shilingi elfu ishirini
nikiwa naenda Musoma, alikuwa mpole na mwenye huruma na hata sasa alikuwa
katika hali hiyo, huu ukawa wakati wangu wa kumwachia chochote kitu,
nikajipekua katika ule mkoba nikatoa shilingi laki tatu na kumpatia kama
matumizi, hakuamini kabisa akakodoa macho lakini nikamwondoa mashaka,
nikamweleza kuwa naenda kufuatilia mali zangu nilizodhulumiwa Musoma.
Baada ya
makubaliano nikambusu Jonas shavuni, na
kumpa yule dada mkono wa heri tukaagana.
Majira ya saa
kumi na mbili asubuhi hiyohiyo nilikuwa katika basi kuelekea Musoma. Sasa
sikuwa na uoga tena moyoni, nilikuwa na kiasi cha pesa ambacho niliamini
sitapata shida Musoma kwa namna yoyote, safari nzima niliwaza ni adhabu gani
ambayo Desmund anayejiita muheshimiwa diwani anastahili, nikamuwazia pia mzee
Matata ambaye alikuwa mtuhumiwa wangu wa kwanza kumuhisi kuwa alinbitupa katika
domo la mamba na nikaokolewa kimiujiza. Huyu kama angekiri ni yeye ni hapo
ningejua nini cha kumfanya.
Nilipofika Musoma nilinunua wigi jeusi na
miwani nyeusi vilevile, nikaliweka kichwani, kisha nikaanza kutembea kwa
kujiamini kabisa, sikutaka kulala kabisa, nikazunguka huku na kule hatimaye
nikapata magari ya kukodisha. Tatizo lilikuwa moja sikuwa na mdhamini wa
kuniwezesha kupewa gari lile mimi kama mimi, hivyo nilitakiwa kuwa na dereva
wao ambaye atakuwa nami kila kona. Jambo hilo sikulitaka hata kidogo, nilihitaji
kuwa peke yangu.
Nikaamua
kuachana na magari ya kukodi, nikaamua kwenda moja kwa moja jirani na duka
kubwa la mke wa Desmund, pale dukani hakuwepo yeye, nikaenda pale kama mnunuzi
wa kawaida tu nikamkuta kijana wa kichaga, nikamchangamkia mara ninunue hiki
mara kile ilimradi tu niweze kujua mambo kadhaa ambayo yangeweza kuja
kunisaidia baada ya siku chache. Mara akaja mtoto mdogo pale, nikajifanya
kustuka.
“Mh!! Mtoto
wa muheshimiwa huyu ama…” nilijisemesha kama nisiyekuwa na athari.
“Mtoto wa
mheshimiwa shangazi yangu.” Alinijibu bila kutilia maanani anachokijibu.
Sikuendelea kuhoji juu ya jibu hilo badala yake nikahamia kwa yule mtoto.
Nikamsemesha
semesha huku nikiwa mchangamfu sana na moyoni nikiwa na hasira kali, mtoto
akawa ananijibu maswali yangu yote vizuri, akaniambia shule anayosoma
akaniambia umri wake na mengine mengi.
Moyo uliniuma
sana nikajisikia aibu kuu, kumbe Desmund alikuwa ana mtoto wakati nipo naye
katika mahusiano, Desmund hakujali hata kidogo kilio changu juu ya lini
tutapata mtoto wetu, kumbe nd’o maana alikuwa mwepesi kunibadilikia, kunipiga
na kunisulubu awezavyo! Kumbe tayari ana mtoto wake wa kumzaa, hakika niliumia
sana. Lakini mbele ya yule mtoto sikuacha kulitoa tabasamu langu.
Baada ya
kulipia vikorokoro nilivyovinunua niliondoka pale.
Nikatafuta
chumba nikajipumzisha huku nikiufikiria unyama wa Desmund ambaye anaheshimika
kabisa kama diwani wa kata yake. Diwani mwongo, mtesaji na muuaji kabisa.
Desmund
asiyejua uchungu wa mwenzake bali kujali masilahi yake, mwanaharamu kabisa
asiyekuwa na chembe ya huruma wananchi wakamchagua aiongoze kata yao tena baada
ya kumuua aliyekuwa diwani mtiifu.
Siku nzima
sikutia chochote mdomoni, hivyo usiku huo nilijilazimisha kuonja chakula, kisha
nikalala, kama kawaida begi langu likiwa kitu cha muhimu zaidi.
Siku
iliyofuata majira ya saa nne nilikuwa nimechanganyikana na watoto wadogo wa
shule fulani hivi ya mtu binafsi. Nilikuwa nawauliza maswali kadha wa kadha na
kisha huku nikitazama huku na huko kama nitaweza kuiona damu ya Desmund.
Naam!
Nikafanikiwa kumuona yule mtoto, uzuri wa watoto akishakuamini mara moja basi
yatosha. Aliponiona akanikumbuka na kunikimbilia akiwa na wenzake, nikawapa
senti kidogo kisha nikabaki na yule mtoto peke yake. Ili kuondoa utata nikaenda
katika uongozi nikajitambulisha kama shangazi yake na yule mtoto ambaye
aliniambia kuwa alikuwa anaitwa Desmund Juniour. Jina baya kupita yote katika
akili yangu.
Walimu
hawakuwa na shaka nilipowaeleza naenda kumnunulia chai mara moja, kwa sababu
mtoto mwenyewe alionyesha kunijua basi hawakuwa na swali.
“Mama yake
leo amechelewa kweli huwa hakosi kupita au ndo amekuagiza.” Mwalimu mmoja
aliniambia.
“Hapana
nadhani ametingwa tu maana yule dah simuwezi.” Nilidanganya na upesi nikaondoka
na yule mtoto, nikiwa katika tahadhari kubwa maana kauli ya kuwa mama mtoto
huwa anakuja mida kama hiyo ilinishtua.
“Gari ya mama
ileee.” Tukiwa nje yule mtoto alinionyesha kwa kidole gari iliyokuwa inaingia
pale shuleni. Akimaanisha ni ya mama yake, nikazidisha mwendo na kukata kona
mbili tatu. Sikutaka kupoteza muda zaidi, nikafanya nilichopanga, nikampa yule
mtoto pipi, akaidaka na kuitupia mdomoni, baada ya dakika ishirini nilikuwa
nimetoa kanga na alikuwa mgongoni kwangu kama mwanangu wa kumzaa vile amelala
hoi. Hatua ya kwanza ilikuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.USIKOSE MWISHO WA SIMULIZI HII
Maoni 1 :
Jamani..Adela nna ombi moja. Naomba usikawie kuweka kwani tunakuwa tunasahau za nyuma. Hata hivyo ubarikiwe sana.
Chapisha Maoni