Pages

Jumatano, Februari 25, 2015

SIMULIZI FUPI "UVUMILIVU UMENISHINDA"


Ilikuwa ni usiku majira ya saa sita, ambapo wakati huo mume wangu alikuwa amesafiri, nilikuwa nikijisikia vibaya sana, kwani nilikuwa naumwa sana, na muda ulivyokuwa unazidi kwenda hali ilizidi kuwa mbaya nilikuwa najisikia maumivu makali , sehemu za kuchwani, na miguu ilikuwa inaishiwa nguvu.

 Nilijaribu kuwaita mawifi zangu ambao walikuwepo wamelala chumba cha pili, lakini sauti yangu ilikuwa ni ndogo sana hivyo niliamua kushuka kitandani taratibu, na kutoka nje huku nikijikokota na jasho likiwa linanibubujika mithili ya mtu aliyejimwagia maji, nilisogea kwenye mlango wa chumba cha wifi zangu, ambao niliwasikia wakiwa wanazungumza kwa mbali hivyo nilijua watakuwa bado hawajalala.

 Nilianza kubisha hodi huku nikiwa nimeegemea ule mlango, kwani nilikuwa nikijisikia vibaya sana, niliita kwa sauti ya upole, lakini hakuna aliyekuja kufungua mlango, ijapokuwa mwanzoni nilikuwa nikiwasikia wanazungumza ila sasa walinyamaza kimya kabisa kisha walizima taa, na kuniacha niendelee kubisha hodi, nilikaa pale mlangoni kama nusu saa, lakini hakuna hata mmoja aliyenyanyuka kufungua mlango ili kunisikiliza, nilijisikia vibaya sana machozi yalinibubujika, ilinibidi nianze kujikokota na kurudi chumbani.

Nikiwa chumbani niliwaza kumpigia simu dada yangu ambaye alikuwa anaishi mbali kidogo, lakini simu yangu ilikuwa haina salio, nilipanda ktandani na kujilaza huku machozi yakinibubujika kutokana na maumivu makali niliyokuwa nikiyasikia, nililala  kitandani huku nikiwa natetemeka mwili  mzima kama mtu anayesikia baridi kali sana, moyoni mwangu nilikuwa nikiwaza "Mungu wangu nisaidie miimi Hasina, hivi  nitapona kweli, hali yangu inazidi kuwa mbaya, na sina msaada wowote, eeh Mungu nisaidie nipate nguvu ikifika asubuhi niweze kwenda hospitali".

Niliendelea kusali sana moyoni huku nikiamini kuwa sina msaada mwingine wowote zaidi ya Mwenyezi Mungu pekee.Usiku ulikuwa mrefu sana lakini baadaye nilipitiwa na usingizi mzito hadi asubuhi ambapo nilishtuka ilikuwa ni saa moja asubuhi, mwili wote ulikuwa ni kama umekufa ganzi, kwani nilijiona mzito sana, kiasi kwamba hata kunyanyuka kitandani ilikuwa ni kazi, nilikaa pale chumbani huku nikiwaza "Hivi kweli hawa wifi zangu nimewakosea nini, yaani mimi naumwa lakini hakuna hata mmoja anayenijali, mbona mimi nimekuwa nikiwajali kwa kila jambo, tizama hapa ndani tupo watu watatu, lakini nakuwa kama naishi peke yangu, Mungu nisadie niweze kujikokota  niende hapo zahanati"

 Baada ya muda kidogo nilijaribu kunyanyuka taratibu na kutoka nje ambapo niliwakuta wifi zangu Warda na Zamda wakiwa wameketi kibarazani huku wakinywa chai, niliwasalimia lakini hawakuitika wote waliangua kicheko huku wakisemeshana "Hahahahahahahah umeliona hilo jitumtu ndiyo linaamka, leo litakula macho yake, sijui kaka alipata wapi mwanamke mvivu kiasi hiki, khaa hata nyumba haijafanyiwa usafi" aliongea  Warda huku Zamda akidakia nakusema "Hivi wewe, unamuonaje jitumtu, ni mchafu hatari, ananuka huyo hata shombo ya dagaa ina afadhali".

Kutokana nahali niliyokuwa nayo nilinyamaza kimya kwani hata nguvu za kuongea ziliniishia. Niliondoka na kwenda Zahanati ambapo nilipatiwa matibabu  na baada ya vipimo niligundulika kuwa na malaria. Hivyo nilipewa dawa na kurudi nyumbani wakati huo ilikuwa ni saa tano asubuhi, nilipofika nyumbani nilimkuta mume wangu amerudi na alikuwa ameketi sebuleni na wadogo zake, nilimsalimia, lakini hakuniitikia, nilishangaa amesimama na kunizaba vibao huku akisema "Hivi wewe changudoa, umetoka wapi asubuhi hii, inamaana mimi nikisafiri wewe ndiyo unapata muda wa kwenda kwa mabwana zako mjinga mkubwa wewe, nimeingia chumbani, kitanda haujatandika mazingira ni machafu, halafu unajiita ni mwanamke, mpuuzi mkubwa umetoka wapi?" 

Wakati akiwa anazungumza nilikuwa nikisikia kizunguzungu sana kwani vile vibao alivyonipiga na hali yangu ilivyokuwa nilikuwa nahisi kama kifo kinaninyemelea, nilimtizama kwa macho ya upole na kusema "Zuberi mbona unaniumiza kiasi hiki jamani nimekukosea nini, mimi nimetoka hospitalini, naumwa sana, tizama hizi dawa nimepewa nitumie hata hawa ndugu zako wanajua mimi ni mgonjwa, kila kukicha nimekuwa nikipata mateso katika nyumba hii na wewe mume wangu hauna hata chembe ya huruma, yaani naumia sana".

 Niliongea kwa uchungu huku machozi yakinitoka, lakini Zuberi hakujali aliendelea kunishambulia kwa maneno na baadaye aliniambia "Kwanza nilikuoa kwa bahati mbaya, ningefurahi kama ungeondoka hapa nyumbani kwangu, hivi wewe ni mwanamke gani ndugu zangu hawakupendi, lakini bado unajilazimisha kuishi hapa siuondoke" Alitamka yale maneno bila aibu, nilinyamaza kimya kisha nikaingia ndani huku nikiwa mwingi wa mawazo, kutokana na hali yangu ilinibidi niwe mvumilivu lakini baada ya siku mbili niliamua kuondoka na kwenda kusihi kwa dada yangu kutokana na vipigo na kejeli kutoka kwa Zuberi.

 Nilihamia kwa dada yangu, na kuishi naye, na hata siku moja Zuberi hakuwahi kuja kunitafuta ila aliniandikia talaka na kuwapa dada zake waniletee, nililia sana kwani wakati nakutana na Zuberi nilimpenda sana na sikuwahi kufikiria kama sikumoja angebadilika kiasi kile. Maisha yaliendelea ulipita kama mwaka mmoja tokea niachane na Zuberi huku nikiwa anaendelea na biashara zangu Mungu alinisadia nikawa na mafanikio pamoja na afya njema ambapo nilipendeza sana na kuonekana mrembo zaidi kwani sasa nilikuwa katika maisha mapya bila mateso yoyote. 

Siku moja nikiwa dukani kwangu Zuberi alikuja akiwa ameongozana na rafiki yake alipofika alinisalimia na kisha akaanza kusema "Hasina najua nilikukosea sana ila naomba unisamehe, nakupenda sana wewe ndiyo chaguo langu tafadhali nakuomba urudi nyumbani tuanze maisha mapya, kwani yaliyopita si ndwele, nakupenda sana".

 Nilimtizama kuanzia chini mpaka juu na kusema "Unajua wewe Zuberi ni mjinga sana mimi hapa nilipo siwezi kurudiana na wewe hata siku moja hata ikiwa ni ndotoni, haiwezekani kamwe, inamaana kipindi kile ulikuwa hujui kama unanipenda, sasa hivi ndiyo umeligundua hilo, sasa ni hivi moyoni mwangu ulishanitoka na mimi huwa sirudi nyuma kama ni kukusamehe nimekusamehe lakini siwezi kurudia matapishi samahani sana. Zuberi alijiinamia kwa aibu na baadaye aliondoka zake. 

Katika maisha unaambiwa usiache mbachao kwa msala upitao, lakini pia ukiona cha nini ujue kuna wengine wanawaza watakipata lini. Wakati mwingine mtu unaweza kuwa mvumilivu sana lakini kuna wakati maji yanafika shingoni unashindwa kuvumilia.Mimi Hasina mateso niliyopata kwa Zuberi uvumilivu umenishinda.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom