Jumanne, Juni 30, 2015

SIMULIZI FUPI: MTIHANI KIPIMO CHA AKILI.


MTUNZI: George Iron

Kikao cha mwisho kilitarajiwa kukaa baada ya siku tano, shamrashamra za hapa na pale zilirindima, wapambe wa bwana harusi mtarajiwa hawakukoma kumtumia jumbe mbalimbaliu za kumtakia mafanikio tele katika ndoa yake aliyotarajia kufunga baada ya siku chache. Upande wa mwanamke napo palikuwa panawaka moto wa furaha. Hatimaye alikuwa anaenda kuolewa.

Mahusiano yao yaliyodumu kwa miaka kadhaa yalikuwa mfano wa kuigwa na vijana wengi wa makamo yao. Walianzia urafiki, upenzi na wakaufikia uchumba hatimaye ndoa ilikuwa inanukia. Hakika walistaajabisha.
Kama ni migongano ilikuwa midogo midogo ambayo haikufika machoni pa watu wengi. Hili jambo liliwaimarisha sana, siri, uvumilivu na kujiamini katika mapenzi yao.
Walishirikiana katika siri zao zote za ndani kabisa, wakati huo Benson akiwa ni masikini wa kutupwa na Grace akilelewa na mjomba wake.


Lilipokuja suala la kujitoa kwa ajili ya mpenzi basi Grace aliongoza. Alifanya kila kitu kwa ajili ya mpenzi wake, jambo hili lilimpa Ben wasaa wa kujiuliza, ni mwanamke gani mwingine anaweza kumja,li na kumthamini kama afanyavyo Grace. Jibu lilikuwa jepesi tu. Hakuna kama Grace.
Jibu hili likamuimarisha na kujikita moja kwa moja katika penzi la Grace, maana aliyofanyiwa na binti huyu ni makuu.
Lakini kuna jambo moja ambalo Ben hakuwa akilitambua, jambo hili lilikuwa ni siri, siri ya aina yake ambayo ni vyema kuiita fumbo gumu.
Fumbo ambalo tangu awali lilimpa maswali lakini hakuweza kuyatatua, alijiuliza mpaka kichwa kikamuua bila kupata majibu. Na hata zilipokuwa zimesalia siku hizo kadhaa waweze kuwa mke na mume fumbo lilikuwa halijafumbuliwa na hakujishughulisha tena katika kulifumbua.
Lakini wakati akiwa amelipuuzia anakutana na jibu la fumbo lile, jibu ambalo linamuweka katika mtihani mgumu kupita yote aliyowahi kukutana nayo maishani. Mtihani wenye mtihani ndani yake.
Akajikuta katika maamuzi ya aina mbili tu na anatakiwa kuchagua moja. Aidha kusuka ama kunyoa.

******

HALI ya chumba ilikuwa swadakta, Ben alikuwa akitabasamu pekee wakati akipitia baadhi ya jumbe katika simu yake, jumbe nyingi zilimpongeza kwa hatua aliyokuwa amefikia hatua ya kumuoa Grace, tena ndoa ya kubarikiwa kabisa. Ben hakuwa na kingine cha kujibu zaidi ya kusema asante.
Ujumbe mmoja ulikuwa tofauti kidogo, ujumbe huu kutoka katika namba mpya ulikuwa si wa kumpongeza bali wa kushangaza.
“Ichukue chini ya godoro uisome.” Ulimalizika hivyo. Ben kidogo asijishulishe na ujumbe ule lakini akaona ni uvivu usiomithirika, yupo kitandani na ujumbe unasema afunue godoro, mbona asifunue? Alijiulize na kujiona mpuuzi sana.
Akafunua godoro lake pasipo na mategemeo ya kukuta chochote kitu.
Maajabu!! Akakutana na bahasha ambayo hakuwahi kuiweka yeye kwa mikono yake. Bahasha ya kaki!!
Akainyofoa taratibu kama anayehofia isichanike kwa namna yoyote ile. Akaipakata mapajani mwake, haikuwa nzito sana na nje haikuwa na neno lolote lile.
Mapigo ya moyo yakaanza kwenda mbio, akajiuliza tofauti na Grace ni nani awezaye kuingia chumbani kwake bila ruhusa? Ama hata akama ameruhusiwa ni nani? Maswali haya alijiuliza huku bahasha ikiwa inatazamana naye.
Benson akataka kumpigia Grace simu na kumuuliza lakini hapohapo akahofia kuwa Grace atataka kujua ni kitu gani kilikuwa katika bahasha ile, ama anaweza kuomba isifunguliwe hadi hapo atakapofika yeye.
Vipi yakikutwa mambo ya ajabu katika bahasha hiyo, si kitakuwa kizaazaa!! Alijionya na kuamua kufanya maamuzi ya kiume.
Akaichana ile bahasha taratibu, kisha akachomoka na karatasi kadhaa nyeupe zikiwa na maandishi meusi yaliyochapishwa kwa kompyuta.
“Mh!” akaguna Benson huku akiyakunjua na kuyaweka vyema ili ajue kuna nini.
Lahaula! Ni barua kama sio tungo!! Tungo tata, ambayo huwezi kuisoma ukaishia katikati na kuijua maana. Benson akajikohoza kisha akaanza kuisoma kwa utulivu na umakini wa hali ya juu.
ILIANDIKWA HIVI.
Wasalaam Benson,
Najua unajiuliza maandiko haya yamefika vipi katika kitanda chako, ni mimi niliyeyaweka hapo ili uyasome na kufanya maamuzi ndani ya siku saba kabla ya ndoa yetu.
Ningeweza kuyasema mbele yako lakini sio kiufasaha kama nilivyoweza kuandika, kwa maneno huenda usingemalizia kunisikiliza lakini katika maandishi naamini utasoma na kumaliza kila herufi moja baada ya nyingine.
Benson, naamini unanipenda sana mume wangu mtarajiwa nami nakupenda sana hilo nadhani unalijua waziwazi, na kamwe sijawahi kuchoka kukupenda. Lakini licha ya kukupenda kote huku sidhani kama nitakuwa shahidi mzuri mbele za mungu iwapo nitaingia katika familia yako kama mke huku nikiwa na mzigo huu moyoni, Benson.
Nadhani unafahamu ni katika mazingira yapi tulikutana, mimi na wewe tulikutana hospitali, mama yako akiwa anaumwa sana. Na siku hiyo dada yangu alikuwa amejifungua mtoto na alikuwa wodi moja na mama yako, ni mimi niliyeuanzisha undugu wetu pale nilipokusalimia kisha nikamjulia mama hali. Haukuwa umechangamka na hata mama alipolalamika njaa ndipo nikagundua hukuwa na pesa ya kumnunulia chakula, nilipojitolea kumnunulia ndipo undugu wetu ulipoanza na ukafikia hatua ya kuniamini na kunielezea juu ya maisha yako ya wakati huo, haukuwa na kazi na ulikuwa wewe pekee unayemuhudumia mama yako. Sikutaka kuuweka ubinadamu wangu kando, nikajitolea pesa yangu japo sikukueleza kuwa ilikuwa pesa ya ada nikamuhudumia mama na wewe kwa wakati ule. Sikuwahi kukuambia kuwa pesa ile ilinivuruga akili sana, na nikajikuta nikitumia mbinu nyingine kuitafuta, nililazimika kuudhalilisha utu wangu ili tu niipate, nikafanya mapenzi na mkufunzi wa chuo chetu, akanipatia pesa nikalipa ada na ule ukawa mwisho wa mahusiano yetu. Nilifanya vile kwa sababu maalum, nisingeweza kuipoteza shule, walezi wangu wasingenielewa hata kidogo.
Sahau kuhusu hili Benson maana lilitokea nikiwa sina mahusiano na wewe, lakini ukumbuke wakati ulipokosa kodi ya nyumba na mwenye nyumba akachachamaa akitaka kuwatolea vyombo nje, nakumbuka jinsi mama alivyolia na mimi nikiwa kama mpenzi wako, msichana ninayekupenda kwa dhati niliguswa sana na kujikuta nikijisikia kufanya kitu kwa ajili yako, shida zako ni shida zangu. Nina kitu gani cha kuuza Ben ili nipate pesa ya upesi ya kukusaidia, lakini wapo watu na pesa zao waliokuwa wakinitaka kimapenzi, si kwamba nilitamanishwa nao na pesa zao la! Niliguswa zaidi na matatizo yako. Nikiwa naumia roho nikajiingiza katika penzi jingine la masaa kadhaa. Baada ya zile siku mbili tulizomuomba mwenye nyumba nilikuja na kukupatia kiasi chote cha pesa na kodi ikalipwa, nilikupa pesa ile nikiwa naumia sana lakini je kipi bora? Mimi kuumia ama mpenzi wangu na mama mkwe wangu kudhalilishwa? Kwangu ilikuwa vyema kuumia mimi kwa ajili yenu.
Nakueleza haya mapema kabla haujafika ule wakati wa maadui kujifanya marafiki kisha waanze kukupamba mwishowe uniache solemba, nakuandikia haya maana ni aibu kukueleza huku nikikutazama usoni.
Na ninaayandika haya hasahasa baada ya kugundua jambo jingine la ziada. Jambo zito zaidi ambalo litamalizia kurasa za barua hii kisha nikusikilize upande wako unasemaje maana siwezi kuishi na siri hii, sitakuwa na amani hata kidogo.
IKUMBUKE siku ambayo nilikaa mimi na wewe kujadili juu ya mahari ambayo walezi wangu walimtajia mshenga uliyemleta. Siku hiyo tulikuwa nyumbani kwako na mahari ikaonekana kuwa kubwa sana, nilikutia moyo kuwa tutaipata na kulitimiza lengo. Haukuamini kwa sababu nilikuwa sina kazi baada ya kuwa tu nimemaliza chuo. Tuliumiza vichwa sana na kisha nikakueleza kuwa nitatafuta mahali niweze kukopa kisha nikupatie ulipe halafu taratibutaratibu tutaitafuta na kuilipa.
Kweli nilifanikiwa kukopa hiyo pesa kutoka kwa mfanyabiashara za samaki, alinikopesha kwa mgongo wa rafiki yangu, nilichukua ile pesa kama ilivyo na kukuletea bila kujua nitairudisha vipi. Mwezi ukakatika na hatimaye miezi miwili mwenye pesaa akaanza usumbufu, sikupenda kukueleza jinsi ninavyosumbuliwa lakini hali ilikuwa mbaya sana Ben, nikaamua kumtafuta tukakaa tukaongea juu ya hilo nikamweleza kuwa nimekaribia kupata kazi nitakuwa namlipa awamu kwa awamu. Nilipomtazama machoni nikagundua kuwa hana shida na pesa tena bali kuna neno anataka kulisema lisilohusiana na pesa. Neno gani jingine tofauti na mapenzi, hakika ilikuwa hivyo alinichombeza hivi akanichombeza vile na mwisho wa siku ilinilazimu nikubali kukusaliti kwa mara ya tatu ili tu kuiepuka aibu ile, unadhani mimi ningetoa wapi pesa ya kumlipa upesi kama alivyotaka. Hakika nisingeweza, nilikubali kuwa naye huku nikijiapiza kuwa sitathubutu tena kukusaliti Ben, nilijipa imani hiyo kwa sababu muda wangu wa kuajiriwa ulikuwa umekaribia na iwapo ningeipata ajira basi matatizo ya pesa yangeishia hapo japo kwa udogo kiasi.
Nilienda nyumbani kwake ile siku niliyokuambia kuwa naenda kwa  mama mdogo, niliondoka huku roho ikiniuma sana maana uliniambia unanipenda sana, kama unakumbuka siku hiyo nililia huku nikiwa nakukumbatia. Niliumizwa na nilichokuwa naenda kufanya mbele yangu.
Hakikuwepo kipingamizi nikafika nyumbani kwake na alikuwa aidha akiishi peke yake ama la alikuwa ameamua kuwa peke yake siku hiyo, pesa zake nikazilipa kwa kulala kitandani kwake. Nililala na kufanya naye mapenzi. Usaliti wa tatu.
Ben najua una hasira sana, lakini lipi heri kukudanganya ama kuishi nawe tukiujua ukweli?
 Na bado unajiuliza kwanini nimekuandikia haya huku huyu mtu wa mwisho nikimsisitizia sana. Ben nimesisitiza juu ya huyu mtu kwa sababu lipo la ziada ambalo mimi lilinishtua sana lakini huenda wewe litakushtua zaidi. Mara ya mwisho kuonana na mzee huyu ni mwezi mmoja nyuma nilipompa penzi kufidia pesa yake. Na unatambua kuwa nina mimba yako kwa sasa, mimba ambayo hakuna ajuaye zaidi yangu mimi na wewe. Nina mashaka na mimba hii mashaka makubwa sana kuwa ni ya huyo mzee, maana nakumbuka kuwa mwanzoni alitumia kinga lakini katika usiku wa giza hakutumia kinga. Huo ni wasiwasi ambao ninao na ninahisi kabisa kuna walakini.
Hilo bado sio zito lililonisukuma kuandika haya, tatizo ni kwamba siku ile kamati inakaa, nilimuona mzee huyo, sasa najiuliza ni nani yako mzee yule. Mzee Daudi Machota, ni nani kweako hadi ahudhurie kikao kikubwa cha harusi. Jambo hili limenitia wasiwasi na kunisukuma kuyaandika yote haya kwako. Ili asijekukuambia kitu kisha ukakichulia kama kilivyo na kunitosa kwa talaka..
Nimeyaandika haya ili kama ni stahili yangu kuhukumiwa basi unihukumu sasa kabla hujaniita mkeo wa ndoa.
Niliyafanya kwa ajili yako na kwa ajili ya penzi letu. Najua ni makosa makuu hata nikisema unisamehe hakuna lolote linalobadilika.
Nisingeweza kuyamaliza haya huku ukiwa mbele yangu maana nakujua nawe unanijua vyema.
Wako katika penzi,
Grace Mbaliga.

Mikono ilikuwa inamtetemeka Ben, karatasi ilikuwa imelowa jasho lililokuwa likitiririka kutoka katika paji la uso wake na mikono pia. Akili ilikuwa imesimama kisha kile chumba akakiona kama kinazidi kuwa kidogo na kumsababishia joto kali, hali ilikuwa tete sana.
Kizito kilichomchanganya ni jina la David ama Daud Machota katika barua ile. Alirudia kusoma mara mbilimbili, akajiuliza iwapo muandishi alikuwa anamaanisha kile alichokuwa amekiandika ama yupo katika utani. Lakini utani gani wa kurasa zote zile zilizoandikwa kiustadi na kumbukumbu ya hali ya juu.

Baba yangu!! Hivi ni baba yangu kweli ama!!! Benson alijiuliza huku akishikwa na kigugumizi, jina hilo lilikuwa na baba yake mzazi ambaye alitoweka miaka mingi iliyopita akimtelekeza yeye na mama yake, sasa amerejea tena katika familia baada ya kusamehewa. Siri hii Ben alitarajia kumweleza Grace siku watakapokutana kwani hata yeye alikuwa hajatarajia jambo hilo. Lakini Grace kumbe aliwahi kuwa mpenzi wa baba yake, na ana mashaka kuwa hiyo mimba ni ya baba yake.
Mungu wangu weee!! Alihamanika Ben. Na kujikuta katika mtihani mkubwa ambao aliamini kabisa kuwa mtihani ule ni mkiubwa kuliko umri wake wa miaka ishirini na saba.
Alikuwa na mtihani wa kimaamuzi, je azuie ndoa kufungwa, je? Amshauri Grace atoe mimba ama …ama……alikosa maamuzi hakika.

Mara alirudisha macho katika ile barua, kumbe kuna mistari miwili ya ziada ambayo bila shaka ilisahaulika wakati wa kuandika, hii iliandikwa kwa wino wa kawaida kwa kutumia mkono.
“Natamani ningeitoa mimba hii maana najua itazua utata lakini tatizo kwetu kutoa mimba ni mwiko, ukitoa mimba na kizazi kinapotea milele.”
Ewalaa!! Mstari huu ukaikoroga kabisa akili ya Ben, akapagawa kabisa, alitamani kupiga kelele lakini akajikuta akiiongoza akili yake kuukwepa wazimu uliokuwa unamnyemelea.
Akajilaza kitandani, akashangaa godoro lake imara likamuumiza mgongo. Ilistaajabisha sana. Akatazama kushoto akakutana na kikopo ambacho huwa anakitumia kuhifadhi dawa zake. Akatoa ‘pilton’ akameza tatu. Hizi zikamchukua baada ya dakika kadhaa, akasinzia haswa. Alifanya hivi ili kujizuia asipagawe.

*****

ZILIKUWA zimesalia siku tatu ndoa kati ya Ben na Grace iweze kufungwa, kwa watu wa nje kila mmoja alikuwa akifurahia ujio wa siku hiyo ya aina yake iliyoongezewa ujazo na muuza samaki, baba mpotevu wa Ben ambaye alikuwa amerejea kwa kishindo.
Ukumbi wa kisasa na mkubwa ulikuwa umekodiwa kwa ajili ya siku hiyo. Hakika ingefana sana, hapakuwa na kipingamizi.
Grace aliyetegemea majibu ya upesi kutoka kwa Ben alikuwa katika sintofahamu akijiuliza ni kipi kinaendelea katika kichwa cha Ben, alifikia hatua ya kujiuliza iwapo Ben anaweza kumkana kanisani wakati wa kuvishana pete. Wazo hili lilimtesa sana na kumfanya  mgonjwa kwa muda.
“Anawaza nini huyu mwanaume sasa!!” Alijiuliza Grace katika namna ya kughafirika. Lakini hii haikusaidia kitu na haikubadili siku ya ndoa yao. Baada ya siku tatu tu!!! Siku tatu!!
Siku hiyo ikamalizika na hatimaye zikabaki siku mbili, moja ya maandalizi ya mwisho na nyingine siku maalum kwa ajili ya kufunga ndoa.
Grace akaona hapana, hakuwa tayari kuaibika mbele za watu, akaamua kumpigia simu Ben.
Hola!! Hakuwa akipatikana katika namba zote..
Akafunga safari kwenda nyumbani kwa Ben.
Kappa!! Hakuna mtu katika nyumba ile.
Hofu yake ikazidi kujikita katika moyo wake, ni kweli walikuwa wamejifunza kila kitu, jinsi ya kutembea na namna ambavyo watafungua muziki lakini yote hii haikuwa na maana bila Grace kulisikia neno la Ben. Ben alikuwa ameamua nini baada ya taarifa ile ndefu na chafu? Hakupata jibu hadi siku ya siku ilipofika. Siku ambayo alishindwa kuitabiria itakuwa ya namna gani, siku ya kwenda kukutana na mwanaume ambaye ameyasoma maovu yake katika karatasi na kisha kukaa kimya bila kusema lolote.
Kidogo Grace akatae kwenda kanisani, lakini hapakuwa na tetesi yoyote ya jambo lolote kuwa haliendi sawa, si upande wa mwanaume wala mwanamke. Kwa kifupi hali ilikuwa shwari.


SIKU YA SIKU IKATIMIA

KANISA lilikuwa limefurika watu, palikuwa na ndoa nyingi zilizofungwa siku hiyo hivyo kila familia ilikuwa na umati wake. Nyimbo zilizopigwa zilikuwa za furaha na shangwe tupu. Nyuso za furaha zilizidi kulipendezesha kanisa.
Magari ya kifahari na ya kawaida yalikuwa yameegeshwa nje ya kanisa, mengi yao yalikuwa yamepambwa kwa maua na mapambo mengineyo. Familia ya akina Grace ilitangulia kufika ikifuatiwa na ile ya akina Ben baadaye kidogo.
Macho ya Ben yakagongana na yale ya Grace, Grace akawahi kuinama lakini Ben hakuonyesha wasiwasi wala hali yoyote ya tofauti.
Utaratibu ukafuatwa na ndoa zikaanza kufungwa.
Grace akiingoja aibu yoyote ambayo inaweza kumkuta kwa kuamua kuwa muwazi, lakini alijitia matumaini kuwa mbele za Mungu alijihesabia haki kwa kuusema ukweli kabla ya ndoa.
Ben akiwa katika suti yake maridadi alijisogeza ubavuni mwa Grace kisha akaanza kunong’ona naye kabla majina yao hayajaitwa kwa ajili ya kufungishwa ndoa.
“Wewe ni mwanamke jasiri na wa aina yake, ni mwanamme mpumbavu pekee awezaye kupumbazwa na vitendo ulivofanya kisha akaamua kuachana nawe. Benson si mwanaume moumbavu na ni mwanaume ambaye ana maamuzi yake sahihi kwa wakati muafaka. Kama ulifanya yale kwa ajili yangu, nikikuacha utaenda kwa nani? Bila shaka utaenda kwa yule ambaye umeyafanya haya bila kumuhusu yeye, wewe ni mwandani wangu, jana, leo, kesho na hata milele. Kabla ya kusema mbele ya umati napenda kukusihi kuwa kamwe sitakukana. Sitakugeuka hata kidogo.
Baba aliyenikana nikiwa mtoto anabaki kuwa kama maharamia wengine uliokutana nao, isikushtue sana hiyo mimba, nitaichukua kama yangu aidha jibu ni ndio ama hapana, hukuwahi kunivua nguo na kunitangaza kuwa mimi ni mwanaume nikutegemeaye kwa kila jambo basi amini kuwa sitathubutu kukuchafua kwa namna yoyote ile. Yawezekana ningeomba ushauri basi tusingekuwa hapa leo, lakini je? Wewe uliomba ushauri kabla ya ya kufanya uliyoyafanya kwa ajili yangu?? Naamini ungeomba ushauri ungeambulia kuambiwa uachane na mimi, basi kama ulivyofanya maamuzi binafsi. Naam! Basi nami nimefanya maamuzi binafsi, wewe ni mke wangu na nitadumu nawe milele yote kwa uweza wa muumba aliyetukutanisha mimi nawe.
Wewe ni jasiri na mwanamke wa kipekee. Amini kuwa ulichaguliwa kwa..” kabla hajamaliza…

“Bwana Benson na Bi Grace” sauti katika kipaza ilisikika, Grace akajifuta machozi yaliyokuwa tanamtiririka. Ben akafanya jambo ambalo lilizua shamrashamra pale kanisani. Akamnyakua Grace na kumweka katika mikono yake, akambeba juu juu katika namna ya kipekee, mpiga kinanda akaliona tukio hilo mara ghafla akaanza kukipiga kinanda katika namna ya kusisimua, kanisa zima likalipuka kwa nderemo na vifijo. Kila mmoja alifurahia tendo alilolifanya Ben.
“Kama nilivyombeba leo mbele yenu basi nitambeba milele hadi yule anayeenda kutuunganisha leo aamue kututenganisha.” Aliyasema haya Ben katika kipaza sauti. Kanisa likalipuka tena kwa shangwe.
Kiongozi wa kiroho akaibariki ndoa ile. Kanisa zima likishangilia. Na hata alipomaliza kufungishwa ndoa ikawa zamu ya Grace kufanya jambo jingine la kuvutia machoni.
Akachutama na kumsihi Ben apande mgongoni. Ben akapanda Grace akaondoka naye kurejea katika siti zao.
“Na nitamlea hivi hivi kama mtoto mdogo hadi atutenganishe aliyetuunganisha.” Grace akatamka. Kanisa likapiga mayowe, akina mama wakawa wanalia, kilio cha furaha. Hakika ilipendeza sana.

BEN hakuwa na masihara aliamua kutoka moyoni kuwa mume wa Grace hivyo alisawazisha yote ambayo yangeonekana kuwa kikwazo hapo baadaye, mzee Daud aliomba msamaha yakapita lakini hakuambiwa kama Grace ni mjamzito. Hilo ndio lilikuwa zito lakinilikaisha kwa wepesi tu.
Maisha yakaendelea huku Ben na Grace wakiipa somo dunia kuwa wakati mwingine mitihani isitufanye tukapoteza uelekeo wetu badala yake ituimarishe zaidi na zaidi.
Ama kwa hakika MITIHANI NI KIPIMO CHA AKILI.


MWISHO.KESHO TUTAENDELA NA SIMULIZI YA NIMEKUCHOKA

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom