Pages

Alhamisi, Mei 21, 2015

SIMULIZI MAALUMU KATIKA KUMBUKUMBU YA AJALI YA MV BUKOBA


NA: GEORGE IRON MOSENYA
KWA: Wote waliopoteza ndugu zao katika ajali ya MV BUKOBA  tarehe 21/05/1996 siku kama hii
Wingu zito lilikuwa limetanda katika anga ya jiji la Mwanza. Wakazi wake waliokuwa na biashara kandokando ya barabara walizianua biashara zao upesi huku wakitokwa na manung’uniko juu ya kile kilichotokea kana kwamba mwamuzi wa mvua inyeshe ama isinyeshe alikuwa yu miongoni mwao.
Wingu hili lilinikuta nikiwa nimejikumbata katika kitanda changu nikiwa nimejifunika gubigubi huku kiubaridi kikianza kulishinda nguvu shuka jepesi nililokuwa nimejifunika.

Hatimaye shuka likazidiwa nikasalimu amri na hapo nikanyanyuka ili niweze kulitafuta shuka zito zaidi linaloweza kupambana na ubaridi ule.
Nikalifunua begi langu katika namna ya utulivu nikapekua na kulipata shuka zito.
Naam! Shuka lile likanifadhaisha nikalisahau lile baridi na hapo macho yangu yakaangalia vitu viwili upesi upesi, kwanza ile hali ya hewa na nje na kasha kalenda iliyokuwa imepachikwa ukutani.
Naam! Ilikuwa tarehe ishirini na moja mwezi wa tano tena.

Hali ya hewa ileile kama ilivyokuwa tarehe ile miaka 19 iliyiopita, lile shuka zito lilikuwa limetimiza miaka 19 pia.
Niliketi kitandani na hapo nikaikukbuka siku kama hii miaka mingi nyuma.
Siku ambayo iliondoka na mambo mengi muhimu katika maisha yangu na hapo ikaniachia kumbukumbu mbaya na zisizofutika kamwe.
Kumbukumbu ambazo kila mwaka zinarejea zikiwa kama kitu kipya kabisa.
Usiku ule miaka kumi na tisa iliyopita nilikuwa peke yangu nyumbani kama ambavyo siku hii nipo peke yangu tena.
Taarifa ililetwa na mmoja wa marafiki zangu wa utotoni, lakini aliileta katika namna ambayo haikuwa ya kustua kwa sababu alikuwa mtoto nami nilikuwa mtoto.
Alinieleza kuwa meli imepinduka!
Sikuelewa nini maana ya meli kupinduka bali nakumbuka mama alinieleza kuwa ipo siku nitapanda meli.
Mvua ilikuwa inanyesha nikakumbuka mama aliniambia si vyema kuzungumza huku mvyua kuwa ikiwa inanyesha nikaachana na na Yule mtoto mwenzangu nikaliendea shujka zito ambalo mama alikuwa amenipatia nikaenda kitandani na kujifunika gubigubi.
Asubuhi nilipoamka hali ilikuwa tofauti na siku zote, ndugu zangu walikuwa bize wakikimbia huku na kule, mara huyu aseme lile na mara huyu alie mwingine ambembeleze.
Hali ilikuwa ya sintofahamu!
Ile hali sikuijua utotoni lakini kadri umri ulivyozidi kwenda ndipo nikaanza kugundua kuwa ile siku ilikuwa siku mbaya kupita zote kuwahi kutokea katika maisha yangu na ni siku hii tena.
Siku ile ilikuwa siku ambayo kaka yangu mkubwa, dada zangu wawili na mpwa wangu walimezwa na ziwa Viktoria.
Ilikuwa siku ile ambapo babu yangu kizaa baba baada ya kusikia mtoto wake yaani baba yangu alikuwa yu ndani ya meli na hadi zinapita siku tatu mwili wake haujaonekana alikumbwa na shinikizo la damu na kupoteza fahamu hata kabla hajafikishwa hospitali ya mkoa ya Bugando.
Siku hiyohiyo miaka kumi na tisa iliyopita, wajomba zangu wanne, shangazi sita na baba zangu wadogo watatu walizidiwa nguvu na maji.. ama walizidiwa mbinu na viumbe hai wa majini.. kamwe sikuwahi kuwaona tena.
Siku kama hii miaka kumi na tisa iliyopita, siku ambayo meli ya Mv. Bukoba ilizama katika ziwa Viktoria na kuondoka na uhai wa watu zaidi ya elfu moja akiwemo bibi yangu kipenzi ambaye alifunga safari kutoka Bukoba akiwang’ang’ania ndugu zangu kuwa anahitaji kuja kuniona mjini Mwanza. Looh! Bibi aling’ang’ania kifo chake… akafia katika maji bibi Yule.
Siku kama hii mwaka mmoja baadaye nyumba ya marehemu baba yangu iliuzwa na waliosema kuwa ni ndugu zangu, walizungumza maneno yao ambayo hadi leo ukiniambia niyanukuu sitaweza hata chembe….. niliishia kupewa shilingi elfu kumi (ile ya bluu) huku nikipewa ahadi tele za kusomeshwa hadi chuo kikuu. Lakini hiyo siku ulikuwa mwanzo wa mimi kukosa elimu na kasha kuingia katika manyanyaso makubwa kabisa ambayo sikuwahi kuyapata popote pale.
Lakini siku kama hii, hali ya hewa kama hii inanikumbusha shuka hili zito ambalo nilipewa na mama yangu mzazi wakati anasafiri kuelekea Bukoba akanisihi kuwa niwe najifunika kila panapokuwa na baridi, akampa maelekezo na dada niliyebaki naye nyumbani.
Naam! Siku kama hii nahitaji kulifunika shuka hili lakini nikitambua wazi kuwa siku kama hii miaka kumi na tisa iliyopita mama yangu kipenzi ambaye ni pekee kati ya familia aliyenusurika kufa…. Baada ya kusimulia kila kitu kama alivyokishuhudia ndani ya meli. Alishindwa kuhimili kuamini kuwa mume wake alikufa, baba yake alikufa, mama yake alikufa, mawifi na dada zake walikufa.
Naam! Mama akakata kauli siku kama hii miaka kumi na tisa iliyopita.
Akaniacha nikiwa yatima!
Nayakumbuka maneno yake, alinisihi nisilie sana kwani kuna watu wamepoteza zaidi ya ndugu zao thelathini kwa mpigo.
Lakini mama kama ulinisihi mimi nisilie mbona wewe ulilia hadi kukata kauli!!
Naam! Siku kama hii imejirudia tena, hali ya hewa ileile, tarehe ileile, upweke uleule.
Yule mtoto aliyenieleza kuwa meli imepinduka aligeuka kuiwa rafiki yangu kipenzi na ndugu pekee, siku kama hii miaka mitatu nyuma aliamua kuoa… akaoa siku kama hii ilimradi kunipa sababu ya kutabasamu inapofika siku kama hii, lakini bado hali ni ileile.
Siku kama hii tarehe 21 mwezi wa tano……….
NILIPOTEZA KILA KITU KILICHOKUWA MUHIMU KATIKA MAISHA YANGU!!
Natambua kilio hiki silii peke yangu na huenda kama mama alivyonieleza kabla hajafa kuwa wapo waliopoteza ukoo mzima, wapo waliozamisha ndoto zao katika wimbi lile la maji….
Ajali ile iliyozaa mayatima, iliyozaa wajane, ajali ile ikauzaa umasikini, ikazaa kila kitu kibaya kibaya.
Lakini ni neno moja tu la kusema… JINA LAKE YEYE MWENYEZI MUNGU BASI LIHIMIDIWE MILELE ni yeye aliyeijua ajali ile hata kabla haijatokea……..
ASANTE MUNGU KWA SABABU HAUKOSEI KATIKA KILA UNALOLITENDA

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom