Askofu
Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinari Pengo (pichani), amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi
kugombea urais, ili wananchi wapate wigo mpana wa kuchagua anayefaa
kuiongoza nchi.
Kardinali Pengo alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati
akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa mahafali ya
saba ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tawi la Dar es Salaam (SJUIT).
Kardnali Pengo alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo ya wahitimu
798 wa ngazi za shahada, stashahada na astashahada ambao walitunikiwa
na Mkuu wa Chuo, Dk. Arul Raj.
Alisema iwapo watajitokeza wagombea wengi wa urais, itawasaidia
wananchi kuwafahamu wagombea wao vizuri, kuwapima kwa kulinganisha sifa
zao kabla ya kuchagua mmoja kuwa kiongozi wa nchi.
Alisema kujitokeza kwa watu wengi wenye nia ya kugombea nafasi ya
urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu ni jambo jema, kwani
watakapo jitokeza wachache au mmoja, wananchi wanaweza kuchagua kiongozi
asiye na sifa.
“Mimi nadhani ni jambo zuri kwa watu wengi kujitokeza kugombea
nafasi ya urais, akijitokeza mtu mmoja kugombea urais wananchi
watashindwa kufahamu kama anafaa kwani hakutakuwa na wa kumlinganisha
naye,” alisema.
Baadhi ya makada ndani ya vyama vya siasa wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo na wengine wanatajwa.
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), makada kadhaa
wamejitokeza kutangaza nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete
atakapong’atuka Oktoba mwaka huu.
Waliotangaza nia hadi sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu; Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalah na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, ambaye alitangaza akiwa ziarani nchini Uingereza na
kueleza kuwa alifanya hivyo kimya kimya.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum); Prof. Mark
Mwandosya na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba, aliyetangazia nia hiyo nchini Uingereza.
Viongozi wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa; Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye; Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Uchukuzi,
Samuel Sitta; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mbunge
wa Sengerema, Willium Ngeleja na Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel
Nchimbi.
Kwa upande wa Tanzania Labour Party (TLP) aliyejitokeza na
alitarajiwa kupitishwa na Mkutano Mkuu ulioanza jana jijini Dar es
Salaam ni Macmillan Lyimo.
Vyama vya Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na NLD vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimepanga kusimamisha mgombea mmoja wa
urais.
Wanaotajwa katika vyama hivyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.
WAGOMBEA WANAOTUMIA FEDHA
Kadhalika, Kardinali Pengo aliwatahadharisha wananchi dhidi ya
wagombea wa nafasi ya urais wanaotoa rushwa ili waingie Ikulu, kwani
uongozi wa taifa hauwezi kununuliwa.
Alisema viongozi wakipatikana kwa njia ya rushwa wakishaingia madarakani watataka walipe madeni badala ya kuwahudumia wananchi.
“Wananchi wanapaswa kufikiri kwa kina na busara na kuachana na
viongozi ambao wanawashawishi wawachague kwa kuwapa rushwa kwani
watakapo ingia madarakani lazima walipe fadhila kwa waliompa fedha za
kutoa rushwa wakati wa mchakato wa uongozi,” alifafanua.
TISHIO LA UGAIDI
Akizungumzia suala la tishio la ugaidi nchini pamoja na ujumbe
mfupi wa maneno unaosambazwa kwa simu za kiganjani na watu kuhusu
matukio hayo, alisema serikali pamoja na wataalamu wa usalama nchini
wanapaswa kuchukua tahadhari mapema kuimarisha ulinzi wa wanachi.
Kardinali Pengo alisema kama kuna hofu juu ya ugaidi, basi serikali iwahakikishie usalama wananchi wake.
Alisema wanaosambaza ujumbe wa tishio hilo kuwa na uhakika wa kile
wanachokisambaza, kwani kwa kufanya hivyo bila uhakika wanaweza
kusababisha maafa makubwa na hofu.
AWASHAURI WAHITIMU
Awali, akiwahutubia wahitimu na uongozi wa chuo hicho, Kardinali
Pengo alisema miaka ya nyuma serikali iliwekeza kwenye masomo ya sanaa
zaidi kuliko sayansi, jambo ambalo limesababisha taifa kukosa wataalamu
wengi wa sekta hiyo.
Alisema hali hiyo imebadilika kwani serikali sasa inawapa
kipaumbele wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kwa kuwapatia mikopo
inayoweza kuwasaidia katika masomo yao.
“Nawashauri wanasayansi wangu mliohitimu leo hii (jana) na wale
ambao bado wapo vyuoni kuondokana na fikra ya kuajiriwa serikalini pale
wanapomaliza masomo yao, unaweza kujiajiri hata ukiwa umesoma masomo ya
sayansi au sanaa,” alisema na kuongeza:
“Sayansi ni kwa ajili ya wanadamu hivyo itumike kuwanufaisha wanadamu kibinadamu.”
Kardinali Pengo alikuwa akitembea kwa kutumia fimbo ya kutembelea.
AELEZEA AFYA YAKE
Aidha, kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kuelezea maendeleo ya
afya yake na jinsi alivyopatiwa matibabu kuwa alifanyiwa upasuaji wa
pili nchini India katika Hospitali ya Manipal iliyopo Bangolore, baada
ya upasuaji wa kwanza aliofanyiwa mwaka 2013 Ujerumani kushindwa kumpa
nafuu.
Alisema kinachomsumbua ni uti wa mgongo na hivi sasa anaendelea
vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji huo ingawa madaktari walimwambia
atapona vizuri na kuacha kutumia fimbo baada ya miaka miwili.
“Kwa wale wanaotaka kujua afya yangu na ambao wananikumbuka kwenye
maombi na wahakikishia kuwa hivi sasa naendelea vizuri,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni