Pages

Jumatatu, Juni 29, 2015

Rais Jakaya Kikwete ameomba radhi kwa Watanzania aliowakosea wakati wa utumishi wake wa miaka kumi Ikulu huku akisisitiza hakuna binadamu aliyemkamilifu.

 
Alisema anaamini kuwa hakuna asiyekosea katika maisha kwani yeye alijaribu alivyoweza na kwa kadri ya uwezo wake lakini inawezekana kukawa na watu ambao aliwakosea hivyo wamsamehe na waelewe ukomo wa uwezo wa binadamu.
 
“Napenda pia kusisitiza kuwa hakuna binadamu aliyekamilifu na kwa wale ambao niliwakosea  naomba waelewe ukomo wa uwezo wa binadamu naacha nyuma nchi yenye amani na utulivu, nchi ambayo inapitia katika kipindi cha ustawi wa kiuchumi na kijamii ambao haujapata kutokea katika historia ya Tanzania," alisema na kuongeza kuwa:
 
"Nina hakika kuwa mrithi wangu ataendeleza kazi nzuri ambayo nimeifanya katika miaka 10 iliyopita hasa ile ya kujenga na kuimarisha uhusiano kati ya Dola na Kanisa.”  

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akizungumza kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka miwili ya Upapa wa Baba Mtakatifu Francis iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa Vatican nchini, Oysterbay jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
 
 Rais Kikwete alitumia pia nafasi hiyo kuwaaga viongozi hao wakuu wa Kanisa Katoliki akiwasisitizia kuwa anaacha nyuma nchi yenye amani na utulivu  huku akiwataka viongozi hao kufanyakazi vizuri na kiongozi mpya na kudumisha amani na utulivu wa kijamii kama walivyofanya kwake.
 
Aidha, aliwaomba viongozi wa dini nchini kusaidia kuendeleza jadi nzuri ya Tanzania kwa kuhakikisha   nchi inabaki na amani, kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, 2015. Alilishukuru Kanisa Katoliki nchini kwa kuendeleza ushirikiano wake na serikali wa kutoa huduma za jamii katika maendeleo mbali mbali likiwamo la elimu na afya.
 
Kikwete pia alisema kuwa kwa sababu Dola na Kanisa ni taasisi zinazoendeshwa na binadamu, inatokea wakati mwingine uhusiano kati ya taasisi hizo mbili ukapitia katika mawimbi lakini ni uhusiano unaoendelea kuwapo na kuimarishwa.
 
 Wengine waliohudhuria sherehe hiyo iliyoandaliwa na Balozi Askofu Mkuu Francisco Padalli, ni  Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki  Dar es Salaam,  Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na maskofu wa karibu majimbo yote ya kanisa hilo nchini.
 
 “Kila miaka mitano, Tanzania hupiga kura kupata ridhaa ya wananchi ya kuongoza. Makabidhiano ya madaraka katika Tanzania limekuwa suala la amani na tunabakia mfano wenye kung’ara katika Afrika kwa kuruhusu makabidhiano ya amani," alisema.
 
"Kwa utaratibu huu mzuri, nitamaliza muda wangu wa uongozi na kukabidhi madaraka kwa rais mpya. Naamini kuwa Kanisa Katoliki litasaidia sana kuhakikisha mchakato wetu wa uchaguzi na makabidhiano ya uongozi vinakuwa  vya amani.”
 
 Kuhusu miaka miwili ya uongozi wa Papa Francis,  Kikwete, alisema kiongozi huyo ameleta matumaini mapya duniani, ujumbe mpya wa amani, heshima kwa utawala wa sheria amani na utulivu. 
 
“Ujumbe wake kuhusu changamoto nyingi duniani, likiwamo lile la tabianchi, umeongeza sauti yenye nguvu sana kwa namna dunia yetu inavyoendeshwa.”
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom