Jumanne, Juni 23, 2015

MADHARA YA DAWA ZA MAPENZI


 Siku ya jana gazeti la Nipashe lilitoa taarifa  maalum iliyoelezea kushamiri kwa biashara ya dawa zinazodaiwa kuwa ni za mapenzi zikiwamo za asili za kuongeza nguvu za kiume jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini.
 
Ripoti hiyo iliyohusisha mahojiano na watumiaji wa dawa hizo, wauzaji na pia wataalam wa afya, ilieleza vilevile juu ya kuwapo kwa tishio la kuongezeka kwa maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi. Hii ni kutokana na taarifa kuwa mojawapo ya masharti kwa baadhi ya dawa hizo za mapenzi ni kwa watumiaji kutakiwa kutotumia mipira ya kiume (kondom) wakati wa kujamiiana.
 
Inalezwa zaidi kuwa miongoni mwa wateja wakubwa wa bidhaa hizo ni vijana. Hawa wamekuwa wakijihusisha zaidi na matumizi ya dawa hizo kutokana na sababu mbalimbali, baadhi zikitajwa kuwa ni kutaka kusifiwa na wapenzi wao na wengine kujiingizia kipato kwa kuwaridhisha wenzi wao wenye fedha na kiu kubwa ya kuwa na mahusiano na vijana.
 
Mmoja wa wataalam wa afya alikaririwa akisema kuwa matumizi makubwa ya dawa hizo ni hatari kwani kwa kufanya hivyo, watumiaji hujiweka katika hatari kadhaa zikiwamo za kujiondolea kabisa uwezo wa kujamiiana, kupata upofu, kukabiliwa na magonjwa ya moyo na zaidi, ni kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

 
Ilielezwa zaidi kuwa uwezekano wa kupata upofu hutokana na ukweli kuwa mishipa ya macho ni midogo na mtumiaji wa dawa za kuongeza nguvu za kiume huwa anatumia nguvu nyingi na kuchelewa kufika kileleni. Hali hiyo husababisha mzunguko wa damu kuwa mkubwa katika mishipa hiyo midogo na hivyo kuiweka katika hatari ya kupasuka na kupata madhara mengine mbalimbali na ndipo mtumiaji anapokuwa katika hatari ya kupata upofu.
 
Hakika, hii siyo habari njema. Ni wazi kwamba sasa kuna tishio kubwa kwa taifa, hasa kwa kuzingatia kuwa walio katika hatari kubwa ya kukumbwa na athari za matumizi ya dawa hizi ni vijana. 
 
Sisi tunadhani kwamba huu ni wakati wa kuliangalia kwa kina suala hili. Kwamba, sasa kuna kila sababu kwa mamlaka zinazoshughulikia tiba zikiwamo za asili kuingilia kati na kuchukua hatua stahili za kuliokoa taifa dhidi ya tishio hili la dawa za mapenzi.
 
Ikumbukwe kuwa jambo kubwa linalozua hofu ni juu ya uwezekano wa kuibuka upya kwa maambukizi ya VVU. Ni dhahiri kuwa kwa kasi hii ya utumiaji holela wa dawa zinazotajwa kuwa ni za mvuto wa mapenzi  huwaweka vijana katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa virusi vya ukimwi. Hali hii ni ya hatari zaidi. Kuiacha iendelee ni sawa na kukubali kuwa kazi kubwa iliyofanywa na taifa katika kupambana na maambukizi mapya ya VVU ni sawa na bure. Fedha nyingi zinazotengwa na serikali kila mwaka katika kitengo cha mapambano dhidi ya Ukimwi zitakosa maana, sawa na ilivyo kwa fedha zinazotoka kwa wafadhili kwa ajili ya kazi hiyo na pia kampeni za kila uchao zinazoongozwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) kwa kushirikiana na asasi mbalimbali binafsi kitaifa na  za kimataifa.  
 
Kwa mfano, taarifa iliyotolewa na Tacaids kuhusiana na hali ya Ukimwi kwa mwaka 2013 ilionyesha kuwa kuna mafanikio makubwa kwani maambukizi mapya ya VVU yalishuka hadi kufikia wastani wa kitaifa wa asilimia 5.1. Aidha, ripoti ya utafiti wa kiashirio cha VVU/Ukimwi na Malaria Tanzania 2011/2012 ilionyesha kuwa vijana wa umri kati ya miaka 15-49 ndiyo waathirika wakubwa wa VVU.
 
Kwa ujumla, kuna madhara makubwa yatokanayo na utumiaji holela wa dawa hizi za mapenzi. Kwa sababu hiyo, hakuna namna ya kutulia kana kwamba hakuna kinachotokea. Bali, kama tulivyogusia, kuna kila sababu ya kuangalia ni kwa namna gani dawa hizi zinaweza kudhibitiwa ili taifa liepukane na athari kama hiyo ya kuwapo kwa uwezekano wa kuibuka kwa maambukizi mapya ya VVU, vifo na mwishowe kuongezeka kwa changamoto nyingine kama za kuwapo kwa watoto yatima wengi zaidi ya ilivyo sasa.
 
Kwa kuanzia, ni vyema serikali kupitia wizara ya afya na vyombo vyake vya dola kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha kuwa wale wote wanaojihusisha na uuzaji holela wa dawa hizi wanakamatwa na kuchukuliwa hatua. Kama hiyo haitoshi, elimu kuhusiana na madhara ya kutumia dawa hizo bila kuzingatia ushauri wa kitaalam iendelee kutolewa vya kutosha na ikibidi ijumuishwe pia katika harakati zinazoendeela sasa za mapambano dhidi ya Ukimwi. Tuzingatie.
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom