ILIPOISHIA
"Dada kwanini baba amekuwa
hivyo, inamaana hawezi tena kuongea, dada Baba aliniambia atanipeleka shule,
inamaana hanipeleki tena, kwanini Baba yangu anatoka damu, halafu
wanambeba na kumuweka kwenye gari, dada mimi namtaka Baba yangu". Aliongea Rony kwa uchungu sana
dada yake alishindwa kumjibu chochote alimkumbatia na kuendelea kulia kwa
uchungu.
INAPOENDELEA
Ritha alikuwa ni msichana mdogo
ambapo kwa wakati huo alikuwa kidato cha tatu, na alikuwa na wadogo zake wawili
mapacha ambaye ni Rony na mwingine anaitwa Rosada. Siku zote walikuwa wakiishi
na Baba yao kwani Mama yao mzazi aliwaacha Rony na Rosada wakiwa wadogo sana kipindi Mama Ritha
anaondoka walikuwa na miezi tisa, wakati Ritha alikuwa anasoma darasa la nne.
Mzee Jengo alikuwa ni mfanyabiashara wa vifaa
vya kilimo na mkulima, ambapo kwa namna
moja au nyingine alikuwa ni Mzee mwenye uwezo kifedha, siku zote za maisha yake
alikuwa ni mchapa kazi, alijituma sana katika kufanya kazi kwa bidii na ndiyo
maana aliweza kufanikiwa na kuwa na maisha mazuri. Alikuwa anafahamika na watu
wengi kwasababu alikuwa akiishi na
watu vizuri na aliwasaidia watu mbalimbali wakiwemo ndugu jamaa na marafiki na
hata wale asiowafahamu. Alikuwa ni mcheshi na mkarimu sana.
Hivyo taarifa za kifo chake ambacho kilitokea
ghafla kiliwashtua watu wengi sana, ambao
walikusanyika katika kuomboleza kwenye nyumba ya Mzee Jengo. Simanzi na vilio
viliendelea kutawala akina Mama na akina Baba na watoto walilia kwa uchungu
sana, taratibu za mazishi ziliendelea baada ya ndugu wa Marehemu kufika na siku
ya kumpumzisha Mzee Jengo katika makazi
yake ya milele ilifika. Siku hiyo Ritha alikuwa kimya asiyeongea chochote ila
alionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana na alikuwa amechoka kutokana na
kupoteza fahamu mara kwa mara.
Rony na Rosada walikuwa wameketi na shangazi
yao anayeitwa Mama Sara ambaye alikuwa
akiwabembeleza wasilie. Ulifika muda wa kwenda kumuaga marehemu kwa mara ya
mwisho ambapo walianza ndugu wa marehemu na baadaye watoto wa marehemu. Ritha
alipofika karibu na Jeneza alisimama na kumshika Baba yake kwenye paji la uso
huku akilia kwa uchungu “Baba, baba amka baba embu tizama sisi tutabaki na
nani, Baba amka Baba inamaana kweli huwezi kuongea jamani Baba yangu uwiiiiii jamani Baba yangu uwiiii Baba
ulisema nikifaulu utaninulia zawadi sasa
mbona umeondoka baba”.
Ritha alikuwa akiongea kwa uchungu
huku machozi yakiendelea kumbubujika, shangazi yake alimshika na kumsogeza
pembeni huku akiendelea kumfariji “Mwanzangu Ritha nyamaza usilie, haya yote ni
mapenzi ya Mungu, Baba amepumzika mahali pema peponi, tafadhali nakuomba
ujikaze mwanangu” Alimfariji Mama Sara lakini Ritha aliendelea kulia bila ya
kupumzika na wakati huo Rony alipofika kumuona Baba yake kwa mara ya
mwisho masikini aliishiwa nguvu na
kuanguka chini.
Ndugu walimbeba na kumlaza pembeni huku wakimpatia huduma ya
kwanza, kwa upande wa Rosada alipomuona Baba yake akiwa amelala usingizi wa
milele alianza kulia huku akisema “Mtoeni
Baba yangu, kwanini mmemuweka huku, Baba amka, Baba amka jamani mtoeni Baba
yangu namtaka Baba yangu” Aliongea Rosada huku akilia sana.
Watu wengi walilia sana kwa namna wavyokuwa wakiwatizama wale watoto walivyokuwa wakilia na kuongea kwa uchungu. Mmoja
kati ya waliohuduria msibani alisikika akisema “Jamani hawa watoto
wanasikitisha sana, embu tizama wanavyolia, na Baba yao alikuwa akiwalea peke
yake, yaani Mama yao sijui yuko wapi, halafu yule Mama ni mjinga sana inamaana hata
taarifa za msiba hajazipata au inakuwaje inaumiza sana kwakweli”.
Alizungumza
dada mmoja huku akimgeukia rafiki yake ambaye walikuwa wamekaa pamoja, na
kuendelea kunong’ona “Mwenzangu yaani Mama yao sijui ni mtu wa namna gani
anawezaje kuwaacha watoto wanaishi na Baba yao pekee, yaani hawa watoto hawajui
mapenzi ya Mama kabisa kwani aliwaacha wadogo sana, ila huyu Baba Mungu
ampunzishe mahali pema peponi jamani amehangaika sana na hawa watoto” Aliongea yule
dada ambaye alionekana kuifahamu vizuri familia ya Mzee Jengo.
Taratibu ziliendelea na hatimaye
Mzee Jengo alipumzika katika makazi yake ya milele na huo ndiyo ukawa mwisho wa
maisha ya Baba Ritha. Maisha yaliendelea
huku familia ikiwa imebaki na simanzi kubwa na baada ya matanga, watoto waliendelea kuishi na
Baba yao mdogo ambaye alikuwa anaitwa Ndama.
Hali ya maisha ilibadilika kwa
upande wa Ritha kwani muda mwingi alikuwa akionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana,
siku moja alikuwa ameketi chumbani kwake huku akiwa anawaza “Baba umetuacha
peke yetu, yaani sisi ni kama yatima, ijapokuwa tunaishi na Baba mdogo, lakini
ni tofauti na tulivyokuwa tunaishi na wewe, hata kama Baba mdogo anatuonyesha
upendo wa dhati lakini kamwe pengo lako halizibiki Baba, natamani ungekuwepo.
Aliwaza Ritha huku akiendelea kulia na kutafakari
"Nikifikiria Mama alituacha tukiwa wadogo, tena bila hata ya huruma, na hata
sijui yuko wapi, angalau Mama angekuwa anatupenda, tungepata faraja lakini
ametutupa na kutuacha peke yetu wakati mwingine huwa najiuliza hivi kweli ni
Mama yangu mzazi? Kwani nikitizama marafiki zangu
wanavyopata mapenzi ya dhati kutoka kwa Mama zao, siamini kama Mama yetu
alitutekeleza, eeh Mungu naomba utusaidie, Moyo wangu unaumia sana, najiona
kama nina kidonda ambacho hakiwezi kupona hata nikipewa dawa yoyote ile.” Alikuwa akiwaza
Ritha huku machozi yakimtoka. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA TATU ITAENDELEA SIKU
YA JUMANNE.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni