Pages

Jumatano, Desemba 31, 2014

SIMULIZI FUPI "NILISAHAU NILIPOTOKEA"

 MTUNZI-ADELA DALLY KAVISHE
John ni kijana ambaye alikuwa anafanya biashara ya kuuza vifaa vya ujenzi, kijana huyu aliweza kufanikiwa sana kupitia biashara anayoifanya, na pamoja na kuwa ni mfanyabiashara mwenye pesa nyingi lakini alikuwa hana mke wala watoto, siku zote alikuwa akijumuika na marafiki zake katika sehemu mbalimbali za starehe, wazazi wake walikuwa wakiishi kijijini pamoja na wadogo zake sita, kwani yeye alikuwa ni mtoto wa kwanza na ambaye amefanikiwa katika maisha.

 Wadogo zake walikuwa wakihitaji msada mkubwa kutoka kwa kaka yao, hususani suala zima la kwenda shule, na sikuzote baba yake na John alikuwa akimsihi kijana wake asiache kuwasaidia wadogo zake, lakini sasa kilichotokea ni kwamba John alikuwa anapenda sana starehe, hivyo pesa nyingi alizokuwa anapata ziliishia kwenye starehe.

 Siku moja Baba yake aliamua kumsafirisha mdogo wake na John ambaye alikuwa anaitwa Fredy ili aweze kuendelea na masomo akiwa mjini, ambapo alijua fika kaka yake angempeleka shule, na hivyo angeendelea na masomo ya sekondari, Alipofika alikaa muda mrefu bila ya John kumtafutia shule, na hata alipokuwa akimuuliza alikuwa mkali sana na kusema kuwa hana pesa za kuchezea hivyo Fredy aliendelea kukaa pale nyumbani, alikuwa akisikitika sana kwani alikuwa anamuona kaka yake jinsi anavyotumia pesa katika starehe kama ulevi na kwenda club kila kukicha lakini pale anapomgusia suala la kumtafutia shule alikuwa mkali sana.

 Baadaye Fredy aliamua kumweleza Baba yake hali halisi, jambo hilo lilimsikitisha sana Baba John lakini hata alivyomweleza alionekana kujibu kwa dharau na kiburi huku akimtaka mdogo wake atafute kazi na si kumtegemea yeye, Maisha yaliendelea huku Fredy akiwa anaishi na kaka yake bila ya msaada wowote baadaye aliamua kurudi kijijini kwani sasa aliona hawezi kupata msaada kutoka kwa kaka yake. 

Baada ya miaka miwili kupita hali ya maisha ya John ilianza kuyumba kiasi kwamba alianza kuuza baadhi ya mali zake, kwani hata wale marafiki aliokuwa akiwakopesha pesa za biashara, wote walimkimbia na alipowafuata ili alipwe madeni yake walimkana na kumcheka sana, hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba ilimbidi arudi kijijini kwao ambapo alipiga magoti mbele ya wazazi wake pamoja na wadogo zake kisha aliomba msamaha

 "Baba Mama pamoja na wadogo zangu naombeni mnisamehe, najuta sana kuwatenga kipindi nilipokuwa nina pesa nyingi, niliona starehe na marafiki ndiyo kila kitu kwangu kumbe nilikuwa nakosea, yalaiti ningewasaidia wadogo zangu leo hii nisingekuwa hapa nilipo kwani pesa nyingi nilikuwa nikifanya starehe, na kuwasaidia marafiki zangu ambao leo wamenikimbia, sina chochote sina lolote naombeni mnisamehe, nimewakosea sana" Aliongea kwa uchungu huku machozi yakimbubujika. Baba na Mama walimuonea huruma sana, waliamua kumsamehe na sasa alianza maisha upya akiwa anashirikiana na ndugu zake katika kila jambo. Mungu alimbariki na aliweza kunyanyuka tena na maisha yake yanaendelea vizuri.WADAU WA SIMULIZI TUENDELEE KUWA PAMOJA MWAKA 2015 TUTAKUWA NA SIMULIZI NYINGI ZAIDI PAMOJA NA MADA ZA KUSISIMUA.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom